Swahili na Waswahili

Swahili na Waswahili
Waswahili na Mswahili Rachel Siwa...Pamoja Daima!!

Monday 29 May 2017

Kikombe Cha Asubuhi;Mambo Ya Walawi..2...


Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje Wapendwa/Waungwana?
Tumshukuru Mungu wetu kwa wema na Fadhili zake..
Asante Baba wa Mbinguni, Mungu wetu, Baba yetu, Muumba wetu,Muumba wa Mbingu na Nchi na Vyote vilivyomo,Mungu wa Abrahamu,Isaka na Yakobo..


Asante Kwa ulinzi wako na kutuamsha salama..
Asante kwakutuchagua na kutupa kibali cha kuendelea kuiona siku/wiki hii..


Tazama Jana imepita Baba Leo ni Siku mpya na Kesho ni siku Nyingine Jehovah..
Tunakuja Mbele zako tukijinyenyekeza na kujiachilia mikononi mwako Yahweh..!
Tunaomba utusamehe pale tulipokwenda kinyume nawe kwa kuwaza,kwakunena,kwakutenda,kwakujua/kutojua..
Tunaomba  Mungu wetu nasi utupe Neema ya kuweza kuwasamehe waliotukosea..
Roho mtakatifu akatuongoze kwenye kunena na kutenda Baba wa Mbinguni tukawe na kiasi..
Ututakase Miili yetu na Akili zetu Jehovah na tupate kutambua/kujitambua..
Ukatuepushe na hila zote za Mwovu na kazi zake..
Utuokoe na kutufunika na Damu ya Mwanao Mpendwa Bwana wetu na Mwokozi wetu Yesu Kristo wa Nazareti..

Mfalme wa Amani tunaiweka Siku/wiki hii na maisha yetu mikononi mwako..Tunaomba ukaibariki na kutubariki katika yote tunayoenda kutenda/kufanya tukafanye sawasawa na mapenzi yako..
Ukabariki ridhiki zetu ziingiazo/zitokazo nasi ukatupe Neema ya kuwabariki  wenye kuhitaji..
Ukatuongoze ee Mungu wetu na Tukawe chombo chema na tukatumike sawasawa na mapenzi yako..

Tazama wenye shida/Tabu Wagonjwa,Wafiwa ukawe mfariji wao,waliokata tamaa,Waliokataliwa,wenye hofu/mashaka na wote waliokatika vifungo mbalimbali Baba wa Mbinguni tunaomba ukawaguse na mkono wako wenye nguvu ukawaponyae na kuwaokoa,wakapate kupona kimwili na kiroho pia..Baba ukaonekane kwenye magumu/mapito yao..


Baba wa Mbinguni ukatupe Hekima, Busara na ufahamu katika kuongoza Familia zetu,Nyumba zetu na tukaambatane na walio wako..
Rafiki mwema anatoka kwako,Jirani mwema anayetoka kwako..yeyote anayetukaribia kwenye maisha yetu Baba wa mbinguni tunaomba awe wako.. sisi hukaribisha kila mtu Baba lakini ukatupe macho ya kuona ukatupe Neema ya kutambua na kujitambua katika mahusiano yetu..

Wapendwa tumkabidhi Mungu mahusiano/familia  zetu,Si wote wanaopenda kuona watoto wako wanafanya vyema,si kila rafiki anapenda kuona nyumba yako inasimama, si kila jirani niwakuombana chumvi,si kila anayekuchekea anacheka kutoka moyoni..si kila anayesema Mungu/Bwana na anamoyo safi..


[Mama yangu alikuwa anatuambia Nyumba njema si mlango..]

[waswahili wa leo wanasema Jiongeze...Hahahaha..!]

Kuishi katika mwanga

Kwa hiyo, mwigeni Mungu, maana nyinyi ni watoto wake wapenzi. Upendo uongoze maisha yenu kama vile Kristo alivyotupenda, na kwa ajili yetu akajitoa mwenyewe kama tambiko yenye harufu nzuri na sadaka impendezayo Mungu. Kwa vile nyinyi ni watu wa Mungu, basi uasherati, uchafu wowote ule au choyo visitajwe kamwe miongoni mwenu. Tena maneno ya aibu, ya upuuzi au ubishi, yote hayo hayafai kwenu; maneno ya kumshukuru Mungu ndiyo yanayofaa. Jueni wazi kwamba mwasherati yeyote au mchafu au mchoyo, (ambao ni sawa na kuabudu sanamu), au mtu yeyote wa aina hiyo hataambulia chochote katika ufalme wa Kristo na wa Mungu. Msikubali kudanganywa na mtu kwa maneno matupu; maana, kwa sababu ya mambo kama hayo ghadhabu ya Mungu huwajia wote wasiomtii. Basi, msishirikiane nao. Zamani nyinyi mlikuwa gizani, lakini sasa nyinyi mko katika mwanga kwa kuungana na Bwana. Ishini kama watoto wa mwanga, maana matokeo ya mwanga ni wema kamili, uadilifu na ukweli. Jaribuni kujua yale yanayompendeza Bwana. Msishiriki katika matendo yasiyofaa ya giza, bali yafichueni. Mambo yanayotendwa kwa siri ni aibu hata kuyataja. Lakini kila kitu kikifichuliwa na mwanga, ukweli wake hudhihirishwa; na kila kilichodhihirishwa huwa mwanga. Ndiyo maana Maandiko yasema: “Amka wewe uliyelala, fufuka kutoka kwa wafu, naye Kristo atakuangaza.” Basi, muwe waangalifu jinsi mnavyoishi. Msiishi kama wapumbavu, bali kama wenye hekima. Tumieni vizuri muda mlio nao maana siku hizi ni mbaya. Kwa hiyo, msiwe wapumbavu, bali jaribuni kujua matakwa ya Bwana. Acheni kulewa divai maana hiyo itawaangamiza, bali mjazwe Roho Mtakatifu. Zungumzeni kwa maneno ya Zaburi, nyimbo na tenzi za kiroho; mwimbieni Bwana nyimbo na Zaburi kwa shukrani mioyoni mwenu. Mshukuruni Mungu Baba daima kwa ajili ya yote, kwa jina la Bwana wetu Yesu Kristo.
Asante Mungu wetu..tunayaweka haya yote mikononi mwako..
kwakua Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu Hata Milele..
Amina..!!
Asanteni sana wote mnaopita hapa..
Mungu akawabariki katika yote..
Akawape sawasawa na mapenzi yake..
Nawapenda.


Sadaka za nafaka
1“Mtu yeyote akileta sadaka ya nafaka kwa Mwenyezi-Mungu, sadaka hiyo iwe ya unga laini. Atautia mafuta na ubani. 2Kisha, atawaletea hao makuhani wa ukoo wa Aroni. Atachukua konzi moja ya unga huo laini wenye mafuta na ubani na kumpelekea kuhani mmojawapo ambaye atauteketeza juu ya madhabahu uwe sadaka ya ukumbusho kwa Mwenyezi-Mungu. Hiyo ni sadaka ya kuteketezwa kwa moto yenye harufu nzuri ya kumpendeza Mwenyezi-Mungu. 3Sehemu inayobaki ya sadaka hiyo ni ya makuhani. Hiyo ni sehemu takatifu kabisa ya sadaka anayotolewa Mwenyezi-Mungu kwa moto.
4“Kama mtu anamtolea Mungu sadaka ya nafaka iliyookwa jikoni, hiyo itakuwa ya mikate isiyotiwa chachu ya unga laini uliochanganywa na mafuta ya zeituni, au ya mikate myembamba isiyo na chachu na isiyopakwa mafuta. 5Iwapo sadaka unayotoa ni ya mkate uliookwa kwenye kikaango, hiyo itakuwa ya unga laini uliochanganywa na mafuta ya zeituni lakini bila chachu. 6Mikate hiyo itakatwakatwa na kumiminiwa mafuta; hiyo ni sadaka ya nafaka. 7Kama sadaka unayotoa ni ya mikate iliyopikwa katika sufuria, hiyo itakuwa ya unga laini na imetiwa mafuta. 8Utaleta sadaka ya nafaka iliyotengenezwa kwa vitu hivyo mbele ya Mwenyezi-Mungu; na kuhani ataipeleka kwenye madhabahu. 9Kuhani atachukua sehemu ya sadaka hiyo ikiwa ni sadaka ya ukumbusho na kuiteketeza juu ya madhabahu. Hiyo ni sadaka ya kuteketezwa kwa moto yenye harufu nzuri ya kumpendeza Mwenyezi-Mungu. 10Sehemu inayobaki ya sadaka ya nafaka, ni ya makuhani. Hiyo ni sehemu takatifu kabisa ya sadaka inayotolewa Mwenyezi-Mungu kwa moto.
11“Sadaka yoyote ya nafaka utakayomletea Mwenyezi-Mungu ni lazima iwe imetengenezwa bila chachu; kwani hakuna ruhusa kamwe kutumia chachu wala asali katika sadaka anazotolewa Mwenyezi-Mungu kwa moto. 12Unaweza kumletea Mwenyezi-Mungu mazao yako ya kwanza kama sadaka. Lakini hayo hayatatolewa madhabahuni kama harufu ya kumpendeza. 13Utakoleza sadaka zako zote za nafaka kwa chumvi. Kamwe usiache kuweka chumvi katika sadaka yako ya nafaka, kwani chumvi ni ishara ya agano alilofanya Mungu pamoja nanyi.
14“Ukimtolea Mwenyezi-Mungu sadaka ya mazao yako ya kwanza utaitoa hiyo ikiwa imechomwa katika masuke yake, au utaitoa katika mikate ya kuokwa iliyotengenezwa kwa ngano iliyosagwa. 15Utaitia mafuta na kuweka ubani; hiyo ni sadaka ya nafaka. 16Kuhani ataiteketeza sehemu ya sadaka hiyo ya nafaka iliyopondwa na mafuta pamoja na ubani wake wote, iwe sadaka ya ukumbusho; hiyo ni sadaka anayotolewa Mwenyezi-Mungu kwa moto.

Mambo Ya Walawi 2;1-16


Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)

"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.

No comments: