Swahili na Waswahili

Swahili na Waswahili
Waswahili na Mswahili Rachel Siwa...Pamoja Daima!!

Friday 23 March 2018

Kikombe Cha Asubuhi ;1 Wafalme 15...





Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?

Haleluyah Haleluyah Haleluyah Mumgu wetu yu mwema sana
Tumshukuru Mungu wetu katika yote..!!

Asante Mungu wetu kwa wema na fadhili zako kwetu
Asante kwa ulinzi wako kwetu wakati wote
Asante kwakutuchagua tena na kutupa kibali cha kuendelea
kuiona leo hii
Asante kwa pumzi/uzima,afya na kuwa tayari kwa majuku yetu...
Utukuzwe ee Mungu wetu,Mungu mwenye nguvu,Mungu mwenye huruma
Mungu wa walio hai,Yahweh...!Jehovah..!Elohim..!El Olam..!El Qanna..!
El Elyon..!El Shaddai..!Emanuel-Mungu pamoja nasi...!!
Neema yako yatutosha Baba wa Mbinguni,Matendo yako ni makuu mno
Matendo yako niya ajabu,hakuna kama wewe Mungu wetu...!!
Sifa na Utukufu tunakurudishia wewe Baba wa Mbinguni!!


Petro na Yohane walipokuwa bado wanawahutubia watu, makuhani na mkuu wa walinzi wa hekalu pamoja na Masadukayo walifika. Walikasirika sana, maana hao mitume walikuwa wanawahubiria watu kwamba Yesu alifufuka, jambo ambalo linaonesha wazi kwamba wafu watafufuka. Basi, waliwatia nguvuni na kwa kuwa usiku ulikuwa umekaribia, wakawaweka chini ya ulinzi mpaka kesho yake. Lakini wengi kati ya wale waliosikia ujumbe wao waliamini, na idadi ya waumini ikawa imefika karibu wanaume 5,000. Kesho yake, viongozi wa Wayahudi, wazee na waalimu wa sheria walikusanyika pamoja huko Yerusalemu. Walikutana pamoja na Anasi kuhani mkuu, Kayafa, Yohane, Aleksanda na wengine waliokuwa wa ukoo wa kuhani mkuu. Walipowasimamisha mitume mbele yao, waliwauliza, “Nyinyi mmefanya jambo hili kwa nguvu gani na kwa jina la nani?”



Yahweh tunakuja mbele zako tukijinyenyekeza,tukijishusha 
na kujiachilia mikononi mwako
Mungu wetu tunaomba utusamehe dhambi zetu zote tulizozifanya
kwakuwaza,kwakunena,kwakutenda,kwakujua/kutojua
Baba wa Mbinguni nasi tunaomba utupe neema ya kuweza
kuwasamehe wale wote ewaliotukosea
Jehovah usitutie katika majaribu Mungu wetu tunaomba utuokoe 
na yule mwovu na kazi zake zote
Yahweh tunaomba ututakase miili yetu na kaili zetu Baba wa Mbinguni
tunaomba utufunike kwa Damu ya Bwana na Mwokozi wetu Yesu kristo
wa Nazareti yeye aliteseka kwanza ili sisi tupate kupona....

Hapo, Petro, akiwa amejawa na Roho Mtakatifu, akawaambia, “Viongozi na wazee wa watu! Ikiwa mnatuuliza leo juu ya kile kitendo chema alichofanyiwa yule mtu aliyekuwa kiwete na jinsi alivyopata kuwa mzima, basi, nyinyi na watu wote wa Israeli mnapaswa kujua kwamba mtu huyu anasimama mbele yenu leo, mzima kabisa, kwa nguvu ya jina lake Yesu wa Nazareti ambaye nyinyi mlimsulubisha, lakini Mungu akamfufua kutoka kwa wafu. Huyu ndiye ambaye Maandiko Matakatifu yanasema: ‘Jiwe mlilokataa nyinyi waashi, sasa limekuwa jiwe kuu la msingi.’ Wokovu haupatikani kwa mtu mwingine yeyote, kwa maana duniani pote, binadamu hawakupewa jina la mtu mwingine ambaye sisi tunaweza kuokolewa naye.”

Baba wa Mbinguni tunaomba ukabariki kazi za mikono yetu
Mungu wetu tunaomba ukatupe ubunifu na maarifa katika utendaji
Jehovah nasi tukatende sawasawa na mapenzi yako
Yahweh tunaomba ukabariki ridhiki zetu ziingiazo/zitokazo
Mungu wetu nasi tunaomba ukatupe neema ya kuweza kuwabariki
wenye kuhitaji,Baba wa Mbinguni tusipungukiwe katika mahitaji yetu
Mungu wetu ukatupe kama inavyokupendeza wewe..

Jehovah tunayaweka maisha yetu mikononi mwako
Mungu wetu tunaomba ukabariki nyumba/ndoa zetu,watoto,wazazi
wetu,familia/ndugu na wote wanaotuzunguka
Yahweh tunaomba ukatubariki tuingiapo/tutokapo, Mungu wetu
tunaomba ulinzi wako kwetu na kwa vyote tunavyovimiliki
Jehovah ukatamalaki na kutuatimia,Mungu wetu tukawe salama
rohoni Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe macho ya kuona na 
masikio ya kusikia sauti yako na kuitii...
Mfalme wa amani tunaomba amani yako ikatawale katika maisha yetu
Mungu wetu ukatupe neema ya kutambua mema na mabaya
Jehovah tunaomba ukatupe neema ya kufuata njia zako Mungu wetu
tukasimamie neno lako amri na sheria zako siku zote za maisha yetu
Yahweh ukaonekane katika maisha yetu Mungu wetu popote tupitapo
na ikajulikane kwamba upo Baba wa Mbinguni...
Yahweh ukatufanye chombo chema Mungu wetu tukatumike kama
inavyokupendeza wewe...
Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi....


Hao wazee wa Baraza, wakiwa wanajua kwamba Petro na Yohane walikuwa watu wasio na kisomo wala elimu yoyote, walishangaa juu ya jinsi walivyosema kwa uhodari. Wakatambua kwamba walikuwa wamejiunga na Yesu. Lakini walipomwona yule mtu aliyeponywa amesimama pamoja nao, hawakuweza kusema kitu. Hivyo, waliwaamuru watoke nje ya baraza, nao wakabaki ndani wakizungumza kwa faragha. Wakaulizana, “Tufanye nini na watu hawa? Kila mtu anayeishi Yerusalemu anajua kwamba muujiza huu wa ajabu umefanyika, nasi hatuwezi kukana jambo hilo. Lakini ili tupate kuzuia jambo hili lisienee zaidi kati ya watu, tuwaonye wasiongee na mtu yeyote kwa jina la Yesu.” Kwa hiyo wakawaita tena ndani, wakawaonya wasiongee tena hadharani, wala kufundisha kwa jina la Yesu. Lakini Petro na Yohane wakawajibu, “Amueni nyinyi wenyewe kama ni sawa mbele ya Mungu kuwatii nyinyi kuliko kumtii Mungu. Kwa maana hatuwezi kuacha kusema juu ya mambo yale tuliyoyaona na kuyasikia.” Basi, hao wazee wa Baraza wakawaonya kwa ukali zaidi, halafu wakawaacha huru. Hawakuweza kuwapa adhabu kwa sababu watu wote walikuwa wakimtukuza Mungu kwa sababu ya tukio hilo. Huyo mtu aliyeponywa alikuwa na umri wa miaka zaidi ya arubaini.

Baba wa Mbinguni tunawaweka mikononi mwako wote wenye
shida/tabu,wagonjwa,wenye njaa,wanaopitia magumu/majaribu
mbalimbali,waliokata tamaa,walio kataliwa,wenye hofu na mashaka
waliopotea/anguka,walio umizwa rohoni,waliokwama kibiashara,
wanaotafuta kazi,walio kwama kimasomo,wanaotafuta watoto,
walio elemewa na mizigo mizito,walio katika vifungo vya yule mwovu,walio magerezani pasipo na hatia  na wote wanaokutafuta
kwa bidii na imani Mungu wetu tunaomba ukawaguse kwa mkono wako
wenye nguvu,Baba wa Mbinguni tunaomba ukawaponye kimwili na kiroho
pia,Yahweh ukawafungue na kuwaweka huru Mungu wetu haki ikatendeke
Jehovah ukawatue mizigo yao na wakawe salama rohoni,Mungu wetu
ukawape neema ya kusamehe na ukawaponye mioyo yao
Baba wa mbinguni ukawaoshe na kuwaokoa,Mungu wetu ukaonekane
katika maisha yao,Jehovah ukawasamehe makosa yao Mungu wetu
ukawape neema ya kujiombea,kufuata njia zako kusimamia Neno lako
nalo likawaweke huru,Jehovah ukawape macho ya rohoni Baba wa Mbinguni ukawape kutambua na kujitambua,Yahweh wakawe na amani
furaha,Neema yako na Nuru yako ikaangaze katika maisha yao..
Ee Baba wa Mbinguni tunaomba ukasikie na ukapokee sala/maombi yetu
Jehovah ukawatendee sawasawa na mapenzi yako..
Kwakuwa ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele..
Amina...!!

Asanteni sana wapendwa katika Kristo Yesu kwa kuwanami/kunisoma
Mungu Baba akawabariki na kuwatendea kama inavyompendeza yeye
Msipungukiwe katika mahitaji yenu Baba wa Mbinguni akawape
sawasawa na mapenzi yake...
Nawapenda.

Mfalme Abiya wa Yuda

(2Nya 13:1–14:1)

1Abiya alianza kutawala huko Yuda mnamo mwaka wa kumi na nane wa utawala wa mfalme Yeroboamu, mwanawe Nebati. 2Alitawala kwa muda wa miaka mitatu akiwa Yerusalemu. Mama yake alikuwa Maaka binti Absalomu.15:2 Absalomu: Au Abishalomu. 3Abiya alitenda dhambi zilezile alizotenda baba yake, wala hakuwa na moyo mwaminifu kwa Mwenyezi-Mungu, Mungu wake, kama alivyokuwa babu yake15:3 babu yake: Kiebrania: Baba yake. Daudi. 4Hata hivyo, kwa ajili ya Daudi, Mwenyezi-Mungu alimpatia Abiya mwana atakayetawala baada yake, kuwa taa ya kuangaza Yerusalemu na kuuweka imara mji wa Yerusalemu. 5Mwenyezi-Mungu alifanya hivyo kwa kuwa Daudi alitenda mema mbele yake na hakukiuka aliyomwamuru Mwenyezi-Mungu siku zake zote, isipokuwa tu ule mkasa wa Uria, Mhiti. 6Kulikuwako vita kati ya Rehoboamu15:6 Rehoboamu: Au Abiya. na Yeroboamu wakati wote alipokuwa mtawala.
7Matendo mengine ya Abiya, na yote aliyoyafanya yameandikwa katika Kitabu cha Mambo ya Nyakati ya Wafalme wa Yuda. Abiya na Yeroboamu waliishi katika hali ya vita. 8Mwishowe, Abiya alifariki na kuzikwa katika mji wa Daudi na mwanawe Asa akatawala mahali pake.

Asa, mfalme wa Yuda

(2Nya 15:16–16:6)

9Mnamo mwaka wa ishirini wa utawala wa Yeroboamu, mfalme wa Israeli, Asa alianza kutawala huko Yuda. 10Alitawala kwa muda wa miaka arubaini na mmoja. Mama yake alikuwa Maaka, binti Absalomu. 11Mfalme Asa alitenda yaliyo mema mbele ya Mwenyezi-Mungu kama alivyofanya Daudi babu yake. 12Aliwafukuza nchini wale wafiraji wa kidini, akaziondoa sanamu zote ambazo babu zake walikuwa wamezitengeneza. 13Alimvua Maaka, mama yake, cheo chake cha mama malkia, kwa sababu alitengeneza sanamu ya Ashera, mungu wa kike, na hiyo sanamu akaivunjavunja na kuiteketeza kwenye bonde la Kidroni. 14Lakini mahali pa juu pa kutambikia miungu hapakuharibiwa; hata hivyo, yeye alikuwa na moyo mwaminifu kwa Mwenyezi-Mungu maisha yake yote. 15Alirudisha nyumbani mwa Mwenyezi-Mungu vyombo vyote vilivyokuwa vimewekwa wakfu na baba yake, pamoja na vile vyake yeye mwenyewe: Vyombo vya fedha, dhahabu na vyombo vinginevyo.
16Mfalme Asa wa Yuda, na mfalme Baasha wa Israeli, walikuwa na vita kati yao wakati wote walipokuwa wakitawala. 17Baasha, mfalme wa Israeli, aliishambulia nchi ya Yuda na kuanza kuujenga Rama ili apate kuzuia mtu yeyote asitoke wala asiingie kwa Asa, mfalme wa Yuda. 18Ndipo mfalme Asa akachukua fedha na dhahabu yote iliyobaki katika hazina ya nyumba ya Mwenyezi-Mungu na katika hazina ya ikulu, akawapa watumishi wake, akawatuma Damasko kwa Ben-hadadi mwana wa Tabrimoni, mjukuu wa Hezioni, mfalme wa Aramu, akasema, 19“Tufanye mkataba wa ushirikiano kati yangu na wewe kama vile walivyofanya baba yangu na baba yako; tazama, nimekupelekea zawadi ya fedha na dhahabu; nenda ukavunje mkataba wa ushirikiano ulioko kati yako na mfalme Baasha wa Israeli, ili aache mashambulizi dhidi yangu.” 20Hapo mfalme Ben-hadadi akakubali pendekezo la mfalme Asa, akawatuma majemadari wake na majeshi yake kwenda kuishambulia miji ya Israeli. Nao wakateka Iyoni, Dani, Abel-beth-maaka, Kinerethi15:20 Kinerothi: Nchi iliyoko karibu na ziwa Galilaya. yote, na nchi yote ya Naftali. 21Mfalme Baasha alipopata habari za mashambulizi hayo aliacha kuujenga mji wa Rama akaishi katika Tirza. 22Ndipo mfalme Asa alipotoa tangazo kwa watu wote wa Yuda, bila kumwacha hata mtu mmoja, wahamishe mawe ya Rama na mbao, vifaa ambavyo Baasha alivitumia kujengea. Kisha mfalme Asa alitumia vifaa hivyo kujengea Geba, katika Benyamini na Mizpa. 23Matendo mengine yote ya Asa, ushujaa wake na miji yote aliyoijenga, yote yameandikwa katika Kitabu cha Mambo ya Nyakati ya Wafalme wa Yuda. Lakini, wakati wa uzee wake, Asa alishikwa na ugonjwa wa miguu. 24Hatimaye, Asa alifariki, akazikwa katika makaburi ya kifalme, katika mji wa Daudi, naye mwanawe Yehoshafati akatawala mahali pake.

Nadabu, mfalme wa Israeli

25Mnamo mwaka wa pili wa utawala wa Asa huko Yuda, Nadabu, mwana wa Yeroboamu, alianza kutawala huko Israeli. Alitawala kwa muda wa miaka miwili. 26Nadabu alitenda maovu mbele ya Mwenyezi-Mungu; akamwiga baba yake ambaye aliwafanya watu wa Israeli watende dhambi. 27Baasha mwana wa Ahiya, wa kabila la Isakari, akala njama dhidi ya Nadabu. Basi, wakati Nadabu na jeshi lake walipokuwa wameuzingira mji wa Gibethoni wa Wafilisti, Baasha akamvamia na kumwua, 28akatawala mahali pake. Huo ulikuwa mwaka wa tatu wa utawala wa mfalme Asa wa Yuda. 29Mara tu alipoanza kutawala, Baasha akawaua watu wote wa jamaa ya Yeroboamu; hakuacha hai hata mtu mmoja wa jamaa ya Yeroboamu; hiyo ilikuwa sawa na yale aliyosema Mwenyezi-Mungu kwa njia ya mtumishi wake, Ahiya wa Shilo. 30Mambo haya yalifanyika kwa sababu Yeroboamu alimkasirisha Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli, kwa dhambi yake na kwa kuwafanya watu wa Israeli watende dhambi.
31Matendo mengine ya Nadabu, yote yameandikwa katika Kitabu cha Mambo ya Nyakati ya Wafalme wa Israeli. 32Mfalme Asa wa Yuda na mfalme Baasha wa Israeli walikuwa na vita kati yao wakati wote walipokuwa wakitawala.

Baasha, mfalme wa Israeli

33Mnamo mwaka wa tatu wa utawala wa Asa mfalme wa Yuda, Baasha mwana wa Ahiya, alianza kutawala Israeli kutoka Tirza. Alitawala kwa muda wa miaka ishirini na minne. 34Baasha alitenda maovu mbele ya Mwenyezi-Mungu, akamwiga Yeroboamu na kutenda dhambi ileile ambayo aliwafanya watu wa Israeli watende.


1Wafalme15;1-34


Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)

"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.

No comments: