Swahili na Waswahili

Swahili na Waswahili
Waswahili na Mswahili Rachel Siwa...Pamoja Daima!!

Monday 14 December 2020

Kikombe Cha Asubuhi; Yohane 19...

 


Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?

Haleluyah ni siku/wiki nyingine tena Mungu wetu ametuchagua

na kutupa kibali cha kuendelea kuiona leo hii
Si kwamba sisi tumetenda mema sana wala si kwa nguvu zetu
si kwa utashi wetu wala si kwa akili zetu si kwamba sisi
ni wazuri mno si kwa uwezo wetu sisi kuwa hivi tulivyo leo hii
Ni kwa rehema/neema zake ni kwa mapenzi yake Mungu wetu....

Tumshukuru Mungu wetu katika yote...

Jinsi gani mji uliokuwa mwaminifu sasa umegeuka kuwa kahaba! Wakati mmoja haki ilitawala humo, lakini sasa umejaa wauaji.

Isaya 1:21

Asante Mungu wetu kwa wema na fadhili zako kwetu
Asante kwa ulinzi wako kwetu wakati wote
Asante kwa pumzi/uzima,afya na kuwa tayari kwa majukumu yetu
Sifa na Utukufu tunakurudshia Mungu wetu....!!

Tazama jana imepita ee Mungu wetu leo ni siku mpya na kesho ni siku nyingine
Jehovah tunakuja mbele zako tukijinyenyekeza,
tukijishusha na kujiachilia mikononi mwako
 Mungu wetu tunaomba utusamehe dhambi zetu zote tulizozifanya kwakuwaza,kwakunena,kwakutenda,kwakujua/kutojua
Baba wa Mbinguni nasi tunaomba utupe neema ya kuweza kuwasamehe wale wote waliotukosea
Jehovah usitutie majaribuni Mungu wetu tunaomba utuepushe na yule mwovu na kazi zake zote
Yahweh tunaomba ututakase miili yetu na akili zetu
Baba wa Mbinguni utufunike kwa Damu ya Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo wa Nazareti
yeye aliteseka kwanza ili sisi tupate kupona

Kwakupigwa kwake sisi tumepata kupona....

Fedha yenu imekuwa takataka; divai yenu imechanganyika na maji.

Isaya 1:22

Yahweh tunaomba ukabariki kazi za mikono yetu

Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe ubunifu na maarifa 
katika utendaji
Jehovah nasi tukatende sawasawa na mapenzi yako
Baba wa Mbinguni tunaomba ukabariki ridhiki zetu
ziingiazo/zitokazo
Mungu wetu nasi tunaomba ukatupe neema ya kuweza
kuwabariki wenye kuhitaji
Yahweh tusipungukiwe katika mahitaji yetu
Mungu wetu ukatupe kama inavyokupendeza wewe

Baba wa Mbinguni tunayaweka maisha yetu mikononi mwako
Mungu wetu tunaomba ukabariki nyumba/ndoa zetu,
watoto,wazazi wetu,familia/ndugu na wote wanaotuzunguka
Jehovah tunaomba ulinzi wako kwetu na kwa vyote tunavyo vimiliki
Yahweh tunaomba ukatubariki tuingiapo/tutokapo
Mungu wetu tunaomba ukavibariki vyote tunavyoenda kugusa/kutumia
Baba wa Mbinguni ukavitakase kwa Damu ya Bwana wetu Yesu Kristo
Mungu wetu ukatamalaki na kutuatamia
Baba wa Mbinguni tukawe salama rohoni
Mfalme wa amani amani yako ikatawale katika maisha yetu
Mungu wetu ukatupe macho ya kuona na masikio ya kusikia 
sauti yako na kuitii
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe neema ya kufuata njia zako
Yahweh tukasimamie Neno lako amri na sheria zako siku zote 
za maisha yetu
Mungu wetu ukaonekane katika maisha yetu
Neema zako zikawe nasi Nuru yako ikaangaze katika maisha yetu
ukatuguse kwa mkono wako wenye nguvu
Ukatufanye chombo chema ee Mungu wetu nasi tukatumike kama
inavyokupendeza wewe
Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi...

Viongozi wako ni waasi; wanashirikiana na wezi. Kila mmoja anapenda hongo, na kukimbilia zawadi. Hawawatetei yatima, haki za wajane si kitu kwao.

Isaya 1:23

Mungu wetu tunawaweka mikononi mwako wenye shida/tabu,wote wanaopitia magumu/majaribu mbalimbali
Mungu wetu tunaomba ukawaguse kwa mkono wako wenye nguvu
 kila mmoja na mahitaji yake 
Mungu wetu tunaomba ukawasamehe pale walipokwenda kinyume nawe
Baba wa Mbinguni ukawape neema ya kujiombea,kufuata njia zako
wakasimamie Neno lako nalo likawaweke huru
Mungu wetu tunaomba ukasikie kuomba kwetu
Mungu wetu ukawatendee sawasawa na mapenzi yako
Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele
Amina...!!


Asanteni sana wapendwa katika Kristo Yesu kwakuwa nami
Mungu Baba aendelee kuwabariki na kuwatendea 
kama inavyompendeza yeye....
Nawapenda.
1Basi, Pilato akaamuru Yesu achukuliwe, apigwe viboko. 2Nao askari wakasokota taji ya miiba, wakamtia kichwani, wakamvika na joho la rangi ya zambarau. 3Wakawa wanakuja mbele yake na kusema: “Shikamoo, Mfalme wa Wayahudi!” Wakampiga makofi. 4Pilato akatoka nje tena, akawaambia, “Tazameni, namleta nje kwenu, mpate kujua kwamba mimi sikuona hatia yoyote kwake.” 5Basi, Yesu akatoka nje amevaa taji ya miiba na joho la rangi ya zambarau. Pilato akawaambia, “Tazameni! Mtu mwenyewe ni huyo.” 6Makuhani wakuu na walinzi walipomwona wakapaza sauti: “Msulubishe! Msulubishe!” Pilato akawaambia, “Mchukueni basi, nyinyi wenyewe mkamsulubishe, kwa maana mimi sikuona hatia yoyote kwake.” 7Wayahudi wakamjibu, “Sisi tunayo sheria, na kufuatana na sheria hiyo, ni lazima afe, kwa sababu alijifanya kuwa Mwana wa Mungu.”
8Pilato aliposikia maneno hayo akazidi kuogopa. 9Basi, akaingia ndani ya ikulu tena, akamwuliza Yesu, “Umetoka wapi wewe?” Lakini Yesu hakumjibu neno. 10Hivyo Pilato akamwambia, “Husemi nami? Je, hujui kwamba ninayo mamlaka ya kukufungua na mamlaka ya kukusulubisha?” 11Yesu akamjibu, “Hungekuwa na mamlaka yoyote juu yangu kama hungepewa na Mungu. Kwa sababu hiyo, yule aliyenikabidhi kwako ana dhambi kubwa zaidi.” 12Tangu hapo, Pilato akawa anatafuta njia ya kumwachilia, lakini Wayahudi wakapiga kelele: “Ukimwachilia huyu mtu, wewe si rafiki yake Kaisari; kila mtu anayejifanya kuwa mfalme humpinga Kaisari!” 13Basi, Pilato aliposikia maneno hayo akamleta Yesu nje, akaketi juu ya kiti cha hukumu, mahali paitwapo “Sakafu ya Mawe” (kwa Kiebrania, Gabatha).
14Ilikuwa yapata saa sita mchana, siku ya maandalio ya Pasaka. Pilato akawaambia Wayahudi, “Tazameni, Mfalme wenu!” 15Wao wakapaza sauti: “Mwondoe! Mwondoe! Msulubishe!” Pilato akawauliza, “Je, nimsulubishe Mfalme wenu?” Makuhani wakuu wakajibu, “Sisi hatuna mfalme isipokuwa Kaisari!” 16Hapo, Pilato akamtia Yesu mikononi mwao ili asulubiwe.
Yesu anasulubiwa msalabani
(Mat 27:32-44; Marko 15:21-32; Luka 23:26-43)
Basi, wakamchukua Yesu. 17Naye akatoka akiwa amejichukulia msalaba wake kwenda mahali paitwapo “Fuvu la Kichwa” (kwa Kiebrania Golgotha). 18Hapo ndipo walipomsulubisha, na pamoja naye waliwasulubisha watu wengine wawili; mmoja upande wake wa kulia na mwingine upande wake wa kushoto, naye Yesu katikati. 19Pilato aliandika ilani akaiweka juu ya msalaba. Nayo ilikuwa imeandikwa hivi: “Yesu Mnazareti, Mfalme wa Wayahudi.” 20Wayahudi wengi waliisoma ilani hiyo, maana mahali hapo aliposulubiwa Yesu palikuwa karibu na mji. Tena ilani hiyo ilikuwa imeandikwa kwa Kiebrania, Kilatini, na Kigiriki. 21Basi, makuhani wakuu wakamwambia Pilato, “Usiandike: ‘Mfalme wa Wayahudi,’ ila ‘Yeye alisema, Mimi ni Mfalme wa Wayahudi.’” 22Pilato akajibu, “Niliyoandika, nimeandika!”
23Askari walipokwisha msulubisha Yesu, walizichukua nguo zake, wakazigawa mafungu manne, fungu moja kwa kila askari. Walichukua pia na kanzu yake; kanzu hiyo ilikuwa imefumwa kwa kipande kimoja tu, bila mshono. 24Taz Zab 22:18 Basi, hao askari wakashauriana: “Tusiipasue, ila tuipigie kura itakuwa ya nani.” Jambo hilo lilifanyika ili yatimie Maandiko Matakatifu yasemayo:
“Waligawana mavazi yangu,
na nguo yangu wakaipigia kura.”
Basi, ndivyo walivyofanya hao askari.
25Karibu na msalaba wake Yesu walikuwa wamesimama mama yake, na dada ya mama yake, Maria mke wa Kleopa, na Maria Magdalene. 26Yesu alipomwona mama yake, na karibu naye amesimama yule mwanafunzi aliyempenda, akamwambia mama yake, “Mama! Tazama, huyo ndiye mwanao.” 27Halafu akamwambia yule mwanafunzi, “Tazama, huyo ndiye mama yako.” Na tangu saa ile huyo mwanafunzi alimchukua akae nyumbani kwake.
Yesu anakufa
(Mat 27:45-56; Marko 15:33-41; Luka 23:44-49)
28 Taz Zab 22:15; 69:21 Kisha, Yesu aliona kwamba yote yalikuwa yametimia; na, ili Maandiko Matakatifu yapate kutimia, akasema, “Naona kiu.” 29Hapo palikuwa na bakuli limejaa siki. Basi, wakachovya sifongo katika hiyo siki, wakaitia juu ya ufito wa husopo, wakamwekea mdomoni. 30Yesu alipokwisha pokea hiyo siki, akasema, “Yametimia!” Kisha akainamisha kichwa, akatoa roho.
Yesu anachomwa mkuki ubavuni
31Ilikuwa Ijumaa, siku ya Maandalio. Kwa hiyo, kusudi miili isikae msalabani siku ya Sabato, maana siku hiyo ya Sabato ilikuwa siku kubwa, Wayahudi walimwomba Pilato miguu ya hao waliosulubiwa ivunjwe na miili yao iondolewe. 32Basi, askari walikwenda, wakaivunja miguu ya yule mtu wa kwanza na yule wa pili ambao walikuwa wamesulubiwa pamoja na Yesu. 33Lakini walipomfikia Yesu, waliona kwamba alikwisha kufa, kwa hivyo hawakumvunja miguu. 34Lakini askari mmoja alimtoboa ubavuni kwa mkuki, na mara ikatoka damu na maji. ( 35Naye aliyeona tukio hilo ameshuhudia ili nanyi mpate kuamini. Na hayo aliyosema ni ukweli, tena yeye anajua kwamba anasema ukweli). 36Taz Zab 34:20 Jambo hilo lilitendwa ili Maandiko Matakatifu yatimie: “Hapana hata mfupa wake mmoja utakaovunjwa.” 37Tena Maandiko mengine yanasema: “Watamtazama yule waliyemtoboa.”
Yesu anazikwa
(Mat 27:57-61; Marko 15:42-47; Luka 23:50-56)
38Baada ya hayo, Yosefu, mwenyeji wa Arimathaya, alimwomba Pilato ruhusa ya kuuchukua mwili wa Yesu. (Yosefu alikuwa mfuasi wa Yesu, lakini kwa siri, maana aliwaogopa viongozi wa Wayahudi). Basi, Pilato akamruhusu. Hivyo Yosefu alikwenda, akauondoa mwili wa Yesu. 39Naye Nikodemo ambaye hapo awali alikuwa amemwendea Yesu usiku, akaja akiwa amechukua mchanganyiko wa manemane na ubani kiasi cha kilo thelathini. 40Basi, waliutwaa mwili wa Yesu, wakaufunga sanda pamoja na manukato kufuatana na desturi ya Wayahudi katika kuzika. 41Mahali hapo aliposulubiwa Yesu palikuwa na bustani, na katika bustani hiyo kulikuwa na kaburi jipya ambalo hakutiwa bado mtu yeyote ndani yake. 42Basi, kwa sababu ya shughuli za Wayahudi za maandalio ya Sabato, na kwa vile kaburi hilo lilikuwa karibu, wakamweka Yesu humo.

Yohane19;1-42
Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)

"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe


No comments: