Swahili na Waswahili

Swahili na Waswahili
Waswahili na Mswahili Rachel Siwa...Pamoja Daima!!

Thursday 18 March 2021

Kikombe Cha Asubuhi: Kitabu cha 2Wakorintho....6


Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?

Tumshukuru Mungu katika yote....

Mungu wetu Baba yetu,Muumba wetu Muumba wa Mbingu na Nchi
Muumba wa vyote vilivyomo vinavyoonekana na visivyoonekana
Mungu wa walio hai,Mungu  mwenye huruma,Mungu wa upendo
Mungu wa Abrahamu,Isaka na Yakobo...
Asante kwa wema na fadhili zako kwetu
Asante kwa ulinzi wako kwetu wakati wote
Asante kwa kutuchagua tena na kutupa
kibali cha kuendelea kuiona leo hii
Asante kwa pumzi/uzima,afya na kuwatayari kwa majukumu yetu

Neema yako yatutosha ee Mungu wetu...

Akasikia sauti ikimwambia: “Petro, amka uchinje, ule!” Petro akajibu, “La, Bwana; mimi sijaonja kamwe chochote ambacho ni najisi au kichafu.”

Matendo 10:13-14

Baba wa Mbinguni tunakuja mbele zako,
Tukijinyenyekeza,tukijiachilia mikononi mwako
Mungu wetu tunamomba utusamehe dhambi zetu
Baba wa Mbinguni nasi tunaomba ukatupe neema
 ya kuweza kuwasamehe wale wote waliotukosea

Usitutie majaribuni Mungu wetu tunaomba utuepushe
na yule mwovu na kazi zake zote
Jehovah ututakase miili yetu na akili zetu
Baba wa Mbinguni tunaomba utufunike kwa Damu
ya Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo wa Nazareti
yeye aliteseka kwanza ili sisi tupate kupona....


Ile sauti ikasikika tena ikimwambia: “Usiviite najisi vitu ambavyo Mungu amevitakasa!” Jambo hili lilifanyika mara tatu, kisha ile shuka ikarudishwa juu mbinguni.

Matendo 10:15-16

Mungu wetu tunaomba ukabariki kazi za mikono yetu
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe ubunifu na maarifa katika utendaji
Jehovah nasi tukatende sawasawa na mapenzi yako
Yahweh tunaomba ukabariki ridhiki zetu ziingiazo/zitokazo
Mungu wetu nasi tunaomna ukatupe neema ya kuweza kuwabariki wenye kuhitaji
Tusipungukiwe katika mahitaji yetu
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe kama inavyokupendeza wewe...


Yahweh tunayaweka maisha yetu mikononi mwako
Mungu wetu tunaomba ukabariki nyumba/ndoa zetu,
Jehovah tunaomba ulinzi wako kwetu na kwa vyote tunavyovimiliki
Yahweh tunaomba ukatubariki tuingiapo/tutokapo
Mungu wetu tunaomba ukavibariki vyote tunavyoenda kugusa/kutumia
Baba wa Mbinguni ukavitakase kwa Damu ya Bwana wetu Yesu Kristo
Mungu wetu ukatamalaki na kutuatamia
Baba wa Mbinguni tukawe salama rohoni
Yahwe ukatupe akili ya kutambua mema na mabaya
Mfalme wa amani amani yako ikatawale katika maisha yetu
Mungu wetu ukatupe macho ya kuona,masikio ya kusikia sauti yako na kuitii..
Baba wa Mbinguni  tunaomba ukatupe neema ya kufuata
njia zako,tukasimamie Neno lako,amri na sheria zako
siku zote za maisha yetu...
Ukatuguse kwa mkono wako wenye nguvu,ukatufanye chombo chema
ee Mungu wetu nasi tukatumike kama inavyokupendeza wewe
Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi....


Petro alipokuwa bado anashangaa juu ya maana ya hayo maono aliyokuwa ameyaona, wale watu waliotumwa na Kornelio, baada ya kuigundua nyumba ya Simoni, walifika mlangoni, wakaita kwa sauti: “Je, kuna mgeni humu aitwaye Simoni Petro?”

Matendo 10:17-18

Tazama watoto wako wenye shida/tabu,wote wanaopitia magumu/majaribu mbalimbali
Mungu wetu tunaomba ukawaguse kwa mkono wako wenye nguvu
kila mmoja na mahitaji yake
Mungu wetu tunaomba ukawasamehe pale walipo kwenda kinyume nawe
Yahweh tunaomba ukawape neema ya kuweza kujiombea,kufuata njia zako nazo zikawaweke huru...
Baba wa Mbinguni tunayaweka haya yote mikononi mwako
Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele...
Amina...!!


Asanteni sana wapendwa katika Kristo Yesu kwakuwa nami,
Baba wa Mbinguni aendelee kuwatendea sawasawa na mapenzi yake...
Nawapenda.



 1Basi, tukiwa wafanyakazi pamoja na Mungu, tunawasihi msikubali ile neema mliyopokea kutoka kwa Mungu ipotee bure. 2Mungu asema hivi:

“Wakati wa kufaa nimekusikiliza,
wakati wa wokovu nikakusaidia.”
Basi, sasa ndio wakati wa kufaa; sasa ndiyo siku ya wokovu!
3Kusudi tusiwe na lawama yoyote katika utumishi wetu, hatupendi kumwekea mtu yeyote kizuizi chochote. 4Badala yake, tunajionesha kuwa kweli watumishi wa Mungu kwa kila kitu: Kwa uvumilivu mwingi wakati wa mateso, shida na taabu. 5Tumepigwa, tumetiwa gerezani na kuzomewa hadharani; tumefanya kazi tukachoka; tumekesha na kukaa bila kula. 6Tunajionesha kuwa watumishi wa Mungu kwa usafi wa moyo, elimu, uvumilivu na wema; kwa Roho Mtakatifu, kwa upendo usio na unafiki, 7kwa ujumbe wa kweli na kwa nguvu ya Mungu. Uadilifu ndiyo silaha yetu kila upande. 8Tuko tayari kupata heshima na kudharauliwa, kulaumiwa na kusifiwa. Twadhaniwa kuwa waongo, kumbe twasema kweli; 9kama wasiojulikana, kumbe twajulikana kwa wote; kama waliokufa, lakini mwonavyo, sisi ni hai kabisa. 10Ingawa tumeadhibiwa, hatukuuawa; ingawa tunayo huzuni, twafurahi daima; ingawa tu maskini, twatajirisha watu wengi; twaonekana kuwa watu tusio na chochote, kumbe tuna kila kitu.
11Ndugu Wakorintho, tumezungumza nanyi kwa unyofu; mioyo yetu iko wazi kabisa. 12Kama mnaona kuna kizuizi chochote kile, kizuizi hicho kiko kwenu nyinyi wenyewe, na si kwa upande wetu. 13Sasa nasema nanyi kama watoto wangu: Wekeni mioyo yenu wazi kama nasi tulivyofanya.
Onyo kuhusu mitindo ya watu wasiomjua Mungu
14Msiambatane na watu wasioamini. Je, wema na uovu vyapatana kweli? Mwanga na giza vyawezaje kukaa pamoja? 15Kristo anawezaje kupatana na Shetani? Mwaamini ana uhusiano gani na asiyeamini? 16Hekalu la Mungu lina uhusiano gani na sanamu za uongo? Maana sisi ni hekalu la Mungu aliye hai. Kama Mungu mwenyewe alivyosema:
“Nitafanya makao yangu kwao,
na kuishi kati yao.
Nitakuwa Mungu wao,
nao watakuwa watu wangu.”
17Kwa hiyo Bwana asema pia:
“Ondokeni kati yao,
mkajitenge nao;
msiguse kitu najisi,
nami nitawapokea.
18Mimi nitakuwa Baba yenu,
nanyi mtakuwa wanangu, waume kwa wake,
asema Bwana Mwenye Nguvu.”

2Wakorintho6;1-18
Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)
"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe

No comments: