Swahili na Waswahili

Swahili na Waswahili
Waswahili na Mswahili Rachel Siwa...Pamoja Daima!!

Tuesday 11 September 2018

Kikombe Cha Asubuhi ; Tunamshukuru Mungu kwakumaliza kitabu cha Nehemia ,Leo tunaanza kitabu cha Esta 1


Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?

Haleluyah Mungu wetu yu mwema sana
Tunamshukuru Mungu kwa kutupa kibali cha 
kupitia/kujifunza/kusoma Neno lake katika kitabu
cha "Nehemia" ni matumaini yangu wote tuliopitia
kitabu hiki tumejifunza mengi....

Leo tunapoenda kuanza kitabu cha "Esta"
tunamuomba Mungu akatupe macho ya rohoni,akili
ya kuelewa,kutambua na kuyashika yote yaliyomo....


Tumshukuru Mungu katika yote....

Mungu wetu Baba yetu,Muumba wetu Muumba wa Mbingu na Nchi
Muumba wa vyote vilivyomo vinavyoonekana na visivyoonekana
Mungu wa walio hai,Mungu  mwenye huruma,Mungu wa upendo
Mungu wa Abrahamu,Isaka na Yakobo..
Yahweh..!Jehovah..! Adonai..!Elohim..!El Olam..!El Qanna..!
El Elyon..!El shaddai..!Emanueli...!-Mungu pamoja nasi...
Unastahili sifa Mungu wetu,Unastahili kuabudiwa Jehovah,
Unastahili kuhimidiwa Yahweh,Unastahili Kutukuzwa Baba wa Mbinguni....!



Asante kwa wema na fadhili zako kwetu
Asante kwa ulinzi wako kwetu wakati wote
Asante kwa kutuchagua tena na kutupa
kibali cha kuendelea kuiona leo hii
Asante kwa pumzi/uzima,afya na kuwatayari kwa majukumu yetu

Neema yako yatutosha ee Mungu wetu....!!




Baadaye mwezi wa saba ulipofika, na watu wa Israeli wakiwa wamekwisha kaa katika miji yao, wote walikusanyika pamoja mjini Yerusalemu. Yeshua, mwana wa Yosadaki, pamoja na makuhani wenzake, na Zerubabeli, mwana wa Shealtieli, pamoja na jamaa zake, waliijenga upya madhabahu ya Mungu wa Israeli, ili waweze kumtolea sadaka za kuteketezwa kama ilivyoandikwa katika sheria ya Mose, mtu wa Mungu. Waliijenga madhabahu hiyo mahali palepale ilipokuwa hapo zamani, kwa kuwa waliwaogopa watu waliokuwa wanaishi katika nchi hiyo. Kisha wakawa wanamtolea Mwenyezi-Mungu sadaka za kuteketezwa juu yake kila siku asubuhi na jioni. Waliiadhimisha sikukuu ya vibanda kama ilivyoandikwa katika sheria; kila siku walitoa sadaka za kuteketezwa zilizohitajika kwa ajili ya siku hiyo. Walitoa pia sadaka za kawaida ambazo ziliteketezwa nzima, sadaka zilizotolewa wakati wa sikukuu ya mwezi mpya na katika sikukuu nyingine zote alizoagiza Mwenyezi-Mungu. Pia, walitoa tambiko zote zilizotolewa kwa hiari. Ingawa msingi wa hekalu la Mwenyezi-Mungu ulikuwa bado kuwekwa, watu walianza kutoa sadaka za kuteketezwa tangu siku ya kwanza ya mwezi wa saba.


Baba wa Mbinguni tunakuja mbele zako tukijinyenyekeza,tukijishusha
na kujiachilia mikononi mwako
Mungu wetu tunaomba utusamehe dhambi zetu zote tulizo zifanya
Kwakuwaza,kwakunena,kwakutenda,kwakujua/kutojua
Baba wa Mbinguni nasi tunaomba ukatupe neema
ya kuweza kuwasamehe wale wote waliotukosea
Usitutie majaribu Mungu wetu tunaomba utuepushe
na yule mwovu na kazi zake zote
Jehovah ututakase miili yetu na akili zetu
Baba wa Mbinguni tunaomba utufunike kwa Damu
ya Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo wa Nazareti
yeye aliteseka kwanza ili sisi tupate kupona....




Watu walitoa fedha za kuwalipa maseremala na waashi, walitoa pia chakula, vinywaji na mafuta, ili vipelekwe katika miji ya Tiro na Sidoni kupata miti ya mierezi kutoka Lebanoni. Miti hiyo ililetwa kwa njia ya bahari hadi Yopa. Haya yote yalifanyika kwa msaada wa mfalme Koreshi wa Persia. Basi, watu walianza kazi mnamo mwezi wa pili wa mwaka wa pili baada ya kufikia nyumba ya Mungu mjini Yerusalemu. Zerubabeli, mwana wa Shealtieli, Yeshua mwana wa Yosadaki, ndugu zao wengine, makuhani, Walawi na watu wengine wote waliorudi Yerusalemu kutoka uhamishoni, walijiunga nao katika kazi hiyo. Walawi wote waliokuwa na umri wa miaka ishirini au zaidi, waliteuliwa ili kusimamia kazi ya kuijenga upya nyumba ya Mwenyezi-Mungu. Yeshua, wanawe na jamaa yake, pamoja na Kadmieli na wanawe, (wa ukoo wa Yuda) walishirikiana kusimamia ujenzi wa nyumba ya Mungu. Walisaidiwa na wazawa wa Henadadi na ndugu zao Walawi.


Mungu wetu tunaomba ukabariki kazi za mikono yetu
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe ubunifu na maarifa katika utendaji

Jehovah nasi tukatende sawasawa na mapenzi yako
Yahweh tunaomba ukabariki ridhiki zetu ziingiazo/zitokazo
Mungu wetu nasi tunaomba ukatupe neema ya kuweza
kuwabariki wenye kuhitaji
Tusipungukiwe katika mahitaji yetu Baba wa Mbinguni
tunaomba ukatupe kama inavyokupendeza wewe....



Yahweh  tunayaweka maisha yetu mikononi mwako
Mungu wetu tunaomba ukabariki nyumba/ndoa zetu,
watoto,wazazi wetu,familia/ndugu na wote wanaotuzunguka
Jehovah tunaomba ulinzi wako kwetu na kwa vyote tunavyo vimiliki
Yahweh tunaomba ukatubariki tuingiapo/tutokapo
Mungu wetu tunaomba ukavibariki vyote tunavyoenda kugusa/kutumia
Baba wa Mbinguni ukavitakase kwa Damu ya Bwana wetu Yesu Kristo
Mungu wetu ukatamalaki na kutuatamia
Baba wa Mbinguni tukawe salama rohoni

Yahweh ukatupe akili ya kutambua mema na mabaya
Mfalme wa amani amani yako ikatawale katika maisha yetu
Mungu wetu ukatupe macho ya kuona na masikio ya kusikia 
sauti yako na kuitii
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe neema ya kufuata njia zako
Yahweh tukasimamie Neno lako amri na sheria zako siku zote 
za maisha yetu
Mungu wetu ukaonekane katika maisha yetu
Baba wa Mbinguni tukanene yaliyo yako
Neema zako zikawe nasi Nuru yako ikaangaze katika maisha yetu
ukatuguse kwa mkono wako wenye nguvu
Ukatufanye chombo chema ee Mungu wetu nasi tukatumike kama
inavyokupendeza wewe
Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi...




Wajenzi walipoanza kuweka msingi wa hekalu la Mwenyezi-Mungu, makuhani wakiwa wamevalia mavazi yao rasmi, walisimama mahali pao na tarumbeta mikononi, nao Walawi wa ukoo wa Asafu wakisimama na matoazi yao; basi, walimtukuza Mwenyezi-Mungu kufuatana na maagizo ya mfalme Daudi wa Israeli. Waliimba kwa kupokezana, wakimsifu na kumtukuza Mwenyezi-Mungu: “Kwa kuwa yu mwema, fadhili zake kwa Israeli zadumu milele.” Watu wote walipaza sauti kwa nguvu zao zote, wakamsifu Mwenyezi-Mungu kwa sababu ya kuanza kujengwa msingi wa nyumba ya Mwenyezi-Mungu. Wengi wa makuhani, Walawi, na viongozi wa koo waliokuwa wazee na ambao walikuwa wameiona nyumba ya kwanza, walilia kwa sauti kubwa walipouona msingi wa nyumba hii mpya unawekwa, ingawa watu wengine wengi walipaza sauti kwa furaha. Watu hawakuweza kutofautisha kati ya sauti za furaha na za kilio kwa sababu zilikuwa nyingi na zilisikika mbali sana.


Tazama watoto wako wanaokutafuta/kukuomba kwa bidii na imani Mungu wetu tunawaweka mikononi mwako wenye shida/tabu,
wote wanaopitia magumu/majaribu mbalimbali
Mungu wetu tunaomba ukawaguse kwa mkono wako wenye nguvu
kila mmoja na mahitaji yake
Baba wa Mbinguni tunaomba ukaonekane katika maisha yao
Mungu wetu tunaomba ukawasamehe pale walipokwenda
kinyume nawe Yahweh tunaomba ukawape neema ya kujiombea
Kufuata njia zako nazo zikawaweke huru
Ukawape macho ya rohoni ee Mungu wetu na masikio ya kusikia
sauti yako,Ukawaokoe na kuwalinda,ukawaponye kimwili na kiroho
Nuru yako ikaangaze katika maisha yao,Amani ikatawale katika maisha yao,Upendo ukadumu kati yao
 

Baba wa Mbinguni tunayaweke haya yote mikono mwako
tukiamini Mungu wetu utawatendea sawasawa na mapenzi yako
Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele
Amina...!!



Asanteni sana wapendwa katika Kristo Yesu
kwakuwanami/kunisoma Mungu Baba aendelee
kuwabariki na kuwatendea kama inavyompendeza yeye
Amani ya Bwana wetu Yesu Kristo na Upendo wa Mungu Baba
ukae nanyi daima
Nawapenda. 
 




Malkia Vashti aasi amri ya mfalme Ahasuero

1Mfalme Ahasuero,1:1 Ahasuero: Au Kherkhesi. alipotawala ufalme wake ulikuwa mikoa 127, toka India hadi Kushi.1:1 Kushi: Taz Mwa 2:13. 2Kiti chake cha enzi kilikuwa katika mji mkuu Susa. 3Mnamo mwaka wa tatu wa utawala wake, mfalme Ahasuero aliwaandalia karamu viongozi na watumishi wake wa serikali, wakuu wa majeshi ya Persia na Media, watu maarufu na wakuu wa mikoa. 4Basi, kwa muda wa miezi sita, Ahasuero akaonesha utajiri wa ufalme wake mtukufu, na fahari ya utawala wake.
5Muda huo ulipomalizika, mfalme aliwaandalia karamu watu wote wa mji mkuu wa Susa, wakubwa kwa wadogo. Karamu hiyo iliyochukua muda wa siku saba,1:5 siku saba: Kigiriki (Septuaginta): Siku sita. ilifanyika uani, katika bustani ya ikulu. 6Mahali hapo palikuwa pamepambwa kwa mapazia ya pamba ya rangi nyeupe na vitambaa vya rangi ya buluu. Mapazia hayo yalikuwa yamefungiwa pete za fedha kwa kamba za kitani safi za zambarau, na kuninginizwa kwenye nguzo za marumaru. Makochi ya dhahabu na fedha yalikuwa yamewekwa kwenye sakafu iliyotengenezwa kwa vijiwe vya rangi, marumaru, lulumizi na mawe ya thamani. 7Watu walipewa vinywaji katika vikombe mbalimbali vya dhahabu, naye mfalme alikuwa mkarimu sana wa divai ya kifalme. 8Kila mtu alikunywa akashiba; mfalme alikuwa ametoa maagizo kwa watumishi wa ikulu wamhudumie kila mtu kadiri ya mahitaji yake.1:8 Kila mtu … yake: Au Watu walikunywa kulingana na sheria, hawakushurutishwa; mfalme alikuwa ametoa amri kwa watumishi wa ikulu wamtendee kila mgeni kadiri ya matakwa yake.
9Wakati huo huo, malkia Vashti naye aliwaandalia akina mama karamu ndani ya ikulu ya Ahasuero.
10Siku ya saba ya karamu hiyo, mfalme Ahasuero, akiwa amejaa furaha kutokana na divai aliyokuwa amekunywa, aliwaita matowashi saba waliomhudumia yeye binafsi: Mehumani, Biztha, Harbona, Bigtha, Abagtha, Zethari na Karkasi. 11Aliwaamuru hao wamlete kwake malkia Vashti, akiwa amevaa taji yake ya kimalkia. Malkia huyo alikuwa na sura ya kuvutia sana, hivyo mfalme alitaka kuwaonesha wageni wake na viongozi uzuri wake. 12Lakini matowashi hao walipomweleza malkia amri ya mfalme, Vashti alikataa kutii. Jambo hilo lilimwudhi sana mfalme, akawa anawaka hasira moyoni.
13Ilikuwa desturi ya mfalme kupata mawaidha kutoka kwa wenye hekima, hivyo aliwaita wanasheria na mahakimu ili wamshauri la kufanya. 14Washauri wake wa kawaida walikuwa Karshena, Shethari, Admatha, Tarshishi, Maresi, Marsena na Memukani – viongozi saba wa Persia na Media waliokuwa na vyeo vya juu kabisa katika utawala wake. 15Aliwauliza hivi: “Je, kulingana na sheria, afanyiwe nini malkia Vashti? Maana, nimewatuma matowashi wangu kwake, lakini yeye amekataa kuitii amri yangu, mimi mfalme Ahasuero!”
16Hapo Memukani akamwambia mfalme na viongozi wake, “Licha ya kumkosea mfalme, malkia Vashti amewakosea viongozi na kila mtu katika mikoa ya mfalme Ahasuero! 17Tendo hili la malkia Vashti litajulikana na wanawake wote, nao watawadharau waume zao, wakisema: ‘Mfalme Ahasuero aliamuru malkia Vashti aje kwake, lakini yeye akakataa.’ 18Leo hii, mabibi wa Persia na Media ambao wamesikia alivyofanya malkia Vashti, watakuwa wanawaeleza viongozi wako; hivyo dharau na chuki vitajaa kila mahali. 19Basi, ukipenda, ewe mfalme, toa amri rasmi Vashti asije tena mbele yako. Amri hiyo na iandikwe katika sheria za Persia na Media, ili isiweze kubadilishwa. Kisha, cheo chake cha umalkia, apewe mwanamke mwingine anayestahili zaidi yake. 20Amri hiyo itakapotangazwa katika eneo lote la utawala wako, kila mwanamke atamheshimu mume wake, awe tajiri au maskini.”
21Wazo hilo lilimpendeza sana mfalme na viongozi wake, akatekeleza kama alivyopendekeza Memukani. 22Basi, akapeleka barua kwa kila mkoa kwa lugha na maandishi yanayoeleweka mkoani: Kwamba kila mwanamume awe bwana wa nyumba yake, na kuitangaza habari hii kwa lugha yake.



Esta1;1-22

Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)

"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.

No comments: