Swahili na Waswahili

Swahili na Waswahili
Waswahili na Mswahili Rachel Siwa...Pamoja Daima!!

Wednesday 11 November 2020

Kikombe Cha Asubuhi; Luka 20...


Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?

Tumshukuru Mungu wetu katika yote...

Asante  Mungu wetu kwa wema na fadhili zako kwetu
Asante kwa ulinzi wako kwetu wakati wote
Asante kwa kutuchagua tena na kutupa
kibali cha kuendelea kuiona leo hii
Asante kwa pumzi/uzima,
afya na kuwatayari kwa majukumu yetu


Utukuzwe ee Mungu wetu,usifiwe Baba wa Mbinguni

Neema yako yatutosha  Mungu wetu..



“Msiwahukumu wengine, msije nanyi mkahukumiwa na Mungu; kwa maana jinsi mnavyowahukumu wengine, ndivyo nanyi mtakavyohukumiwa; na kipimo kilekile mnachotumia kwa wengine ndicho Mungu atakachotumia kwenu.

Mathayo 7:1-2

Baba wa Mbinguni tunakuja mbele zako tukijinyenyekeza,
tukijishusha na kujiachilia mikononi mwako

Mungu wetu tunaomba utusamehe dhambi zetu zote
Baba wa Mbinguni nasi tunaomba utupe neema ya kuweza kuwasamehe wale wote waliotukosea,Usitutie majaribuni Mungu wetu tunaomba utuepushe na yule mwovu na kazi zake zote,Jehovah ututakase miili yetu na akili zetu Baba wa Mbinguni tunaomba utufunike kwa  Damu ya Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo wa Nazareti,
Yeye aliteseka kwanza ili sisi tupate kupona....



Kwa nini wakiona kibanzi kilicho jichoni mwa ndugu yako, na papo hapo huioni boriti iliyoko jichoni mwako? Au, wawezaje kumwambia ndugu yako, ‘Ndugu, ngoja nikuondoe kibanzi jichoni mwako,’ wakati wewe mwenyewe unayo boriti jichoni mwako?

Mathayo 7:3-4

Mungu wetu tunaomba ukabariki kazi za mikono yetu 
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe ubunifu na maarifa 

katika utendaji
Jehovah nasi tukatende sawasawa na mapenzi yako
Baba wa Mbinguni tunaomba ukabariki ridhiki zetu
ziingiazo/zitokazo
Mungu wetu nasi tunaomba ukatupe neema ya kuweza
kuwabariki wenye kuhitaji
Yahweh tusipungukiwe katika mahitaji yetu
Mungu wetu ukatupe kama inavyokupendeza wewe



Jehovah tunayaweka maisha yetu mikononi mwako
Baba wa Mbinguni tunaomba ukabariki nyumba/ndoa zetu,
watoto,wazazi wetu,familia/ndugu na wote wanaotuzunguka
Jehovah tunaomba ulinzi wako kwetu na kwa vyote tunavyo vimiliki
Yahweh tunaomba ukatubariki tuingiapo/tutokapo
Mungu wetu tunaomba ukavibariki vyote tunavyoenda kugusa/kutumia
Baba wa Mbinguni ukavitakase kwa Damu ya Bwana wetu Yesu Kristo
Mungu wetu ukatamalaki na kutuatamia
Baba wa Mbinguni tukawe salama rohoni
Mfalme wa amani amani yako ikatawale katika maisha yetu
Mungu wetu ukatupe macho ya kuona na masikio ya kusikia 
sauti yako na kuitii
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe neema ya kufuata njia zako
Yahweh tukasimamie Neno lako amri na sheria zako siku zote 
za maisha yetu

Mungu  wetu ukaonekane katika maisha yetu popote tupitapo na ikajulikane kwamba upo 

Neema zako zikawe nasi Nuru yako ikaangaze katika maisha yetu
Ukatufanye barua njema ee Mungu wetu nasi tukasomeke kama
inavyokupendeza wewe
Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi...



Mnafiki wewe! Ondoa kwanza boriti iliyomo jichoni mwako na hapo ndipo utaona sawasawa kiasi cha kuweza kuondoa kibanzi kilichomo jichoni mwa ndugu yako. “Msiwape mbwa vitu vitakatifu wasije wakageuka na kuwararua nyinyi; wala msiwatupie nguruwe lulu zenu wasije wakazikanyaga.

Mathayo 7:5-6

Tazama wenye shida/tabu,Mungu wetu tunaomba
 ukawaguse kila mmoja na mahitaji yake
Baba wa Mbinguni tunaomba ukawasamehe pale walipokwenda
kinyume nawe
Mungu wetu ukawape neema ya kujiombea,macho ya rohoni,masikio yakusikia sauti yako,wakafuate njia zako nazo zikawaweke huru
Mungu wetu tunaomba ukasikie kulia kwao
Baba wa Mbinguni tunomba ukawafute machozi yao
Nuru yako ikaangaze katika maisha yao
Mungu wetu tunaomba ukawatendee sawasawa na mapenzi yako
Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele
Amina....!!!

Wapendwa katika Kristo Yesu asanteni sana
kwakuwanami/kunisoma

Mungu Baba aendelee kuwabariki na kuwatendea
kama inavyompendeza yeye
Amani ya Bwana wetu Yesu Kristo na upendo wa Mungu Baba
ukae nanyi daima....

Nawapenda.




 Suala juu ya mamlaka ya Yesu

(Mat 21:23-27; Marko 11:27-33)
1Siku moja, Yesu alipokuwa akiwafundisha watu hekaluni na kuwahubiria juu ya Habari Njema, makuhani wakuu na waalimu wa sheria pamoja na wazee walifika, 2wakasema, “Tuambie! Unafanya mambo haya kwa mamlaka gani?” 3Yesu akawaambia, “Na mimi nitawaulizeni swali: 4Mamlaka ya Yohane ya kubatiza yalitoka kwa Mungu au kwa watu?” 5Lakini wao wakajadiliana hivi: “Tukisema yalitoka kwa Mungu, yeye atatuuliza: ‘Mbona hamkumsadiki?’ 6Na tukisema yalitoka kwa binadamu, watu wote hapa watatupiga mawe, maana wote wanaamini kwamba Yohane alikuwa nabii.” 7Basi, wakamwambia, “Hatujui mamlaka hayo yalitoka wapi.” 8Yesu akawaambia, “Hata mimi sitawaambia ninafanya mambo haya kwa mamlaka gani.”
Mfano wa shamba la mizabibu na wakulima
(Mat 21:33-46; Marko 12:1-12)
9Yesu akaendelea kuwaambia watu mfano huu: “Mtu mmoja alilima shamba la mizabibu, akalikodisha kwa wakulima; kisha akasafiri hadi nchi ya mbali, akakaa huko kwa muda mrefu. 10Wakati wa mavuno, mtu huyo alimtuma mtumishi wake kwa wale wakulima, akachukue sehemu ya matunda ya shamba la mizabibu. Lakini wale wakulima wakampiga mtumishi huyo, wakamrudisha mikono mitupu. 11Yule bwana akamtuma tena mtumishi mwingine; lakini wao wakampiga huyo vilevile na kumtendea vibaya, wakamrudisha mikono mitupu. 12Akamtuma tena wa tatu; huyu naye, baada ya kumwumiza, wakamfukuza. 13Yule mwenye shamba akafikiri: ‘Nitafanya nini? Nitamtuma mwanangu mpenzi; labda watamjali yeye.’ 14Wale wakulima walipomwona tu, wakasemezana: ‘Huyu ndiye mrithi. Basi, tumuue ili urithi wake uwe wetu.’ 15Basi, wakamtoa nje ya lile shamba la mizabibu, wakamuua.” Yesu akauliza, “Yule mwenye shamba atawafanya nini hao wakulima? 16Atakuja kuwaangamiza wakulima hao, na kuwapa wakulima wengine hilo shamba la mizabibu.” Watu waliposikia maneno hayo, walisema: “Hasha! Yasitukie hata kidogo!”
17Lakini Yesu akawatazama, akawaambia, “Maandiko haya Matakatifu yana maana gani, basi?
‘Jiwe walilokataa waashi,
sasa limekuwa jiwe kuu la msingi!’
18Mtu yeyote akianguka juu ya jiwe hilo atavunjika vipandevipande; na likimwangukia mtu yeyote, litamponda.”
Kulipa kodi kwa Kaisari
(Mat 22:15-22; Marko 12:13-17)
19Waalimu wa sheria na makuhani wakuu walifahamu kwamba mfano huo ulikuwa unawahusu, na hivyo walitaka kumkamata palepale, ila tu waliogopa watu. 20Basi, wakawa wanatafuta wakati wa kufaa. Wakawahonga watu fulani wajisingizie kuwa wema, wakawatuma wamnase Yesu kwa maswali, na hivyo waweze kumtia nguvuni na kumpeleka kwa wakuu wa serikali. 21Hao wapelelezi wakamwambia, “Mwalimu, tunajua kwamba unasema na kufundisha mambo ya kweli; tunajua kwamba wewe huna ubaguzi; wewe wafundisha ukweli juu ya njia ya Mungu. 22Basi, tuambie kama ni halali au la, kulipa kodi kwa Kaisari!”
23Yesu alitambua mtego wao, akawaambia, 24“Nionesheni sarafu. Je, sura na chapa ni vya nani?” 25Nao wakamjibu, “Ni ya Kaisari.” Yesu akawaambia, “Basi, ya Kaisari mpeni Kaisari, na ya Mungu mpeni Mungu.” 26Hawakufaulu kumnasa kwa neno lolote pale mbele ya watu na hivyo wakakaa kimya wakilistaajabia jibu lake.
Suala juu ya ufufuo
(Mat 22:23-33; Marko 12:18-27)
27Kisha Masadukayo, ambao husema kwamba wafu hawafufuki, wakamjia Yesu, wakasema: 28“Mwalimu, Mose alituandikia kwamba kama ndugu ya mtu fulani akifa na kumwacha mjane wake bila watoto, ni lazima ndugu yake amchukue huyo mama mjane, ili ampatie ndugu yake watoto. 29Sasa, wakati mmoja kulikuwa na ndugu saba. Yule wa kwanza alioa na baadaye akafa bila kuacha mtoto. 30Yule ndugu wa pili akamwoa yule mjane, naye pia akafa; 31na ndugu wa tatu vilevile. Mambo yakawa yaleyale kwa wote saba – wote walikufa bila kuacha watoto. 32Mwishowe akafa pia yule mwanamke. 33Je, siku wafu watakapofufuliwa, mama huyo atakuwa mke wa nani? Maana wote saba walikuwa wamemwoa.”
34Yesu akawaambia, “Watu wa nyakati hizi huoa na kuolewa; 35lakini wale ambao Mungu atawawezesha kushiriki ule wakati wa ufufuo, hawataoa wala kuolewa. 36Ama hakika, hawawezi kufa tena, kwa sababu watakuwa kama malaika, na ni watoto wa Mungu kwa vile wamefufuliwa katika wafu. 37Lakini, kwamba kuna kufufuka kutoka kwa wafu, hata Mose alithibitisha jambo hilo katika Maandiko Matakatifu. Katika sehemu ya Maandiko Matakatifu juu ya kile kichaka kilichokuwa kinawaka moto, anamtaja Bwana kama Mungu wa Abrahamu, Mungu wa Isaka na Mungu wa Yakobo. 38Basi, yeye si Mungu wa wafu, bali ni Mungu wa wale walio hai; maana kwake wote wanaishi.”
39Baadhi ya wale waalimu wa sheria wakasema, “Mwalimu, umejibu vema kabisa.” 40Walisema hivyo kwa sababu hawakuthubutu kumwuliza tena maswali mengine.
Suala juu ya Kristo
(Mat 22:41-46; Marko 12:35-37)
41Yesu akawauliza, “Yasemekanaje kwamba Kristo ni mwana wa Daudi? 42Daudi mwenyewe anasema katika Zaburi:
‘Bwana alimwambia Bwana wangu:
Keti upande wangu wa kulia
43mpaka niwaweke maadui zako kuwa kiti cha kuwekea miguu yako.’
44Ikiwa Daudi anamwita yeye, ‘Bwana,’ basi, atakuwaje mwanawe?”
Yesu anawaonya watu kuhusu waalimu wa sheria
(Mat 23:1-36; Marko 12:38-40)
45Yesu aliwaambia wanafunzi wake mbele ya watu wote, 46“Jihadharini na waalimu wa sheria ambao hupenda kupitapita wamevalia kanzu. Hupenda kusalimiwa na watu kwa heshima masokoni, huketi mahali pa heshima katika masunagogi na kuchukua nafasi za heshima katika karamu. 47Huwadhulumu wajane huku wakisingizia kuwa wema kwa kusali sala ndefu. Hao watapata hukumu kali zaidi!”

Luka20;1-47

Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)

"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe

No comments: