Swahili na Waswahili

Swahili na Waswahili
Waswahili na Mswahili Rachel Siwa...Pamoja Daima!!

Tuesday 6 March 2018

Kikombe Cha Asubuhi ;1 Wafalme 2....



Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?

Haleluyah Mungu wetu yu mwema sana 
Tumshukuru Mungu wetu katika yote...

Mungu wetu Baba yetu,Muumba wetu Muumba wa Mbingu na Nchi
Muumba wa vyote vilivyomo vinavyoonekana na visivyoonekana
Mungu mwenye nguvu,Mungu wa wote walio hai..
Mungu wa Abrahamu,Isaka na Yakobo,Mungu  unayeponya..
Jehovah Jireh..Jehovah Nissi..!Jehovah Raah..!Jehovah Rapha..!
Jehovah Shammah..!Jehovah Shalom..!Emanueli-Mungu pamoja nasi..!

Asante kwa wema na fadhili zako kwetu..
Asante kwa ulinzi wako wakati wote kwetu..
Asante kwakutuchagua tena na kutupa kibali cha kuendelea
kuiona leo hii...
Asante kwa pumzi/uzima,afya na kuwa tayari kwa majumu yetu
Utukuzwe ee Baba wa Mbinguni,Unastahili sifa Yahweh
Unastahili kuabudiwa Jehovah,Unastahili kuhimidiwa Mungu wetu
Matendo yako ni makuu sana,Matendo yako ni ya ajabu...
Neema yako yatutosha ee Baba wa Mbinguni...!!


Habari Njema ya Yesu Kristo, Mwana wa Mungu. Ilianza kama ilivyoandikwa katika kitabu cha nabii Isaya: “Mungu alisema, ‘Namtuma mjumbe wangu akutangulie, ambaye atakutayarishia njia yako.’ Sauti ya mtu anaita jangwani: ‘Mtayarishieni Bwana njia yake, nyosheni barabara zake.’”

Mungu wetu tunakuja mbele zako tukijinyenyekeza,tukijishusha
na kujiachilia mikononi mwako Yahweh..
Jehovah tunaomba utusamehe makosa yetu yote tuliyoyafanya
kwakuwaza,kwakunena,kwakutenda,kwakujua/kutojua
Mungu wetu nasi tunaomba utupe neema ya kuweza kuwasamehe
wale wote waliotukosea..
Baba wa Mbinguni usitutie katika majaribu Mungu wetu
tunaomba utuokoe na yule mwovu na kazi zake zote
Yahweh tunaomba ututakase miili yetu na akili zetu
Mungu wetu utufunike kwa Damu ya Bwana na Mwokozi
wetu Yesu Kristo wa Nazareti yeye aliteseka kwanza
ili sisi tupate kupona...


Yohane Mbatizaji alitokea jangwani, akahubiri kwamba watu watubu na kubatizwa ili Mungu awasamehe dhambi zao. Watu kutoka sehemu zote za Yudea na wenyeji wote wa Yerusalemu walimwendea, wakaziungama dhambi zao, naye akawabatiza katika mto Yordani. Yohane alikuwa amevaa vazi lililofumwa kwa manyoya ya ngamia, na ukanda wa ngozi kiunoni mwake. Chakula chake kilikuwa nzige na asali ya mwituni. Naye alihubiri akisema, “Baada yangu anakuja mwenye nguvu zaidi kuliko mimi, ambaye mimi sistahili hata kuinama na kufungua kamba za viatu vyake. Mimi ninawabatiza kwa maji, lakini yeye atawabatiza kwa Roho Mtakatifu.”

Jehovah tunaomba ukabariki kazi za mikono yetu
 Mungu wetu tunaomba utupe ubunifu na maarifa katika utendaji
Yahweh nasi tukatende sawasawa na mapenzi yako
Baba wa Mbinguni tunaomba ukabariki ridhiki zetu ziingiazo/zitokazo
Yahweh nasi tunaomba utupe neema ya kuweza kuwabariki
wenye kuhitaji..
Mungu wetu tusipungukiwe katika mahitaji yetu
baba wa Mbinguni ukatupe kama inavyokupendeza wewe..

Mfalme wa amani tunayaweka maisha yetu mikononi mwako
Baba wa Mbinguni tunaomba ukabariki nyumba/ndoa zetu,
watoto,wazazi wetu,familia/ndugu na wote wanaotuzunguka
Yahweh tunaomba ulinzi wako kwetu na kwa vyote tunavyovimiliki
Mungu wetu tunaomba ukatubariki tuingiapo/tutokapo
Yahweh tukawe salama moyoni Baba wa Mbinguni tunaomba
ukatupe macho ya kuona na masikio ya kusikia sauti yako na kuitii
Mungu wetu ukaonekane popote tupitapo na kajulikane kwamba upo
Baba wa mbinguni..
Yahweh neema yako na Nuru yako ikaangze katika maisha yetu
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe neema ya kufuata njia
zako Jehovah tukasimamie Neno lako amri na sheria zako 
siku zote za maisha yetu....
Yahweh ukatufanye kuwa  barua njema nasi tukasomeke kama inavyokupendeza wewe...
Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi....


Siku hizo, Yesu alifika kutoka Nazareti, mji wa Galilaya, akabatizwa na Yohane katika mto Yordani. Mara tu alipotoka majini, aliona mbingu zimefunguliwa, na Roho akishuka juu yake kama njiwa. Sauti ikasikika kutoka mbinguni: “Wewe ni Mwanangu mpendwa, nimependezwa nawe.” Mara akaongozwa na Roho kwenda jangwani, akakaa huko siku arubaini akijaribiwa na Shetani. Alikuwa huko pamoja na wanyama wa porini, nao malaika wakawa wanamhudumia.

Yahweh tazama wenye shida/tabu,wagonjwa,wenye njaa
walio katika magumu/majaribu mbalimbalia,walio katika vifungo
vya yule mwovu,walio magerezani pasipo na hatia,wenye hofu na
mashaka,walio kataliwa,walio kata tamaa,walio anguka/potea
na wote wanaokutafuta kwa bidii na imani Mungu wetu tunaomba
ukawaguse kwa mkono wako wenye nguvu,Baba wa Mbinguni
tunaomba ukawaponye kimwili na kiroho, Yahweh tunaomba ukawape chakula na kubariki mashamba/kazi zao Mungu wetu ukawaokoe na kuwafungua Jehovah ukawe tumaini lao Mungu wetu ukawape neema
ya kujiombea,kufuata njia zako,kusimamia Neno lako,Neema,Baraka
na amani vikawe nao,ukawape kutambua/kujitambua..
Baba wa Mbinguni ukawasamehe na kuwaokoa,Mungu wetu ukasikie
kulia kwao Yahweh ukawafute machozi ya watoto wako
Jehovah tunaomba ukasikie na ukapokee sala/maombi yetu
Baba wa Mbinguni ukawatendee saswasawa na mapenzi yako
Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na utukufu hata Milele
Amina..!!

Asanteni sana wapendwa/waungwana kwakuwa nami/kunisoma
Mungu Baba aendelee kuwabariki na kuwatendea kama 
inavyompendeza yeye..
Amani ya Kristo Yesu ikae nanyi Daima...
Nawapenda.



Daudi anampa Solomoni wosia

1Daudi alipokaribia kufariki, alimwita mwanawe Solomoni, akampa wosia akisema, 2“Mwanangu, kama ilivyo kawaida kwa viumbe vyote kufa, siku zangu zimekwisha. Uwe imara na hodari. 3Timiza maagizo ya Mwenyezi-Mungu, Mungu wako, ufuate njia zake na kushika masharti yake, amri zake, hukumu zake na kuheshimu maamuzi yake kama ilivyoandikwa katika sheria ya Mose, ili upate kufanikiwa katika kila ufanyalo na kokote uendako, pia 4ili Mwenyezi-Mungu atimize ahadi yake aliyotoa aliponiambia kuwa, ikiwa wazawa wangu watatii amri zake na kumtumikia kwa uaminifu na kwa moyo wote, hakutakosekana mmoja wao kutawala Israeli nyakati zote.
5“Zaidi ya hayo, unajua pia yale aliyonitendea Yoabu, mwana wa Seruya; jinsi alivyowatendea majemadari wawili wa majeshi ya Israeli, Abneri mwana wa Neri, na Amasa mwana wa Yetheri. Aliwaua wakati wa amani akitaka kulipiza kisasi kwa mauaji waliyofanya wakati wa vita. Aliwaua watu wasiokuwa na hatia, nami nikachukua lawama kwa ajili ya vitendo vyake ambavyo vimeniletea mateso. 6Basi, wewe fanya kadiri ya hekima yako, ila tu usimwache afe kwa amani.
7“Lakini uwatendee mema wana wa Barzilai, Mgileadi, na uwatunze kwa ukarimu wawe kati ya wale wanaokula mezani pako; kwa sababu walinitendea mema wakati nilipomkimbia ndugu yako Absalomu. 8Pia, yupo Shimei mwana wa Gera, Mbenyamini wa Bahurimu, ambaye aliniapiza na kunilaani vikali nilipokwenda Mahanaimu; lakini alipokuja kunilaki kwenye mto Yordani, nilimwapia kwa jina la Mwenyezi-Mungu nikimwambia, ‘Sitakuua kwa upanga.’ 9Lakini wewe usimwache bila kumwadhibu. Wewe una hekima; utajua utakalomfanyia; ingawa yeye ana mvi, usimwache; muue ingawa ni mzee.”

Kifo cha Daudi

10Daudi alifariki, akazikwa katika mji wake. 11Alikuwa ametawala Israeli kwa muda wa miaka arubaini; miaka saba akiwa Hebroni, na miaka thelathini na mitatu akiwa Yerusalemu. 12Basi, Solomoni akaketi katika kiti cha enzi mahali pa Daudi, baba yake; na ufalme wake ukaimarika.

Kifo cha Adoniya

13Baadaye, Adoniya mwana wa Hagithi, alimwendea Bathsheba, mama yake Solomoni. Bathsheba akamwuliza, “Je, unakuja kwa amani?” Adoniya akamjibu, “Ndiyo, nakuja kwa amani. 14Ila, nina jambo moja tu la kukuambia.” Bathsheba akamwambia, “Sema tu.” 15Adoniya akamwambia, “Unajua kwamba mimi ningalikuwa mfalme, na hata Israeli yote ilikuwa inanitazamia niwe mfalme. Lakini, mambo yakageuka na ndugu yangu akanipindua, kwani hayo ndio yaliyokuwa mapenzi yake Mwenyezi-Mungu. 16Sasa, ninalo ombi moja tu ambalo nakusihi usinikatalie.” Bathsheba akamwambia, “Sema tu.” 17Naye akasema, “Tafadhali, nakusihi umwombe mfalme Solomoni aniruhusu nimchukue Abishagi, yule Mshunami, awe mke wangu, kwa maana najua hatakukatalia wewe.” 18Bathsheba akamwambia, “Sawa; nitazungumza na mfalme kwa niaba yako.”
19Basi, Bathsheba akamwendea mfalme Solomoni kumweleza ombi la Adoniya. Mfalme akainuka kwenda kumlaki mama yake, akamwinamia. Halafu, akaketi katika kiti chake cha enzi, akaagiza mama yake aletewe kiti; naye akakaa upande wa kulia wa mfalme. 20Bathsheba akasema, “Nina ombi dogo tafadhali ulikubali, na ninakuomba usinikatalie.” Mfalme akamwambia, “Sema ombi lako mama yangu, kwa sababu sitakukatalia.” 21Naye akasema, “Mruhusu ndugu yako Adoniya amwoe Abishagi, huyo Mshunami.” 22Mfalme Solomoni akamwuliza mama yake, “Kwa nini unataka nimpe Abishagi? Hii ni sawa kabisa na kumtakia ufalme wangu! Kumbuka ya kwamba yeye ni kaka yangu mkubwa, na isitoshe, kuhani Abiathari na jemadari Yoabu mwana wa Seruya, wako upande wake!” 23Hapo mfalme Solomoni akaapa kwa jina la Mwenyezi-Mungu, akisema, “Mungu na aniulie mbali ikiwa Adoniya hatakufa kwa sababu ya kutoa ombi hili! 24Sasa basi, kwa jina la Mwenyezi-Mungu aliye hai, aliyeniweka na kuniimarisha katika ufalme wa baba yangu Daudi, na aliyetimiza ahadi yake, akanipa enzi mimi na wazawa wangu, naapa kwamba hivi leo Adoniya atakufa!” 25Ndipo mfalme Solomoni akatoa amri kwa Benaya mwana wa Yehoyada; naye akamwendea Adoniya, akamuua.

Abiathari anapigwa marufuku; Yoabu anauawa

26Mfalme Solomoni akamwambia kuhani Abiathari, “Ondoka uende shambani kwako, huko Anathothi; unastahili kufa wewe! Lakini sasa, sitakuua kwa sababu ulilishughulikia sanduku la agano la Mwenyezi-Mungu ulipokuwa na baba yangu Daudi, ukateswa pamoja naye.” 27Basi, mfalme Solomoni akamfukuza Abiathari, asiwe kuhani wa Mwenyezi-Mungu; hivyo likatimia neno alilosema Mwenyezi-Mungu huko Shilo, juu ya Eli na ukoo wake.
28Yoabu alipopata habari, alikimbilia hemani mwa Mungu na kushikilia pembe za madhabahu; kwa maana alikuwa amemwunga mkono Adoniya na si Absalomu. 29Mfalme Solomoni aliposikia kwamba Yoabu yumo katika hema la Mungu na kwamba amesimama madhabahuni, alimtuma Benaya mwana wa Yehoyada, akisema, “Nenda ukampige.” 30Basi, Benaya akaenda katika hema la Mungu, akamwambia Yoabu, “Mfalme ameamuru utoke nje.” Yoabu akajibu, “Mimi sitoki; nitakufa papa hapa.” Benaya akarudi kwa mfalme na kumweleza alivyojibu Yoabu. 31Solomoni akasema, “Fanya alivyosema; umuue na kumzika. Hivyo, mimi na wazawa wengine wote wa Daudi hatutalaumiwa kwa vitendo vya Yoabu vya kuwaua watu wasio na hatia. 32Mungu atamwadhibu Yoabu kwa mauaji hayo aliyoyafanya bila baba yangu kuwa na habari. Yeye aliwaua watu wawili ambao walikuwa wa maana zaidi kuliko yeye, pia walimzidi kwa wema; aliwaua Abneri mwana wa Neri, jemadari wa jeshi la Israeli, na Amasa mwana wa Yetheri, jemadari wa jeshi la Yuda. 33Adhabu ya mauaji hayo itakuwa juu ya Yoabu na wazawa wake milele. Bali Mwenyezi-Mungu atawapa ufanisi daima, Daudi na wazawa wake watakaokalia kiti chake cha enzi.”
34Basi, Benaya mwana wa Yehoyada, akaenda hemani, akamuua Yoabu ambaye alizikwa shambani mwake, nyikani. 35Mfalme akamweka Benaya mwana wa Yehoyada, kuwa jemadari wa jeshi mahali pa Yoabu, na Sadoki akawa kuhani mahali pa Abiathari.

Kifo cha Shimei

36Halafu mfalme akaagiza Shimei aitwe, akamwambia, “Jijengee nyumba humu Yerusalemu, ukae hapa bila kwenda mahali pengine popote pale. 37Maana siku utakapotoka na kuvuka kijito Kidroni, nakuambia kweli utakufa, na kujilaumu wewe mwenyewe kwa kifo chako.” 38Shimei akajibu, “Vema mfalme. Nitafanya kama ulivyosema.” Basi, akakaa Yerusalemu muda mrefu.
39Lakini mwishoni mwa mwaka wa tatu, watumwa wawili wa Shimei walitoroka, wakaenda kwa Akishi mwana wa Maaka, mfalme wa Gathi. Habari zilipomfikia kwamba wako Gathi, 40Shimei alipanda punda wake, akaenda huko kuwatafuta, kwa mfalme Akishi. Basi, akafika, akawapata, akawarudisha nyumbani. 41Mfalme Solomoni alipopata habari kwamba Shimei alikuwa ametoka Yerusalemu, akaenda Gathi na kurudi, 42alimwita Shimei na kumwambia, “Je, hukuniapia kwa jina la Mwenyezi-Mungu kwamba hutatoka Yerusalemu, nami sikukuonya kwa dhati kwamba, hakika utakufa kama utathubutu kwenda nje? Nawe ulikubali, ukaniambia, ‘Vema, nitatii.’ 43Mbona basi, umevunja kiapo chako kwa Mwenyezi-Mungu na kutojali amri niliyokupa?” 44Mfalme aliendelea kumwambia Shimei, “Unayajua wazi maovu uliyomtendea baba yangu Daudi, na sasa, kwa sababu ya hayo, Mwenyezi-Mungu atakuadhibu. 45Lakini mimi atanibariki, na kiti cha enzi cha Daudi kitaimarishwa mbele ya Mwenyezi-Mungu milele.” 46Hapo, mfalme akamwamuru Benaya mwana wa Yehoyada, naye akatoka, akampiga na kumuua Shimei. Basi, ufalme ukaimarika chini ya Solomoni.



1Wafalme2;1-46


Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)

"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.

No comments: