Swahili na Waswahili

Swahili na Waswahili
Waswahili na Mswahili Rachel Siwa...Pamoja Daima!!

Tuesday 10 October 2017

Kikombe Cha Asubuhi ;Leo tunaanza Kitabu cha Yoshua 1..




Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?

Haleluyah..!Tunamshukuru Mungu kwa kumemaliza kitabu
cha 

Kumbukumbu la Sheria  (Kumbukumbu la Torati katika tafsiri nyingine)

Ni matumaini yangu tumekuwa pamoja katika kujifunza mengi
katika kitabu kilichopita na vinginevyo huko nyuma..
Mungu wetu yu mwema sana,Si kwa nguvu zetu wala si kwa uwezo
wetu ni kwa Neema yake Mungu katuwezesha kuwa na utaratibu huu.
Basi kufikia mwisho na isiwe mwisho wa kusoma tena..
Hapana tujiwekee  muda wa kusoma na kurudia pia huko tulikopita
ili tuweze kuhifadhi ,kujikumbusha na kujifunza zaidi..
Tuzidi kumuomba Mungu wetu akatupe Neema,Kiu,Shauku
zaidi ya kusoma Neno lake na kusimamia Amri na Sheria zake..
Neno la uhai

Habari hii yahusu Neno la uhai lililokuwako tangu mwanzo. Sisi tumepata kulisikia na kuliona kwa macho yetu wenyewe; tulilitazama na kulishika kwa mikono yetu wenyewe. Uhai huo ulipotokea sisi tuliuona na sasa tunasema habari zake na kuwaambieni juu ya uhai huo wa milele uliokuwa kwa Baba na uliodhihirishwa kwetu. Tulichokiona na kukisikia ndicho tunachowatangazieni nyinyi pia, ili nanyi mpate kushirikiana nasi katika umoja tulio nao na Baba na Mwanae Yesu Kristo. Tunawaandikia nyinyi mambo haya kusudi furaha yetu ikamilike.
Baba wa Mbinguni akatupe maalifa,uelewa tunapoenda kuanza kusoma
 kitabu cha "YOSHUA",Mungu wetu akawe nasi katika kitabu hiki
na vingine vijavyo..


Mungu ni mwanga

Basi, habari tuliyoisikia kwake Yesu na tunayowahubirieni ndiyo hii: Mungu ni mwanga na hamna giza lolote ndani yake. Tukisema kwamba tuna umoja naye, na papo hapo tunaishi gizani, tutakuwa tumesema uongo wala hatuishi kwa ukweli kwa maneno na matendo. Lakini tukiishi katika mwanga, kama naye alivyo katika mwanga, basi, tutakuwa na umoja sisi kwa sisi, na damu yake Yesu Kristo, Mwanae, inatutakasa dhambi zote. Tukisema kwamba hatuna dhambi, tunajidanganya wenyewe, na ukweli haumo ndani yetu. Lakini tukiziungama dhambi zetu, basi, Mungu ni mwaminifu na mwadilifu, naye atatusamehe dhambi zetu na kututakasa uovu wote. Tukisema kwamba hatujatenda dhambi, tutakuwa tumemfanya Mungu mwongo, na neno lake halimo ndani yetu.

Tumshukuru Mungu wetu kwa wema na fadhili zake kwetu..
Tumshukuru Mungu kwa ulinzi wake kwetu wakati wote..
Asante Baba wa Mbinguni kwa mema meengi
 uliyotutendea na unayoendelea kututendea...

Utukuzwe Mungu wetu,Usifiwe Baba wa Mbinguni,Uhimidiwe Jehovah..
Unastahili kuabudiwa Yahweh,Unasthahili Mungu wetu..
Hakuna kama wewe Baba wa Mbinguni,Baba wa Baraka,Baba wa Upendo
Baba wa Faraja,Mfariji wetu,Mungu mwenye huruma..
Unatosha Yahweh,Matendo yako ni makuu sana,Matendo yako ni ya Ajabu..
Sifa na Utukufu ni wako Mungu wetu..



Mungu wetu tunakuja mbele zako tukijinyenyekeza,tukijishusha
na kujiachilia mikononi mwako Baba wa Mbinguni..
Tunaomba utusamehe makosa yetu yote tuliyoyafanya
 kwakuwaza,kwakunena,kwakutenda,kwakujua/kutojua..
Baba wa Mbinguni nasi tunaomba utupe neema ya kuweza
kuwasamehe wale wote waliotukosea..
Yahweh tunaomba utuepushe katika majaribu Mungu wetu
 utuokoe na yule mwovu na kazi zake zote..
Baba wa Mbinguni tunaomba ututakase miili yetu na akili zetu
Jehovah utufunike kwa Damu ya Bwana wetu Yesu Kristo wa
Nazareti yeye aliteseka kwanza ili sisi tupate kupona..


Watoto wangu, ninawaandikieni mambo haya, kusudi msitende dhambi. Lakini, ikijatokea mtu akatenda dhambi, tunaye mmoja ambaye hutuombea kwa Baba, ndiye Yesu Kristo aliye mwadilifu kabisa. Kristo ndiye sadaka iondoayo dhambi zetu; wala si dhambi zetu sisi tu, bali pia dhambi za ulimwengu wote. Tukizitii amri za Mungu, basi, tunaweza kuwa na hakika kwamba tunamjua. Mtu akisema kwamba anamjua, lakini hazitii amri zake, basi mtu huyo ni mwongo, na ukweli haumo ndani yake. Lakini mtu yeyote anayeshika neno la Mungu, huyo ndiye aliye na upendo kamili wa Mungu ndani yake. Hivi ndivyo tunavyoweza kuwa na hakika kwamba tunaungana naye: Mtu yeyote anayesema kwamba ameungana na Mungu, anapaswa kuishi kama alivyoishi Yesu Kristo.
Baba wa Mbinguni tunaomba ukabariki kazi za mikono yetu
Biashara,masomo na vyote tunavyoenda kufanya/kutenda
Mungu wetu tukatende kama inavyokupendeza wewe..
Yahweh tunaomba ukabariki ridhiki zetu ziingiazo/zitokazo
Mungu wetu ukatupe nasi neema ya kuweza kuwabariki
wenye kuhitaji..
Mungu wetu tusipungukiwe katika mahitaji yetu
Baba wa Mbinguni ukatupe sawasawa na mapenzi yako..

Mfalme wa Amani tunaomba Amani yako ikatawale katika
Nyumba/ndoa zetu,watoto,wazazi wetu,familia/ndugu na wote
wanaotuzunguka,Mungu wetu pendo lako likadumu,furaha ikatawale
hekima na busara ziwe nasi,utuwema na fadhili visipungue
msamaha na kusamehe tunapokosa kuelewana tukaelimishane
kwa upendo na Amani,tuchukuliane na kuhurumiana..
Mungu wetu ukatupe Neema ya kusimamia Neno lako
Amri na Sheria zako siku zote za maisha yetu..
Ukatufanye chombo chema nasi tukatumike sawasawa na
mapenzi yako..


Wapenzi wangu, amri hii ninayowaandikieni si amri mpya; ni amri ileile ya zamani mliyokuwa nayo tangu mwanzo. Amri hiyo ya zamani ni ule ujumbe mliousikia. Hata hivyo, amri hii ninayowaandikieni ni amri mpya, na ukweli wake unaonekana ndani ya Kristo na ndani yenu pia. Maana giza linatoweka, na mwanga wa kweli umekwisha anza kuangaza. Yeyote asemaye kwamba yumo katika mwanga, lakini anamchukia ndugu yake, mtu huyo bado yumo gizani. Yeyote ampendaye ndugu yake yuko katika mwanga, na hamna chochote ndani yake kiwezacho kumkwaza mtu mwingine. Lakini anayemchukia ndugu yake yumo gizani; anatembea gizani, na hajui anakokwenda, maana giza limempofusha. Ninawaandikieni nyinyi watoto kwa kuwa dhambi zenu zimeondolewa kwa jina la Kristo. Nawaandikieni nyinyi kina baba kwani mnamjua yeye ambaye amekuwako tangu mwanzo. Nawaandikieni nyinyi vijana kwa sababu mmemshinda yule Mwovu. Nawaandikieni nyinyi watoto kwa sababu mnamjua Baba. Nawaandikieni nyinyi kina baba kwa kuwa mnamjua yeye ambaye amekuwako tangu mwanzo. Nawaandikieni nyinyi vijana kwa sababu mna nguvu; neno la Mungu limo ndani yenu na mumemshinda yule Mwovu. Msiupende ulimwengu, wala chochote kilicho cha ulimwengu. Mtu anayeupenda ulimwengu, upendo wa Baba hauwezi kuwamo ndani yake. Vitu vyote vya ulimwengu – tamaa mbaya za mwili, vitu wanavyoviona watu na kuvitamani, majivuno yasababishwayo na mali – vyote hivyo havitoki kwa Baba, bali vyatoka kwa ulimwengu. Ulimwengu pamoja na vitu vyake vyote vyenye kutamanika unapita; lakini mtu atendaye atakalo Mungu, anaishi milele.

Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi..

Baba wa Mbinguni tunaomba ukawaguse kwa mkono wako
wenye nguvu wote wanaopitia vikwazo,majaribu,shida/tabu
wagonjwa,wenye njaa,waliokatika vifungo mbalimbali
Mungu wetu ukawaponye kimwili na kiroho pia
wakapate tumaini jipya,amani na wakasimame tena
ukawape neema ya kuweza kujiombea,kutambua/kujitambua
na kufuata nja zako nazo ziwaweke huru..


Watoto, mwisho u karibu! Mlikwisha sikia kwamba mpinzani wa Kristo anakuja, na sasa wapinzani wengi wa Kristo wamekwisha fika, na hivyo twajua kwamba mwisho u karibu. Watu hao wametokea kati yetu lakini hawakuwa kweli wa kwetu na ndiyo maana walituacha; kama wangalikuwa wa kwetu, wangalibaki nasi. Lakini waliondoka, wakaenda zao, kusudi ionekane wazi kwamba hawakuwa kamwe wa kwetu. Nyinyi, lakini, mlipata kumiminiwa Roho Mtakatifu na Kristo, na hivyo mnaujua ukweli. Basi, nawaandikieni, si kwa kuwa hamwujui ukweli, bali kwa sababu mnaujua; na pia mnajua kwamba uongo wowote haupatikani katika ukweli. Mwongo ni nani? Ni yule anayekana kwamba Yesu ni Kristo. Mtu wa namna hiyo ni mpinzani wa Kristo – anamkana Baba na Mwana. Maana yeyote anayemkana Mwana, anamkana pia Baba; na yeyote anayemkubali Mwana, anampata Baba pia. Basi, ujumbe ule mliousikia tangu mwanzo na ukae mioyoni mwenu. Kama ujumbe huo mliousikia tangu mwanzo ukikaa ndani yenu, basi, mtaishi daima katika umoja na Mwana na Baba. Na ahadi aliyotuahidia sisi ndiyo hii: Uhai wa milele. Nimewaandikieni mambo haya kuhusu wale wanaotaka kuwapotosha nyinyi. Lakini, kwa upande wenu nyinyi, Kristo aliwatia mafuta kwa Roho wake. Na kama Roho huyo akiendelea kukaa ndani yenu, hamhitaji kufundishwa na mtu yeyote. Maana yeye anawafundisheni kila kitu, na mafundisho yake ni ya kweli, si ya uongo. Basi, shikeni mafundisho ya huyo Roho na kubaki katika muungano na Kristo. Naam, watoto, kaeni ndani yake kusudi wakati atakapotokea tuwe hodari bila kuwa na sababu ya kujificha kwa aibu siku ya kuja kwake.

Asante Mungu wetu yote tunayaweka mikononi mwako
Tukishukuru na kuamini Mungu wetu u pamoja nasi..
Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele..
Amina..!
Wapendwa katika Bwana niwatakiwe Amani ya Bwana..
iwe nanyi,Baraka na upendo wa Kristo uwe nanyi
muingiapo/mtokapo Mungu awe nanyi daima..
Nawapenda.


Mungu anamwamuru Yoshua kuiteka nchi ya Kanaani

1Baada ya kifo cha Mose, mtumishi wa Mwenyezi-Mungu, Mwenyezi-Mungu alimwambia Yoshua mwana wa Nuni, mtumishi wa Mose: 2“Mtumishi wangu Mose amefariki, sasa vukeni mto Yordani, wewe pamoja na Waisraeli wote hadi kwenye nchi ile ambayo ninawapa. 3Kila mahali mtakapokanyaga nimewapeni kama nilivyomwahidi Mose. 4Mipaka ya nchi yenu itakuwa hivi: Kusini ni jangwa, kaskazini ni milima ya Lebanoni, mashariki ni mto ule mkubwa Eufrate, kupitia nchi yote ya Wahiti hadi bahari ya Mediteranea upande wa magharibi. 5Hakuna mtu atakayekushinda siku zote za maisha yako. Nitakuwa pamoja nawe kama nilivyokuwa pamoja na Mose. Daima nitakuwa nawe wala sitakuacha kamwe. 6Uwe imara na hodari kwa kuwa wewe utawaongoza watu hawa kuirithi nchi ambayo niliwaahidi wazee wao kuwa nitawapa. 7Ila tu, uwe imara na hodari; uwe mwangalifu na kuzingatia sheria yote aliyokuamuru mtumishi wangu Mose. Fuata kila sehemu ya sheria hiyo nawe utafanikiwa popote uendapo. 8Hakikisha kuwa hutakisahau kamwe kitabu hiki cha sheria; bali kila siku utajifunza kitabu hiki, mchana na usiku, ili upate kutekeleza yote yaliyoandikwa humu, nawe utafanikiwa na kustawi popote uendapo. 9Kumbuka kuwa mimi nimekuamuru uwe imara na hodari. Usiogope wala usifadhaike kwa kuwa mimi Mwenyezi-Mungu, Mungu wako, niko pamoja nawe popote uendapo.”

Yoshua anawatayarisha watu kuvuka mto Yordani

10Kisha Yoshua akawaamuru viongozi wa watu, 11“Piteni katika kambi na kuwaamrisha watu watayarishe chakula, kwa kuwa baada ya siku tatu mtavuka mto Yordani, kwenda kuimiliki nchi ambayo Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu anawapeni iwe mali yenu.”
12 Taz Hes 32:28-32; Kumb 3:18-20; Yosh 22:1-6 Yoshua akawaambia watu wa kabila la Reubeni na Gadi na nusu ya kabila la Manase: 13“Kumbukeni lile jambo ambalo Mose, mtumishi wa Mwenyezi-Mungu, aliwaamuru akisema, ‘Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, atawapa mahali pa kupumzika, na atawapa nchi hii’. 14Wake zenu, watoto wenu na wanyama wenu wa kufugwa watabaki katika nchi hiyo ambayo Mose aliwapeni, ngambo ya mto Yordani. Lakini wanaume wote hodari wakiwa na silaha watavuka mto na kuwatangulia ndugu zenu. 15Mtawasaidia mpaka Mwenyezi-Mungu atakapowapa ndugu zenu pia mahali pa kupumzikia, kama alivyowapa nyinyi, nao pia wamiliki nchi ambayo wanapewa na Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu. Kisha mtarudi katika nchi ambayo ni mali yenu na kuimiliki, nchi ambayo mlipewa na Mose, mtumishi wa Mwenyezi-Mungu, mashariki ya mto Yordani.”
16Wakamjibu Yoshua, “Mambo yote uliyotuamuru tutayafanya, na popote utakapotutuma tutakwenda. 17Kama vile tulivyomtii Mose katika mambo yote, ndivyo tutakavyokutii wewe; Mwenyezi-Mungu, Mungu wako na awe pamoja nawe kama alivyokuwa pamoja na Mose. 18Mtu yeyote atakayeasi amri yako au kukataa kutii maneno yako au jambo lolote unalomwamuru, atauawa. Wewe, lakini, uwe na nguvu na kuwa hodari.”

Yoshua 1;1-18

Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)

"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.

No comments: