Swahili na Waswahili

Swahili na Waswahili
Waswahili na Mswahili Rachel Siwa...Pamoja Daima!!

Wednesday 31 March 2021

Kikombe Cha Asubuhi;Kitabu cha Wagalatia....2

 


Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?

Tumshukuru Mungu katika yote....

Mungu wetu Baba yetu,Muumba wetu Muumba wa Mbingu na Nchi
Muumba wa vyote vilivyomo vinavyoonekana na visivyoonekana
Mungu wa walio hai,Mungu  mwenye huruma,Mungu wa upendo
Mungu wa Abrahamu,Isaka na Yakobo...
Asante kwa wema na fadhili zako kwetu
Asante kwa ulinzi wako kwetu wakati wote
Asante kwa kutuchagua tena na kutupa
kibali cha kuendelea kuiona leo hii
Asante kwa pumzi/uzima,afya na kuwatayari kwa majukumu yetu

Neema yako yatutosha ee Mungu wetu...

Au labda unaudharau wema wake mkuu, uvumilivu wake na saburi yake, bila kutambua kwamba wema wake huo una shabaha ya kukuongoza upate kutubu?

Waroma 2:4

Baba wa Mbinguni tunakuja mbele zako,
Tukijinyenyekeza,tukijiachilia mikononi mwako
Mungu wetu tunamomba utusamehe dhambi zetu
Baba wa Mbinguni nasi tunaomba ukatupe neema
 ya kuweza kuwasamehe wale wote waliotukosea

Usitutie majaribuni Mungu wetu tunaomba utuepushe
na yule mwovu na kazi zake zote
Jehovah ututakase miili yetu na akili zetu
Baba wa Mbinguni tunaomba utufunike kwa Damu
ya Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo wa Nazareti
yeye aliteseka kwanza ili sisi tupate kupona....

Lakini unao ugumu na ukaidi wa moyo, na hivyo unajirundikia adhabu kwa siku ile ya ghadhabu wakati hukumu ya haki ya Mungu itakapodhihirishwa.

Waroma 2:5


Mungu wetu tunaomba ukabariki kazi za mikono yetu
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe ubunifu na maarifa katika utendaji
Jehovah nasi tukatende sawasawa na mapenzi yako
Yahweh tunaomba ukabariki ridhiki zetu ziingiazo/zitokazo
Mungu wetu nasi tunaomna ukatupe neema ya kuweza kuwabariki wenye kuhitaji
Tusipungukiwe katika mahitaji yetu
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe kama inavyokupendeza wewe...


Yahweh tunayaweka maisha yetu mikononi mwako
Mungu wetu tunaomba ukabariki nyumba/ndoa zetu,
Jehovah tunaomba ulinzi wako kwetu na kwa vyote tunavyovimiliki
Yahweh tunaomba ukatubariki tuingiapo/tutokapo
Mungu wetu tunaomba ukavibariki vyote tunavyoenda kugusa/kutumia
Baba wa Mbinguni ukavitakase kwa Damu ya Bwana wetu Yesu Kristo
Mungu wetu ukatamalaki na kutuatamia
Baba wa Mbinguni tukawe salama rohoni
Yahwe ukatupe akili ya kutambua mema na mabaya
Mfalme wa amani amani yako ikatawale katika maisha yetu
Mungu wetu ukatupe macho ya kuona,masikio ya kusikia sauti yako na kuitii..
Baba wa Mbinguni  tunaomba ukatupe neema ya kufuata
njia zako,tukasimamie Neno lako,amri na sheria zako
siku zote za maisha yetu...
Ukatuguse kwa mkono wako wenye nguvu,ukatufanye chombo chema
ee Mungu wetu nasi tukatumike kama inavyokupendeza wewe
Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi....

Siku hiyo Mungu atamlipa kila mmoja kufuatana na matendo yake. Wale wanaozingatia kutenda mema, kutafuta utukufu na heshima ya Mungu na kutokufa, watapata uhai wa milele.

Waroma 2:6-7


Tazama watoto wako wenye shida/tabu,wote wanaopitia magumu/majaribu mbalimbali
Mungu wetu tunaomba ukawaguse kwa mkono wako wenye nguvu
kila mmoja na mahitaji yake
Mungu wetu tunaomba ukawasamehe pale walipo kwenda kinyume nawe
Yahweh tunaomba ukawape neema ya kuweza kujiombea,kufuata njia zako nazo zikawaweke huru...
Baba wa Mbinguni tunayaweka haya yote mikononi mwako
Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele...
Amina...!!


Asanteni sana wapendwa katika Kristo Yesu kwakuwa nami,
Baba wa Mbinguni aendelee kuwatendea sawasawa na mapenzi yake...
Nawapenda.


Paulo na mitume wengine

1Baada ya miaka kumi na minne, nilikwenda tena Yerusalemu pamoja na Barnaba; nilimchukua pia Tito pamoja nami. 2Kwenda kwangu kulitokana na ufunuo alionipa Mungu. Katika kikao cha faragha niliwaeleza hao viongozi ujumbe wa Injili niliohubiri kwa watu wa mataifa. Nilifanya hivyo kusudi kazi yangu niliyokuwa nimefanya, na ile ninayofanya sasa, isije ikawa bure. 3Lakini, hata mwenzangu Tito, ambaye ni Mgiriki, hakulazimika kutahiriwa, 4ingawa kulikuwa na ndugu wengine wa uongo waliotaka atahiriwe. Watu hawa walijiingiza kwa ujanja na kupeleleza uhuru wetu tulio nao katika kuungana na Kristo Yesu, ili wapate kutufanya watumwa. 5Hatukukubaliana nao hata kidogo ili ukweli wa Injili ubaki nanyi daima.
6Lakini watu hawa wanaosemekana kuwa ni viongozi – kama kweli walikuwa hivyo au sivyo, kwangu si kitu, maana Mungu hahukumu kwa kuangalia mambo ya nje – watu hawa hawakuwa na mawazo ya kuniongezea. 7Badala yake, walitambua kwamba Mungu alikuwa amenituma kuhubiri Injili kwa watu wa mataifa mengine kama vile Petro alivyokuwa ametumwa kuihubiri kwa Wayahudi. 8Maana, yule aliyemwezesha Petro kuwa mtume kwa Wayahudi, ndiye aliyeniwezesha nami pia kuwa mtume kwa watu wa mataifa mengine. 9Basi, Yakobo, Kefa na Yohane, ambao waonekana kuwa viongozi wakuu, walitambua kwamba Mungu alinijalia neema hiyo, wakatushika sisi mkono, yaani Barnaba na mimi, iwe ishara ya ushirikiano. Sisi ilitupasa tukafanye kazi kati ya watu wa mataifa mengine, na wao kati ya Wayahudi. 10Wakatuomba lakini kitu kimoja: Tuwakumbuke maskini; jambo ambalo nimekuwa nikijitahidi kutekeleza.
Paulo anamkaripia Petro
11Lakini Kefa alipofika Antiokia nilimpinga waziwazi maana alikuwa amekosea. 12Awali, kabla ya watu kadhaa waliokuwa wametumwa na Yakobo kuwasili hapo, Petro alikuwa akila pamoja na watu wa mataifa mengine. Lakini, baada ya hao watu kufika, aliacha kabisa kula pamoja na watu wa mataifa mengine, kwa kuogopa kikundi cha waliosisitiza tohara. 13Hata ndugu wengine Wayahudi walimuunga mkono Petro katika kitendo hiki cha unafiki, naye Barnaba akakumbwa na huo unafiki wao. 14Basi, nilipoona kuwa msimamo wao kuhusu ukweli wa Injili haukuwa umenyooka, nikamwambia Kefa mbele ya watu wote: “Ingawa wewe ni Myahudi, unaishi kama watu wa mataifa mengine na si kama Myahudi! Unawezaje, basi kujaribu kuwalazimisha watu wa mataifa mengine kuishi kama Wayahudi?”
Wayahudi na watu wa mataifa mengine huokolewa kwa imani
15Kweli, sisi kwa asili ni Wayahudi, na si watu wa mataifa mengine wenye dhambi! 16Taz Zab 143:2 Lakini, tunajua kwa hakika kwamba mtu hawezi kufanywa mwadilifu kwa kuitii sheria, bali tu kwa kumwamini Yesu Kristo. Na sisi pia tumemwamini Yesu Kristo ili tupate kufanywa waadilifu kwa njia ya imani yetu kwa Kristo, na si kwa kuitii sheria. 17Sasa, ikiwa katika kutafuta tufanywe waadilifu kwa kuungana na Kristo sisi tunaonekana kuwa wenye dhambi, je, jambo hili lina maana kwamba Kristo anasaidia utendaji wa dhambi? Hata kidogo! 18Lakini ikiwa ninajenga tena kile nilichokwisha bomoa, basi nahakikisha kwamba mimi ni mhalifu. 19Maana, kuhusu sheria hiyo, mimi nimekufa; sheria yenyewe iliniua, nipate kuishi kwa ajili ya Mungu. Mimi nimeuawa pamoja na Kristo msalabani, 20na sasa naishi, lakini si mimi tena, bali Kristo anaishi ndani yangu. Maisha haya ninayoishi sasa naishi kwa imani, imani katika Mwana wa Mungu aliyenipenda hata akayatoa maisha yake kwa ajili yangu. 21Sipendi kuikataa neema ya Mungu. Kama mtu hufanywa mwadilifu kwa njia ya sheria, basi, Kristo alikufa bure!

Wagalatia2;1-21
Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)
"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe

No comments: