Swahili na Waswahili

Swahili na Waswahili
Waswahili na Mswahili Rachel Siwa...Pamoja Daima!!

Tuesday 15 June 2021

Kikombe Cha Asubuhi; Tunamshukuru Mungu kwa kumaliza Kitabu cha Waebrania Leo Tunaanza Kitabu cha Yakobo....1


Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?

Tunamshukuru Mungu kwa kutupa kibali cha
 kupitia kitabu cha "Waebrania
"
Ni matumaini yangu kuna mengi tumejifunza/kufaidika
na kutupa mwanga/kuelewa kwenye kitabu hiki...

Leo tunapokwenda anza kupitia Kitabu cha"Yakobo"
tunamuomba Mungu wetu akatupe kibali,macho ya rohoni
 na akili ya kuelewa katika kujifunza NENO lake...
Ee Mungu  tunaomba ukatuongoze...!!
Tumshukuru Mungu wetu katika yote...

Mungu wetu Baba yetu,Muumba wetu Muumba wa Mbingu na Nchi
Muumba wa vyote vilivyomo vinavyoonekana na visivyoonekana
Mungu wa walio hai,Mungu  mwenye huruma,Mungu wa upendo
Mungu wa Abrahamu,Isaka na Yakobo...


Asante kwa wema na fadhili zako kwetu
Asante kwa ulinzi wako kwetu wakati wote
Asante kwa kutuchagua tena na kutupa
kibali cha kuendelea kuiona leo hii
Asante kwa pumzi/uzima,afya na kuwatayari kwa majukumu yetu

Neema yako yatutosha ee Mungu wetu....!!

“Kisha hapo baadaye nitaimimina roho yangu juu ya binadamu wote. Watoto wenu wa kike na wa kiume watatabiri, wazee wenu wataota ndoto, na vijana wenu wataona maono.

Yoeli 2:28

Baba wa Mbinguni tunakuja mbele zako,
Tukijinyenyekeza,tukijiachilia mikononi mwako
Mungu wetu tunamomba utusamehe dhambi zetu
Baba wa Mbinguni nasi tunaomba ukatupe neema
 ya kuweza kuwasamehe wale wote waliotukosea

Usitutie majaribuni Mungu wetu tunaomba utuepushe
na yule mwovu na kazi zake zote
Jehovah ututakase miili yetu na akili zetu
Baba wa Mbinguni tunaomba utufunike kwa Damu
ya Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo wa Nazareti
yeye aliteseka kwanza ili sisi tupate kupona...

Hata juu ya watumishi wa kiume na wa kike, nitaimimina roho yangu wakati huo. “Nitatoa ishara mbinguni na duniani; kutakuwa na damu, moto na minara ya moshi.

Yoeli 2:29-30

Yahweh tunayaweka maisha yetu mikononi mwako
Mungu wetu tunaomba ukabariki nyumba/ndoa zetu,
Jehovah tunaomba ulinzi wako kwetu na kwa vyote tunavyovimiliki
Yahweh tunaomba ukatubariki tuingiapo/tutokapo
Mungu wetu tunaomba ukavibariki vyote tunavyoenda kugusa/kutumia
Baba wa Mbinguni ukavitakase kwa Damu ya Bwana wetu Yesu Kristo
Mungu wetu ukatamalaki na kutuatamia
Baba wa Mbinguni tukawe salama rohoni
Yahwe ukatupe akili ya kutambua mema na mabaya
Mfalme wa amani amani yako ikatawale katika maisha yetu
Mungu wetu ukatupe macho ya kuona,masikio ya kusikia sauti yako na kuitii..
Baba wa Mbinguni  tunaomba ukatupe neema ya kufuata
njia zako,tukasimamie Neno lako,amri na sheria zako
siku zote za maisha yetu...
Ukatuguse kwa mkono wako wenye nguvu,ukatufanye chombo chema
ee Mungu wetu nasi tukatumike kama inavyokupendeza wewe
Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi....

Jua litatiwa giza, na mwezi utakuwa mwekundu kama damu, kabla ya kufika siku ya Mwenyezi-Mungu, siku iliyo kuu na ya kutisha. Hapo watu wote watakaoomba kwa jina la Mwenyezi-Mungu wataokolewa. Maana katika mlima Siyoni na Yerusalemu, watakuwako watu watakaosalimika, kama nilivyosema mimi Mwenyezi-Mungu.

Yoeli 2:31-32

Tazama watoto wako wenye shida/tabu,wote wanaopitia magumu/majaribu mbalimbali
Mungu wetu tunaomba ukawaguse kwa mkono wako wenye nguvu
kila mmoja na mahitaji yake
Mungu wetu tunaomba ukawasamehe pale walipo kwenda kinyume nawe
Yahweh tunaomba ukawape neema ya kuweza kujiombea,kufuata njia zako nazo zikawaweke huru...
Baba wa Mbinguni tunayaweka haya yote mikononi mwako
Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele...
Amina...!!


Asanteni sana wapendwa katika Kristo Yesu kwakuwa nami,
Baba wa Mbinguni aendelee kuwatendea sawasawa na mapenzi yake...
Nawapenda.

 Salamu

1Mimi Yakobo, mtumishi wa Mungu na wa Bwana Yesu Kristo, nawaandikia nyinyi, makabila kumi na mawili, yaliyotawanyika ulimwenguni! Salamu!
Imani na hekima
2Ndugu zangu, muwe na furaha mnapopatwa na majaribu mbalimbali, 3kwani mwajua kwamba imani yenu ikisha stahimili, itawapatieni uvumilivu. 4Muwe na hakika kwamba uvumilivu wenu utawategemeza mpaka mwisho, mpate kuwa wakamilifu na watimilifu, bila kupungukiwa chochote. 5Lakini kama mmoja wenu ametindikiwa hekima, basi, anapaswa kumwomba Mungu ambaye atampatia; kwani Mungu huwapa wote kwa wingi na kwa ukarimu. 6Lakini anapaswa kuomba kwa imani bila mashaka yoyote. Mtu aliye na mashaka ni kama mawimbi ya bahari ambayo husukumwa na kutupwatupwa na upepo. 7,8Kwa hiyo mtu aliye na mashaka, mwenye nia mbili na asiye na msimamo katika mwenendo wake wote, asidhani ya kwamba atapata chochote kile kutoka kwa Bwana.
Umaskini na utajiri
9Ndugu aliye maskini anapaswa kufurahi wakati Mungu anapomkweza, 10naye tajiri anapaswa kufurahi anaposhushwa na Mungu. Maana tajiri atatoweka kama ua la porini. 11Jua huchomoza na kwa joto lake kali hukausha mimea, nayo maua yake huanguka, na uzuri wake wote huharibika. Vivyo hivyo, tajiri ataangamizwa katika shughuli zake.
Majaribio
12Heri mtu anayebaki mwaminifu katika majaribu, kwani akisha stahimili, atapewa tuzo la uhai ambalo Mungu aliwaahidi wale wanaompenda. 13Kama mtu akijaribiwa, asiseme: “Ninajaribiwa na Mungu.” Maana Mungu hawezi kujaribiwa na uovu, wala yeye hamjaribu mtu yeyote. 14Lakini mtu hujaribiwa anapovutwa na kunaswa na tamaa zake mbaya. 15Tamaa ikiiva huzaa dhambi; nayo dhambi ikikomaa huzaa kifo.
16Ndugu zangu wapenzi, msidanganyike! 17Kila kipaji chema na kila zawadi kamilifu hutoka mbinguni; hutoka kwa Baba, Muumba wa mianga, ambaye habadiliki wala hana alama yoyote ya ugeugeu. 18Kwa kupenda kwake mwenyewe alituzaa kwa neno lake la ukweli, ili tuwe katika nafasi ya kwanza miongoni mwa viumbe vyake.
Kusikia na kutenda
19Ndugu zangu wapenzi, kumbukeni jambo hili! Kila mtu na awe mwepesi wa kusikia lakini si mwepesi wa kusema wala mwepesi wa kukasirika. 20Mwenye hasira hawezi kutimiza matakwa ya Mungu yaliyo ya haki. 21Kwa hiyo, tupilieni mbali mwenendo mchafu na tabia zote mbovu; jiwekeni chini ya Mungu na kupokea lile neno lililopandwa mioyoni mwenu, ambalo laweza kuziokoa nafsi zenu.
22Msijidanganye wenyewe kwa kusikiliza tu neno lake, bali litekelezeni kwa vitendo. 23Yeyote anayesikiliza hilo neno lakini halitekelezi, huyo ni kama mtu anayejiangalia sura yake mwenyewe katika kioo. 24Hujiangalia mwenyewe, kisha huenda zake, na mara husahau jinsi alivyo. 25Lakini mtu anayeangalia kwa makini sheria kamilifu ambayo huwapa watu uhuru, mtu anayeendelea kuizingatia, na si kuisikia tu na kuisahau baadaye, bali anaitekeleza, mtu huyo atabarikiwa katika kila kitu anachofanya.
26Kama mtu akijiona kuwa ni mtu mwenye dini, lakini hawezi kuutawala ulimi wake, dini yake haifai kitu, na anajidanganya mwenyewe. 27Dini iliyo safi na isiyo na hitilafu mbele ya Mungu Baba ni hii: Kuwasaidia yatima na wajane katika shida zao, na kujilinda mwenyewe usichafuliwe na ulimwengu huu.
Yakobo1;1-27
Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)
"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe

No comments: