Swahili na Waswahili

Swahili na Waswahili
Waswahili na Mswahili Rachel Siwa...Pamoja Daima!!

Monday 30 November 2020

Kikombe Cha Asubuhi; Yohane 9...


Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?

Haleluyah ni siku/wiki nyingine tena Mungu wetu ametuchagua

na kutupa kibali cha kuendelea kuiona leo hii
Si kwamba sisi tumetenda mema sana wala si kwa nguvu zetu
si kwa utashi wetu wala si kwa akili zetu si kwamba sisi
ni wazuri mno si kwa uwezo wetu sisi kuwa hivi tulivyo leo hii
Ni kwa rehema/neema zake ni kwa mapenzi yake Mungu wetu....

Tumshukuru Mungu wetu katika yote...

Asante Mungu wetu kwa wema na fadhili zako kwetu
Asante kwa ulinzi wako kwetu wakati wote
Asante kwa pumzi/uzima,afya na kuwa tayari kwa majukumu yetu
Sifa na Utukufu tunakurudshia Mungu wetu....!!


Mwenyezi-Mungu anatawala, mataifa yanatetemeka! Ameketi juu ya viumbe vyenye mabawa, nayo dunia inatikisika! Mwenyezi-Mungu ni mkuu katika Siyoni; ametukuka juu ya mataifa yote. Wote na walisifu jina lake kuu la kutisha. Mtakatifu ndiye yeye!

Zaburi 99:1-3

Tazama jana imepita ee Mungu wetu leo ni siku mpya na kesho ni siku nyingine
Jehovah tunakuja mbele zako tukijinyenyekeza,
tukijishusha na kujiachilia mikononi mwako
 Mungu wetu tunaomba utusamehe dhambi zetu zote tulizozifanya kwakuwaza,kwakunena,kwakutenda,kwakujua/kutojua
Baba wa Mbinguni nasi tunaomba utupe neema ya kuweza kuwasamehe wale wote waliotukosea
Jehovah usitutie majaribuni Mungu wetu tunaomba utuepushe na yule mwovu na kazi zake zote
Yahweh tunaomba ututakase miili yetu na akili zetu
Baba wa Mbinguni utufunike kwa Damu ya Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo wa Nazareti
yeye aliteseka kwanza ili sisi tupate kupona

Kwakupigwa kwake sisi tumepata kupona....

Ee mfalme mkuu, mpenda uadilifu! Umethibitisha haki katika Israeli; umeleta uadilifu na haki. Msifuni Mwenyezi-Mungu, Mungu wetu; angukeni kifudifudi mbele zake. Mtakatifu ndiye yeye! Mose na Aroni walikuwa makuhani wake; Samueli alikuwa miongoni mwa waliomlilia. Walimlilia Mwenyezi-Mungu naye akawasikiliza.

Zaburi 99:4-6

Yahweh tunaomba ukabariki kazi za mikono yetu

Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe ubunifu na maarifa 
katika utendaji
Jehovah nasi tukatende sawasawa na mapenzi yako
Baba wa Mbinguni tunaomba ukabariki ridhiki zetu
ziingiazo/zitokazo
Mungu wetu nasi tunaomba ukatupe neema ya kuweza
kuwabariki wenye kuhitaji
Yahweh tusipungukiwe katika mahitaji yetu
Mungu wetu ukatupe kama inavyokupendeza wewe

Baba wa Mbinguni tunayaweka maisha yetu mikononi mwako
Mungu wetu tunaomba ukabariki nyumba/ndoa zetu,
watoto,wazazi wetu,familia/ndugu na wote wanaotuzunguka
Jehovah tunaomba ulinzi wako kwetu na kwa vyote tunavyo vimiliki
Yahweh tunaomba ukatubariki tuingiapo/tutokapo
Mungu wetu tunaomba ukavibariki vyote tunavyoenda kugusa/kutumia
Baba wa Mbinguni ukavitakase kwa Damu ya Bwana wetu Yesu Kristo
Mungu wetu ukatamalaki na kutuatamia
Baba wa Mbinguni tukawe salama rohoni
Mfalme wa amani amani yako ikatawale katika maisha yetu
Mungu wetu ukatupe macho ya kuona na masikio ya kusikia 
sauti yako na kuitii
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe neema ya kufuata njia zako
Yahweh tukasimamie Neno lako amri na sheria zako siku zote 
za maisha yetu
Mungu wetu ukaonekane katika maisha yetu
Neema zako zikawe nasi Nuru yako ikaangaze katika maisha yetu
ukatuguse kwa mkono wako wenye nguvu
Ukatufanye chombo chema ee Mungu wetu nasi tukatumike kama
inavyokupendeza wewe
Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi...

Alisema nao katika mnara wa wingu; waliyazingatia matakwa yake na amri alizowapa. Ee Mwenyezi-Mungu, Mungu wetu, wewe uliwasikiliza; kwao ulikuwa Mungu mwenye kusamehe, ingawa uliwaadhibu kwa makosa yao. Msifuni Mwenyezi-Mungu, Mungu wetu; abuduni katika mlima wake mtakatifu! Mwenyezi-Mungu, Mungu wetu, ni mtakatifu.

Zaburi 99:7-9

Mungu wetu tunawaweka mikononi mwako wenye shida/tabu,wote wanaopitia magumu/majaribu mbalimbali
Mungu wetu tunaomba ukawaguse kwa mkono wako wenye nguvu
 kila mmoja na mahitaji yake 
Mungu wetu tunaomba ukawasamehe pale walipokwenda kinyume nawe
Baba wa Mbinguni ukawape neema ya kujiombea,kufuata njia zako
wakasimamie Neno lako nalo likawaweke huru
Mungu wetu tunaomba ukasikie kuomba kwetu
Mungu wetu ukawatendee sawasawa na mapenzi yako
Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele
Amina...!!


Asanteni sana wapendwa katika Kristo Yesu kwakuwa nami
Mungu Baba aendelee kuwabariki na kuwatendea 
kama inavyompendeza yeye....
Nawapenda.
Yesu anamponya mtu aliyezaliwa Kipofu
1Yesu alipokuwa akipita alimwona mtu mmoja, kipofu tangu kuzaliwa. 2Basi, wanafunzi wakamwuliza, “Mwalimu! Ni nani aliyetenda dhambi: Mtu huyu, ama wazazi wake, hata akazaliwa kipofu?” 3Yesu akajibu, “Jambo hili halikutukia kwa sababu ya dhambi zake yeye, wala dhambi za wazazi wake; ila alizaliwa kipofu ili nguvu ya Mungu ionekane ikifanya kazi ndani yake. 4Kukiwa bado mchana yatupasa kuendelea kufanya kazi za yule aliyenituma; maana usiku unakuja ambapo mtu hawezi kufanya kazi. 5Wakati ningali ulimwenguni, mimi ni mwanga wa ulimwengu.” 6Baada ya kusema hayo, akatema mate chini, akafanyiza tope, akampaka yule kipofu machoni, 7akamwambia, “Nenda ukanawe katika bwawa la Siloamu.” (Maana ya jina hili ni “aliyetumwa”). Hapo, huyo kipofu akaenda, akanawa, kisha akarudi akiwa anaona.
8Basi, jirani zake na wale waliokuwa wanajua kwamba hapo awali alikuwa maskini mwombaji, wakasema, “Je, huyu siye yule maskini aliyekuwa akiketi na kuomba?” 9Baadhi yao wakasema, “Ndiye.” Wengine wakasema, “La! Ila anafanana naye.” Lakini huyo aliyekuwa kipofu akasema, “Ni mimi!” 10Basi, wakamwuliza, “Sasa, macho yako yalipataje kufumbuliwa?” 11Naye akawajibu, “Yule mtu aitwaye Yesu alifanya tope, akanipaka machoni na kuniambia: ‘Nenda ukanawe katika bwawa la Siloamu.’ Hapo, mimi nikaenda, nikanawa, nikapata kuona.” 12Wakamwuliza, “Yeye yuko wapi?” Naye akawajibu, “Mimi sijui!”
Uchunguzi kuhusu kuponywa kipofu
13Kisha wakampeleka huyo mtu aliyekuwa kipofu kwa Mafarisayo. 14Siku hiyo Yesu alipofanya tope na kumfumbua macho mtu huyo, ilikuwa siku ya Sabato. 15Basi, Mafarisayo wakamwuliza mtu huyo, “Umepataje kuona?” Naye akawaambia, “Alinipaka tope machoni, nami nikanawa na sasa naona.” 16Baadhi ya Mafarisayo wakasema, “Mtu huyu hakutoka kwa Mungu, maana hashiki sheria ya Sabato.” Lakini wengine wakasema, “Mtu mwenye dhambi awezaje kufanya ishara za namna hii?” Kukawa na mafarakano kati yao. 17Wakamwuliza tena huyo mtu aliyekuwa kipofu, “Maadamu yeye amekufungua macho, wasemaje juu yake?” Naye akawaambia, “Yeye ni nabii!”
18Viongozi wa Wayahudi hawakusadiki kwamba mtu huyo alikuwa kipofu hapo awali na sasa anaona, mpaka walipowaita wazazi wake. 19Basi, wakawauliza hao wazazi, “Je, huyu ndiye mtoto wenu ambaye nyinyi mwasema alizaliwa kipofu? Sasa amepataje kuona?” 20Wazazi wake wakajibu, “Tunajua kwamba huyu ni mtoto wetu, na kwamba alizaliwa kipofu. 21Lakini amepataje kuona, hatujui; na wala hatumjui yule aliyemfumbua macho. Mwulizeni yeye mwenyewe; yeye ni mtu mzima, anaweza kujitetea mwenyewe.” 22Wazazi wake walisema hivyo kwa sababu waliwaogopa viongozi wa Wayahudi kwani viongozi hao walikuwa wamepatana ya kwamba mtu yeyote atakayekiri kwamba Yesu ni Kristo atafukuzwa nje ya sunagogi. 23Ndiyo maana wazazi wake walisema: “Yeye ni mtu mzima, mwulizeni.”
24Basi, wakamwita tena huyo aliyekuwa kipofu, wakamwambia, “Sema ukweli mbele ya Mungu! Sisi tunajua kwamba mtu huyu ni mwenye dhambi.” 25Yeye akajibu, “Kama ni mwenye dhambi mimi sijui. Lakini kitu kimoja najua: Nilikuwa kipofu, na sasa naona.” 26Basi, wakamwuliza, “Alikufanyia nini? Alikufumbuaje macho yako?” 27Huyo mtu akawajibu, “Nimekwisha waambieni, nanyi hamkusikiliza; kwa nini mwataka kusikia tena? Je, nyinyi pia mnataka kuwa wafuasi wake?” 28Lakini wao wakamtukana wakisema, “Wewe ni mfuasi wake; sisi ni wafuasi wa Mose. 29Sisi tunajua kwamba Mungu alisema na Mose, lakini mtu huyu hatujui ametoka wapi!” 30Naye akawajibu, “Hili ni jambo la kushangaza! Nyinyi hamjui ametoka wapi, lakini amenifumbua macho yangu! 31Tunajua kwamba Mungu hawasikilizi watu wenye dhambi, ila humsikiliza yeyote mwenye kumcha na kutimiza mapenzi yake. 32Tangu mwanzo wa ulimwengu haijasikika kwamba mtu ameyafumbua macho ya mtu aliyezaliwa kipofu. 33Kama mtu huyu hakutoka kwa Mungu, hangeweza kufanya chochote!” 34Wao wakamjibu, “Wewe ulizaliwa na kulelewa katika dhambi; unawezaje kutufundisha sisi?” Basi, wakamfukuza sunagogini.
Upofu wa roho
35Yesu alisikia kwamba walikuwa wamemfukuza sunagogini. Basi, alipomkuta akamwuliza, “Je, wewe unamwamini Mwana wa Mtu?” 36Huyo mtu akajibu, “Mheshimiwa, niambie yeye ni nani, ili nipate kumwamini.” 37Yesu akamwambia, “Umekwisha mwona, naye ndiye anayesema nawe sasa.” 38Basi, huyo mtu akasema, “Ninaamini Bwana!” Akamsujudia.
39Yesu akasema, “Mimi nimekuja ulimwenguni kutoa hukumu, kusudi wasioona wapate kuona, na wale wanaoona wawe vipofu.” 40Baadhi ya Mafarisayo waliokuwa pamoja naye walisikia maneno hayo, wakamwuliza, “Je, sisi pia ni vipofu?” 41Yesu akawajibu, “Kama mngekuwa vipofu, hamngekuwa na hatia; lakini sasa nyinyi mwasema: ‘Sisi tunaona,’ na hiyo yaonesha kwamba mna hatia bado.

Yohane9;1-41
Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)
"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe

No comments: