Swahili na Waswahili

Swahili na Waswahili
Waswahili na Mswahili Rachel Siwa...Pamoja Daima!!

Monday 1 March 2021

Kikombe Cha Asubuhi: Kitabu cha 1Wakorintho....9


Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?

Haleluyah ni siku/wiki/mwezi mwingine tena Mungu wetu ametuchagua

na kutupa kibali cha kuendelea kuiona leo hii
Si kwamba sisi tumetenda mema sana wala si kwa nguvu zetu
si kwa utashi wetu wala si kwa akili zetu si kwamba sisi
ni wazuri mno si kwa uwezo wetu sisi kuwa hivi tulivyo leo hii
Ni kwa rehema/neema zake ni kwa mapenzi yake Mungu wetu....

Tumshukuru Mungu wetu katika yote...

Asante Mungu wetu kwa wema na fadhili zako kwetu
Asante kwa ulinzi wako kwetu wakati wote
Asante kwa pumzi/uzima,afya na kuwa tayari kwa majukumu yetu
Sifa na Utukufu tunakurudshia Mungu wetu....!!


Kisha, Samueli aliwaeleza watu juu ya wajibu na haki za mfalme, akaziandika katika kitabu ambacho alikiweka mbele ya Mwenyezi-Mungu. Kisha, Samueli aliwaaga watu wote, kila mtu aende nyumbani kwake.

1 Samueli 10:25

Tazama jana imepita ee Mungu wetu leo ni siku mpya na kesho ni siku nyingine
Jehovah tunakuja mbele zako tukijinyenyekeza,
tukijishusha na kujiachilia mikononi mwako
 Mungu wetu tunaomba utusamehe dhambi zetu zote tulizozifanya kwakuwaza,kwakunena,kwakutenda,kwakujua/kutojua
Baba wa Mbinguni nasi tunaomba utupe neema ya kuweza kuwasamehe wale wote waliotukosea
Jehovah usitutie majaribuni Mungu wetu tunaomba utuepushe na yule mwovu na kazi zake zote
Yahweh tunaomba ututakase miili yetu na akili zetu
Baba wa Mbinguni utufunike kwa Damu ya Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo wa Nazareti
yeye aliteseka kwanza ili sisi tupate kupona

Kwakupigwa kwake sisi tumepata kupona....

Pia, Shauli pamoja na wapiganaji hodari ambao awali Mungu aligusa mioyo yao, alikwenda nyumbani kwake huko mjini Gibea.

1 Samueli 10:26

Yahweh tunaomba ukabariki kazi za mikono yetu

Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe ubunifu na maarifa 
katika utendaji
Jehovah nasi tukatende sawasawa na mapenzi yako
Baba wa Mbinguni tunaomba ukabariki ridhiki zetu
ziingiazo/zitokazo
Mungu wetu nasi tunaomba ukatupe neema ya kuweza
kuwabariki wenye kuhitaji
Yahweh tusipungukiwe katika mahitaji yetu
Mungu wetu ukatupe kama inavyokupendeza wewe

Baba wa Mbinguni tunayaweka maisha yetu mikononi mwako
Mungu wetu tunaomba ukabariki nyumba/ndoa zetu,
watoto,wazazi wetu,familia/ndugu na wote wanaotuzunguka
Jehovah tunaomba ulinzi wako kwetu na kwa vyote tunavyo vimiliki
Yahweh tunaomba ukatubariki tuingiapo/tutokapo
Mungu wetu tunaomba ukavibariki vyote tunavyoenda kugusa/kutumia
Baba wa Mbinguni ukavitakase kwa Damu ya Bwana wetu Yesu Kristo
Mungu wetu ukatamalaki na kutuatamia
Baba wa Mbinguni tukawe salama rohoni
Mfalme wa amani amani yako ikatawale katika maisha yetu
Mungu wetu ukatupe macho ya kuona na masikio ya kusikia 
sauti yako na kuitii
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe neema ya kufuata njia zako
Yahweh tukasimamie Neno lako amri na sheria zako siku zote 
za maisha yetu
Mungu wetu ukaonekane katika maisha yetu
Neema zako zikawe nasi Nuru yako ikaangaze katika maisha yetu
ukatuguse kwa mkono wako wenye nguvu
Ukatufanye chombo chema ee Mungu wetu nasi tukatumike kama
inavyokupendeza wewe
Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi...

Lakini watu wengine wasiofaa kitu, walisema, “Je, mtu huyu anaweza kutuokoa?” Walimdharau Shauli na hawakumpa zawadi yoyote. Lakini yeye hakukasirika.

1 Samueli 10:27

Mungu wetu tunawaweka mikononi mwako wenye shida/tabu,wote wanaopitia magumu/majaribu mbalimbali
Mungu wetu tunaomba ukawaguse kwa mkono wako wenye nguvu
 kila mmoja na mahitaji yake 
Mungu wetu tunaomba ukawasamehe pale walipokwenda kinyume nawe
Baba wa Mbinguni ukawape neema ya kujiombea,kufuata njia zako
wakasimamie Neno lako nalo likawaweke huru
Mungu wetu tunaomba ukasikie kuomba kwetu
Mungu wetu ukawatendee sawasawa na mapenzi yako
Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele
Amina...!!


Asanteni sana wapendwa katika Kristo Yesu kwakuwa nami
Mungu Baba aendelee kuwabariki na kuwatendea 
kama inavyompendeza yeye....
Nawapenda.

Haki na jukumu la mitume
1Je, mimi si mtu huru? Je, mimi si mtume? Je, mimi sikumwona Yesu Bwana wetu? Je, nyinyi si matokeo ya kazi yangu kwa ajili ya Bwana? 2Hata kama kwa watu wengine mimi si mtume, lakini walau kwenu nyinyi mimi ni mtume. Nyinyi ni uthibitisho wa utume wangu kwa sababu ya kuungana kwenu na Bwana.
3Hoja yangu kwa wale wanaonipinga ndiyo hii: 4Je, hatuna haki ya kula na kunywa? 5Je, hatuna ruhusa kumchukua mke Mkristo katika ziara zetu, kama vile wafanyavyo mitume wengine, ndugu zake Bwana, na pia Kefa? 6Au ni mimi tu na Barnaba ambao tunapaswa kujipatia maslahi yetu kwa kufanya kazi? 7Je, mwanajeshi gani anayelipia utumishi wake jeshini? Mkulima gani asiyekula matunda ya shamba lake la mizabibu? Mchungaji gani asiyekunywa maziwa ya mifugo yake?
8Je, nasema mambo haya kibinadamu tu? Je, sheria nayo haisemi hivyo? 9Imeandikwa katika sheria: “Usimfunge kinywa ng'ombe anapopura nafaka.” Je, ndio kusema Mungu anajishughulisha na ng'ombe? 10Je, hakuwa anatufikiria sisi aliposema hivyo? Naam, haya yaliandikwa kwa ajili yetu; maana yule anayelima na yule anayevuna, wote wawili wana haki ya kutumaini kupata sehemu ya mavuno. 11Ikiwa sisi tumepanda mbegu ya kiroho kati yenu, je, ni jambo kubwa tukichuma kwenu faida ya kidunia? 12Ikiwa wengine wanayo haki ya kutazamia hayo kutoka kwenu, je, sisi hatuna haki zaidi kuliko hao?
Lakini, sisi hatukuitumia haki hiyo. Badala yake, tumestahimili kila kitu ili tusiiwekee kizuizi chochote Habari Njema ya Kristo. 13Je, hamjui kwamba wanaotumikia hekaluni hupata chakula chao hekaluni, na kwamba wanaotoa sadaka madhabahuni hupata sehemu ya hiyo sadaka? 14Bwana aliagiza vivyo hivyo; wahubiri wa Habari Njema wapate riziki zao kutokana nayo.
15Lakini, mimi sikutumia hata mojawapo ya haki hizo. Na wala siandiki nijipatie haki hizo; kwangu mimi ni afadhali kufa kuliko kumfanya yeyote aone kwamba najisifu bure. 16Ikiwa ninaihubiri injili, hilo si jambo la kujivunia; hilo ni jukumu nililopewa. Na, ole wangu kama sitaihubiri injili! 17Ningekuwa nimeichagua kazi hii kwa hiari, basi, ningetazamia malipo; lakini maadamu naifanya ikiwa ni wajibu, hiyo ina maana kwamba ni jukumu nililopewa nitekeleze. 18Mshahara wangu ni kitu gani, basi? Mshahara wangu ni fursa ya kuihubiri Habari Njema bure, bila kudai haki ninazostahili kwa kuihubiri.
19Kwa hiyo, ingawa mimi si mtumwa wa mtu yeyote, nimejifanya mtumwa wa kila mtu ili nimpatie Kristo watu wengi iwezekanavyo. 20Kwa Wayahudi nimeishi kama Myahudi ili niwapate Wayahudi; yaani, ingawa mimi siko chini ya sheria, nimejiweka chini ya sheria kwao, ili niwapate hao walio chini ya sheria. 21Na kwa wale walio nje ya sheria, naishi kama wao, nje ya sheria, ili niwapate hao walio nje ya sheria. Hii haimaanishi kwamba mimi niko nje ya sheria ya Mungu, maana nabanwa na sheria ya Kristo. 22Kwao walio dhaifu nimejifanya dhaifu ili niwapate hao walio dhaifu. Nimejifanya kila kitu kwa wote ili nipate kuwaokoa baadhi yao kwa kila njia.
23Nafanya haya yote kwa ajili ya Injili, nipate kushiriki baraka zake. 24Je, hamjui kwamba katika uwanja wa michezo, ingawa wapiga mbio wote hukimbia, ni mmoja tu anayejinyakulia zawadi? 25Wanariadha hujipa mazoezi na nidhamu kali; hufanya hivyo ili wajipatie taji iharibikayo! Lakini sisi twafanya hivyo tupate taji isiyoharibika. 26Ndivyo basi, ninavyopiga mbio nikiwa na nia ya kushinda; ndivyo ninavyopigana, na si kama bondia anayetupa ngumi zake hewani. 27Naupa mwili wangu mazoezi magumu na kuutia katika nidhamu kamili, nisije mimi mwenyewe nikakataliwa baada ya kuwahubiria wengine.

1Wakorintho9;1-27
Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)
"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe

No comments: