Swahili na Waswahili

Swahili na Waswahili
Waswahili na Mswahili Rachel Siwa...Pamoja Daima!!

Thursday 2 May 2019

Kikombe Cha Asubuhi ;Zaburi 116...



Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?

Tumshukuru Mungu katika yote....

Mungu wetu Baba yetu,Muumba wetu Muumba wa Mbingu na Nchi
Muumba wa vyote vilivyomo vinavyoonekana na visivyoonekana
Mungu wa walio hai,Mungu  mwenye huruma,Mungu wa upendo
Mungu wa Abrahamu,Isaka na Yakobo...
Asante kwa wema na fadhili zako kwetu
Asante kwa ulinzi wako kwetu wakati wote
Asante kwa kutuchagua tena na kutupa
kibali cha kuendelea kuiona leo hii
Asante kwa pumzi/uzima,afya na kuwatayari kwa majukumu yetu

Neema yako yatutosha ee Mungu wetu....!!

Nani awezaye kupima maji ya bahari kwa konzi yake, kuzipima mbingu kwa mikono yake? Nani awezaye kuutia udongo wa dunia kikombeni; kuipima milima kwa mizani au vilima kwa kipimo cha uzani?
Baba wa Mbinguni tunakuja mbele zako tukijinyenyekeza,tukijishusha na kujiachilia mikononi mwako
Mungu wetu tunaomba utusamehe dhambi zetu zote tulizo zifanya
Kwakuwaza,kwakunena,kwakutenda,kwakujua/kutojua
Baba wa Mbinguni nasi tunaomba ukatupe neema
ya kuweza kuwasamehe wale wote waliotukosea
Usitutie majaribuni Mungu wetu tunaomba utuepushe
na yule mwovu na kazi zake zote
Jehovah ututakase miili yetu na akili zetu
Baba wa Mbinguni tunaomba utufunike kwa Damu
ya Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo wa Nazareti
yeye aliteseka kwanza ili sisi tupate kupona....

Nani awezaye kuiongoza akili ya Mwenyezi-Mungu, au kuwa mshauri wake na kumfunza? Mwenyezi-Mungu alimtaka nani shauri, ndipo akapata kuwa mwenye ujuzi? Nani aliyemfunza njia za haki? Nani aliyemfundisha maarifa, na kumwonesha namna ya kuwa na akili?
Mungu wetu tunaomba ukabariki kazi za mikono yetu
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe ubunifu na maarifa katika utendaji
Jehovah nasi tukatende sawasawa na mapenzi yako
Yahweh tunaomba ukabariki ridhiki zetu ziingiazo/zitokazo
Mungu wetu nasi ukatupe neema ya kuweza kuwabariki wenye kuhitaji
Tusipungukiwe katika mahitaji yetu Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe kama inavyokupendeza wewe....
Yahweh  tunayaweka maisha yetu mikononi mwako
Mungu wetu tunaomba ukabariki nyumba/ndoa zetu,
watoto,wazazi wetu,familia/ndugu na wote wanaotuzunguka
Jehovah tunaomba ulinzi wako kwetu na kwa vyote tunavyo vimiliki
Yahweh tunaomba ukatubariki tuingiapo/tutokapo
Mungu wetu tunaomba ukavibariki vyote tunavyoenda kugusa/kutumia
Baba wa Mbinguni ukavitakase kwa Damu ya Bwana wetu Yesu Kristo
Mungu wetu ukatamalaki na kutuatamia
Baba wa Mbinguni tukawe salama rohoni

Yahweh ukatupe akili ya kutambua mema na mabaya
Mfalme wa amani amani yako ikatawale katika maisha yetu
Mungu wetu ukatupe macho ya kuona na masikio ya kusikia 
sauti yako na kuitii
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe neema ya kufuata njia zako
Yahweh tukasimamie Neno lako amri na sheria zako siku zote 
za maisha yetu
Neema zako zikawe nasi Nuru yako ikaangaze katika maisha yetu
ukatuguse kwa mkono wako wenye nguvu
Ukatufanye chombo chema ee Mungu wetu nasi tukatumike kama
inavyokupendeza wewe

Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi...

Kwake mataifa ni kama tone la maji katika ndoo, ni kama vumbi juu ya mizani. Kwake visiwa ni vyepesi kama vumbi laini. Kuni zote za Lebanoni na wanyama wake wote havitoshi kwa sadaka ya kuteketezwa mbele yake.
Mungu wetu tunawaweka mikononi mwako wenye shida/tabu,
wote wanaopitia magumu/majaribu mbalimbali
Jehovah ukawaguse kwa mkono wako wenye nguvu kila mmoja na mahitaji yake...
Mungu wetu tunaomba ukawasamehe pale walipokwenda kinyume nawe
Yahweh tunaomba ukawape neema ya kujiombea,kufuata njia zako nazo zikawaweke huru...
Nuru yako ikaangaze katika maisha yao....
Baba wa Mbinguni tunayaweka haya yote mikononi mwako,
Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele....
Amina..!

Asanteni sana wapendwa katika Kristo Yesu kwakuwa nami,
Mungu Baba aendelee kuwatendea sawasawa na mapezni yake...

Nawapenda.

Shukrani kwa kuokolewa kifoni
1Nampenda Mwenyezi-Mungu,
kwa maana anisikia,
maana amesikia kilio cha ombi langu.
2Yeye amenitegea sikio,
hivyo nitamwomba muda wote niishio.
3Hatari ya kifo ilinizunguka,
vitisho vya kaburi vilinivamia;
nilijawa na mahangaiko na majonzi.
4Kisha nikamlilia Mwenyezi-Mungu:
“Ee Mwenyezi-Mungu, tafadhali unisalimishe!”
5Mwenyezi-Mungu amejaa wema na uaminifu;
Mungu wetu ni mwenye huruma.
6Mwenyezi-Mungu huwalinda wanyofu;
nilipokuwa nimekandamizwa aliniokoa.
7Uwe na utulivu mkuu, ee nafsi yangu,
maana Mwenyezi-Mungu amenitendea mema.
8Ameniokoa kifoni na kufuta machozi yangu;
akanilinda nisije nikaanguka.
9Nitatembea mbele yake Mwenyezi-Mungu,
katika nchi ya watu walio hai.
10 Taz 2Kor 4:13 Nilikuwa na imani hata niliposema:
“Mimi nimetaabika mno.”
11Hata nilisema kwa hofu yangu:
“Binadamu wote hawaaminiki!”
12Nimrudishie nini Mwenyezi-Mungu,
kwa ukarimu wote alionitendea?
13Nitamtolea tambiko ya divai kwa kunikomboa,
nitaomba kwa jina lake Mwenyezi-Mungu.
14Nitamtimizia Mwenyezi-Mungu nadhiri zangu,
mbele ya watu wake wote.
15Kifo cha waaminifu wake Mwenyezi-Mungu
si jambo dogo mbele yake.
16Ee Mwenyezi-Mungu, mimi ni mtumishi wako;
ni mtumishi wako, mtoto wa mjakazi wako;
umenifungulia vifungo vyangu.
17Nitakutolea tambiko za shukrani,
na kukupa heshima zangu.
18Nitakutimizia ahadi zangu, ee Mwenyezi-Mungu
mbele ya watu wako wote,
19waliokusanyika hekaluni mwako,
katikati ya Yerusalemu.
Msifuni Mwenyezi-Mungu!


Zaburi116;1-19

Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)

"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.

No comments: