Swahili na Waswahili

Swahili na Waswahili
Waswahili na Mswahili Rachel Siwa...Pamoja Daima!!

Tuesday 22 December 2020

Kikombe Cha Asubuhi; Matendo 4...


Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?

Tumshukuru Mungu katika yote....

Mungu wetu Baba yetu,Muumba wetu Muumba wa Mbingu na Nchi
Muumba wa vyote vilivyomo vinavyoonekana na visivyoonekana
Mungu wa walio hai,Mungu  mwenye huruma,Mungu wa upendo
Mungu wa Abrahamu,Isaka na Yakobo...
Asante kwa wema na fadhili zako kwetu
Asante kwa ulinzi wako kwetu wakati wote
Asante kwa kutuchagua tena na kutupa
kibali cha kuendelea kuiona leo hii
Asante kwa pumzi/uzima,afya na kuwatayari kwa majukumu yetu

Neema yako yatutosha ee Mungu wetu...


“Usimwekee kisasi ndugu yako moyoni mwako, bali upatane daima na jirani yako ili usije ukatenda dhambi. Usijilipize kisasi au kuwa na kinyongo dhidi ya wazawa wa watu wako bali umpende jirani yako kama unavyojipenda wewe mwenyewe. Mimi ndimi Mwenyezi-Mungu.

Walawi 19:17-18

Baba wa Mbinguni tunakuja mbele zako,
Tukijinyenyekeza,tukijiachilia mikononi mwako
Mungu wetu tunamomba utusamehe dhambi zetu
Baba wa Mbinguni nasi tunaomba ukatupe neema
 ya kuweza kuwasamehe wale wote waliotukosea

Usitutie majaribuni Mungu wetu tunaomba utuepushe
na yule mwovu na kazi zake zote
Jehovah ututakase miili yetu na akili zetu
Baba wa Mbinguni tunaomba utufunike kwa Damu
ya Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo wa Nazareti
yeye aliteseka kwanza ili sisi tupate kupona....


“Yakupasa kuyashika masharti yangu. Usiiache mifugo yako ipandwe na wanyama wa aina nyingine. Shambani mwako usipande mbegu za aina mbili. Usivae vazi lililofumwa kwa aina mbili za nguo.

Walawi 19:19

Mungu wetu tunaomba ukabariki kazi za mikono yetu
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe ubunifu na maarifa katika utendaji
Jehovah nasi tukatende sawasawa na mapenzi yako
Yahweh tunaomba ukabariki ridhiki zetu ziingiazo/zitokazo
Mungu wetu nasi tunaomna ukatupe neema ya kuweza kuwabariki wenye kuhitaji
Tusipungukiwe katika mahitaji yetu
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe kama inavyokupendeza wewe...


Yahweh tunayaweka maisha yetu mikononi mwako
Mungu wetu tunaomba ukabariki nyumba/ndoa zetu,
Jehovah tunaomba ulinzi wako kwetu na kwa vyote tunavyovimiliki
Yahweh tunaomba ukatubariki tuingiapo/tutokapo
Mungu wetu tunaomba ukavibariki vyote tunavyoenda kugusa/kutumia
Baba wa Mbinguni ukavitakase kwa Damu ya Bwana wetu Yesu Kristo
Mungu wetu ukatamalaki na kutuatamia
Baba wa Mbinguni tukawe salama rohoni
Yahwe ukatupe akili ya kutambua mema na mabaya
Mfalme wa amani amani yako ikatawale katika maisha yetu
Mungu wetu ukatupe macho ya kuona,masikio ya kusikia sauti yako na kuitii..
Baba wa Mbinguni  tunaomba ukatupe neema ya kufuata
njia zako,tukasimamie Neno lako,amri na sheria zako
siku zote za maisha yetu...
Ukatuguse kwa mkono wako wenye nguvu,ukatufanye chombo chema
ee Mungu wetu nasi tukatumike kama inavyokupendeza wewe
Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi....



“Mwanamume akilala na mwanamke mtumwa ambaye ameposwa na mwanamume mwingine, lakini bado hajakombolewa wala kupewa uhuru, uchunguzi ufanywe. Lakini wasiuawe kwa sababu mwanamke huyo hakuwa bado huru.

Walawi 19:20

Tazama watoto wako wenye shida/tabu,wote wanaopitia magumu/majaribu mbalimbali
Mungu wetu tunaomba ukawaguse kwa mkono wako wenye nguvu
kila mmoja na mahitaji yake
Mungu wetu tunaomba ukawasamehe pale walipo kwenda kinyume nawe
Yahweh tunaomba ukawape neema ya kuweza kujiombea,kufuata njia zako nazo zikawaweke huru...
Baba wa Mbinguni tunayaweka haya yote mikononi mwako
Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele...
Amina...!!


Asanteni sana wapendwa katika Kristo Yesu kwakuwa nami,Baba wa Mbinguni aendelee kuwatendea sawasawa na mapenzi yake...

Nawapenda.



 Petro na Yohane wanapelekwa mahakamani

1Petro na Yohane walipokuwa bado wanawahutubia watu, makuhani na mkuu wa walinzi wa hekalu pamoja na Masadukayo walifika. 2Walikasirika sana, maana hao mitume walikuwa wanawahubiria watu kwamba Yesu alifufuka, jambo ambalo linaonesha wazi kwamba wafu watafufuka. 3Basi, waliwatia nguvuni na kwa kuwa usiku ulikuwa umekaribia, wakawaweka chini ya ulinzi mpaka kesho yake. 4Lakini wengi kati ya wale waliosikia ujumbe wao waliamini, na idadi ya waumini ikawa imefika karibu wanaume 5,000.
5Kesho yake, viongozi wa Wayahudi, wazee na waalimu wa sheria walikusanyika pamoja huko Yerusalemu. 6Walikutana pamoja na Anasi kuhani mkuu, Kayafa, Yohane, Aleksanda na wengine waliokuwa wa ukoo wa kuhani mkuu. 7Walipowasimamisha mitume mbele yao, waliwauliza, “Nyinyi mmefanya jambo hili kwa nguvu gani na kwa jina la nani?”
8Hapo, Petro, akiwa amejawa na Roho Mtakatifu, akawaambia, “Viongozi na wazee wa watu! 9Ikiwa mnatuuliza leo juu ya kile kitendo chema alichofanyiwa yule mtu aliyekuwa kiwete na jinsi alivyopata kuwa mzima, 10basi, nyinyi na watu wote wa Israeli mnapaswa kujua kwamba mtu huyu anasimama mbele yenu leo, mzima kabisa, kwa nguvu ya jina lake Yesu wa Nazareti ambaye nyinyi mlimsulubisha, lakini Mungu akamfufua kutoka kwa wafu. 11Huyu ndiye ambaye Maandiko Matakatifu yanasema:
‘Jiwe mlilokataa nyinyi waashi,
sasa limekuwa jiwe kuu la msingi.’
12Wokovu haupatikani kwa mtu mwingine yeyote, kwa maana duniani pote, binadamu hawakupewa jina la mtu mwingine ambaye sisi tunaweza kuokolewa naye.”
13Hao wazee wa Baraza, wakiwa wanajua kwamba Petro na Yohane walikuwa watu wasio na kisomo wala elimu yoyote, walishangaa juu ya jinsi walivyosema kwa uhodari. Wakatambua kwamba walikuwa wamejiunga na Yesu. 14Lakini walipomwona yule mtu aliyeponywa amesimama pamoja nao, hawakuweza kusema kitu. 15Hivyo, waliwaamuru watoke nje ya baraza, nao wakabaki ndani wakizungumza kwa faragha. 16Wakaulizana, “Tufanye nini na watu hawa? Kila mtu anayeishi Yerusalemu anajua kwamba muujiza huu wa ajabu umefanyika, nasi hatuwezi kukana jambo hilo. 17Lakini ili tupate kuzuia jambo hili lisienee zaidi kati ya watu, tuwaonye wasiongee na mtu yeyote kwa jina la Yesu.”
18Kwa hiyo wakawaita tena ndani, wakawaonya wasiongee tena hadharani, wala kufundisha kwa jina la Yesu. 19Lakini Petro na Yohane wakawajibu, “Amueni nyinyi wenyewe kama ni sawa mbele ya Mungu kuwatii nyinyi kuliko kumtii Mungu. 20Kwa maana hatuwezi kuacha kusema juu ya mambo yale tuliyoyaona na kuyasikia.” 21Basi, hao wazee wa Baraza wakawaonya kwa ukali zaidi, halafu wakawaacha huru. Hawakuweza kuwapa adhabu kwa sababu watu wote walikuwa wakimtukuza Mungu kwa sababu ya tukio hilo. 22Huyo mtu aliyeponywa alikuwa na umri wa miaka zaidi ya arubaini.
Waumini wanamwomba Mungu awaimarishe
23Mara tu walipoachwa huru, Petro na Yohane walirudi kwa wenzao, wakawaeleza yale waliyoambiwa na makuhani wakuu na wazee. 24Nao waliposikia habari hizo waliungana pamoja katika kumwomba Mungu wakisema, “Bwana, wewe ni Muumba wa mbingu na dunia, bahari na vyote vilivyomo! 25Ndiwe uliyemfanya mtumishi wako, baba yetu Daudi, aseme kwa nguvu ya Roho Mtakatifu:
‘Kwa nini mataifa yameghadhibika?
Mbona watu wamefanya mipango ya bure?
26Wafalme wa dunia walijiweka tayari,
na watawala walikutana pamoja,
dhidi ya Bwana na dhidi ya Kristo wake.’
27“Maana, kwa hakika, ndivyo Herode, Pontio Pilato, watu wa Israeli na watu wa mataifa walivyokutanika papa hapa mjini, kumpinga Yesu Mtumishi wako Mtakatifu ambaye ulimweka wakfu. 28Naam, walikutana ili wafanye mambo yale uliyokusudia na kupanga tangu mwanzo kwa uwezo wako na mapenzi yako. 29Lakini sasa, ee Bwana, angalia vitisho vyao. Utuwezeshe sisi watumishi wako kuhubiri neno lako kwa uhodari. 30Nyosha mkono wako ili uponye watu. Fanya ishara na maajabu kwa jina la Yesu Mtumishi wako Mtakatifu.”
31Walipomaliza kusali, pale mahali walipokuwa wamekutanika pakatikiswa, nao wote wakajazwa Roho Mtakatifu. Wote wakaanza kuhubiri neno la Mungu bila woga.
Waliishi kama jamaa moja
32Jumuiya yote ya waumini ilikuwa na moyo mmoja na roho moja. Hakuna hata mmoja aliyekuwa na kitu chochote akakiweka kuwa mali yake binafsi, ila waligawana vyote walivyokuwa navyo. 33Mitume walishuhudia kwa nguvu nyingi kufufuka kwa Bwana Yesu, naye Mungu akawapa baraka nyingi. 34Hakuna mtu yeyote aliyetindikiwa kitu, maana waliokuwa na mashamba au nyumba walikuwa wanaviuza 35na kuwakabidhi mitume fedha hizo, zikagawiwa kila mmoja kadiri ya mahitaji yake.
36Kulikuwa na Mlawi mmoja, mzaliwa wa Kupro, jina lake Yosefu, ambaye mitume walimwita Barnaba (maana yake, “Mtu mwenye kutia moyo”). 37Yeye pia alikuwa na shamba lake, akaliuza; akazichukua zile fedha, akawakabidhi mitume.

Matendo4;1-37
Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)
"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe

No comments: