Swahili na Waswahili

Swahili na Waswahili
Waswahili na Mswahili Rachel Siwa...Pamoja Daima!!

Monday 10 September 2018

Kikombe Cha Asubuhi ; Nehemia 13...


Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?

Haleluyah Mungu wetu yu mwema sana
Tumshukuru Mungu wetu kila wakati
Asante Mungu wetu kwa wema na fadhili zako kwetu
Asante kwa ulinzi wako kwetu wakati wote
Asante kwa kutuchagua tena na kutupa
kibali cha kuendelea kuiona leo hii
Asante kwa pumzi/uzima,afya na kuwatayari kwa majukumu yetu

Utukuzwe ee Mungu wetu,usifiwe Baba wa Mbinguni
Uabudiwe Jehovah,Uhimidiwe Yahweh,Matendo yako ni makuu mno,
Matendo yako ni ya ajabu,Matendo yako yanatisha
Hakuna kama wewe ee Mungu wetu..

Neema yako yatutosha Baba wa Mbinguni...!!

Lakini mtu anaweza kuuliza: “Wafu watafufuliwaje? Watakuwa na mwili wa namna gani?” Hayo ni maswali ya kijinga! Ukipanda mbegu, isipokufa kwanza haitaota. Unachopanda ni mbegu tu, labda ya ngano au nafaka nyingine, na si mmea mzima ambao hutokea baadaye. Mungu huipa hiyo mbegu mwili anaoutaka mwenyewe; kila mbegu hupata mwili wake wa pekee. Miili ya viumbe vyote si sawa. Miili ya binadamu ni ya namna moja, ya wanyama ni ya namna nyingine, ya ndege ni ya namna nyingine na miili ya samaki pia ni ya namna nyingine. Iko miili ya mbinguni na miili ya duniani; uzuri wa miili ya mbinguni ni mwingine, na uzuri wa miili ya duniani ni mwingine. Uko uzuri wa jua, wa mwezi na wa nyota; hata nyota nazo huhitilafiana kwa uzuri.

Baba wa Mbinguni tunakuja mbele zako tukijinyenyekeza,tukijishusha
na kujiachilia mikononi mwako
Mungu wetu tunaomba utusamehe dhambi zetu zote tulizo zifanya
Kwakuwaza,kwakunena,kwakutenda,kwakujua/kutojua
Baba wa Mbinguni nasi tunaomba ukatupe neema
ya kuweza kuwasamehe wale wote waliotukosea
Usitutie majaribu Mungu wetu tunaomba utuepushe
na yule mwovu na kazi zake zote
Jehovah ututakase miili yetu na akili zetu
Baba wa Mbinguni tunaomba utufunike kwa Damu
ya Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo wa Nazareti
yeye aliteseka kwanza ili sisi tupate kupona

Kwakupigwa kwake sisi tumepata kupona...



Ndivyo ilivyo kuhusu ufufuo wa wafu. Kama vile mbegu, mwili huzikwa ardhini ukiwa katika hali ya kuharibika, lakini hufufuliwa katika hali ya kutoharibika. Huzikwa katika hali duni, hufufuliwa katika hali tukufu; huzikwa katika hali dhaifu, hufufuliwa ukiwa wenye nguvu. Unapozikwa ni mwili wa kawaida, unapofufuliwa ni mwili wa kiroho. Kuna mwili wa kawaida na kutakuwa na mwili wa kiroho. Maana Maandiko yasema: “Mtu wa kwanza, Adamu, alikuwa kiumbe mwenye uhai;” lakini Adamu wa mwisho ni Roho awapaye watu uhai. Lakini unaotangulia kuwako si ule mwili wa kiroho, ila ule mwili wa kawaida, kisha ule mwili wa kiroho.

Mungu wetu tunaomba ukabariki kazi za mikono yetu
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe ubunifu na maarifa 
katika utendaji
Jehovah nasi tukatende sawasawa na mapenzi yako
Baba wa Mbinguni tunaomba ukabariki ridhiki zetu
ziingiazo/zitokazo
Mungu wetu nasi tunaomba ukatupe neema ya kuweza
kuwabariki wenye kuhitaji
Yahweh tusipungukiwe katika mahitaji yetu
Mungu wetu ukatupe kama inavyokupendeza wewe

Baba wa Mbinguni tunayaweka maisha yetu mikononi mwako
Mungu wetu tunaomba ukabariki nyumba/ndoa zetu,
watoto,wazazi wetu,familia/ndugu na wote wanaotuzunguka
Jehovah tunaomba ulinzi wako kwetu na kwa vyote tunavyo vimiliki
Yahweh tunaomba ukatubariki tuingiapo/tutokapo
Mungu wetu tunaomba ukavibariki vyote tunavyoenda kugusa/kutumia
Baba wa Mbinguni ukavitakase kwa Damu ya Bwana wetu Yesu Kristo
Mungu wetu ukatamalaki na kutuatamia
Baba wa Mbinguni tukawe salama rohoni
Mfalme wa amani amani yako ikatawale katika maisha yetu
Mungu wetu ukatupe macho ya kuona na masikio ya kusikia 
sauti yako na kuitii

 Mungu wetu ukatupe akili ya kutambua mema na mabaya
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe neema ya kufuata njia zako
Yahweh tukasimamie Neno lako amri na sheria zako siku zote 
za maisha yetu
Mungu wetu ukaonekane katika maisha yetu
Neema zako zikawe nasi Nuru yako ikaangaze katika maisha yetu
ukatuguse kwa mkono wako wenye nguvu
Ukatufanye barua  njema ee Mungu wetu nasi tukasomeke kama
inavyokupendeza wewe
Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi...



Adamu wa kwanza aliumbwa kwa udongo, alitoka ardhini; mtu wa pili alitoka mbinguni. Wote walio wa dunia wako kama huyo mtu aliyeumbwa kwa udongo; wale walio wa mbinguni wako kama yule aliyetoka mbinguni. Kama vile tulivyofanana na yule aliyeumbwa kwa udongo, vivyo hivyo tutafanana na huyo aliyetoka mbinguni. Basi, ndugu, nasema hivi: Kile kilichofanywa kwa mwili na damu hakiwezi kuushiriki ufalme wa Mungu; na chenye kuharibika hakiwezi kuwa na hali ya kutoharibika. Sikilizeni, nawaambieni siri: Sisi hatutakufa sote, ila sote tutageuzwa, wakati wa mbiu ya mwisho, kwa nukta moja, kufumba na kufumbua. Maana tarumbeta ya mwisho itakapolia, wafu watafufuliwa katika hali ya kutoweza kufa tena, na sisi tutageuzwa. Maana ni lazima kila kiharibikacho kijivalie hali ya kutoharibika, mwili uwezao kufa ujivalie hali ya kutokufa. Basi, mwili huu wenye kuharibika utakapojivalia hali ya kutoharibika, na kile chenye kufa kitakapojivalia hali ya kutokufa, hapo ndipo litakapotimia lile neno lililoandikwa: “Kifo kimeangamizwa; ushindi umekamilika!” “Kifo, ushindi wako uko wapi? Uwezo wako wa kuumiza uko wapi?” Kifo hupata sumu yake katika dhambi, nayo dhambi hupata nguvu yake katika sheria. Lakini tumshukuru Mungu anayetupatia ushindi kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo. Basi, ndugu zangu wapenzi, simameni imara na thabiti. Endeleeni daima kuwa na bidii katika kazi ya Bwana, mkijua kwamba kazi mnayofanya katika utumishi wa Bwana haitapotea bure.

Baba wa Mbinguni tunawaweka mikononi mwako wenye shida/tabu
wote wanaopotia magumu/majaribu mbalimbali
watoto wako wanaokuomba kwa bidii na imani
Mungu wetu tunaomba ukawaguse kwa mkono wako wenye nguvu
 kila mmoja na mahitaji yake 
Yahweh tunaomba ukaonekane katika maisha yao
Jehovah tunaomba ukawaokoe,ukawavushe salama na  kuwalinda
Mungu wetu tunaomba ukawasamehe pale walipokwenda kinyume nawe
Baba wa Mbinguni ukawape neema ya kujiombea,kufuata njia zako
wakasimaie Neno lako nalo likaweke huru
Mungu wetu tunaomba ukasikie kuomba kwetu
Baba wa Mbinguni ukapokee sala/maombi yetu
Mungu wetu ukawatendee  kama inavyokupendeza wewe
Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele
Amina...!!

Asanteni sana wapendwa katika Kristo Yesu kwakuwa nami
Mungu Baba aendelee kuwabariki na kuwatendea 
sawasawa na mapenzi yake....

Amani ya Bwana wetu Yesu Kristo na Upendo 
wa Mungu Baba ukae nanyi daima....
Nawapenda.





Kujitenga na watu wengine

1Katika siku hiyo ya sherehe, kitabu cha Mose kilisomwa na ilifahamika kuwa Waamoni na Wamoabu kamwe wasiingie katika mkutano wa watu wa Mungu. 2Maana watu wa Israeli, walipokuwa wanasafiri toka Misri, hawakuwapa chakula wala maji ya kunywa, badala yake walimkodisha Balaamu kuwalaani watu wa Israeli, lakini Mungu wetu aligeuza laana yao kuwa baraka. 3Watu wa Israeli waliposikia sheria hiyo waliwatenga watu wa mataifa mengine.

Matengenezo ya Nehemia

4Kabla ya siku ya sherehe, kuhani Eliashibu aliyekuwa ameteuliwa kuangalia vyumba vya nyumba ya Mungu wetu, na mwenye uhusiano mwema na Tobia, 5alimruhusu Tobia kutumia chumba kikubwa ambamo hapo awali walikuwa wameweka tambiko za nafaka, ubani, vyombo, zaka za nafaka, divai, mafuta; vitu hivyo vyote Waisraeli walivyoagizwa kuwapa Walawi, waimbaji, walinda malango, na matoleo kwa makuhani. 6Wakati mambo haya yalipokuwa yanatendeka mimi sikuwako Yerusalemu; kwani katika mwaka wa thelathini na mbili wa utawala wa mfalme Artashasta wa Babuloni, nilikuwa nimeomba likizo; nami nikaenda kutoa ripoti kwake. 7Niliporudi Yerusalemu ndipo nikagundua uovu wa Eliashibu wa kumpa Tobia chumba katika ua wa nyumba ya Mungu. 8Nilikasirika sana na nikavitupa nje vyombo vyote vya Tobia. 9Niliamuru watu, nao wakatakasa vyombo hivyo, ndipo nikarudisha humo vifaa vya nyumba ya Mungu, pamoja na tambiko za nafaka na ubani.
10Tena nikagundua kuwa Walawi hawakupewa haki zao; na matokeo yake ni kwamba Walawi na waimbaji waliokuwa wakifanya kazi hapo awali, sasa walikwisha rudia mashamba yao. 11Nikawakemea viongozi, nikasema, “Kwa nini nyumba ya Mungu imeachwa?” Niliwakusanya pamoja na kuwarudisha kazini. 12Kisha, watu wote wa Israeli, wakaanza tena kuleta zaka zao za nafaka, divai na mafuta kwenye ghala. 13Nikawateua watu wafuatao kuwa watunzaji wa ghala: Kuhani Shelemia, mwandishi Sadoki na Pedaia Mlawi. Hanani, mwana wa Zakuri, mwana wa Matania akawa msaidizi wao. Walikuwa waaminifu na kazi yao ilikuwa kuwagawia ndugu zao mahitaji yao.
14Ee, Mungu wangu, nikumbuke kwa ajili ya haya yote na usiyasahau matendo yangu mema niliyofanya kwa ajili ya nyumba yako na kwa ajili ya huduma yako.
15Wakati huohuo, nikawaona watu wa Yuda wakisindika na kukamua zabibu siku za Sabato. Tena wengine walikuwa wakiwabebesha punda wao nafaka, divai, zabibu, tini na vitu vingine wakivipeleka mjini Yerusalemu. Nikawaonya kuwa hawana ruhusa kuuza vitu siku hiyo. 16Watu wengine toka mji wa Tiro walileta samaki na bidhaa nyingine mjini Yerusalemu na kuwauzia watu wetu siku ya Sabato. 17Nikawakemea viongozi wa watu wa Yuda, nikisema, “Uovu gani huu mnaofanya, kuikufuru Sabato? 18Je, babu zetu hawakufanya uovu wa namna hii hii na kumfanya Mungu wetu kutuletea maafa pamoja na mji huu? Na bado mnaleta ghadhabu yake juu ya watu wa Israeli kwa kuikufuru Sabato.”
19Hivyo, niliamuru kuwa malango ya mji wa Yerusalemu yafungwe mara Sabato inapoanza jioni, wakati giza linapoanza kuingia, na yasifunguliwe mpaka Sabato imekwisha. Niliweka baadhi ya watumishi wangu kwenye malango na kuwaagiza kuwa kitu chochote kisiletwe mjini siku ya Sabato. 20Mara mbili au tatu hivi wafanyabiashara waliokuwa wakiuza bidhaa za aina mbalimbali iliwabidi kulala nje ya mji. 21Niliwaonya na kuwaambia: “Hakuna maana kulala nje ya mji. Mkijaribu tena nitatumia nguvu.” Hivyo tangu wakati huo hawakurudi tena siku ya Sabato. 22Niliagiza Walawi kujitakasa na kwenda kuyalinda malango ili kutunza Sabato iwe takatifu.
Ee, Mungu wangu, nikumbuke hata na kwa hili pia na unihurumie kutokana na fadhili zako kuu.
23Tena wakati huo niliona Wayahudi waliooa wanawake kutoka Ashdodi, Amoni na Moabu; 24na nusu ya watoto wao walizungumza Kiashdodi au lugha nyingine na hawakuweza kuzungumza lugha ya Yuda. 25Niliwakemea na kuwaapiza, hata nikawapiga baadhi yao na kuwavuta nywele zao. Niliwalazimisha kuapa kwa jina la Mungu, nikisema, “Binti zenu msiwaoze kwa vijana wao, wala binti zao wasiolewe na vijana wenu au na nyinyi wenyewe. 26Je, Solomoni hakutenda dhambi kwa sababu ya wanawake wa namna hiyo? Yeye alikuwa mfalme mkuu kuliko wafalme wa mataifa mengine. Mungu alimpenda na akamfanya kuwa mfalme juu ya watu wote wa Israeli, hata hivyo wanawake wa mataifa mengine, walimfanya hata yeye atende dhambi. 27Je, sasa tufuate mfano wenu na tutende dhambi hii kubwa ya kutomtii Mungu wetu kwa kuoa wanawake wa kigeni?”
28Mmoja kati ya wana wa Yoyada, mwana wa kuhani mkuu Eliashibu, alioa binti Sanbalati kutoka mji wa Beth-horoni; kwa sababu hiyo nilimfukuza kutoka mbele yangu. 29Ee Mungu, kumbuka jinsi watu walivyochafua ukuhani na agano la kikuhani na la Walawi.
30Niliwatakasa watu kutokana na chochote kilichokuwa cha kigeni. Nikatayarisha mwongozo kwa ajili ya makuhani na Walawi kuhusu kazi ya kila mmoja wao. 31Niliagiza matoleo ya kuni kufanyika katika wakati unaopaswa na malimbuko wakati wake. Ee Mungu wangu, nikumbuke kwa ajili ya haya yote na unijalie mema.



Nehemia13;1-31

Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)

"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.

No comments: