Swahili na Waswahili

Swahili na Waswahili
Waswahili na Mswahili Rachel Siwa...Pamoja Daima!!

Thursday 13 September 2018

Kikombe Cha Asubuhi ; Esta 3.....


Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?

Haleluyah Mungu wetu yu mwema sana..
Tumshukuru Mungu wetu katika yote....

Mungu wetu Baba yetu,Muumba wetu Muumba wa Mbingu na Nchi
Baba wa Upendo,Baba wa faraja,Baba wa huruma,Baba wa Baraka
Mungu mwenye nguvu,Mungu mwenye kuponya
Mungu wa Abrahamu,Isaka na Yakobo,Muweza wa yote
Wewe ni mwanzo na wewe ni mwisho,Alfa na Omega...!!


Asante kwa wema na fadhili zako kwetu
Asante kwa ulinzi wako kwetu wakati wote
Asante kwa kutuchagua tena na kutupa
kibali cha kuendelea kuiona leo hii
Asante kwa pumzi/uzima,afya na kuwatayari kwa majukumu yetu

Sifa na Utukufu tunakurudishia wewe ee Mungu wetu....!!



Usihangaike kwa sababu ya waovu; usiwaonee wivu watendao mabaya. Maana hao watatoweka mara kama nyasi; watanyauka kama mimea mibichi. Mtumainie Mwenyezi-Mungu na kutenda mema, upate kuishi katika nchi na kuwa salama. Uitafute furaha yako kwa Mwenyezi-Mungu, naye atakujalia unayotamani moyoni. Mkabidhi Mwenyezi-Mungu maisha yako; mtumainie yeye naye atafanya kitu. Ataufanya wema wako ungae kama mwanga, na uadilifu wako kama jua la adhuhuri. Tulia mbele ya Mwenyezi-Mungu, mngojee kwa saburi; usihangaike juu ya wale wanaofanikiwa, watu wanaofaulu katika mipango yao mibaya.


Tazama Jana imepita ee Mungu wetu Leo ni siku mpya na kesho ni siku nyingineJehovah...
Yahweh tunakuja mbele zako tukijinyenyekeza,tukijishusha

na kujiachilia mikononi mwako
Mungu wetu tunaomba utusamehe dhambi zetu zote tulizo zifanya
Kwakuwaza,kwakunena,kwakutenda,kwakujua/kutojua
Baba wa Mbinguni nasi tunaomba ukatupe neema
ya kuweza kuwasamehe wale wote waliotukosea
Usitutie majaribu Mungu wetu tunaomba utuepushe
na yule mwovu na kazi zake zote
Jehovah ututakase miili yetu na akili zetu
Baba wa Mbinguni tunaomba utufunike kwa Damu
ya Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo wa Nazareti 

yeye aliteseka kwanza ili sisi tupate kupona....



Epuka hasira wala usiwe na ghadhabu; usihangaike maana hiyo huzidisha ubaya. Watu watendao mabaya wataangamizwa, bali wanaomtumaini Mwenyezi-Mungu wataimiliki nchi. Bado kitambo kidogo, naye mwovu atatoweka; utamtafuta pale alipokuwa, wala hutamwona. Lakini wapole wataimiliki nchi, hao watafurahia wingi wa fanaka. Mwovu hula njama dhidi ya mwadilifu, na kumsagia meno kwa chuki. Lakini Mwenyezi-Mungu humcheka mwovu, kwani ajua mwisho wake u karibu. Waovu huchomoa panga na kuvuta pinde zao, wapate kuwaua maskini na fukara; wawachinje watu waishio kwa unyofu. Lakini panga zao zitawapenya wao wenyewe, na pinde zao zitavunjwavunjwa.


Mungu wetu tunaomba ukabariki kazi za mikono yetu
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe ubunifu na maarifa katika utendaji

Jehovah nasi tukatende sawasawa na mapenzi yako
Yahweh tunaomba ukabariki ridhiki zetu ziingiazo/zitokazo
Mungu wetu nasi tunaomba ukatupe neema ya kuweza
kuwabariki wenye kuhitaji
Tusipungukiwe katika mahitaji yetu Baba wa Mbinguni
tunaomba ukatupe kama inavyokupendeza wewe....



Baba wa Mbinguni tunayaweka maisha yetu mikononi mwako
Mungu wetu tunaomba ukabariki nyumba/ndoa zetu,
watoto,wazazi wetu,familia/ndugu na wote wanaotuzunguka
Jehovah tunaomba ulinzi wako kwetu na kwa vyote tunavyo vimiliki
Yahweh tunaomba ukatubariki tuingiapo/tutokapo
Mungu wetu tunaomba ukavibariki vyote tunavyoenda kugusa/kutumia
Baba wa Mbinguni ukavitakase kwa Damu ya Bwana wetu Yesu Kristo
Mungu wetu ukatamalaki na kutuatamia
Baba wa Mbinguni tukawe salama rohoni
Mfalme wa amani amani yako ikatawale katika maisha yetu
Mungu wetu ukatupe macho ya kuona na masikio ya kusikia 
sauti yako na kuitii

 Mungu wetu ukatupe akili ya kutambua mema na mabaya
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe neema ya kufuata njia zako
Yahweh tukasimamie Neno lako amri na sheria zako siku zote 
za maisha yetu

Mungu wetu ukaonekane katika maisha yetu

Baba wa Mbinguni tukanene yaliyo yako
Neema zako zikawe nasi Nuru yako ikaangaze katika maisha yetu
ukatuguse kwa mkono wako wenye nguvu
Tukawe barua njema  ee Mungu wetu nasi tukasomeke kama
inavyokupendeza wewe
Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi...



Afadhali mali kidogo ya mtu mwadilifu kuliko utajiri wa watu waovu wengi. Maana nguvu za waovu zitavunjwa, lakini Mwenyezi-Mungu huwategemeza waadilifu. Mwenyezi-Mungu hutunza maisha ya watu waaminifu, na urithi wao utadumu milele. Hawataaibika zikifika nyakati mbaya; siku za njaa watakuwa na chakula tele. Lakini waovu wataangamia, maadui za Mwenyezi-Mungu watanyauka kama maua nyikani; naam, watatoweka kama moshi. Mtu mwovu hukopa bila kurudisha; lakini mwadilifu hutoa kwa ukarimu. Waliobarikiwa na Mwenyezi-Mungu wataimiliki nchi, lakini waliolaaniwa naye watafutiliwa mbali. Mwenyezi-Mungu huziongoza nyayo za mtu, humlinda yule ampendezaye. Ajapoanguka, haanguki akabaki chini, kwa sababu Mwenyezi-Mungu humtegemeza. Nilikuwa kijana na sasa ni mzee; kamwe sijaona mwadilifu ameachwa na Mungu, au watoto wake wakiombaomba chakula. Daima huwapa wengine kwa furaha na kukopesha, na watoto wake ni baraka.


Mungu Baba tunawaweka mikononi mwako wenye shida/tabuwote wanaopotia magumu/majaribu mbalimbali
watoto wako wanaokuomba kwa bidii na imani
Mungu wetu tunaomba ukawaguse kwa mkono wako wenye nguvu
 kila mmoja na mahitaji yake 
Yahweh tunaomba ukaonekane katika maisha yao
Jehovah tunaomba ukawaokoe,ukawavushe salama na  kuwalinda
Mungu wetu tunaomba ukawasamehe pale walipokwenda kinyume nawe
Baba wa Mbinguni ukawape neema ya kujiombea,kufuata njia zako
wakasimaie Neno lako nalo likaweke huru
Mungu wetu tunaomba ukasikie kuomba kwetu
Baba wa Mbinguni ukapokee sala/maombi yetu
Mungu wetu ukawatendee sawasawa na mapenzi yako
Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele
Amina...!!

Asanteni sana wapendwa katika Kristo Yesu kwakuwa nami
Mungu Baba aendelee kuwabariki na kuwatendea 
kama inavyompendeza yeye....
Nawapenda.


Hamani ala njama kuwaangamiza Wayahudi

1Baada ya mambo hayo, mfalme Ahasuero alimpandisha cheo Hamani, akawa waziri mkuu. Hamani alikuwa mwanawe Hamedatha, na wa uzao wa Agagi.3:1 Agagi: Huyu alikuwa mfalme wa Amaleki; watu wake walikuwa maadui wa watu wa Israeli. 2Mfalme aliamuru maofisa wote wa serikali yake wamtii Hamani kwa kumwinamia na kumsujudia. Lakini Mordekai, hakumwinamia wala kumsujudia. 3Maofisa kadhaa wa mfalme waliokuwa penye lango la mfalme, wakamwuliza Mordekai, “Mbona wewe waidharau amri ya mfalme?” 4Kila siku walimshauri aache tabia hiyo, lakini Mordekai hakukubaliana nao. Alikataa kufanya hivyo kwa madai kwamba yeye ni Myahudi na kwa hiyo hawezi kumsujudia Hamani. Basi, wakamwarifu Hamani ili waone kama ataivumilia tabia ya Mordekai. 5Hamani aliwaka hasira alipojua kwamba Mordekai hamwinamii wala hamsujudii. 6Tena alipogundua kuwa Mordekai alikuwa Myahudi, aliamua kwamba kumwadhibu peke yake haitoshi. Basi akala njama kuwaangamiza Wayahudi wote, watu wa ukoo wa Mordekai, katika utawala wa mfalme Ahasuero.
7Katika mwaka wa kumi na mbili wa utawala wa mfalme Ahasuero, mnamo mwezi wa kwanza uitwao Nisani, Hamani aliagiza kura (yaani Purimu) ifanywe kupata siku na mwezi ambapo angetekeleza njama zake. Basi, kura ikaangukia siku ya kumi na nne ya mwezi wa kumi na mbili uitwao Adari.
8Basi, Hamani akamwambia mfalme: “Wapo watu wa taifa fulani walioko kila mahali katika utawala wako, nao wako katika kila mkoa. Watu hao wana sheria zilizo tofauti kabisa na za watu wengine. Isitoshe, wao hawazitii sheria zako, kwa hiyo haikufaidi chochote kuwavumilia.
9“Ukipenda, ewe mfalme, amri na itolewe, watu hawa waangamizwe. Nami naahidi, kama utaamuru hivyo, nitatoa kiasi cha kilo 10,000 za fedha ziwekwe katika hazina ya mfalme.”
10Mfalme akaivua pete yake, ambayo ilitumiwa kupigia mhuri matangazo, akampa adui wa Wayahudi Hamani mwana wa Hamedatha wa uzao wa Agagi. 11Ndipo mfalme akamwambia Hamani, “Umepewa watu wote na hizo fedha, tumia upendavyo.”
12Basi, siku ya kumi na tatu ya mwezi wa kwanza, Hamani aliwaita makatibu wote wa mfalme, akawapa tangazo ambalo alitaka litafsiriwe kwa kila lugha na kila namna ya maandishi katika utawala huo, halafu nakala zisambazwe kwa watawala wote, wakuu wa mikoa yote, na viongozi wa makabila – kufuatana na lugha zinazotumika kwao. Tangazo hilo lilitolewa kwa jina la mfalme Ahasuero, na kupigwa mhuri kwa pete yake. 13Matarishi walizipeleka nyaraka hizo kwa kila mkoa katika utawala huo. Tangazo hilo lilisema kwamba kwa siku moja tu, yaani siku ya kumi na tatu ya mwezi wa kumi na mbili uitwao Adari, Wayahudi wote – vijana kwa wazee, wanawake kwa watoto, wote lazima wauawe, waangamizwe na kufutiliwa mbali, na mali zao zote zichukuliwe. 14Taarifa hiyo ilitakiwa iandikwe hadharani katika kila mkoa, ili kila mtu ajiandae kwa ajili ya siku hiyo.
15Kwa amri ya mfalme, tangazo hili lilitolewa katika mji mkuu wa Susa, nao matarishi wakalitangaza katika mikoa yote. Mfalme na Hamani walikaa chini kunywa wakati watu mjini Susa wanafadhaika.



Esta3;1-15

Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)

"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.

No comments: