Swahili na Waswahili

Swahili na Waswahili
Waswahili na Mswahili Rachel Siwa...Pamoja Daima!!

Friday 19 February 2021

Kikombe Cha Asubuhi: Kitabu cha Wakorintho....3

 


Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?

Tumshukuru Mungu katika yote....

Mungu wetu Baba yetu,Muumba wetu Muumba wa Mbingu na Nchi
Muumba wa vyote vilivyomo vinavyoonekana na visivyoonekana
Mungu wa walio hai,Mungu  mwenye huruma,Mungu wa upendo
Mungu wa Abrahamu,Isaka na Yakobo...
Asante kwa wema na fadhili zako kwetu
Asante kwa ulinzi wako kwetu wakati wote
Asante kwa kutuchagua tena na kutupa
kibali cha kuendelea kuiona leo hii
Asante kwa pumzi/uzima,afya na kuwatayari kwa majukumu yetu

Neema yako yatutosha ee Mungu wetu...


Ndugu aliyeudhiwa ni mgumu kuliko mji wa ngome; magomvi hubana kama makufuli ya ngome. Maneno ya mtu yaweza kumshibisha; hutosheka kwa matokeo ya maneno yake.

Methali 18:19-20

Baba wa Mbinguni tunakuja mbele zako,
Tukijinyenyekeza,tukijiachilia mikononi mwako
Mungu wetu tunamomba utusamehe dhambi zetu
Baba wa Mbinguni nasi tunaomba ukatupe neema
 ya kuweza kuwasamehe wale wote waliotukosea

Usitutie majaribuni Mungu wetu tunaomba utuepushe
na yule mwovu na kazi zake zote
Jehovah ututakase miili yetu na akili zetu
Baba wa Mbinguni tunaomba utufunike kwa Damu
ya Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo wa Nazareti
yeye aliteseka kwanza ili sisi tupate kupona....


Ulimi una nguvu ya kufanya hai na kuua; wanaopenda kuutumia watakula matunda yake. Anayempata mke amepata bahati njema; hiyo ni fadhili kutoka kwa Mwenyezi-Mungu.

Methali 18:21-22

Mungu wetu tunaomba ukabariki kazi za mikono yetu
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe ubunifu na maarifa katika utendaji
Jehovah nasi tukatende sawasawa na mapenzi yako
Yahweh tunaomba ukabariki ridhiki zetu ziingiazo/zitokazo
Mungu wetu nasi tunaomna ukatupe neema ya kuweza kuwabariki wenye kuhitaji
Tusipungukiwe katika mahitaji yetu
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe kama inavyokupendeza wewe...


Yahweh tunayaweka maisha yetu mikononi mwako
Mungu wetu tunaomba ukabariki nyumba/ndoa zetu,
Jehovah tunaomba ulinzi wako kwetu na kwa vyote tunavyovimiliki
Yahweh tunaomba ukatubariki tuingiapo/tutokapo
Mungu wetu tunaomba ukavibariki vyote tunavyoenda kugusa/kutumia
Baba wa Mbinguni ukavitakase kwa Damu ya Bwana wetu Yesu Kristo
Mungu wetu ukatamalaki na kutuatamia
Baba wa Mbinguni tukawe salama rohoni
Yahwe ukatupe akili ya kutambua mema na mabaya
Mfalme wa amani amani yako ikatawale katika maisha yetu
Mungu wetu ukatupe macho ya kuona,masikio ya kusikia sauti yako na kuitii..
Baba wa Mbinguni  tunaomba ukatupe neema ya kufuata
njia zako,tukasimamie Neno lako,amri na sheria zako
siku zote za maisha yetu...
Ukatuguse kwa mkono wako wenye nguvu,ukatufanye chombo chema
ee Mungu wetu nasi tukatumike kama inavyokupendeza wewe
Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi....


Maskini huomba kwa unyenyekevu, bali tajiri hujibu kwa ukali. Marafiki wengi waweza kumwangusha mtu, lakini wapo marafiki waaminifu kuliko ndugu.

Methali 18:23-24

Tazama watoto wako wenye shida/tabu,wote wanaopitia magumu/majaribu mbalimbali
Mungu wetu tunaomba ukawaguse kwa mkono wako wenye nguvu
kila mmoja na mahitaji yake
Mungu wetu tunaomba ukawasamehe pale walipo kwenda kinyume nawe
Yahweh tunaomba ukawape neema ya kuweza kujiombea,kufuata njia zako nazo zikawaweke huru...
Baba wa Mbinguni tunayaweka haya yote mikononi mwako
Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele...
Amina...!!


Asanteni sana wapendwa katika Kristo Yesu kwakuwa nami,
Baba wa Mbinguni aendelee kuwatendea sawasawa na mapenzi yake...


Watumishi wa Bwana
1Ndugu, mimi sikuweza kusema nanyi kama watu mlio na huyo Roho. Nilipaswa kusema nanyi kama watu wa kidunia, kama watoto wachanga katika maisha ya Kikristo. 2Ilinibidi kuwalisheni kwa maziwa, na si kwa chakula kigumu, kwani hamkuwa tayari kukipokea. Hata sasa hamko tayari. 3Maana bado nyinyi ni watu wa kidunia. Je, si kweli kwamba bado uko wivu na ugomvi kati yenu? Mambo hayo yanaonesha wazi kwamba nyinyi bado ni watu wa kidunia, mnaishi mtindo wa kidunia. 4Mmoja wenu anaposema, “Mimi ni wa Paulo”, na mwingine, “Mimi ni wa Apolo”, je, hiyo haionyeshi kwamba mnaishi bado kama watu wa dunia hii tu?
5Apolo ni nani? Na Paulo ni nani? Sisi ni watumishi tu ambao tuliwaleteeni nyinyi imani. Kila mmoja wetu anafanya kazi aliyopewa na Bwana. 6Mimi nilipanda mbegu, Apolo akamwagilia maji; lakini aliyeiotesha mbegu ni Mungu. 7Wa maana si yule aliyepanda mbegu, au yule aliyemwagilia maji; wa maana ni Mungu aliyeiwezesha mbegu kuota. 8Yule aliyepanda na yule aliyemwagilia maji wote ni sawa, ingawa kila mmoja atapokea tuzo lake kufuatana na jitihada yake mwenyewe. 9Maana sisi ni ndugu, wafanyakazi pamoja na Mungu; na nyinyi ni shamba lake; nyinyi ni jengo lake.
10Kwa msaada wa neema aliyonipa Mungu, nimefaulu, kama mwashi stadi mwenye busara, kuweka msingi ambao juu yake mtu mwingine anajenga. Basi, kila mmoja awe mwangalifu jinsi anavyojenga juu yake. 11Hakuna mtu awezaye kuweka msingi mwingine badala ya ule uliokwisha wekwa, yaani Yesu Kristo. 12Juu ya msingi huo mtu anaweza kujenga kwa dhahabu, fedha au mawe ya thamani; anaweza kutumia miti, majani au nyasi. 13Iwe iwavyo, ubora wa kazi ya kila mmoja utaonekana wakati siku ile ya Kristo itakapoifichua. Maana, siku hiyo itatokea na moto, na huo moto utaipima na kuonesha ubora wake. 14Ikiwa alichojenga mtu juu ya huo msingi kitaustahimili huo moto, atapokea tuzo; 15lakini kama alichojenga kitaunguzwa, basi, atapoteza tuzo lake; lakini yeye mwenyewe ataokolewa kana kwamba ameponyoka kutoka motoni.
16Je, hamjui kwamba nyinyi ni hekalu la Mungu, na kwamba Roho wa Mungu anakaa ndani yenu? 17Basi, mtu akiliharibu hekalu la Mungu, Mungu atamharibu; maana hekalu la Mungu ni takatifu, na hekalu hilo ni nyinyi wenyewe.
18Msijidanganye! Mtu yeyote miongoni mwenu akijidhania mwenye hekima mtindo wa kidunia, heri awe mjinga kusudi apate kuwa na hekima ya kweli. 19Maana, hekima ya kidunia ni upumbavu mbele ya Mungu. Kwani Maandiko Matakatifu yasema: “Mungu huwanasa wenye hekima katika ujanja wao.” 20Taz Zab 94:11 Na tena: “Bwana ajua kwamba mawazo ya wenye hekima hayafai.” 21Basi, mtu asijivunie watu. Maana kila kitu ni chenu. 22Paulo, Apolo na Kefa, ulimwengu, maisha na kifo; mambo ya sasa na ya baadaye, yote ni yenu. 23Lakini nyinyi ni wa Kristo, naye Kristo ni wa Mungu.
Wakorintho3;1-22
Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)
"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe

No comments: