Swahili na Waswahili

Swahili na Waswahili
Waswahili na Mswahili Rachel Siwa...Pamoja Daima!!

Thursday 12 November 2020

Kikombe Cha Asubuhi; Luka 21...


Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?

Tumshukuru Mungu katika yote....

Mungu wetu Baba yetu,Muumba wetu Muumba wa Mbingu na Nchi
Muumba wa vyote vilivyomo vinavyoonekana na visivyoonekana
Mungu wa walio hai,Mungu  mwenye huruma,Mungu wa upendo
Mungu wa Abrahamu,Isaka na Yakobo...
Asante kwa wema na fadhili zako kwetu
Asante kwa ulinzi wako kwetu wakati wote
Asante kwa kutuchagua tena na kutupa
kibali cha kuendelea kuiona leo hii
Asante kwa pumzi/uzima,afya na kuwatayari kwa majukumu yetu

Neema yako yatutosha ee Mungu wetu....!!


“Ombeni, nanyi mtapewa; tafuteni, nanyi mtapata; bisheni mlango, nanyi mtafunguliwa. Maana, yeyote aombaye hupewa, atafutaye hupata, na abishaye mlango hufunguliwa.

Mathayo 7:7-8

Baba wa Mbinguni tunakuja mbele zako,
Tukijinyenyekeza,tukijiachilia mikononi mwako
Mungu wetu tunamomba utusamehe dhambi zetu
Baba wa Mbinguni nasi tunaomba ukatupe neema
 ya kuweza kuwasamehe wale wote waliotukosea

Usitutie majaribuni Mungu wetu tunaomba utuepushe
na yule mwovu na kazi zake zote
Jehovah ututakase miili yetu na akili zetu
Baba wa Mbinguni tunaomba utufunike kwa Damu
ya Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo wa Nazareti
yeye aliteseka kwanza ili sisi tupate kupona....



Je, kuna yeyote miongoni mwenu ambaye mtoto wake akimwomba mkate, atampa jiwe? Au je, akimwomba samaki, atampa nyoka?

Mathayo 7:9-10

Mungu wetu tunaomba ukabariki kazi za mikono yetu
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe ubunifu na maarifa katika utendaji
Jehovah nasi tukatende sawasawa na mapenzi yako
Yahweh tunaomba ukabariki ridhiki zetu ziingiazo/zitokazo
Mungu wetu nasi tunaomna ukatupe neema ya kuweza kuwabariki wenye kuhitaji
Tusipungukiwe katika mahitaji yetu
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe kama inavyokupendeza wewe...


Yahweh tunayaweka maisha yetu mikononi mwako
Mungu wetu tunaomba ukabariki nyumba/ndoa zetu,
Jehovah tunaomba ulinzi wako kwetu na kwa vyote tunavyovimiliki
Yahweh tunaomba ukatubariki tuingiapo/tutokapo
Mungu wetu tunaomba ukavibariki vyote tunavyoenda kugusa/kutumia
Baba wa Mbinguni ukavitakase kwa Damu ya Bwana wetu Yesu Kristo
Mungu wetu ukatamalaki na kutuatamia
Baba wa Mbinguni tukawe salama rohoni
Yahwe ukatupe akili ya kutambua mema na mabaya
Mfalme wa amani amani yako ikatawale katika maisha yetu
Mungu wetu ukatupe macho ya kuona,masikio ya kusikia sauti yako na kuitii..
Baba wa Mbinguni  tunaomba ukatupe neema ya kufuata
njia zako,tukasimamie Neno lako,amri na sheria zako
siku zote za maisha yetu...
Ukatuguse kwa mkono wako wenye nguvu,ukatufanye chombo chema
ee Mungu wetu nasi tukatumike kama inavyokupendeza wewe
Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi....



Kama basi nyinyi, ingawa ni waovu, mwajua kuwapa watoto wenu vitu vizuri, hakika Baba yenu wa mbinguni atafanya zaidi: Atawapa mema wale wanaomwomba. “Yote mnayotaka watu wawatendee nyinyi, watendeeni wao vivyo hivyo. Hii ndiyo maana ya sheria ya Mose na mafundisho ya manabii.

Mathayo 7:11-12

Tazama watoto wako wenye shida/tabu,wote wanaopitia magumu/majaribu mbalimbali
Mungu wetu tunaomba ukawaguse kwa mkono wako wenye nguvu
kila mmoja na mahitaji yake
Mungu wetu tunaomba ukawasamehe pale walipo kwenda kinyume nawe
Yahweh tunaomba ukawape neema ya kuweza kujiombea,kufuata njia zako nazo zikawaweke huru...
Baba wa Mbinguni tunayaweka haya yote mikononi mwako
Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele...
Amina...!!


Asanteni sana wapendwa katika Kristo Yesu kwakuwa nami,Baba wa Mbinguni aendelee kuwatendea sawasawa na mapenzi yake...

Nawapenda.

 Sadaka ya mama mjane

(Marko 12:41-44)
1Yesu alitazama kwa makini, akawaona matajiri walivyokuwa wanatia sadaka zao katika hazina ya hekalu, 2akamwona pia mama mmoja mjane akitumbukiza humo sarafu mbili ndogo. 3Basi, akasema, “Nawaambieni kweli, mama huyu mjane maskini ametia katika hazina kiasi kikubwa kuliko walichotia wote. 4Kwa maana, wengine wote wametoa sadaka zao kutokana na ziada ya mali zao, lakini huyu mama, ingawa ni maskini, ametoa kila kitu alichohitaji kwa kuishi.”
Yesu anatabiri kuharibiwa kwa hekalu
(Mat 24:1-2; Marko 13:1-2)
5Baadhi ya wanafunzi walikuwa wanazungumza juu ya hekalu, jinsi lilivyopambwa kwa mawe ya thamani, pamoja na sadaka zilizotolewa kwa Mungu. Yesu akasema, 6“Haya yote mnayoyaona – zitakuja siku ambapo hakuna hata jiwe moja litakalosalia juu ya lingine; kila kitu kitaharibiwa.”
Taabu na mateso
(Mat 24:3-14; Marko 13:3-13)
7Basi, wakamwuliza, “Mwalimu, mambo hayo yatatokea lini? Na ni ishara gani zitakazoonesha kwamba karibu mambo hayo yatokee?”
8Yesu akawajibu, “Jihadharini, msije mkadanganyika. Maana wengi watatokea na kulitumia jina langu, kila mmoja akidai kwamba yeye ni mimi, na kwamba wakati ule umekaribia. Lakini nyinyi msiwafuate! 9Basi, mtakaposikia habari za vita na misukosuko, msitishike; maana ni lazima hayo yatokee kwanza, lakini mwisho wa yote, bado.”
10Halafu akaendelea kusema: “Taifa moja litapigana na taifa lingine, na ufalme mmoja utapigana na ufalme mwingine. 11Kila mahali kutakuwa na mitetemeko mikubwa ya ardhi, njaa na tauni. Kutakuwa na vituko vya kutisha na ishara kubwa angani. 12Lakini kabla ya kutokea hayo yote, watawatieni nguvuni, watawatesa na kuwapelekeni katika masunagogi na kuwatia gerezani; mtapelekwa mbele ya wafalme na watawala kwa ajili ya jina langu, 13mpate kunishuhudia kwao. 14Muwe na msimamo huu mioyoni mwenu: Hakuna kufikiria kabla ya wakati juu ya jinsi mtakavyojitetea, 15kwa sababu mimi mwenyewe nitawapeni ufasaha wa maneno na hekima, hata maadui zenu hawataweza kustahimili wala kupinga. 16Wazazi wenu, ndugu, jamaa na rafiki zenu watawasaliti nyinyi; na baadhi yenu mtauawa. 17Watu wote watawachukieni nyinyi kwa sababu ya jina langu. 18Lakini, hata unywele mmoja wa vichwa vyenu hautapotea. 19Kwa uvumilivu wenu, mtayaokoa maisha yenu.
Yesu anatabiri kuharibiwa kwa mji wa Yerusalemu
(Mat 24:15-21; Marko 13:14-19)
20“Mtakapoona mji wa Yerusalemu umezungukwa na majeshi, basi jueni ya kwamba wakati umefika ambapo mji huo utaharibiwa. 21Hapo, walioko Yudea wakimbilie milimani; wale walio mjini watoke; na wale walio mashambani wasirudi mjini. 22Kwa maana siku hizo ni siku za adhabu, ili yote yaliyoandikwa yatimie. 23Ole wao waja wazito na wanyonyeshao siku hizo! Kwa maana kutakuwa na dhiki kubwa katika nchi, na hasira ya Mungu itawajia watu hawa. 24Wengine watauawa kwa upanga, wengine watachukuliwa mateka katika nchi zote; na mji wa Yerusalemu utakanyagwa na watu wa mataifa mengine, hadi nyakati zao zitakapotimia.
Kuja kwake Mwana wa Mtu
(Mat 24:29-31; Marko 13:24-27)
25“Kutakuwa na ishara katika jua na mwezi na nyota. Mataifa duniani yatakuwa na dhiki kwa sababu ya wasiwasi kutokana na mshindo wa mawimbi ya bahari. 26Watu watazirai kwa sababu ya woga, wakitazamia mambo yatakayoupata ulimwengu; kwa maana nguvu za mbingu zitatikiswa. 27Halafu, watamwona Mwana wa Mtu akija katika wingu, mwenye nguvu na utukufu mwingi. 28Wakati mambo hayo yatakapoanza kutukia, simameni na kuinua vichwa vyenu juu, kwa maana ukombozi wenu umekaribia.”
Mfano wa mtini
(Mat 24:32-35; Marko 13:28-31)
29Kisha akawaambia mfano: “Angalieni mtini na miti mingine yote. 30Mnapoona kwamba imeanza kuchipua majani, mwatambua kwamba majira ya mavuno yamekaribia. 31Vivyo hivyo, mtakapoona mambo hayo yanatendeka, mtatambua kwamba ufalme wa Mungu umekaribia. 32Kweli nawaambieni, kizazi hiki cha sasa hakitapita kabla ya hayo yote kutendeka. 33Mbingu na dunia zitapita, lakini maneno yangu hayatapita kamwe.
Lazima kuwa macho
34“Muwe macho, mioyo yenu isije ikalemewa na anasa, ulevi na shughuli za maisha haya. La sivyo, siku ile itawajieni ghafla. 35Kwa maana itawajia kama mtego wote wanaoishi duniani pote. 36Muwe waangalifu basi, na salini daima ili muweze kupata nguvu ya kupita salama katika mambo haya yote yatakayotokea, na kusimama mbele ya Mwana wa Mtu.”
37Wakati wa mchana, siku hizo, Yesu alikuwa akifundisha watu hekaluni; lakini usiku alikuwa akienda katika mlima wa Mizeituni na kukaa huko. 38Watu wote walikuwa wanakwenda hekaluni asubuhi na mapema, wapate kumsikiliza.

Luka21;1-38

Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)

"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe

No comments: