Swahili na Waswahili

Swahili na Waswahili
Waswahili na Mswahili Rachel Siwa...Pamoja Daima!!

Tuesday 3 November 2020

Kikombe Cha Asubuhi; Luka 14...

 



Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?

Tumshukuru Mungu katika yote....

Mungu wetu Baba yetu,Muumba wetu Muumba wa Mbingu na Nchi
Muumba wa vyote vilivyomo vinavyoonekana na visivyoonekana
Mungu wa walio hai,Mungu  mwenye huruma,Mungu wa upendo
Mungu wa Abrahamu,Isaka na Yakobo...
Asante kwa wema na fadhili zako kwetu
Asante kwa ulinzi wako kwetu wakati wote
Asante kwa kutuchagua tena na kutupa
kibali cha kuendelea kuiona leo hii
Asante kwa pumzi/uzima,afya na kuwatayari kwa majukumu yetu

Neema yako yatutosha ee Mungu wetu....!!



Mimi Yakobo, mtumishi wa Mungu na wa Bwana Yesu Kristo, nawaandikia nyinyi, makabila kumi na mawili, yaliyotawanyika ulimwenguni! Salamu!

Yakobo 1:1

Baba wa Mbinguni tunakuja mbele zako,
Tukijinyenyekeza,tukijiachilia mikononi mwako
Mungu wetu tunamomba utusamehe dhambi zetu
Baba wa Mbinguni nasi tunaomba ukatupe neema
 ya kuweza kuwasamehe wale wote waliotukosea

Usitutie majaribuni Mungu wetu tunaomba utuepushe
na yule mwovu na kazi zake zote
Jehovah ututakase miili yetu na akili zetu
Baba wa Mbinguni tunaomba utufunike kwa Damu
ya Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo wa Nazareti
yeye aliteseka kwanza ili sisi tupate kupona....


Ndugu zangu, muwe na furaha mnapopatwa na majaribu mbalimbali, kwani mwajua kwamba imani yenu ikisha stahimili, itawapatieni uvumilivu.

Yakobo 1:2-3

Mungu wetu tunaomba ukabariki kazi za mikono yetu
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe ubunifu na maarifa katika utendaji
Jehovah nasi tukatende sawasawa na mapenzi yako
Yahweh tunaomba ukabariki ridhiki zetu ziingiazo/zitokazo
Mungu wetu nasi tunaomna ukatupe neema ya kuweza kuwabariki wenye kuhitaji
Tusipungukiwe katika mahitaji yetu
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe kama inavyokupendeza wewe...


Yahweh tunayaweka maisha yetu mikononi mwako
Mungu wetu tunaomba ukabariki nyumba/ndoa zetu,
Jehovah tunaomba ulinzi wako kwetu na kwa vyote tunavyovimiliki
Yahweh tunaomba ukatubariki tuingiapo/tutokapo
Mungu wetu tunaomba ukavibariki vyote tunavyoenda kugusa/kutumia
Baba wa Mbinguni ukavitakase kwa Damu ya Bwana wetu Yesu Kristo
Mungu wetu ukatamalaki na kutuatamia
Baba wa Mbinguni tukawe salama rohoni
Yahwe ukatupe akili ya kutambua mema na mabaya
Mfalme wa amani amani yako ikatawale katika maisha yetu
Mungu wetu ukatupe macho ya kuona,masikio ya kusikia sauti yako na kuitii..
Baba wa Mbinguni  tunaomba ukatupe neema ya kufuata
njia zako,tukasimamie Neno lako,amri na sheria zako
siku zote za maisha yetu...
Ukatuguse kwa mkono wako wenye nguvu,ukatufanye chombo chema
ee Mungu wetu nasi tukatumike kama inavyokupendeza wewe
Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi....


Muwe na hakika kwamba uvumilivu wenu utawategemeza mpaka mwisho, mpate kuwa wakamilifu na watimilifu, bila kupungukiwa chochote.

Yakobo 1:4

Tazama watoto wako wenye shida/tabu,wote wanaopitia magumu/majaribu mbalimbali
Mungu wetu tunaomba ukawaguse kwa mkono wako wenye nguvu
kila mmoja na mahitaji yake
Mungu wetu tunaomba ukawasamehe pale walipo kwenda kinyume nawe
Yahweh tunaomba ukawape neema ya kuweza kujiombea,kufuata njia zako nazo zikawaweke huru...
Baba wa Mbinguni tunayaweka haya yote mikononi mwako
Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele...
Amina...!!


Asanteni sana wapendwa katika Kristo Yesu kwakuwa nami,Baba wa Mbinguni aendelee kuwatendea sawasawa na mapenzi yake...

Nawapenda.




Yesu anamponya mtu mmoja

1Siku moja ya Sabato, Yesu alikwenda kula chakula nyumbani kwa mmoja wa viongozi wa Mafarisayo, na watu waliokuwapo hapo wakawa wanamchunguza. 2Mbele yake Yesu palikuwa na mtu mmoja aliyekuwa na ugonjwa wa kuvimba mwili. 3Yesu akawauliza waalimu wa sheria na Mafarisayo, “Je, ni halali au la kumponya mtu siku ya Sabato?” 4Lakini wao wakakaa kimya. Yesu akamshika huyo mgonjwa, akamponya, akamwacha aende zake. 5Halafu akawaambia, “Ni nani kati yenu ambaye mtoto wake au ng'ombe wake akitumbukia shimoni, hangemtoa hata kama ni siku ya Sabato?” 6Nao hawakuweza kumjibu swali hilo.
Ukarimu na unyenyekevu
7Yesu aliona jinsi wale walioalikwa walivyokuwa wanajichagulia nafasi za heshima, akawaambia mfano: 8“Kama mtu akikualika harusini, usiketi mahali pa heshima, isije ikawa amealikwa mwingine mheshimiwa kuliko wewe; 9na mwenyeji wenu nyinyi wawili atakuja na kukuambia: ‘Mwachie huyu nafasi.’ Hapo utaaibika mbele ya wote na kulazimika kwenda kuchukua nafasi ya mwisho. 10Bali ukialikwa kwenye karamu, keti mahali pa mwisho, ili mwenyeji wako atakapokuja akuambie: ‘Rafiki, njoo hapa mbele, mahali pazuri zaidi.’ Hapo utakuwa umeheshimika mbele ya wote wanaoketi pamoja nawe. 11Kwa maana yeyote anayejikweza atashushwa na anayejishusha, atakwezwa.”
12Halafu akamwambia na yule aliyemwalika, “Kama ukiwaandalia watu karamu mchana au jioni, usiwaalike rafiki zako au jamaa zako au jirani zako walio matajiri wasije nao wakakualika, nawe ukawa umelipwa kile ulichowatendea. 13Badala yake, unapofanya karamu, waalike maskini, vilema, viwete na vipofu, 14nawe utakuwa umepata baraka, kwa kuwa hao hawana cha kukulipa. Maana Mungu atakupa tuzo lako wakati watu wema watakapofufuka.”
Mfano kwa karamu kubwa
(Mat 22:1-10)
15Mmoja wa wale waliokuwa wameketi pamoja na Yesu akasema, “Ana heri mtu yule atakayekula chakula katika ufalme wa Mungu.”
16Yesu akamjibu, “Mtu mmoja alifanya karamu kubwa, akawaalika watu wengi. 17Wakati wa karamu ulipofika alimtuma mtumishi wake akawaambie walioalikwa, ‘Njoni, kila kitu ni tayari.’ 18Lakini wote, mmoja baada ya mwingine, wakaanza kuomba radhi. Wa kwanza akamwambia mtumishi: ‘Nimenunua shamba, na hivyo sina budi niende kuliangalia; nakuomba uniwie radhi.’ 19Mwingine akasema: ‘Nimenunua ng'ombe jozi tano wa kulima, sasa nimo njiani kwenda kuwajaribu; nakuomba uniwie radhi.’ 20Na mwingine akasema: ‘Nimeoa kwa hiyo siwezi kuja.’ 21Mtumishi huyo akarudi na kumwarifu bwana wake jambo hilo. Yule mwenye nyumba alikasirika, akamwambia mtumishi wake: ‘Nenda upesi kwenye barabara na vichochoro vya mji, uwalete hapa ndani maskini, viwete, vipofu na vilema wengine.’ 22Baadaye, mtumishi huyo akasema: ‘Bwana, mambo yamefanyika kama ulivyoamuru, lakini bado iko nafasi.’ 23Yule bwana akamwambia mtumishi: ‘Nenda katika barabara na vichochoro vya mji uwashurutishe watu kuingia ili nyumba yangu ijae. 24Kwa maana, nawaambieni, hakuna hata mmoja wa wale walioalikwa atakayeonja karamu yangu.’”
Gharama ya kuwa mfuasi
(Mat 10:37-38)
25Hapo, makundi mengi yakawa yanaandamana pamoja na Yesu. Basi, akawageukia watu akawaambia, 26“Mtu yeyote akija kwangu, asipomchukia baba yake, mama yake, mke wake, watoto, ndugu na dada zake, naam, hata na nafsi yake mwenyewe, hawezi kuwa mwanafunzi wangu. 27Mtu asiyechukua msalaba wake na kunifuata hawezi kuwa mwanafunzi wangu. 28Kwa maana, ni nani miongoni mwenu ambaye akitaka kujenga mnara hataketi kwanza akadirie gharama zake ili ajue kama ana kiasi cha kutosha cha kumalizia? 29La sivyo, baada ya kuweka msingi na kushindwa kumaliza, watu watamcheka 30wakisema: ‘Mtu huyu alianza kujenga, lakini hakumalizia.’
31“Au, ni mfalme gani ambaye akitaka kwenda kupigana na mfalme mwingine, hataketi kwanza na kufikiri kama ataweza, kwa askari wake10,000, kumkabili yule aliye na askari 20,000? 32Kama anaona hataweza, atawatuma wajumbe kutaka masharti ya amani wakati mfalme huyo mwingine angali mbali. 33Vivyo hivyo, basi, hakuna hata mmoja wenu atakayekuwa mwanafunzi wangu kama asipoachilia kila kitu alicho nacho.
Chumvi isiyo na ladha
(Mat 5:13; Marko 9:50)
34“Chumvi ni nzuri; lakini ikipoteza ladha yake, itakolezwa na nini? 35Haifai kitu wala kwa udongo wala kwa mbolea. Watu huitupilia mbali. Mwenye masikio na asikie!”

Luka14;1-35
Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)

"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe

No comments: