Swahili na Waswahili

Swahili na Waswahili
Waswahili na Mswahili Rachel Siwa...Pamoja Daima!!

Thursday 26 November 2020

Kikombe Cha Asubuhi; Yohane 7...


Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?

Tumshukuru Mungu wetu katika yote...

Asante  Mungu wetu kwa wema na fadhili zako kwetu
Asante kwa ulinzi wako kwetu wakati wote
Asante kwa kutuchagua tena na kutupa
kibali cha kuendelea kuiona leo hii
Asante kwa pumzi/uzima,
afya na kuwatayari kwa majukumu yetu


Utukuzwe ee Mungu wetu,usifiwe Baba wa Mbinguni

Neema yako yatutosha  Mungu wetu..



Inuka, ee Mwenyezi-Mungu, uwakabili na kuwaporomosha. Kwa upanga uiokoe nafsi yangu kutoka kwa waovu.

Zaburi 17:13

Baba wa Mbinguni tunakuja mbele zako tukijinyenyekeza,
tukijishusha na kujiachilia mikononi mwako

Mungu wetu tunaomba utusamehe dhambi zetu zote
Baba wa Mbinguni nasi tunaomba utupe neema ya kuweza kuwasamehe wale wote waliotukosea,Usitutie majaribuni Mungu wetu tunaomba utuepushe na yule mwovu na kazi zake zote,Jehovah ututakase miili yetu na akili zetu Baba wa Mbinguni tunaomba utufunike kwa  Damu ya Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo wa Nazareti,
Yeye aliteseka kwanza ili sisi tupate kupona....



Kwa mkono wako, ee Mwenyezi-Mungu, uniokoe mikononi mwa watu hao, watu ambao riziki yao ni dunia hii tu. Uwajaze adhabu uliyowawekea, wapate ya kuwatosha na watoto wao, wawaachie hata na wajukuu zao.

Zaburi 17:14

Mungu wetu tunaomba ukabariki kazi za mikono yetu 
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe ubunifu na maarifa 

katika utendaji
Jehovah nasi tukatende sawasawa na mapenzi yako
Baba wa Mbinguni tunaomba ukabariki ridhiki zetu
ziingiazo/zitokazo
Mungu wetu nasi tunaomba ukatupe neema ya kuweza
kuwabariki wenye kuhitaji
Yahweh tusipungukiwe katika mahitaji yetu
Mungu wetu ukatupe kama inavyokupendeza wewe



Jehovah tunayaweka maisha yetu mikononi mwako
Baba wa Mbinguni tunaomba ukabariki nyumba/ndoa zetu,
watoto,wazazi wetu,familia/ndugu na wote wanaotuzunguka
Jehovah tunaomba ulinzi wako kwetu na kwa vyote tunavyo vimiliki
Yahweh tunaomba ukatubariki tuingiapo/tutokapo
Mungu wetu tunaomba ukavibariki vyote tunavyoenda kugusa/kutumia
Baba wa Mbinguni ukavitakase kwa Damu ya Bwana wetu Yesu Kristo
Mungu wetu ukatamalaki na kutuatamia
Baba wa Mbinguni tukawe salama rohoni
Mfalme wa amani amani yako ikatawale katika maisha yetu
Mungu wetu ukatupe macho ya kuona na masikio ya kusikia 
sauti yako na kuitii
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe neema ya kufuata njia zako
Yahweh tukasimamie Neno lako amri na sheria zako siku zote 
za maisha yetu

Mungu  wetu ukaonekane katika maisha yetu popote tupitapo na ikajulikane kwamba upo 

Neema zako zikawe nasi Nuru yako ikaangaze katika maisha yetu
Ukatufanye barua njema ee Mungu wetu nasi tukasomeke kama
inavyokupendeza wewe
Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi...


Lakini mimi nitauona uso wako, kwani ni mwadilifu; niamkapo nitajaa furaha kwa kukuona.

Zaburi 17:15

Tazama wenye shida/tabu,Mungu wetu tunaomba
 ukawaguse kila mmoja na mahitaji yake
Baba wa Mbinguni tunaomba ukawasamehe pale walipokwenda
kinyume nawe
Mungu wetu ukawape neema ya kujiombea,macho ya rohoni,masikio yakusikia sauti yako,wakafuate njia zako nazo zikawaweke huru
Mungu wetu tunaomba ukasikie kulia kwao
Baba wa Mbinguni tunomba ukawafute machozi yao
Nuru yako ikaangaze katika maisha yao
Mungu wetu tunaomba ukawatendee sawasawa na mapenzi yako
Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele
Amina....!!!


Wapendwa katika Kristo Yesu asanteni sana
kwakuwanami/kunisoma

Mungu Baba aendelee kuwabariki na kuwatendea
kama inavyompendeza yeye
Amani ya Bwana wetu Yesu Kristo na upendo wa Mungu Baba
ukae nanyi daima....

Nawapenda.



 Yesu na ndugu zake

1Baada ya hayo, Yesu alikuwa akitembea huko Galilaya. Hakutaka kutembea mkoani Yudea kwa sababu viongozi wa Wayahudi walikuwa wanataka kumuua. 2Sikukuu ya Wayahudi ya vibanda ilikuwa imekaribia. 3Basi, ndugu zake wakamwambia, “Ondoka hapa uende Yudea ili wanafunzi wako wazione kazi unazozifanya. 4Mtu hafanyi mambo kwa siri kama anataka kujulikana kwa watu. Maadamu unafanya mambo haya, basi, jidhihirishe kwa ulimwengu.” 5(Hata ndugu zake hawakumwamini). 6Basi, Yesu akawaambia, “Wakati wangu ufaao haujafika bado. Lakini kwenu nyinyi kila wakati unafaa. 7Ulimwengu hauwezi kuwachukia nyinyi, lakini mimi wanichukia kwa sababu mimi nashuhudia juu yake kwamba matendo yake ni maovu. 8Nyinyi nendeni kwenye sikukuu hiyo. Mimi siendi kwenye sikukuu hiyo, maana saa yangu ifaayo haijafika.” 9Alisema hayo kisha akabaki huko Galilaya.
Yesu kwenye sikukuu ya vibanda
10Baada ya ndugu zake kwenda kwenye sikukuu, Yesu naye alikwenda, lakini hakuenda kwa hadhara bali kwa siri. 11Viongozi wa Wayahudi walikuwa wanamtafuta kwenye sikukuu hiyo; wakauliza, “Yuko wapi?”
12Kulikuwa na minongono mingi katika umati wa watu. Baadhi yao walisema, “Ni mtu mwema.” Wengine walisema, “La! Anawapotosha watu.” 13Hata hivyo hakuna mtu aliyethubutu kusema habari zake hadharani kwa kuwaogopa viongozi wa Wayahudi.
14Sikukuu hiyo ilipofikia katikati, Yesu naye alikwenda hekaluni, akaanza kufundisha. 15Basi, Wayahudi wakashangaa na kusema, “Mtu huyu amepataje elimu naye hakusoma shuleni?” 16Hapo Yesu akawajibu, “Mafundisho ninayofundisha si yangu, bali ni yake yeye aliyenituma. 17Mtu anayependa kufanya yale anayotaka Mungu, atajua kama mafundisho yangu yametoka kwa Mungu, au mimi najisemea tu mwenyewe. 18Yeye anayejisemea tu mwenyewe anatafuta sifa yake mwenyewe; lakini anayetafuta sifa ya yule aliyemtuma, huyo ni mwaminifu, na ndani yake hamna uovu wowote. 19Je, Mose hakuwapeni sheria? Hata hivyo, hakuna hata mmoja wenu anayeishika sheria. Kwa nini mnataka kuniua?” 20Hapo watu wakamjibu, “Una pepo wewe! Nani anataka kukuua?”
21Yesu akawajibu, “Kuna jambo moja nililofanya, nanyi mnalistaajabia. 22Mose aliwapeni ile desturi ya kutahiri. (Si kwamba desturi hiyo ilitoka kwa Mose, bali ilitoka kwa mababu). Sasa nyinyi humtahiri mtu hata siku ya Sabato. 23Ikiwa basi, mtu hutahiriwa hata siku ya Sabato kusudi sheria isivunjwe, mbona mnanikasirikia kwa sababu nimemfanya mtu kuwa mzima kabisa siku ya Sabato? 24Msihukumu mambo kwa nje tu; toeni hukumu ya haki.”
Je, huyu ni Kristo?
25Baadhi ya watu wa Yerusalemu walisema, “Je, yule mtu wanayemtafuta wamuue si huyu? 26Tazameni sasa! Anawaonya hadharani, wala hakuna mtu anayemwambia hata neno. Je, yawezekana kuwa viongozi wametambua kweli kwamba huyu ndiye Kristo? 27Kristo atakapokuja hakuna mtu atakayejua mahali alikotoka, lakini sisi tunajua alikotoka mtu huyu!”
28Basi, Yesu alipokuwa anafundisha hekaluni alipaza sauti na kusema, “Ati mnanijua; hata nilikotoka mnakujua! Hata hivyo, sikuja kwa mamlaka yangu mwenyewe; ila yeye aliyenituma mimi ni wa kweli, nanyi hamumjui. 29Lakini mimi namjua kwa sababu nimetoka kwake, naye ndiye aliyenituma.”
30Basi, watu wakataka kumtia nguvuni, lakini hakuna mtu aliyethubutu kumkamata kwa sababu saa yake ilikuwa haijafika bado. 31Wengi katika ule umati wa watu walimwamini, wakasema, “Je, Kristo akija atafanya ishara kubwa zaidi kuliko alizozifanya huyu?”
Walinzi wanatumwa kumkamata Yesu
32Mafarisayo waliwasikia watu wakinongona maneno hayo juu ya Yesu. Basi, wao pamoja na makuhani wakuu wakawatuma walinzi wamtie nguvuni. 33Yesu akasema, “Bado niko nanyi kwa muda mfupi, kisha nitamwendea yule aliyenituma. 34Mtanitafuta lakini hamtaniona, na pale nitakapokuwa nyinyi hamwezi kufika.” 35Viongozi wa Wayahudi wakasema wao kwa wao, “Mtu huyu atakwenda wapi ambapo hatutaweza kumpata? Atakwenda kwa Wayahudi waliotawanyika kati ya Wagiriki, na kuwafundisha Wagiriki? 36Ana maana gani anaposema: ‘Mtanitafuta lakini hamtanipata, na pale nitakapokuwa nyinyi hamwezi kufika?’”
Mito ya maji ya uhai
37Siku ya mwisho ya sikukuu hiyo ilikuwa siku maalumu. Yesu alisimama, akasema kwa sauti kubwa, “Aliye na kiu na aje kwangu anywe. 38Kama yasemavyo Maandiko Matakatifu: ‘Anayeniamini mimi, mito ya maji ya uhai itatiririka kutoka moyoni mwake!’” 39(Alisema hayo kumhusu Roho ambaye wale waliomwamini yeye watampokea. Wakati huo Roho alikuwa hajafika kwa sababu Yesu alikuwa hajatukuzwa bado).
Mafarakano kati ya watu juu ya Yesu
40Baadhi ya watu katika ule umati walisikia maneno hayo, wakasema, “Kweli mtu huyu ndiye yule nabii!” 41Wengine wakasema, “Huyu ndiye Kristo!” Lakini wengine walisema, “Je, yawezekana Kristo akatoka Galilaya? 42Maandiko Matakatifu yasemaje? Yanasema: ‘Kristo atatoka katika ukoo wa Daudi, na atazaliwa Bethlehemu, mji wa Daudi!’” 43Basi, kukatokea mafarakano juu yake katika ule umati wa watu. 44Baadhi ya watu walitaka kumtia nguvuni lakini hakuna aliyejaribu kumkamata.
Viongozi wa Wayahudi hawana imani
45Kisha wale walinzi wakarudi kwa makuhani wakuu na Mafarisayo; nao wakawauliza, “Kwa nini hamkumleta?” 46Walinzi wakawajibu, “Hakuna mtu aliyepata kamwe kusema kama asemavyo mtu huyu!” 47Mafarisayo wakawauliza, “Je, nanyi pia mmedanganyika? 48Je, mmekwisha kumwona hata mmoja wa viongozi wa watu, au mmoja wa Mafarisayo aliyemwamini? 49Lakini umati huu haujui sheria ya Mose; umelaaniwa!”
50Mmoja wao alikuwa Nikodemo ambaye hapo awali alikuwa amemwendea Yesu. Basi, yeye akawaambia, 51“Je, sheria yetu humhukumu mtu kabla ya kumsikia kwanza na kujua anafanya nini?” 52Nao wakamjibu, “Je, wewe pia umetoka Galilaya? Haya, kayachunguze Maandiko Matakatifu nawe utaona kwamba Galilaya hakutoki kamwe nabii!”
Mwanamke mzinzi
53Basi, wote wakaondoka, kila mtu akaenda nyumbani;

Yohane7;1-53
Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)
"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe

No comments: