Swahili na Waswahili

Swahili na Waswahili
Waswahili na Mswahili Rachel Siwa...Pamoja Daima!!

Thursday 24 June 2021

Kikombe Cha Asubuhi; Kitabu cha 1Petro....3


Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?

Tumshukuru Mungu wetu katika yote...

Asante  Mungu wetu kwa wema na fadhili zako kwetu
Asante kwa ulinzi wako kwetu wakati wote
Asante kwa kutuchagua tena na kutupa
kibali cha kuendelea kuiona leo hii
Asante kwa pumzi/uzima,
afya na kuwatayari kwa majukumu yetu


Utukuzwe ee Mungu wetu,usifiwe Baba wa Mbinguni

Neema yako yatutosha  Mungu wetu..

Mpumbavu anayejaribu kutumia methali, ni kama mlevi anayejaribu kungoa mwiba mkononi. Mtu amwajiriye mpumbavu au mlevi, ni kama mpiga upinde anayejeruhi kila mtu.

Methali 26:9-10

Baba wa Mbinguni tunakuja mbele zako tukijinyenyekeza,
tukijishusha na kujiachilia mikononi mwako

Mungu wetu tunaomba utusamehe dhambi zetu zote
Baba wa Mbinguni nasi tunaomba utupe neema ya kuweza kuwasamehe wale wote waliotukosea,Usitutie majaribuni Mungu wetu tunaomba utuepushe na yule mwovu na kazi zake zote,Jehovah ututakase miili yetu na akili zetu Baba wa Mbinguni tunaomba utufunike kwa  Damu ya Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo wa Nazareti,
Yeye aliteseka kwanza ili sisi tupate kupona....
Mungu wetu tunaomba ukabariki kazi za mikono ye
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe ubunifu na maarifa 
katika utendaji
Jehovah nasi tukatende sawasawa na mapenzi yako
Baba wa Mbinguni tunaomba ukabariki ridhiki zetu
ziingiazo/zitokazo
Mungu wetu nasi tunaomba ukatupe neema ya kuweza
kuwabariki wenye kuhitaji
Yahweh tusipungukiwe katika mahitaji yetu
Mungu wetu ukatupe kama inavyokupendeza wewe..

Mpumbavu anayerudiarudia upumbavu wake, ni kama mbwa anayekula matapishi yake. Wamwona mtu ajionaye kuwa mwenye hekima? Nakuambia mpumbavu ni nafuu kuliko huyo.

Methali 26:11-12


Jehovah tunayaweka maisha yetu mikononi mwako
Baba wa Mbinguni tunaomba ukabariki nyumba/ndoa zetu,
watoto,wazazi wetu,familia/ndugu na wote wanaotuzunguka
Jehovah tunaomba ulinzi wako kwetu na kwa vyote tunavyo vimiliki
Yahweh tunaomba ukatubariki tuingiapo/tutokapo
Mungu wetu tunaomba ukavibariki vyote tunavyoenda kugusa/kutumia
Baba wa Mbinguni ukavitakase kwa Damu ya Bwana wetu Yesu Kristo
Mungu wetu ukatamalaki na kutuatamia
Baba wa Mbinguni tukawe salama rohoni
Mfalme wa amani amani yako ikatawale katika maisha yetu
Mungu wetu ukatupe macho ya kuona na masikio ya kusikia 
sauti yako na kuitii
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe neema ya kufuata njia zako
Yahweh tukasimamie Neno lako amri na sheria zako siku zote 
za maisha yetu

Mungu  wetu ukaonekane katika maisha yetu popote tupitapo na ikajulikane kwamba upo 

Neema zako zikawe nasi Nuru yako ikaangaze katika maisha yetu
Ukatufanye barua njema ee Mungu wetu nasi tukasomeke kama
inavyokupendeza wewe
Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi...

Mvivu husema: “Huko nje kuna simba; siwezi kwenda huko.” Kama vile mlango uzungukiapo bawaba zake, ndivyo mvivu juu ya kitanda chake. Mvivu huutia mkono wake katika sahani ya chakula, lakini hawezi kuuinua hadi mdomoni.

Methali 26:13-15

Tazama wenye shida/tabu,Mungu wetu tunaomba
 ukawaguse kila mmoja na mahitaji yake
Baba wa Mbinguni tunaomba ukawasamehe pale walipokwenda
kinyume nawe
Mungu wetu ukawape neema ya kujiombea,macho ya rohoni,masikio yakusikia sauti yako,wakafuate njia zako nazo zikawaweke huru
Mungu wetu tunaomba ukasikie kulia kwao
Baba wa Mbinguni tunomba ukawafute machozi yao
Nuru yako ikaangaze katika maisha yao
Mungu wetu tunaomba ukawatendee sawasawa na mapenzi yako
Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele
Amina....!!!


Wapendwa katika Kristo Yesu asanteni sana
kwakuwanami/kunisoma

Mungu Baba aendelee kuwabariki na kuwatendea
kama inavyompendeza yeye
Amani ya Bwana wetu Yesu Kristo na upendo wa Mungu Baba
ukae nanyi daima....

Nawapenda.


 Mume na mke

1Nanyi wake, jiwekeni chini ya mamlaka ya waume zenu, ili kama wako waume wowote wasioamini neno la Mungu, wapate kuamini kwa kuuona mwenendo wenu. Haitakuwa lazima kwenu kusema neno, 2kwani wataona jinsi mwenendo wenu ulivyo safi na wa kumcha Mungu. 3Katika kujipamba kwenu msitegemee mambo ya njenje, kama vile mitindo ya kusuka nywele, kujivalia vitu vya dhahabu na nguo maridadi. 4Bali, uzuri wenu unapaswa kutokana na hali ya ndani ya utu wa kweli, uzuri usioharibika wa wema na utulivu wa roho, ambao ni wa thamani kubwa mbele ya Mungu. 5Ndivyo walivyojipamba hapo kale wanawake waadilifu waliomtumainia Mungu; walijiweka chini ya mamlaka ya waume zao. 6Sara kwa mfano alimtii Abrahamu na kumwita yeye bwana. Nyinyi mmekuwa sasa binti zake kama mkitenda mema bila kuogopa tisho lolote.
7Kadhalika nanyi waume, katika kuishi na wake zenu mnapaswa kutambua kwamba wao ni dhaifu na hivyo muwatendee kwa heshima; maana nao pia watapokea pamoja nanyi zawadi ya uhai anaowapeni Mungu. Hapo sala zenu hazitatiliwa kizuizi.
Kuteseka kwa sababu ya kutenda mema
8Mwisho nasema hivi: Mnapaswa kuwa na moyo mmoja, na fikira moja; mnapaswa kupendana kindugu, kuwa wapole na wanyenyekevu nyinyi kwa nyinyi. 9Msiwalipe watu ovu kwa ovu, au tusi kwa tusi; bali watakieni baraka, maana nyinyi mliitwa na Mungu mpate kupokea baraka. 10Kama yasemavyo Maandiko Matakatifu:
“Anayetaka kufurahia maisha,
na kuona siku za fanaka,
ajizuie asiseme mabaya
aepe kusema uongo.
11Ajiepushe na uovu, atende mema,
atafute amani na kuizingatia.
12Maana Bwana huwatazama kwa wema waadilifu
na kuzisikiliza sala zao.
Lakini huwapa kisogo watu watendao maovu.”
13Ni nani atakayeweza kuwadhuru nyinyi kama mkizingatia kutenda mema? 14Lakini, hata kama itawapasa kuteseka kwa sababu ya kutenda mema, basi, mna heri. Msimwogope mtu yeyote, wala msikubali kutiwa katika wasiwasi. 15Lakini mtukuzeni Kristo kama Bwana mioyoni mwenu. Muwe tayari kumjibu yeyote atakayewaulizeni juu ya matumaini yaliyo ndani yenu, 16lakini fanyeni hivyo kwa upole na heshima. Muwe na dhamiri njema, kusudi mnapotukanwa, wale wanaosema ubaya juu ya mwenendo wenu mwema kama Wakristo, waone aibu. 17Maana ni afadhali kuteseka kwa sababu ya kutenda mema, kama Mungu akipenda, kuliko kuteseka kwa sababu ya kutenda uovu. 18Kwa maana Kristo mwenyewe alikufa kwa ajili ya dhambi zenu; alikufa mara moja tu na ikatosha, mtu mwema kwa ajili ya waovu, ili awapeleke nyinyi kwa Mungu. Aliuawa kimwili lakini akafanywa hai kiroho; 19na kwa maisha yake ya kiroho alikwenda kuwahubiria wale roho waliokuwa kifungoni. 20Hao ndio wale waliokataa kumtii Mungu alipowangoja kwa saburi wakati Noa alipokuwa anatayarisha ile safina. Ndani ya chombo hicho ni watu wachache tu, yaani watu wanane, waliookolewa katika maji, 21ambayo yalikuwa mfano wa ubatizo unaowaokoa nyinyi sasa. Ubatizo si shauri la kuondoa uchafu mwilini, bali ni ahadi kwa Mungu inayofanyika katika dhamiri njema. Huwaokoeni kwa njia ya ufufuo wa Yesu Kristo 22ambaye alikwenda mbinguni na sasa amekaa upande wa kulia wa Mungu, anatawala juu ya malaika, wakuu na wenye enzi.
1Petro3;1-22
Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)
"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe

No comments: