Swahili na Waswahili

Swahili na Waswahili
Waswahili na Mswahili Rachel Siwa...Pamoja Daima!!

Monday 15 May 2017

Kikombe Cha Asubuhi;Kutoka 32...


Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje Wapendwa/Waungwana?
Tumshukuru Mungu katika yote...
Mtakatifu..!Mtakatifu..!Mtakatifu..! Baba wa Mbinguni, Baba yetu,Mungu wetu, Muumba wetu, Muumba mbingu na Nchi, Na vyote vilivyomo, Mungu wa Abrahamu, Isaka na Yakobo..

Asante kwa wema na fadhili zako,Asante kwa  ulinzi wako usiku mzima na kutuamsha salama, Asante kwa kutuchagua  na kutupa kibali cha kuendelea kuiona Wiki/siku hii..
si kwa uwezo wetu, Nguvu zetu/utashi wetu, si kwamba sisi ni wema sana na tumetenda mazuri sana, si kwamba sisi ni wajuaji na wenye sifa zote, si kwamba sisi ni wazuri mno.. Hapana Baba wa Mbinguni ni kwa Neema/Rehema zako tuu sisi kuendelea kuiona leo hii..


Tunakuja mbele zako tukijinyenyekeza na kujiachilia mikononi mwako Baba wa Mbinguni, Tunaomba utusamehe pale tulipokwenda kinyume nawe kwa kuwaza,kwakunena, kwakutenda, kwakujua/kutojua..

Baba tunaomba utupe nasi Neema ya kuweza kuwasamehe waliotukosea na kuachilia kabisa..
Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi..
Ukatupe kutambua na kujitambua..
Tazama Jana imepita Yahweh..! Leo ni siku mpya na Kesho ni siku nyingine..Mfalme wa Amani tunaomba ukatawale maisha yetu,Ukabariki ridhiki zetu ziingiazo na zitokazo nasi tukaweze kuwabariki wengine wenye kuhitaji..
Ukabariki kuingia kwetu na kutoka kwetu, vyombo vya usafiri na tutembeapo hatua zetu ziwe nawe..
Ukabariki Kazi zetu,Biashara, Masomo na ukabariki vilaji/vinywaji na vyote tunavyoenda kugusa/kutumia Jehovah ukavitakase kwa Damu ya mwanao mpendwa Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo wa Nazareti..


Ukatutakase Miili yetu na Akili zetu... Ukatamalaki na ukaonekane katika maisha yetu..
Ukatuokoe na kutulinda na yule mwovu na kazi zake, ukatufunike na Damu ya Bwana wetu Yesu Kristo,Ukatuponye rohoni Baba wa Mbinguni na tukawe barua njema tukasomoke sawasawa na mapenzi yako..


Ukabariki familia zetu na tunaziweka Ndoa zetu mikononi mwako Mfalme wa Amani...
Ukawabariki Yatima na Wajane Mfalme wa Amani na ukawabariki na kuwakugusa na mkono wako wenye nguvu wote wanaopitia magumu/majaribu,vifungo mbalimabali,wagonjwa, wafiwa ukawe mfariji wao..
Baba tazama waliokata tamaa, wenye hofu/mashaka,waliokataliwa na waliokwama katika maisha yao, maisha  hayaendi iwe kazi, iwe masomo,Biashara,watoto watukutu/hawasikii, Amani kwenye nyumba/maisha yao imepotea..Baba ukawape kupona kiroho na ukawaongoze na wakapate tumaini na ukaonekane kwenye maisha yao ukawaonyeshe njia..
Ndugu yangu unayepita kweye Magumu/Majaribu usisite kumpa Yesu maisha yako,mtafute Mungu anapatikana, Fanya bidii ya kumjua yeye naye atakuinua..


mkabidhi kazi zako, maisha yako,masomo yako na kabla ya kufanya vyote hivyo muulize Mungu unachofanya ndicho chako?yeye akakuongoze, fanya bidii katika unalolifanya na Mungu akawe kiongozi wako..

Mtafuteni Mwenyezi-Mungu wakati bado anapatikana, mwombeni msaada wakati yupo bado karibu. Waovu na waache njia zao mbaya, watu wabaya waachane na mawazo yao mabaya; wamrudie Mwenyezi-Mungu apate kuwahurumia, wamwendee Mungu wetu maana atawasamehe. Maana, Mwenyezi-Mungu asema hivi: “Mawazo yangu si kama mawazo yenu, wala njia zangu si kama njia zenu. Kama vile mbingu zilivyo mbali na dunia, ndivyo njia zangu zilivyo mbali na zenu, na mawazo yangu mbali na mawazo yenu. “Kama vile mvua na theluji ishukavyo toka mbinguni, wala hairudi huko bali huinywesha ardhi, ikaifanya ichipue mimea ikakua, ikampatia mpanzi mbegu na kuwapa watu chakula, vivyo hivyo na neno langu mimi: Halitanirudia bila mafanikio, bali litatekeleza matakwa yangu, litafanikiwa lengo nililoliwekea.

Tunakushuru Mungu wetu na tunayaweka haya yote mikononi mwako..
tukiamini na kukusifu daima..
Amina..!!
Niwashukuru wote mnaopita hapa..
Mungu aendelee kuwabariki na kuwatendea makuu,
Nawapenda.

Sanamu ya ndama wa dhahabu

(Kumb 9:6-29)

1 Taz Mate 7:40,41; 1Fal 12:28 Watu walipoona kuwa Mose amechelewa kurudi kutoka mlimani, walikusanyika mbele ya Aroni na kumwambia, “Haya! Tutengenezee miungu itakayotuongoza maana hatujui lililompata huyo Mose aliyetutoa nchini Misri.” 2Aroni akawajibu, “Chukueni vipuli vya dhahabu masikioni mwa wake zenu, wana wenu na binti zenu, mniletee.” 3Basi, watu wote wakatoa vipuli vyote vya dhahabu masikioni mwao, wakamletea Aroni. 4Naye akavichukua akaviyeyusha, akatengeneza ndama wa kusubu. Watu wakapaza sauti, “Ee Israeli, huyu ndiye mungu wetu aliyetutoa nchini Misri.”
5Kisha Aroni akamjengea huyo ndama madhabahu, halafu akatangaza, “Kesho kutakuwa na sikukuu kwa ajili ya Mwenyezi-Mungu.” 6Taz 1Kor 10:7 Kesho yake watu waliamka mapema wakatoa sadaka za kuteketezwa, na sadaka za amani. Watu wakaketi chini kula na kunywa; kisha wakasimama na kucheza.
7Mwenyezi-Mungu akamwambia Mose, “Teremka chini kwa maana watu wako uliowaleta kutoka nchini Misri wamejipotosha wenyewe; 8wameiacha mara moja njia niliyowaamuru, wakajifanyia ndama wa kusubu, nao wamemwabudu na kumtolea tambiko wakisema, ‘Ee Israeli, huyu ndiye mungu wetu aliyetutoa nchini Misri!’ 9Nawafahamu watu hawa; wao wana vichwa vigumu. 10Sasa, usijaribu kunizuia. Niache niwaangamize kwa ghadhabu kali; kisha kutokana nawe nitaunda taifa kubwa.”
11 Taz Hes l4:13-19 Lakini Mose akamsihi Mwenyezi-Mungu, Mungu wake, akisema, “Ee Mwenyezi-Mungu, kwa nini hasira yako inawaka vikali dhidi ya watu wako uliowatoa nchini Misri kwa uwezo mkuu na mkono wenye nguvu? 12Ukifanya hivyo, hakika Wamisri watasema, ‘Aliwatoa kwa nia mbaya ili kuwaulia mlimani na kuwateketeza kabisa duniani.’ Ee Mwenyezi-Mungu, tuliza hasira yako kali na kuacha jambo hilo baya ulilokusudia kufanya dhidi ya watu wako. 13Taz Mwa 22:16-17; 17:8 Wakumbuke watumishi wako, Abrahamu, Isaka na Israeli, ambao uliwaapia kwa nafsi yako mwenyewe, ukisema, ‘Nitawazidisha wazawa wenu kama nyota za mbinguni na nchi yote hii niliyowaahidia nitawapa vizazi vyenu wairithi milele.’” 14Basi, Mwenyezi-Mungu akaacha kuwafanyia watu wake lile jambo baya alilokuwa amesema.
15Kisha Mose akashuka kutoka mlimani akiwa na vibao viwili vya mawe mikononi mwake, vimeandikwa amri za Mungu pande zote. 16Vibao hivyo vilikuwa kazi yake Mungu mwenyewe na maandishi hayo aliyachora Mungu mwenyewe.
17Yoshua aliposikia kelele za watu, akamwambia Mose, “Kuna kelele za vita kambini.” 18Lakini Mose akamjibu, “Si kelele ya ushindi au kushindwa, bali kelele ninayosikia ni kelele ya watu wanaoimba.” 19Mara tu walipoikaribia kambi walipomwona yule ndama na watu wakicheza; hapo hasira ya Mose ikawaka kama moto, akavitupa chini vile vibao kutoka mikononi mwake na kuvivunja pale chini ya mlima. 20Basi, akamchukua yule ndama akamchoma moto, akamsaga mpaka akawa unga, akaukoroga unga huo katika maji na kuwalazimisha Waisraeli wanywe.
21Mose akamwuliza Aroni, “Walikufanya nini watu hawa hata ukawaingiza katika dhambi kubwa hivyo?” 22Aroni akamjibu, “Nakuomba ee bwana wangu hasira yako isiniwakie mimi mtumishi wako. Unawafahamu jinsi watu hawa walivyo tayari kutenda maovu. 23Walikuja wakaniambia, ‘Tufanyie miungu ambayo itatuongoza kwani huyo Mose aliyetutoa nchini Misri hatujui lililompata’. 24Nami nikawaambia, kila mmoja aliye na vito vya dhahabu na avilete. Basi, wakaniletea, nami nikaviyeyusha motoni na huyu ndama akatokea.”
25Basi, Mose alipoona kuwa watu wameasi na kufanya wapendavyo (kwa kuwa Aroni aliwafanya waasi na kufanya wapendavyo, na kujiletea aibu mbele ya adui zao), 26Mose akasimama mbele ya lango la kambi na kuuliza, “Ni nani aliye upande wa Mwenyezi-Mungu? Na aje kwangu.” Wana wote wa Lawi wakakusanyika pamoja mbele yake. 27Akawaambia, “Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli, anasema hivi: ‘Kila mtu na ajifunge upanga wake kiunoni, azunguke kila mahali kambini, kutoka lango moja hadi lingine, na kila mmoja amuue ndugu yake, rafiki yake na jirani yake.’” 28Wana wa Lawi wakafanya kama Mose alivyowaagiza. Siku hiyo waliuawa watu wapatao 3,000. 29Mose akasema, “Leo mmejiweka wakfu32:29 Leo … wakfu: Makala ya Kiebrania: Jiwekeni wakfu leo au Mmewekwa wakfu leo. nyinyi wenyewe kumhudumia Mwenyezi-Mungu, kwa vile hamkusita hata kuwaua watoto wenu au ndugu zenu. Mungu awajalie baraka leo hii.”

Mose anawaombea Waisraeli

30Kesho yake Mose akawaambia watu, “Mmetenda dhambi kubwa! Sasa nitamwendea Mwenyezi-Mungu juu mlimani; labda nitafanya upatanisho kwa ajili ya dhambi yenu.” 31Hivyo Mose akarudi kwa Mwenyezi-Mungu, akamwambia, “Nasikitika! Watu hawa wametenda dhambi kubwa; wamejifanyia wenyewe miungu ya dhahabu. 32Taz Zab 69:28; Ufu 3:5 Lakini sasa, nakuomba uwasamehe dhambi yao. Ikiwa hutawasamehe, nakusihi unifute mimi katika kitabu chako ulichowaandika watu wako.” 33Lakini Mwenyezi-Mungu akamwambia Mose, “Nitamfuta katika kitabu changu mtu yeyote aliyenitendea dhambi. 34Lakini sasa nenda ukawaongoze watu mpaka mahali nilipokuambia. Tazama, malaika wangu atakutangulia. Hata hivyo, siku nitakapowajia, nitawaadhibu kwa sababu ya dhambi yao.”
35Mwenyezi-Mungu akawapelekea watu ugonjwa wa tauni, kwa kuwa walimwomba Aroni awafanyie yule ndama wa dhahabu.
Kutoka32;1-35


Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)

"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.

No comments: