Swahili na Waswahili

Swahili na Waswahili
Waswahili na Mswahili Rachel Siwa...Pamoja Daima!!

Wednesday 2 June 2021

Kikombe Cha Asubuhi; Kitabu cha Waebrania....5



Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?

Tumshukuru Mungu katika yote....

Mungu wetu Baba yetu,Muumba wetu Muumba wa Mbingu na Nchi
Muumba wa vyote vilivyomo vinavyoonekana na visivyoonekana
Mungu wa walio hai,Mungu  mwenye huruma,Mungu wa upendo
Mungu wa Abrahamu,Isaka na Yakobo...
Asante kwa wema na fadhili zako kwetu
Asante kwa ulinzi wako kwetu wakati wote
Asante kwa kutuchagua tena na kutupa
kibali cha kuendelea kuiona leo hii
Asante kwa pumzi/uzima,afya na kuwatayari kwa majukumu yetu

Neema yako yatutosha ee Mungu wetu...


Nchi yake ijae yote yaliyo mema, ibarikiwe kwa wema wa Mwenyezi-Mungu, ambaye alitokea katika kichaka. Baraka hizi ziwashukie watu wa kabila la Yosefu, aliyekuwa mkuu miongoni mwa ndugu zake.

Kumbukumbu la Sheria 33:16

Baba wa Mbinguni tunakuja mbele zako,
Tukijinyenyekeza,tukijiachilia mikononi mwako
Mungu wetu tunamomba utusamehe dhambi zetu
Baba wa Mbinguni nasi tunaomba ukatupe neema
 ya kuweza kuwasamehe wale wote waliotukosea

Usitutie majaribuni Mungu wetu tunaomba utuepushe
na yule mwovu na kazi zake zote
Jehovah ututakase miili yetu na akili zetu
Baba wa Mbinguni tunaomba utufunike kwa Damu
ya Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo wa Nazareti
yeye aliteseka kwanza ili sisi tupate kupona....

Fahari yake ni fahari ya fahali wa kwanza, pembe zake ni za nyati dume. Atazitumia kuyasukuma mataifa; yote atayasukuma mpaka miisho ya dunia. Efraimu atakuwa na pembe hizo 10,000 na Manase kwa maelfu.”

Kumbukumbu la Sheria 33:17

Mungu wetu tunaomba ukabariki kazi za mikono yetu
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe ubunifu na maarifa katika utendaji
Jehovah nasi tukatende sawasawa na mapenzi yako
Yahweh tunaomba ukabariki ridhiki zetu ziingiazo/zitokazo
Mungu wetu nasi tunaomna ukatupe neema ya kuweza kuwabariki wenye kuhitaji
Tusipungukiwe katika mahitaji yetu
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe kama inavyokupendeza wewe...


Yahweh tunayaweka maisha yetu mikononi mwako
Mungu wetu tunaomba ukabariki nyumba/ndoa zetu,
Jehovah tunaomba ulinzi wako kwetu na kwa vyote tunavyovimiliki
Yahweh tunaomba ukatubariki tuingiapo/tutokapo
Mungu wetu tunaomba ukavibariki vyote tunavyoenda kugusa/kutumia
Baba wa Mbinguni ukavitakase kwa Damu ya Bwana wetu Yesu Kristo
Mungu wetu ukatamalaki na kutuatamia
Baba wa Mbinguni tukawe salama rohoni
Yahwe ukatupe akili ya kutambua mema na mabaya
Mfalme wa amani amani yako ikatawale katika maisha yetu
Mungu wetu ukatupe macho ya kuona,masikio ya kusikia sauti yako na kuitii..
Baba wa Mbinguni  tunaomba ukatupe neema ya kufuata
njia zako,tukasimamie Neno lako,amri na sheria zako
siku zote za maisha yetu...
Ukatuguse kwa mkono wako wenye nguvu,ukatufanye chombo chema
ee Mungu wetu nasi tukatumike kama inavyokupendeza wewe
Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi....

Juu ya kabila la Zebuluni na kabila la Isakari, alisema, “Zebuluni, furahi katika safari zako; nawe Isakari, furahi katika mahema yako. Watawaalika wageni kwenye milima yao, na huko watu watatoa sadaka zinazotakiwa. Maana wao watapata utajiri wao kutoka baharini na hazina zao katika mchanga wa pwani.”

Kumbukumbu la Sheria 33:18-19

Tazama watoto wako wenye shida/tabu,wote wanaopitia magumu/majaribu mbalimbali
Mungu wetu tunaomba ukawaguse kwa mkono wako wenye nguvu
kila mmoja na mahitaji yake
Mungu wetu tunaomba ukawasamehe pale walipo kwenda kinyume nawe
Yahweh tunaomba ukawape neema ya kuweza kujiombea,kufuata njia zako nazo zikawaweke huru...
Baba wa Mbinguni tunayaweka haya yote mikononi mwako
Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele...
Amina...!!


Asanteni sana wapendwa katika Kristo Yesu kwakuwa nami,
Baba wa Mbinguni aendelee kuwatendea sawasawa na mapenzi yake...
Nawapenda.



 1Kila kuhani mkuu ambaye huchaguliwa miongoni mwa watu hupewa jukumu la kushughulikia mambo ya Mungu kwa niaba ya watu, kutolea zawadi na tambiko kwa ajili ya dhambi. 2Maadamu yeye mwenyewe ni dhaifu, anaweza kuwatendea kwa huruma wale wasiojua kitu na wanaofanya makosa. 3Kwa sababu hiyo anapaswa kutoa tambiko si tu kwa ajili ya watu, bali pia kwa ajili ya dhambi zake mwenyewe. 4Hakuna mtu awezaye kujifanya mwenyewe kuwa kuhani mkuu. Kila mmoja huteuliwa na Mungu kuwa kuhani mkuu kama alivyokuwa Aroni.

5 Taz Zab 2:7 Hali kadhalika naye Kristo; yeye hakujitwalia mwenyewe heshima ya kuwa kuhani mkuu, bali Mungu alimteua na kumwambia:
“Wewe ni Mwanangu;
mimi leo nimekuwa baba yako.”
6 Taz Zab 110:4 Alisema pia mahali pengine:
“Wewe ni kuhani milele,
kwa utaratibu wa ukuhani wa Melkisedeki.”
7Yesu alipokuwa anaishi hapa duniani, kwa kilio kikuu na machozi, alisali na kumwomba Mungu ambaye alikuwa na uwezo wa kumwokoa kifoni; naye alisikilizwa kwa sababu ya kumcha Mungu. 8Lakini, ingawa alikuwa Mwana wa Mungu, alijifunza kutii kwa njia ya mateso. 9Na alipofanywa mkamilifu, akawa chanzo cha wokovu wa milele kwa wote wanaomtii, 10naye Mungu akamteua kuwa kuhani mkuu kwa utaratibu wa ukuhani wa Melkisedeki.
Onyo kuhusu uasi
11Tunayo mengi ya kusema juu ya jambo hili, lakini ni vigumu kuwaelezeni, kwa sababu nyinyi si wepesi wa kuelewa. 12Kwa wakati huu nyinyi mngalipaswa kuwa waalimu tayari, lakini mnahitaji bado mtu wa kuwafundisheni mafundisho ya mwanzo juu ya neno la Mungu. Mnahitaji maziwa badala ya chakula kigumu. 13Kila anayepaswa kunywa maziwa ni mtoto bado, hajui uadilifu ni nini. 14Lakini chakula kigumu ni kwa ajili ya watu waliokomaa, waliofunzwa kwa vitendo kubainisha mema na mabaya.
Waebrania5;1-14
Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)
"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe

No comments: