Swahili na Waswahili

Swahili na Waswahili
Waswahili na Mswahili Rachel Siwa...Pamoja Daima!!

Thursday 15 March 2018

Kikombe Cha Asubuhi ;1 Wafalme 9...



Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?

Haleluyah Mungu wetu yu mwema sana...
Tumshukuru Mungu wetu katika yote..

Asante Baba wa Mbinguni kwa wema na fadhili zako kwetu
Asante kwa ulinzi wako kwetu wakati wote
Asante kwa kutuchagua tena na kutupa kibali cha kuendelea
kuiona leo hii
Asante kwa pumzi/uzima,afya na kuwa tayari kwa majukumu yetu
Utukuzwe ee Mungu wetu,Matendo yako ni makuu mno,Matendo
yako ni ya ajabu,Matendo yako yanatisha..
Hakuna kama wewe ee Mungu wetu,hakuna lililogumu mbele yako....


Mwenyezi-Mungu aliniambia hivi: “Chukua ubao mkubwa, uandike juu yake maneno yanayosomeka kwa urahisi: ‘TEKA-HARAKA-POKONYA-UPESI.’” Basi, nikajipatia mashahidi wawili waaminifu ambao wangenishuhudia: Kuhani Uria na Zekaria, mwana wa Yeberekia. Nililala na mke wangu ambaye pia ni nabii, akapata mimba, akajifungua mtoto wa kiume. Mwenyezi-Mungu akaniambia, “Mpe mtoto huyo jina ‘Teka-haraka-pokonya-upesi.’ Maana kabla mtoto huyu hajafikia umri wa kuweza kutamka: ‘Baba’ au ‘Mama,’ utajiri wa Damasko na nyara walizoteka huko Samaria zitapelekwa kwa mfalme wa Ashuru.”


Mungu wetu si kiziwi anasikia,Mungu wetu si kipofu anaona,
Mungu wetu si bubu anajibu,Mungu wetu ni muweza wa yote..
Yeye ni mwanzo na yeye ni mwisho,Alfa na Omega...!!
Neema yako yatutosha ee Mungu wetu..!!

Mwenyezi-Mungu aliongea nami tena, akaniambia, “Kwa kuwa watu hawa wameyakataa maji ya Shiloa yatiririkayo polepole, wakafa moyo mbele ya mfalme Resini na mfalme Peka mwana wa Remalia, basi, mimi Bwana nitawaletea mafuriko makuu ya maji ya mto Eufrate yaani mfalme wa Ashuru na nguvu zake zote; yatafurika na kupita kingo zake. Utaingia nchini Yuda kwa nguvu na kufurika na kupanda mpaka shingoni; utaenea juu ya nchi yako yote, ee Emanueli!”

Tazama jana imepita Baba wa Mbinguni Leo ni siku mpya
na kesho ni siku nyingine Mungu wetu..
Yahweh tunakuja mbele zako tukijinyenyekeza,tukijishusha na
kujiachilia mikononi mwako Mungu wetu
Jehovah tunaomba utusamehe makosa yetu yote tuliyoyafanya
kwakuwaza,kwakunena,kwakutenda,kwakujua/kutojua
Baba wa Mbinguni nasi tunaomba utupe neema ya kuweza
kuwasamehe wale wote waliotukosea...
Yahweh tunaomba usitutie katika majaribu Mungu wetu utuokoe 
na yule mwovu na kazi zake zote
nguvu za giza,nguvu za mapepo,nguvu za mizimu na nguvu
za mpinga kristo zikashindwe katika jina lililokuu jina la
Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo ..
Mungu wetu tunaomba ututakase miili yetu na akili zetu
Baba wa Mbinguni utufunike kwa Damu ya Mwanao Mpendwa
Bwana wetu Yesu Kristo wa Nazareti yeye aliteseka kwanza
ili sisi tupate kupona,kwakupigwa kwakwe sisi tumepona...


Unganeni enyi watu wa mataifa nanyi mtafedheheshwa! Sikilizeni enyi nchi za mbali duniani! Jiwekeni tayari na kufedheheshwa; naam, kaeni tayari na kufedheheshwa. Shaurianeni pamoja lakini itakuwa bure; fanyeni mipango lakini haitafaulu, maana Mungu yu pamoja nasi. Mwenyezi-Mungu alinionya kwa nguvu nisifuate njia za watu hawa, akaniambia, “Usijumuike nao katika njama zao, wala usiogope yale wanayoyaogopa wala kuwa na hofu. Nitambue mimi peke yangu, Mwenyezi-Mungu wa majeshi, kuwa mtakatifu; utaniogopa na kunicha mimi peke yangu. Mimi nitakuwa kimbilio, nitakuwa pia kama jiwe la kujikwaa, mwamba wa kuziangusha falme za Israeli na Yuda; nitakuwa mtego wa kuwatega na kuwanasa wakazi wa Yerusalemu. Watu wengi watajikwaa, wataanguka na kupondeka; watanaswa katika mtego huo na kuchukuliwa mateka.” Nitalihifadhi agizo hilo na kulifunga fundisho hilo miongoni mwa wafuasi wangu. Nitamngojea Mwenyezi-Mungu ambaye amejificha mbali na wazawa wa Yakobo; nitamtumainia. Mimi pamoja na watoto alionipa Mwenyezi-Mungu ni ishara na alama katika Israeli kwa jina la Mwenyezi-Mungu wa majeshi akaaye mlimani Siyoni. Baadhi watawaambieni: “Nendeni mkatake shauri kwa mizimu na mizuka iliayo kama ndege; kwani ni kawaida watu kutaka shauri kwa miungu yao, na kutaka shauri kwa wafu kwa ajili ya walio hai.” Hakika anayesema hivyo hajapata kuona mwanga. Lakini nyinyi shikilieni lile agizo na fundisho la Mungu. Watu watatangatanga nchini wamefadhaika sana na wenye njaa. Na wakiwa na njaa, hasira zitawawaka na kumlaani mfalme wao kadhalika na Mungu wao. Watatazama juu mbinguni na kuiangalia dunia, lakini wataona tu taabu, giza na mauzauza ya shida. Hakuna atakayeliepa giza hilo kuu.

Jehovah tunaomba ukabariki kazi za mikono yetu
Mungu wetu tunaomba ukatupe ubunifu na maarifa katika
utendaji Yahweh nasi tukatende sawasawa na mapenzi yako
Baba wa Mbinguni tunaomba ukabariki ridhiki zetu ziingiazo/zitokazo
Mungu wetu nasi tunaomba utupe neema ya kuweza kuwabariki
wenye kuhitaji...
Jehovah tunaomba tusipungukiwe katika mahitaji yetu
Yahweh ukatupe kama inavyokupendeza wewe...


Mungu wetu tunayaweka maisha yetu mikononi mwako
Baba wa Mbinguni tunaomba ukabariki nyumba/ndoa zetu
watoto,wazazi wetu,familia/ndugu na wote wanaotuzunguka
Mungu wetu tunaomba ulinzi wako kwetu na kwa vyote tunavyo
vimiliki,Yahweh tunaomba ukatamalaki na kutuatamia
Mungu wetu tunaomba ukatubariki tuingiapo/tutokapo Yahweh
tunaomba ukabariki vyote tunavyoenda kugusa/kutumia
Mungu wetu tunaomba ukavitakase na kuvifunika kwa Damu
ya Bwana wetu Yesu Kristo..
Baba wa Mbinguni tunaomba tukawe salama rohoni Jehovah
tunaomba ukatupe macho ya kuona na masikio ya kusikia sauti
yako na kuitii...
Mungu wetu tunaomba utupe neema ya kufuata njia zako Jehovah
tukasimamie Neno lako amri na sheria zako siku zote za maisha yetu
Yahweh neema zako na Nuru yako ikaangaze katika maisha yetu
Mungu wetu ukaonekane popote tupitapo na ikajulikane kwamba
upo Baba wa Mbinguni...
Yahweh ukatufanye chombo chema Mungu wetu nasi tukatumike
kama inavyokupendeza wewe..
Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi....

Lakini nchi ile iliyokuwa imekumbwa na huzuni haitabaki daima katika giza hilo kuu. Hapo awali Mungu alizifedhehesha nchi za Zebuluni na Naftali, lakini siku za usoni ataifanikisha sehemu hii ya baharini na nchi iliyo ngambo ya Yordani na hata Galilaya wanamoishi watu wa mataifa. Watu waliotembea gizani wameona mwanga mkubwa. Watu walioishi katika nchi ya giza kuu, sasa mwanga umewaangazia. Wewe, ee Mungu, umelikuza taifa, umeiongeza furaha yake. Watu wanafurahi mbele yako, wana furaha kama wakati wa mavuno, kama wafurahivyo wanaogawana nyara. Maana nira nzito walizobeba, nira walizokuwa wamefungwa, na fimbo ya wanyapara wao, umezivunjavunja kama wakati wa Wamidiani. Viatu vyote vya washambulizi vitani na mavazi yote yenye madoa ya damu yatateketezwa kama kuni za kuwasha moto. Maana mtoto amezaliwa kwa ajili yetu, tumepewa mtoto wa kiume. Naye atapewa mamlaka ya kutawala. Ataitwa: “Mshauri wa Ajabu”. “Mungu Mwenye Nguvu”, “Baba wa Milele”, “Mfalme wa Amani”. Utawala wake utastawi daima, amani ya ufalme wake haitakoma. Atachukua wadhifa wa mfalme Daudi na kutawala juu ya ufalme wake; ataustawisha na kuuimarisha, kwa haki na uadilifu, tangu sasa na hata milele. Hayo atayafanya Mwenyezi-Mungu wa majeshi.

Yahweh tazama wenye shida/tabu,Mungu wetu tunaomba ukawaguse
 kwa mkono wako wenye nguvu ,Yahweh tunaomba ukawaponye 
wagonjwa na ukawape nguvu na uvumilivu wanaowaguza
Baba wa mbinguni tazama wenye njaa Mungu wetu tunaomba ukabariki
mashamba/vyanzo vyao Baba wa Mbinguni wakapate chakula cha
kutosha kuweka akiba na kuwabariki wengine
Mungu wetu tunawaweka mikononi mwako walio kataka tamaa,
waliokataliwa,wenye hofu na mashaka Mungu wetu ukawe tumaini lao
Baba wa Mbinguni tazama  waliokuwa katika vifungo vya yule mwovu
na walio magerezani pasipo na hatia Mungu wetu tunaomba ukawaweke
huru na haki ikatendeke Yahweh tunaomba ukawavushe salama wote
wanaopitia magumu/majaribu mbalimbali Baba wa Mbinguni tazama waliokwama kibiashara,wanaotafuta kazi,wanaohitaji kuendelea na masomo,Mungu wetu ukawape ubunifu na maarifa Yahweh ukawape
mbinu na uelewa Jehova ukawabariki na kuwainua Yahweh ukawape
macho ya rohoni Mungu wetu ukaonenakne katika mapito yao..
Baba wa Mbinguni ukawasamehe wale wote waliokwenda kinyume nawe
Mungu wetu ukawape neema ya kujiombea,kufuata njia zako nazo
ziwaweke huru,Nuru yako ikaangaze katika maisha yao Jehovah
tunaomba ukasikie na ukapokee sala/maombi yetu
Mungu wetu ukawatendee sawasawa na mapenzi yako
Kwakuwa Ufalme ni wako nguvu na Utukufu hata Milele...
Amina...!!

Asanteni sana wapendwa/waungwana kwakuwanami/kunisoma
Mungu andelee kuwabariki na kuwatendea kama inavyompendeza
yeye,Amani ya Bwana wetu Yesu Kristo na Upendo wa Mungu Baba
vikawe nanyi daima...
Nawapenda.



Mungu amtokea Solomoni mara ya pili

(2Nya 7:11-22)

1Mfalme Solomoni alipomaliza kujenga nyumba ya Mwenyezi-Mungu na ikulu na majengo mengine yote aliyokusudia kujenga, 2Mwenyezi-Mungu alimtokea tena kama alivyomtokea kule Gibeoni. 3Mwenyezi-Mungu alimwambia, “Nimesikia sala yako na ombi lako. Nimeitakasa nyumba hii ambayo umenijengea ili watu waliabudu jina langu hapa milele. Nitaichunga na kuipenda wakati wote. 4Nawe kama ukinitumikia kwa unyofu wa moyo na uadilifu kama baba yako Daudi alivyofanya, ukitii amri zangu na kutimiza yale yote niliyokuamuru, ukifuata masharti yangu na maagizo yangu; 5basi, mimi nitakiimarisha kiti chako cha kifalme juu ya Israeli milele, kama nilivyomwahidi Daudi baba yako, nikisema, Hutakosa mtu wa kukaa juu ya kiti cha enzi cha Israeli. 6Lakini wewe au watoto wako mkigeuka na kuacha kunifuata, msiposhika amri zangu na maongozi niliyowapani, mkienda kutumikia miungu mingine na kuiabudu, 7basi, nitawahamisha watu wangu, Israeli, kutoka nchi hii ambayo nimewapa; kadhalika na nyumba hii ambayo nimeiweka wakfu kwa ajili ya jina langu, nitaitupilia mbali nami, na kuifanya kitu cha kupuuzwa na kudharauliwa miongoni mwa mataifa yote. 8Na nyumba hii itabomoka na kuwa magofu; kila apitaye karibu atashtuka na kutikisa kichwa, na kuuliza, ‘Kwa nini Mwenyezi-Mungu amefanya hivyo kwa nchi hii na kwa nyumba hii?’ 9Watu wengine watajibu, ‘Ni kwa sababu walimwacha Mwenyezi-Mungu, Mungu wao, aliyewatoa babu zao katika nchi ya Misri, wakashikamana na miungu mingine, wakaiabudu na kuitumikia; kwa hiyo, Mwenyezi-Mungu amewaletea maafa haya yote.’”

Solomoni anampa Hiramu miji ishirini

(2Nya 8:1-2)

10Kisha miaka ishirini ilipokwisha pita, ambayo Solomoni alizijenga zile nyumba mbili: Nyumba ya Mwenyezi-Mungu na ikulu, 11mfalme Solomoni alimpa Hiramu mfalme wa Tiro, miji ishirini katika mkoa wa Galilaya (kwa sababu huyo Hiramu alikuwa amempelekea Solomoni mbao za mierezi na miberoshi, na dhahabu pia, kadiri alivyohitaji kwa ujenzi). 12Lakini Hiramu alipowasili kutoka Tiro na kuiona miji hiyo aliyokuwa amepewa na Solomoni hakupendezwa nayo. 13Basi, akamwuliza Solomoni, “Ndugu yangu, ni miji gani hii ambayo umenipa?” Ndio sababu miji hiyo inaitwa nchi ya Kabuli hata leo. 14Hiramu alikuwa amempelekea mfalme Solomoni dhahabu kilo 3,600.

Shughuli nyingine za Solomoni

(2Nya 8:3-18)

15Yafuatayo ni maelezo juu ya jinsi mfalme Solomoni alivyotumia kazi za kulazimishwa kujenga nyumba ya Mwenyezi-Mungu, ikulu yake, ngome ya Milo na ukuta wa Yerusalemu, na pia katika kujenga upya miji ya Hazori, Megido na Gezeri; 16(Gezeri ndio mji ambao Farao, mfalme wa Misri, alikuwa ameuteka, akauchoma moto na kuwaua Wakanaani, wakazi wake. Baadaye, binti Farao alipoolewa na Solomoni, mfalme wa Misri alimpa binti yake mji huo wa Gezeri uwe zawadi ya harusi. 17Basi, Solomoni aliujenga upya mji wa Gezeri); hali kadhalika alijenga Beth-horoni ya chini; 18kadhalika miji ifuatayo: Baalathi, na Tamari, mji ulio nyikani katika nchi ya Yuda9:18 Yuda: Kiebrania hakina Yuda. 19na miji yake yote ya ghala, magari yake ya kukokotwa, na wapandafarasi wake; pia chochote alichotaka kujenga katika Yerusalemu, Lebanoni au kwingineko katika ufalme wake. 20Watu wengine wote waliobaki miongoni mwa Waamori, Wahiti, Waperizi, Wahivi na Wayebusi, yaani wote hao ambao hawakuwa wa taifa la Israeli, 21pamoja na wazawa wao ambao Waisraeli hawakuweza kuwaangamiza kabisa, Solomoni aliwafanyiza kazi za kulazimishwa hata leo. 22Lakini kati ya Waisraeli, Solomoni hakumfanya mtu yeyote kuwa mtumwa; wao ndio waliokuwa askari, watumishi wake, makamanda wake, maofisa wake, makamanda wa magari yake ya kukokotwa, na wapandafarasi wake. 23Ifuatayo ndiyo jumla ya maofisa wakuu waliohusika na uangalizi wa kazi ya Solomoni: Watu 550, hao ndio waliosimamia watu waliofanya kazi.
24Baadaye binti Farao aliuhama mji wa Daudi, akaenda kukaa katika nyumba yake mwenyewe ambayo Solomoni alimjengea; kisha Solomoni akajenga ngome ya Milo.
25Mara tatu kila mwaka, Solomoni alitoa tambiko za kuteketezwa na tambiko za amani juu ya madhabahu aliyokuwa amemjengea Mwenyezi-Mungu, akamfukizia Mwenyezi-Mungu ubani; pia alifanya marekebisho ya nyumba.
26Mfalme Solomoni aliunda merikebu nyingi huko Esion-geberi, karibu na Elothi iliyo pwani ya Bahari ya Shamu, katika nchi ya Edomu. 27Naye mfalme Hiramu akawatuma maofisa wake na mabaharia pamoja na watumishi wa Solomoni. 28Walisafiri kwenda nchi ya Ofiri, na kuchukua toka huko dhahabu, wakamletea mfalme Solomoni kadiri ya kilo 14,000.




1Wafalme9;1-28


Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)

"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.

No comments: