Swahili na Waswahili

Swahili na Waswahili
Waswahili na Mswahili Rachel Siwa...Pamoja Daima!!

Monday 15 February 2021

Kikombe Cha Asubuhi;Waroma...15


Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?

Haleluyah ni siku/wiki nyingine tena Mungu wetu ametuchagua

na kutupa kibali cha kuendelea kuiona leo hii
Si kwamba sisi tumetenda mema sana wala si kwa nguvu zetu
si kwa utashi wetu wala si kwa akili zetu si kwamba sisi
ni wazuri mno si kwa uwezo wetu sisi kuwa hivi tulivyo leo hii
Ni kwa rehema/neema zake ni kwa mapenzi yake Mungu wetu....

Tumshukuru Mungu wetu katika yote...

Asante Mungu wetu kwa wema na fadhili zako kwetu
Asante kwa ulinzi wako kwetu wakati wote
Asante kwa pumzi/uzima,afya na kuwa tayari kwa majukumu yetu
Sifa na Utukufu tunakurudshia Mungu wetu....!!


Kilio changu kikufikie, ee Mwenyezi-Mungu! Unijalie akili kama ulivyoahidi. Ombi langu likufikie; uniokoe kama ulivyoahidi.

Zaburi 119:169-170

Tazama jana imepita ee Mungu wetu leo ni siku mpya na kesho ni siku nyingine
Jehovah tunakuja mbele zako tukijinyenyekeza,
tukijishusha na kujiachilia mikononi mwako
 Mungu wetu tunaomba utusamehe dhambi zetu zote tulizozifanya kwakuwaza,kwakunena,kwakutenda,kwakujua/kutojua
Baba wa Mbinguni nasi tunaomba utupe neema ya kuweza kuwasamehe wale wote waliotukosea
Jehovah usitutie majaribuni Mungu wetu tunaomba utuepushe na yule mwovu na kazi zake zote
Yahweh tunaomba ututakase miili yetu na akili zetu
Baba wa Mbinguni utufunike kwa Damu ya Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo wa Nazareti
yeye aliteseka kwanza ili sisi tupate kupona

Kwakupigwa kwake sisi tumepata kupona....

Nitasema sifa zako mfululizo, maana wanifundisha masharti yako. Nitaimba juu ya neno lako, maana amri zako zote ni za haki. Uwe daima tayari kunisaidia, maana nimeamua kufuata kanuni zako.

Zaburi 119:171-173 

Yahweh tunaomba ukabariki kazi za mikono yetu

Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe ubunifu na maarifa 
katika utendaji
Jehovah nasi tukatende sawasawa na mapenzi yako
Baba wa Mbinguni tunaomba ukabariki ridhiki zetu
ziingiazo/zitokazo
Mungu wetu nasi tunaomba ukatupe neema ya kuweza
kuwabariki wenye kuhitaji
Yahweh tusipungukiwe katika mahitaji yetu
Mungu wetu ukatupe kama inavyokupendeza wewe

Baba wa Mbinguni tunayaweka maisha yetu mikononi mwako
Mungu wetu tunaomba ukabariki nyumba/ndoa zetu,
watoto,wazazi wetu,familia/ndugu na wote wanaotuzunguka
Jehovah tunaomba ulinzi wako kwetu na kwa vyote tunavyo vimiliki
Yahweh tunaomba ukatubariki tuingiapo/tutokapo
Mungu wetu tunaomba ukavibariki vyote tunavyoenda kugusa/kutumia
Baba wa Mbinguni ukavitakase kwa Damu ya Bwana wetu Yesu Kristo
Mungu wetu ukatamalaki na kutuatamia
Baba wa Mbinguni tukawe salama rohoni
Mfalme wa amani amani yako ikatawale katika maisha yetu
Mungu wetu ukatupe macho ya kuona na masikio ya kusikia 
sauti yako na kuitii
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe neema ya kufuata njia zako
Yahweh tukasimamie Neno lako amri na sheria zako siku zote 
za maisha yetu
Mungu wetu ukaonekane katika maisha yetu
Neema zako zikawe nasi Nuru yako ikaangaze katika maisha yetu
ukatuguse kwa mkono wako wenye nguvu
Ukatufanye chombo chema ee Mungu wetu nasi tukatumike kama
inavyokupendeza wewe
Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi...

Natazamia sana uniokoe, ee Mwenyezi-Mungu; sheria yako ndiyo furaha yangu. Unijalie kuishi nipate kukusifu; na maagizo yako yanisaidie. Natangatanga kama kondoo aliyepotea; uje kunitafuta mimi mtumishi wako, maana sikusahau amri zako.

Zaburi 119:174-176

Mungu wetu tunawaweka mikononi mwako wenye shida/tabu,wote wanaopitia magumu/majaribu mbalimbali
Mungu wetu tunaomba ukawaguse kwa mkono wako wenye nguvu
 kila mmoja na mahitaji yake 
Mungu wetu tunaomba ukawasamehe pale walipokwenda kinyume nawe
Baba wa Mbinguni ukawape neema ya kujiombea,kufuata njia zako
wakasimamie Neno lako nalo likawaweke huru
Mungu wetu tunaomba ukasikie kuomba kwetu
Mungu wetu ukawatendee sawasawa na mapenzi yako
Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele
Amina...!!


Asanteni sana wapendwa katika Kristo Yesu kwakuwa nami
Mungu Baba aendelee kuwabariki na kuwatendea 
kama inavyompendeza yeye....
Nawapenda.



 Acheni ubinafsi

1Sisi tulio imara katika imani tunapaswa kuwasaidia wale walio dhaifu wayakabili matatizo yao. Tusijipendelee sisi wenyewe tu. 2Kila mmoja wetu anapaswa kumpendeza jirani yake kwa wema ili huyo apate kujijenga katika imani. 3Taz Zab 69.9 Maana Kristo hakujipendelea mwenyewe; ila alikuwa kama yasemavyo Maandiko: “Kashfa zote walizokutolea wewe zimenipata mimi.” 4Maana, yote yaliyoandikwa yameandikwa kwa ajili ya kutufundisha sisi ili kutokana na saburi na faraja tupewayo na hayo Maandiko Matakatifu tupate kuwa na matumaini. 5Mungu aliye msingi wa saburi na faraja yote, awajalieni nyinyi kuwa na msimamo mmoja kufuatana na mfano wake Kristo Yesu, 6ili nyinyi nyote, kwa nia moja na sauti moja, mumtukuze Mungu, Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo.
Habari Njema kwa watu wote
7Basi, karibishaneni kwa ajili ya utukufu wa Mungu kama naye Kristo alivyowakaribisheni. 8Maana, nawaambieni Kristo aliwatumikia Wayahudi apate kuonesha uaminifu wa Mungu, na zile ahadi Mungu alizowapa babu zetu zipate kutimia; 9Taz Zab 18:49 ili nao watu wa mataifa mengine wapate kumtukuza Mungu kwa sababu ya huruma yake. Kama yasemavyo Maandiko Matakatifu:
“Kwa hiyo nitakusifu miongoni mwa watu wa mataifa.
Nitaziimba sifa za jina lako.”
10Tena Maandiko yasema:
“Furahini, enyi watu wa mataifa;
furahini pamoja na watu wake.”
11 Taz Zab 117:1 Na tena:
“Enyi mataifa yote, msifuni Bwana;
enyi watu wote, msifuni.”
12Tena Isaya asema:
“Atatokea chipukizi katika ukoo wa Yese,
naye atawatawala watu wa mataifa;
nao watamtumainia.”
13Basi, Mungu aliye msingi wa matumaini, awajazeni furaha yote na amani kutokana na imani yenu; tumaini lenu lipate kuongezeka kwa nguvu ya Roho Mtakatifu.
Huduma ya Paulo
14Ndugu zangu, mimi binafsi nina hakika kwamba nyinyi pia mmejaa wema, elimu yote, na mnaweza kushauriana nyinyi kwa nyinyi. 15Lakini nimewaandikia hapa na pale katika barua hii bila woga, nipate kuwakumbusheni juu ya mambo fulani. Nimefanya hivyo kwa sababu ya neema aliyonijalia Mungu 16ya kuwa mtumishi wa Yesu Kristo kwa watu wa mataifa. Ni jukumu langu la kikuhani kuihubiri Habari Njema ya Mungu ili watu wa mataifa mengine wapate kuwa tambiko inayokubaliwa na Mungu, tambiko iliyotakaswa na Roho Mtakatifu. 17Kwa hiyo, nikiwa nimeungana na Kristo Yesu, naweza kujivunia huduma yangu kwa ajili ya Mungu. 18Sithubutu kusema kitu kingine chochote isipokuwa tu kile ambacho Kristo Yesu amekifanya kwa kunitumia mimi ili watu wa mataifa wapate kutii. Amefanya hivyo kwa maneno na vitendo, 19kwa nguvu ya miujiza na maajabu, na kwa nguvu ya Roho wa Mungu. Basi, kwa kusafiri kila mahali, tangu kule Yerusalemu mpaka Iluriko, nimeihubiri kikamilifu Habari Njema ya Kristo. 20Nia yangu imekuwa daima kuihubiri Habari Njema popote pale ambapo jina la Kristo halijapata kusikika, nisije nikajenga juu ya msingi wa mtu mwingine. 21Kama yasemavyo Maandiko Matakatifu:
“Watu wote ambao hawakuambiwa habari zake wataona;
nao wale ambao hawajapata kusikia, wataelewa.”
Mpango wa Paulo wa kutembelea Roma
22Kwa sababu hiyo nilizuiwa mara nyingi kuja kwenu. 23Lakini maadamu sasa nimemaliza kazi yangu pande hizi, na kwa kuwa kwa miaka mingi nimekuwa na nia kubwa ya kuja kwenu, 24natumaini kufanya hivyo sasa. Ningependa kuwaoneni nikiwa safarini kwenda Spania na kupata msaada wenu kwa safari hiyo baada ya kufurahia kuwa kwa muda pamoja nanyi. 25Lakini, kwa sasa nakwenda kuwahudumia watu wa Mungu kule Yerusalemu. 26Maana makanisa ya Makedonia na Akaya yemeamua kutoa mchango wao kuwasaidia watu wa Mungu walio maskini huko Yerusalemu. 27Wao wenyewe wameamua kufanya hivyo; lakini, kwa kweli, hilo ni jukumu lao kwa hao. Maana, ikiwa watu wa mataifa mengine wameshiriki baraka za kiroho za Wayahudi, wanapaswa nao pia kuwahudumia Wayahudi katika mahitaji yao ya kidunia. 28Nitakapokwisha tekeleza kazi hiyo na kuwakabidhi mchango huo uliokusanywa kwa ajili yao, nitawatembeleeni nyinyi nikiwa safarini kwenda Spania. 29Najua ya kuwa nikija kwenu nitawaletea wingi wa baraka za Kristo.
30Basi, ndugu zangu, nawasihi kwa Bwana wetu Yesu Kristo na kwa upendo uletwao na Roho, mniunge mkono kwa kuniombea kwa Mungu. 31Ombeni nipate kutoka salama miongoni mwa wale wasioamini walioko Uyahudi, nayo huduma yangu huko Yerusalemu ipate kukubaliwa na watu wa Mungu walioko huko. 32Hivyo, Mungu akipenda, nitaweza kuja kwenu na moyo wa furaha, nikapumzike pamoja nanyi. 33Mungu aliye chanzo cha amani na awe nanyi nyote! Amina!

Waroma15;1-33
Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)
"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe

No comments: