Swahili na Waswahili

Swahili na Waswahili
Waswahili na Mswahili Rachel Siwa...Pamoja Daima!!

Wednesday 18 October 2017

Kikombe Cha Asubuhi ;Yoshua 7...




Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?

Tumshukuru Mungu wetu kwa mema mengi 

aliyotutendea/anayoendelea kututendea..
Mungu wetu ,Baba yetu,Muumba wetu,Muumba wa Mbingu na Nchi..
Mungu wa Abrahamu,Isaka na Yakobo,Mungu mwenye huruma..
wewe ndiye Ndimi Mwenyezi-Mungu  Mungu wa wote wenye mwili
hakuna jambo lolote lililogumu linaloweza kukushinda Mungu wetu..
Utukuzwe Mungu wetu,Usifiwe Baba wa Mbingu,Uhimidiwe Jehovah
Uabudiwe Yahweh,Hakuna kama wewe Mungu wetu,Matendo yako
ni ya ajabu mno,Matendo yako ni makuu sana,Unatosha Baba wa Mbinguni


Mungu ni kimbilio letu na nguvu yetu; yeye ni msaada wetu daima wakati wa taabu. Kwa hiyo hatutaogopa chochote, dunia ijapoyeyuka na milima kutikisika kutoka baharini; hata kama bahari ikichafuka na kutisha, na milima ikatetemeka kwa machafuko yake. Kuna mto ambao maji yake hufurahisha mji wa Mungu, makao matakatifu ya Mungu Mkuu. Mungu yumo mjini humo, nao hauwezi kutikiswa; Mungu ataupa msaada alfajiri na mapema. Mataifa yaghadhibika na tawala zatikisika; Mungu anguruma nayo dunia yayeyuka. Mwenyezi-Mungu wa majeshi yu pamoja nasi, Mungu wa Yakobo ni kimbilio letu. Njoni mwone matendo ya Mwenyezi-Mungu; oneni maajabu aliyoyafanya duniani. Hukomesha vita popote duniani, huvunjavunja pinde na mikuki, nazo ngao huziteketeza. Asema: “Nyamazeni na kujua kuwa mimi ni Mungu! Mimi natukuka katika mataifa yote; mimi natukuzwa ulimwenguni kote!” Mwenyezi-Mungu wa majeshi yu pamoja nasi, Mungu wa Yakobo ni kimbilio letu.

Asante Mungu wetu Baba yetu kwa wema na fadhili zako kwetu

Asante kwa ulinzi wako kwetu wakati wote..
Asante kwakutuchagua tena na kutupa kibali cha kuendelea kuiona leo hii Mungu wetu..


Mwenyezi-Mungu asipoijenga nyumba, waijengao wanajisumbua bure. Mwenyezi-Mungu asipoulinda mji, waulindao wanakesha bure. Mnajisumbua bure kuamka mapema asubuhi na kuchelewa kwenda kupumzika jioni, mjipatie chakula kwa jasho lenu. Mungu huwaruzuku walio wake hata walalapo.
Tazama Jana imepita Jehovah Leo ni siku mpya Yahweh
na Kesho ni siku nyingine Mungu wetu..
Baba wa Mbinguni tukakuja mbele zako tukijinyenyekeza tukijishusha na kujiachilia mikononi mwako..
Mungu wetu tunaomba utusamehe dhambi zetu zote tulizozifanya kwakuwaza,kwakunena,kwakutenda,kwakujua/kutojua..
Mungu wetu nasi tunaomba utupe neema ya kuweza kuwasamehe
wale wote waliotukosea..
Baba wa Mbinguni tunaomba utuepushe katika majaribu na 
utuokoe na yule mwovu na kazi zake zote..
Mungu wetu tunaomba ututakase miili yetu na akili zetu
Baba tunaomba utufunike kwa Damu ya Bwana wetu
Yesu Kristo wa Nazareti,yeye aliteseka kwanza ili sisi tupate kupona..

Yahweh tunaomba ukabariki kazi za mikono yetu,Biashara,masomo

na vyote tunavyoenda kufanya/kutenda Mungu wetu tukatende
sawasawa na mapenzi yako...
Mungu wetu tunaomba ukabariki ridhiki zetu ziingiazo/zitokazo
Yahweh nasi tunaomba utupe neema ya kuweza kuwabariki
wenye kuhitaji..
Mungu wetu tusipungukiwe katika mahitaji yetu Baba ukatupe 
sawasawa na mapenzi yako..

Mfalme wa Amani tunaomba amani yako ikatawale katika Nyumba/ndoa zetu,watoto,wazazi wetu,familia/ndugu na wote wanotuzunguka..

Mungu wetu tunaomba ukatupe neema ya hekima,busara,kutambua/kujitambu katika yote,tukanene yaliyo yako tukachukuliane,tukapendane na pendo letu likawe la kweli nasi  kwa unafiki,tukaonyane na kuelemishana kwa upendo,tukasameheane,tukawe wanyeyekevu kwa watu wote,na Mungu wetu ukaonekane popote tupitapo/tuendapo,tukasimamie Neno lako Amri na Sheria zako siku zote za maisha yetu..
Ukatufanye chombo chema nasi tukatumike kama inavyokupendeza wewe
Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi..


Heri wote wamchao Mwenyezi-Mungu, wanaoishi kufuatana na amri zake. Utapata matunda ya jasho lako, utafurahi na kupata fanaka. Mkeo atakuwa kama mzabibu wa matunda mengi nyumbani mwako; watoto wako kama chipukizi za mzeituni kuzunguka meza yako. Naam, ndivyo atakavyobarikiwa mtu amchaye Mwenyezi-Mungu. Mwenyezi-Mungu akubariki kutoka Siyoni! Uione fanaka ya Yerusalemu, siku zote za maisha yako. Uishi na hata uwaone wajukuu zako! Amani iwe na Israeli!

Mungu wetu ukawakuguse na mkono wako wenye nguvu wote 

wenye shida/tabu,wagonjwa,wenye njaa,waliokatika vifungo
vya yule mwovu,wanaopitia magumu/majaribu mbalimbali..
Yahweh ukawaponye kimwili na kiroho pia,Baba ukawasimamishe
wale wote walioanguka,Mungu wetu ukawasamehe wale wote
waliokwenda kinyume nawe,Mungu wetu ukawape neema ya kujiombea
Baba ukapokee sala/maombi ya watoto wako wote wakuombao
kwa imani na wafiwa ukawape nguvu,uvumilivu ,Baba ukawafariji..


Ee Mwenyezi-Mungu, sina moyo wa kiburi; mimi si mtu wa majivuno. Sijishughulishi na mambo makuu, au yaliyo ya ajabu mno kwangu. Ila nafsi yangu imetulia na kuwa na amani, kama mtoto mchanga alivyotulia na mama yake; ndivyo nafsi yangu ilivyo tulivu. Ee Israeli, umtumainie Mwenyezi-Mungu, tangu sasa na hata milele.
Asante Mungu wetu sifa na utukufu tunakurudishia wewe
Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele
Amina..!!
Asanteni sana wapendwa kwa kuwa nami
UPendo Wenu Ukadumu Daima..
Mungu wetu aendelee kuwabariki na kuwatendea katika yote
Baraka,Amani na furaha viwe nanyi daima..
Nawapenda.



Kosa na adhabu ya Akani

1Lakini Waisraeli hawakuwa waaminifu kuhusu vile vitu vilivyotolewa viangamizwe kwani Akani mwana wa Karmi, mwana wa Zabdi, mwana wa Zera, wa kabila la Yuda, alichukua baadhi ya vitu vilivyoamriwa viteketezwe. Kwa hiyo hasira ya Mwenyezi-Mungu ikawaka dhidi ya Waisraeli.
2Yoshua akawatuma watu kutoka Yeriko kwenda mji wa Ai, ulio karibu ya Beth-aveni, mashariki ya Betheli, akawaambia, “Nendeni mkaipeleleze nchi.” Nao wakaenda na kuupeleleza mji wa Ai. 3Waliporudi, wakamwambia Yoshua, “Hakuna haja kupeleka watu wote kuushambulia mji wa Ai, maana wakazi wake ni wachache tu. Watu elfu mbili au tatu watatosha.” 4Basi, watu kama elfu tatu hivi wakaenda kuushambulia mji wa Ai, lakini wakakimbizwa na wakazi wa mji huo. 5Watu wa Ai wakawaua Waisraeli thelathini na sita na kuwafukuza wengine kutoka lango la mji mpaka Shebarimu, wakawaua kwenye mteremko. Waisraeli wakafa moyo na kulegea kama maji.
6Yoshua akayararua mavazi yake, yeye pamoja na wazee wa Israeli. Wakajitupa chini mbele ya sanduku la Mwenyezi-Mungu mpaka jioni; wakajitia mavumbi vichwani mwao. 7Yoshua akasema, “Ole wetu, ee Bwana Mungu! Kwa nini umetuvusha mto Yordani ili kututia mikononi mwa Waamori watuangamize? Tungaliridhika kubaki ngambo ya mto Yordani! 8Ee Bwana, niseme nini hali Waisraeli wamewakimbia adui zao? 9Basi, Wakanaani pamoja na wakazi wote wa nchi hii watakapopata habari hiyo watatuzingira na kutufuta kabisa duniani. Sasa utafanya nini kuonesha ukuu wa jina lako?”
10Mwenyezi-Mungu akamwambia Yoshua, “Simama! Mbona umejitupa chini hivyo? 11Waisraeli wametenda dhambi, maana wamelivunja agano langu nililowaamuru washike; wamevichukua baadhi ya vitu vilivyowekwa wakfu viangamizwe; wameviiba na kudanganya, wakaviweka pamoja na vitu vyao. 12Kwa hiyo Waisraeli hawawezi kuwakabili maadui zao; wanawakimbia adui zao kwa sababu wamejifanya wenyewe kuwa kitu cha kuangamizwa! Sitakuwa pamoja nao tena msipoharibu vitu vilivyomo kati yenu vilivyotolewa viangamizwe. 13Basi, inuka uwatakase watu, waambie wajitakase na kujitayarisha kwa siku ya kesho, maana mimi Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli, nasema hivi: ‘Miongoni mwenu kuna vitu vilivyotolewa viangamizwe; hamwezi kuwakabili adui zenu mpaka vitu hivyo vimeondolewa kati yenu! 14Kwa hiyo kesho asubuhi wote mtakuja mbele yangu, kabila baada ya kabila. Kabila nitakalolichagua litakwenda mbele, ukoo baada ya ukoo. Ukoo nitakaouchagua utakwenda mbele, jamaa baada ya jamaa. Na jamaa nitakayoichagua itakwenda mbele, mtu mmojammoja. 15Mtu yeyote atakayepatikana akiwa na vitu vilivyotolewa viangamizwe atateketezwa kwa moto, yeye pamoja na kila kitu chake maana ameliasi agano langu mimi Mwenyezi-Mungu, akatenda jambo la aibu katika Israeli.’”
16Basi, Yoshua akaamka asubuhi na mapema, akawaleta Waisraeli wote karibu, kabila baada ya kabila; kabila la Yuda likachaguliwa. 17Akazileta karibu koo za Yuda, ukoo baada ya ukoo; na ukoo wa Zerahi ukachaguliwa. Akazileta karibu jamaa za ukoo wa Zerahi, jamaa baada ya jamaa; na jamaa ya Zabdi ikachaguliwa. 18Yoshua akaileta jamaa ya Zabdi karibu, nyumba baada ya nyumba; na nyumba ya Akani mwana wa Karmi, mwana wa Zabdi, mwana wa Zera, wa kabila la Yuda, ikachaguliwa. 19Yoshua akamwambia Akani, “Mwanangu, mtukuze Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli, msifu na kisha uniambie yale uliyotenda, wala usinifiche.” 20Akani akamjibu; “Ni kweli nimetenda dhambi mbele ya Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli. Na hivi ndivyo nilivyofanya: 21Nilipoona vazi moja zuri kutoka Shinari kati ya nyara, shekeli 200 za fedha na mchi wa dhahabu wenye uzito wa shekeli 50, nikavitamani na kuvichukua; nimevificha ardhini ndani ya hema langu; na fedha iko chini ya vitu hivyo.”
22Basi, Yoshua akawatuma wajumbe, nao wakakimbia hemani kwa Akani. Na kumbe, vilikuwa vimefichwa hemani na fedha ikiwa chini yake. 23Wakavichukua hemani na kuvipeleka kwa Yoshua na watu wote wa Israeli; nao wakaviweka chini, mbele ya Mwenyezi-Mungu. 24Yoshua pamoja na Waisraeli wote, wakamchukua Akani, mwana wa Zera, pamoja na fedha, vazi, dhahabu, watoto wake wa kiume na binti zake, ng'ombe, punda na kondoo wake, hema lake na kila kitu alichokuwa nacho na kuwapeleka kwenye bonde la Akori. 25Yoshua akamwuliza Akani, “Kwa nini umetuletea taabu? Mwenyezi-Mungu atakuletea taabu wewe mwenyewe leo.” Waisraeli wote wakampiga Akani kwa mawe mpaka akafa. Kisha wakawapiga jamaa yake yote kwa mawe mpaka wakafa, wakawateketeza wote kwa moto. 26Halafu wakarundika mawe mengi juu yake, ambayo yako hadi leo. Hapo hasira ya Mwenyezi-Mungu ikapoa; na mahali hapo pakaitwa Bonde la Akori7:26 Akori: Maana yake “taabu”. mpaka hivi leo.


Yoshua 7;1-26

Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)

"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.


No comments: