Swahili na Waswahili

Swahili na Waswahili
Waswahili na Mswahili Rachel Siwa...Pamoja Daima!!

Wednesday, 9 December 2020

Kikombe Cha Asubuhi; Yohane 16...


Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?

Tumshukuru Mungu katika yote....

Mungu wetu Baba yetu,Muumba wetu Muumba wa Mbingu na Nchi
Muumba wa vyote vilivyomo vinavyoonekana na visivyoonekana
Mungu wa walio hai,Mungu  mwenye huruma,Mungu wa upendo
Mungu wa Abrahamu,Isaka na Yakobo...
Asante kwa wema na fadhili zako kwetu
Asante kwa ulinzi wako kwetu wakati wote
Asante kwa kutuchagua tena na kutupa
kibali cha kuendelea kuiona leo hii
Asante kwa pumzi/uzima,afya na kuwatayari kwa majukumu yetu

Neema yako yatutosha ee Mungu wetu....!!Ole wako wewe taifa lenye dhambi, watu waliolemewa na uovu, wazawa wa wenye kutenda maovu, watu waishio kwa udanganyifu! Nyinyi mmemwacha Mwenyezi-Mungu, mmemdharau Mtakatifu wa Israeli, mmefarakana naye na kurudi nyuma.

Isaya 1:4

Baba wa Mbinguni tunakuja mbele zako,
Tukijinyenyekeza,tukijiachilia mikononi mwako
Mungu wetu tunamomba utusamehe dhambi zetu
Baba wa Mbinguni nasi tunaomba ukatupe neema
 ya kuweza kuwasamehe wale wote waliotukosea

Usitutie majaribuni Mungu wetu tunaomba utuepushe
na yule mwovu na kazi zake zote
Jehovah ututakase miili yetu na akili zetu
Baba wa Mbinguni tunaomba utufunike kwa Damu
ya Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo wa Nazareti
yeye aliteseka kwanza ili sisi tupate kupona....


Kwa nini huachi uasi wako? Mbona wataka kuadhibiwa bado? Kichwa chote ni majeraha matupu, na moyo wote unaugua! Toka wayo hadi kichwa hamna penye nafuu, umejaa majeraha na vidonda vitoavyo damu, navyo havikuoshwa, kufungwa wala kutiwa mafuta.

Isaya 1:5-6

Mungu wetu tunaomba ukabariki kazi za mikono yetu
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe ubunifu na maarifa katika utendaji
Jehovah nasi tukatende sawasawa na mapenzi yako
Yahweh tunaomba ukabariki ridhiki zetu ziingiazo/zitokazo
Mungu wetu nasi tunaomna ukatupe neema ya kuweza kuwabariki wenye kuhitaji
Tusipungukiwe katika mahitaji yetu
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe kama inavyokupendeza wewe...


Yahweh tunayaweka maisha yetu mikononi mwako
Mungu wetu tunaomba ukabariki nyumba/ndoa zetu,
Jehovah tunaomba ulinzi wako kwetu na kwa vyote tunavyovimiliki
Yahweh tunaomba ukatubariki tuingiapo/tutokapo
Mungu wetu tunaomba ukavibariki vyote tunavyoenda kugusa/kutumia
Baba wa Mbinguni ukavitakase kwa Damu ya Bwana wetu Yesu Kristo
Mungu wetu ukatamalaki na kutuatamia
Baba wa Mbinguni tukawe salama rohoni
Yahwe ukatupe akili ya kutambua mema na mabaya
Mfalme wa amani amani yako ikatawale katika maisha yetu
Mungu wetu ukatupe macho ya kuona,masikio ya kusikia sauti yako na kuitii..
Baba wa Mbinguni  tunaomba ukatupe neema ya kufuata
njia zako,tukasimamie Neno lako,amri na sheria zako
siku zote za maisha yetu...
Ukatuguse kwa mkono wako wenye nguvu,ukatufanye chombo chema
ee Mungu wetu nasi tukatumike kama inavyokupendeza wewe
Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi....


Nchi yenu imeharibiwa kabisa; miji yenu imeteketezwa kwa moto. Wageni wananyakua nchi yenu mkiona kwa macho, imeharibiwa kama uharibifu wa Sodoma. Mji Siyoni umeachwa kama kibanda shambani, kama kitalu katika shamba la matango, kama mji uliozingirwa.

Isaya 1:7-8

Tazama watoto wako wenye shida/tabu,wote wanaopitia magumu/majaribu mbalimbali
Mungu wetu tunaomba ukawaguse kwa mkono wako wenye nguvu
kila mmoja na mahitaji yake
Mungu wetu tunaomba ukawasamehe pale walipo kwenda kinyume nawe
Yahweh tunaomba ukawape neema ya kuweza kujiombea,kufuata njia zako nazo zikawaweke huru...
Baba wa Mbinguni tunayaweka haya yote mikononi mwako
Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele...
Amina...!!


Asanteni sana wapendwa katika Kristo Yesu kwakuwa nami,Baba wa Mbinguni aendelee kuwatendea sawasawa na mapenzi yake...

Nawapenda. 1“Nimewaambieni hayo kusudi msiiache imani yenu. 2Watu watawafukuza nyinyi katika masunagogi yao. Tena, wakati unakuja ambapo kila atakayewaua nyinyi atadhani anamhudumia Mungu. 3Watawatendeeni mambo hayo kwa sababu hawamjui Baba, wala hawanijui mimi. 4Basi, nimewaambieni mambo haya ili saa yake itakapofika mkumbuke kwamba niliwaambieni.

Kazi ya Roho Mtakatifu
“Sikuwaambieni mambo haya tangu mwanzo kwa sababu nilikuwa pamoja nanyi. 5Lakini sasa namwendea yule aliyenituma; na hakuna hata mmoja wenu anayeniuliza: ‘Unakwenda wapi?’ 6Kwa kuwa nimewaambieni mambo hayo mmejaa huzuni mioyoni mwenu. 7Lakini, nawaambieni ukweli: Afadhali kwenu mimi niende zangu, maana nisipokwenda Msaidizi hatakuja kwenu. Lakini nikienda, basi, nitamtuma kwenu. 8Naye atakapokuja atawathibitishia walimwengu kwamba wamekosea kuhusu dhambi, uadilifu na hukumu ya Mungu. 9Wamekosea kuhusu dhambi kwa sababu hawaniamini; 10kuhusu uadilifu, kwa sababu nakwenda zangu kwa Baba, nanyi hamtaniona tena; 11kuhusu hukumu, kwa sababu mkuu wa ulimwengu huu amekwisha hukumiwa.
12“Ninayo bado mengi ya kuwaambieni, ila kwa sasa hamwezi kuyastahimili. 13Lakini atakapokuja huyo Roho wa ukweli atawaongoza kwenye ukweli wote; maana hatasema kwa mamlaka yake mwenyewe, bali atasema atakayoyasikia na kuwajulisheni yatakayokuja. 14Yeye atanitukuza mimi kwa kuwa atawajulisheni yale atakayopata kutoka kwangu. 15Vyote alivyo navyo Baba ni vyangu; ndiyo maana nimesema kwamba huyo Roho atawajulisheni yale atakayopata kutoka kwangu.
Huzuni na furaha
16“Bado kitambo kidogo nanyi hamtaniona; na baada ya kitambo kidogo tena mtaniona!” 17Hapo baadhi ya wanafunzi wake wakaulizana, “Ana maana gani anapotuambia: ‘Bado kitambo kidogo nanyi hamtaniona; na baada ya kitambo kidogo tena mtaniona?’ Tena anasema: ‘Kwa kuwa ninakwenda kwa Baba!’” 18Basi, wakawa wanaulizana, “Ana maana gani anaposema: ‘Bado kitambo kidogo?’ Hatuelewi anasema nini.” 19Yesu alijua kwamba walitaka kumwuliza, basi akawaambia, “Je, mnaulizana juu ya yale niliyosema: ‘Bado kitambo kidogo nanyi hamtaniona; na baada ya kitambo kidogo tena mtaniona?’ 20Nawaambieni kweli, nyinyi mtalia na kuomboleza, lakini ulimwengu utafurahi; mtaona huzuni lakini huzuni yenu itageuka kuwa furaha. 21Wakati mama anapojifungua huona huzuni kwa sababu saa ya maumivu imefika; lakini akisha jifungua hayakumbuki tena maumivu hayo kwa sababu ya furaha kwamba mtu amezaliwa duniani. 22Nyinyi pia mna huzuni sasa; lakini nitawajieni tena, nanyi mtajaa furaha mioyoni mwenu, na furaha hiyo hakuna mtu atakayeiondoa kwenu. 23Siku hiyo hamtaniomba chochote. Kweli nawaambieni, chochote mtakachomwomba Baba kwa jina langu, atawapeni. 24Mpaka sasa hamjaomba chochote kwa jina langu. Ombeni nanyi mtapata ili furaha yenu ikamilike.
Nimeushinda ulimwengu
25“Nimewaambieni mambo hayo kwa mafumbo. Lakini wakati utakuja ambapo sitasema tena nanyi kwa mafumbo, bali nitawaambieni waziwazi juu ya Baba. 26Siku hiyo mtaomba kwa jina langu, na siwaambii kwamba nitamwomba Baba kwa niaba yenu; 27maana yeye mwenyewe anawapenda nyinyi, kwa sababu nyinyi mmenipenda mimi na mmeamini kwamba nimetoka kwa Mungu. 28Mimi nilitoka kwa Baba, nikaja ulimwenguni; na sasa nauacha ulimwengu na kurudi kwa Baba.”
29Basi, wanafunzi wake wakamwambia, “Ahaa! Sasa unasema waziwazi kabisa bila kutumia mafumbo. 30Sasa tunajua kwamba wewe unajua kila kitu, na huna haja ya kuulizwa maswali na mtu yeyote; kwa hiyo tunaamini kwamba umetoka kwa Mungu.” 31Yesu akawajibu, “Je, mnaamini sasa? 32Wakati unakuja, tena umekwisha fika, ambapo nyinyi nyote mtatawanywa kila mtu kwake, nami nitaachwa peke yangu. Kumbe, lakini mimi siko peke yangu, maana Baba yu pamoja nami. 33Nimewaambieni mambo haya ili mpate kuwa na amani katika kuungana nami. Ulimwenguni mtapata masumbuko; lakini jipeni moyo! Mimi nimeushinda ulimwengu!”

Yohane16;1-33
Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)
"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe

No comments: