Swahili na Waswahili

Swahili na Waswahili
Waswahili na Mswahili Rachel Siwa...Pamoja Daima!!

Friday 4 June 2021

Kikombe Cha Asubuhi; Kitabu cha Waebrania....7


Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?

Tumshukuru Mungu katika yote....

Mungu wetu Baba yetu,Muumba wetu Muumba wa Mbingu na Nchi
Muumba wa vyote vilivyomo vinavyoonekana na visivyoonekana
Mungu wa walio hai,Mungu  mwenye huruma,Mungu wa upendo
Mungu wa Abrahamu,Isaka na Yakobo...
Asante kwa wema na fadhili zako kwetu
Asante kwa ulinzi wako kwetu wakati wote
Asante kwa kutuchagua tena na kutupa
kibali cha kuendelea kuiona leo hii
Asante kwa pumzi/uzima,afya na kuwatayari kwa majukumu yetu

Neema yako yatutosha ee Mungu wetu...


Juu ya kabila la Dani alisema hivi: “Dani ni mwanasimba arukaye kutoka Bashani.” Juu ya kabila la Naftali alisema: “Ee Naftali fadhili, uliyejaa baraka za Mwenyezi-Mungu, nchi yako ni kusini kwenye ziwa Kinerethi.”

Kumbukumbu la Sheria 33:22-23

Baba wa Mbinguni tunakuja mbele zako,
Tukijinyenyekeza,tukijiachilia mikononi mwako
Mungu wetu tunamomba utusamehe dhambi zetu
Baba wa Mbinguni nasi tunaomba ukatupe neema
 ya kuweza kuwasamehe wale wote waliotukosea

Usitutie majaribuni Mungu wetu tunaomba utuepushe
na yule mwovu na kazi zake zote
Jehovah ututakase miili yetu na akili zetu
Baba wa Mbinguni tunaomba utufunike kwa Damu
ya Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo wa Nazareti
yeye aliteseka kwanza ili sisi tupate kupona....

Juu ya kabila la Asheri alisema: “Asheri abarikiwe kuliko watoto wote wa Yakobo, na upendelewe na ndugu zako wote; na achovye mguu wake katika mafuta. Miji yako ni ngome za chuma na shaba. Usalama wako utadumu maisha yako yote!”

Kumbukumbu la Sheria 33:24-25

Mungu wetu tunaomba ukabariki kazi za mikono yetu
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe ubunifu na maarifa katika utendaji
Jehovah nasi tukatende sawasawa na mapenzi yako
Yahweh tunaomba ukabariki ridhiki zetu ziingiazo/zitokazo
Mungu wetu nasi tunaomna ukatupe neema ya kuweza kuwabariki wenye kuhitaji
Tusipungukiwe katika mahitaji yetu
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe kama inavyokupendeza wewe...


Yahweh tunayaweka maisha yetu mikononi mwako
Mungu wetu tunaomba ukabariki nyumba/ndoa zetu,
Jehovah tunaomba ulinzi wako kwetu na kwa vyote tunavyovimiliki
Yahweh tunaomba ukatubariki tuingiapo/tutokapo
Mungu wetu tunaomba ukavibariki vyote tunavyoenda kugusa/kutumia
Baba wa Mbinguni ukavitakase kwa Damu ya Bwana wetu Yesu Kristo
Mungu wetu ukatamalaki na kutuatamia
Baba wa Mbinguni tukawe salama rohoni
Yahwe ukatupe akili ya kutambua mema na mabaya
Mfalme wa amani amani yako ikatawale katika maisha yetu
Mungu wetu ukatupe macho ya kuona,masikio ya kusikia sauti yako na kuitii..
Baba wa Mbinguni  tunaomba ukatupe neema ya kufuata
njia zako,tukasimamie Neno lako,amri na sheria zako
siku zote za maisha yetu...
Ukatuguse kwa mkono wako wenye nguvu,ukatufanye chombo chema
ee Mungu wetu nasi tukatumike kama inavyokupendeza wewe
Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi....

Mose akamalizia kwa kusema, “Ee Israeli, hakuna aliye kama Mungu wako, yeye hupita mbinguni kuja kukusaidia, hupita juu angani katika utukufu wake. Mungu wa milele ndiye kimbilio lenu; nguvu yake yaonekana duniani. Aliwafukuza maadui mbele yenu; aliwaamuru: ‘Waangamizeni.’ Kwa hiyo, watu wa Israeli wakakaa salama, wazawa wa Yakobo peke yao, katika nchi iliyojaa nafaka na divai, nchi ambayo anga lake hudondosha umande. Heri yenu nyinyi Waisraeli. Nani aliye kama nyinyi, watu mliookolewa na Mwenyezi-Mungu, ambaye ndiye ngao ya msaada wenu, na upanga unaowaletea ushindi! Adui zenu watakuja wananyenyekea mbele yenu, nanyi mtawakanyaga chini.”

Kumbukumbu la Sheria 33:26-29

Tazama watoto wako wenye shida/tabu,wote wanaopitia magumu/majaribu mbalimbali
Mungu wetu tunaomba ukawaguse kwa mkono wako wenye nguvu
kila mmoja na mahitaji yake
Mungu wetu tunaomba ukawasamehe pale walipo kwenda kinyume nawe
Yahweh tunaomba ukawape neema ya kuweza kujiombea,kufuata njia zako nazo zikawaweke huru...
Baba wa Mbinguni tunayaweka haya yote mikononi mwako
Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele...
Amina...!!


Asanteni sana wapendwa katika Kristo Yesu kwakuwa nami,
Baba wa Mbinguni aendelee kuwatendea sawasawa na mapenzi yake...
Nawapenda.



 Kuhani Melkisedeki

1Huyo Melkisedeki alikuwa mfalme wa Salemu, na kuhani wa Mungu Mkuu. Abrahamu alipokuwa anarudi kutoka vitani ambako aliwaua wafalme, Melkisedeki alikutana naye, akambariki, 2naye Abrahamu akampa sehemu moja ya kumi ya vitu vyote alivyokuwa navyo. (Maana ya kwanza ya jina Melkisedeki ni “Mfalme wa Uadilifu;” na, kwa vile yeye alikuwa mfalme wa Salemu, jina lake pia lina maana ya “Mfalme wa Amani.”) 3Baba yake na mama yake hawatajwi, wala ukoo wake hautajwi; haisemwi alizaliwa lini au alikufa lini. Anafanana na Mwana wa Mungu, na anaendelea kuwa kuhani daima.
4Basi, mwaona jinsi mtu huyu alivyokuwa maarufu. Babu Abrahamu alimpa sehemu moja ya kumi ya vitu vyote alivyoteka nyara vitani. 5Tunajua pia kwamba kufuatana na sheria, wazawa wa Lawi ambao ni makuhani, wanayo haki ya kuchukua sehemu moja ya kumi kutoka kwa watu, yaani ndugu zao, ingawaje nao ni wazawa wa Abrahamu. 6Lakini huyo Melkisedeki hakuwa wa ukoo wa Lawi, hata hivyo alipokea sehemu ya kumi kutoka kwa Abrahamu; tena akambariki yeye ambaye alikuwa amepewa ahadi ya Mungu. 7Hakuna mashaka hata kidogo kwamba anayebariki ni mkuu kuliko yule anayebarikiwa. 8Tena, hao makuhani wanaopokea sehemu ya kumi, ni watu ambao hufa; lakini hapa anayepokea sehemu ya kumi, yaani Melkisedeki, anasemekana kwamba hafi. 9Twaweza, basi, kusema kwamba Abrahamu alipotoa sehemu moja ya kumi, Lawi (ambaye wazawa wake hupokea sehemu moja ya kumi) alitoa sehemu moja ya kumi pia. 10Maana Lawi hakuwa amezaliwa bado, bali ni kama alikuwa katika mwili wa baba yake, Abrahamu, wakati Melkisedeki alipokutana naye.
11Kutokana na ukuhani wa Walawi, watu wa Israeli walipewa sheria. Sasa, kama huduma ya Walawi ingalikuwa kamilifu, hapangekuwa tena na haja ya kutokea ukuhani mwingine tofauti, na ambao umefuata utaratibu wa ukuhani wa Melkisedeki, na si ule wa Aroni. 12Maana ukuhani ukibadilika, ni lazima sheria nayo ibadilike. 13Naye Bwana wetu ambaye mambo hayo yote yanasemwa juu yake, alikuwa wa kabila lingine, na wala hakuna hata mmoja wa kabila lake aliyepata kutumikia madhabahuni akiwa kuhani. 14Inafahamika wazi kwamba yeye alizaliwa katika kabila la Yuda ambalo Mose hakulitaja alipokuwa anasema juu ya makuhani.
Kuhani mwingine
15Tena jambo hili ni dhahiri zaidi: Kuhani mwingine anayefanana na Melkisedeki amekwisha tokea. 16Yeye hakufanywa kuhani kwa sheria na maagizo ya kibinadamu, bali kwa nguvu ya uhai ambao hauna mwisho. 17Taz Zab 110:4 Maana Maandiko yasema: “Wewe ni kuhani milele, kwa utaratibu wa ukuhani wa Melkisedeki.” 18Basi, ile amri ya zamani ilifutwa kwa sababu ilikuwa hafifu na isiyofaa kitu. 19Maana sheria ya Mose haikuweza kukamilisha jambo lolote. Lakini sasa, mahali pake pamewekwa tumaini lililo bora zaidi ambalo kwalo tunaweza kumkaribia Mungu.
20Zaidi ya hayo, hapa pana kiapo cha Mungu. Wakati wale wengine walipofanywa makuhani hapakuwako kiapo. 21Taz Zab 110:4 Lakini Yesu alifanywa kuhani kwa kiapo wakati Mungu alipomwambia:
“Bwana ameapa,
wala hatabadili nia yake:
‘Wewe ni kuhani milele.’”
22Basi, kutokana na tofauti hii, Yesu amekuwa mdhamini wa agano lililo bora zaidi.
23Tena: Hao makuhani wengine walikuwa wengi kwa sababu walikufa na hawakuweza kuendelea na kazi yao. 24Lakini Yesu si kama wao, yeye anaishi milele; ukuhani wake hauondoki kwake. 25Hivyo, yeye anaweza daima kuwaokoa kabisa wote wanaomwendea Mungu kwa njia yake, maana yeye anaishi milele kuwaombea kwa Mungu.
26Basi, ilikuwa jambo la kufaa sana kwetu kuwa na kuhani kama huyo, mtakatifu, asiye na hatia wala dhambi ndani yake; ametenganishwa mbali na wenye dhambi, na ameinuliwa juu ya mbingu. 27Tofauti na makuhani wengine, yeye hahitaji kutoa tambiko kila siku, kwanza kwa ajili ya dhambi zake mwenyewe, kisha kwa ajili ya dhambi za watu. Yeye alifanya hivyo mara moja kwa ajili ya watu wote, alipojitoa yeye mwenyewe, na hiyo yatosha kwa nyakati zote. 28Sheria huwateua watu walio dhaifu kuwa makuhani wakuu; lakini ahadi ya Mungu aliyoifanya kwa kiapo na ambayo imefika baada ya sheria imemteua Mwana ambaye amefanywa mkamilifu milele.
Waebrania7;1-28
Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)
"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe

No comments: