Swahili na Waswahili

Swahili na Waswahili
Waswahili na Mswahili Rachel Siwa...Pamoja Daima!!

Wednesday 30 December 2020

Kikombe Cha Asubuhi; Matendo 10...


Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?

Tumshukuru Mungu wetu katika yote...

Asante  Mungu wetu kwa wema na fadhili zako kwetu
Asante kwa ulinzi wako kwetu wakati wote
Asante kwa kutuchagua tena na kutupa
kibali cha kuendelea kuiona leo hii
Asante kwa pumzi/uzima,
afya na kuwatayari kwa majukumu yetu


Utukuzwe ee Mungu wetu,usifiwe Baba wa Mbinguni

Neema yako yatutosha  Mungu wetu..


Walikuwa kama farasi walioshiba wenye tamaa, kila mmoja akimtamani mke wa jirani yake. Je, nisiwaadhibu kwa mambo haya yote? Nisilipize kisasi juu ya taifa kama hili?

Yeremia 5:8-9

Baba wa Mbinguni tunakuja mbele zako tukijinyenyekeza,
tukijishusha na kujiachilia mikononi mwako

Mungu wetu tunaomba utusamehe dhambi zetu zote
Baba wa Mbinguni nasi tunaomba utupe neema ya kuweza kuwasamehe wale wote waliotukosea,Usitutie majaribuni Mungu wetu tunaomba utuepushe na yule mwovu na kazi zake zote,Jehovah ututakase miili yetu na akili zetu Baba wa Mbinguni tunaomba utufunike kwa  Damu ya Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo wa Nazareti,
Yeye aliteseka kwanza ili sisi tupate kupona....


“Pandeni mpite katika mashamba yake ya mizabibu mkaharibu kila kitu bila kumaliza kabisa. Yakateni matawi yake, kwani hayo si yangu mimi Mwenyezi-Mungu.

Yeremia 5:10

Mungu wetu tunaomba ukabariki kazi za mikono ye
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe ubunifu na maarifa 
katika utendaji
Jehovah nasi tukatende sawasawa na mapenzi yako
Baba wa Mbinguni tunaomba ukabariki ridhiki zetu
ziingiazo/zitokazo
Mungu wetu nasi tunaomba ukatupe neema ya kuweza
kuwabariki wenye kuhitaji
Yahweh tusipungukiwe katika mahitaji yetu
Mungu wetu ukatupe kama inavyokupendeza wewe



Jehovah tunayaweka maisha yetu mikononi mwako
Baba wa Mbinguni tunaomba ukabariki nyumba/ndoa zetu,
watoto,wazazi wetu,familia/ndugu na wote wanaotuzunguka
Jehovah tunaomba ulinzi wako kwetu na kwa vyote tunavyo vimiliki
Yahweh tunaomba ukatubariki tuingiapo/tutokapo
Mungu wetu tunaomba ukavibariki vyote tunavyoenda kugusa/kutumia
Baba wa Mbinguni ukavitakase kwa Damu ya Bwana wetu Yesu Kristo
Mungu wetu ukatamalaki na kutuatamia
Baba wa Mbinguni tukawe salama rohoni
Mfalme wa amani amani yako ikatawale katika maisha yetu
Mungu wetu ukatupe macho ya kuona na masikio ya kusikia 
sauti yako na kuitii
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe neema ya kufuata njia zako
Yahweh tukasimamie Neno lako amri na sheria zako siku zote 
za maisha yetu

Mungu  wetu ukaonekane katika maisha yetu popote tupitapo na ikajulikane kwamba upo 

Neema zako zikawe nasi Nuru yako ikaangaze katika maisha yetu
Ukatufanye barua njema ee Mungu wetu nasi tukasomeke kama
inavyokupendeza wewe
Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi...


Naam, watu wa Israeli na watu wa Yuda, wamekosa kabisa uaminifu kwangu. Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema.”

Yeremia 5:11

Tazama wenye shida/tabu,Mungu wetu tunaomba
 ukawaguse kila mmoja na mahitaji yake
Baba wa Mbinguni tunaomba ukawasamehe pale walipokwenda
kinyume nawe
Mungu wetu ukawape neema ya kujiombea,macho ya rohoni,masikio yakusikia sauti yako,wakafuate njia zako nazo zikawaweke huru
Mungu wetu tunaomba ukasikie kulia kwao
Baba wa Mbinguni tunomba ukawafute machozi yao
Nuru yako ikaangaze katika maisha yao
Mungu wetu tunaomba ukawatendee sawasawa na mapenzi yako
Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele
Amina....!!!


Wapendwa katika Kristo Yesu asanteni sana
kwakuwanami/kunisoma

Mungu Baba aendelee kuwabariki na kuwatendea
kama inavyompendeza yeye
Amani ya Bwana wetu Yesu Kristo na upendo wa Mungu Baba
ukae nanyi daima....

Nawapenda.



 Petro na Kornelio

1Kulikuwa na mtu mmoja huko Kaisarea aitwaye Kornelio, jemadari wa kikosi kimoja kiitwacho “Kikosi cha Italia.” 2Alikuwa mtu mwema; naye pamoja na jamaa yake yote walimcha Mungu; alikuwa anafanya mengi kusaidia maskini wa Kiyahudi na alikuwa anasali daima. 3Yapata saa tisa alasiri, aliona dhahiri katika maono malaika wa Mungu akiingia ndani na kumwambia, “Kornelio!” 4Kornelio alimkodolea macho huyo malaika kwa hofu, akamwambia, “Kuna nini Mheshimiwa?” Huyo malaika akamwambia, “Mungu amezipokea sala na sadaka zako kwa maskini wala hatazisahau. 5Sasa, watume watu Yopa wakamwite mtu mmoja aitwaye Simoni, kwa jina lingine Petro. 6Yeye yumo nyumbani kwa Simoni mtengenezaji wa ngozi ambaye nyumba yake iko karibu na bahari.” 7Huyo malaika aliyesema hayo alipokwisha kwenda zake, Kornelio aliwaita watumishi wawili wa nyumbani na mmoja wa askari zake ambaye alikuwa mcha Mungu, 8akawaeleza yote yaliyotukia, akawatuma Yopa.
9Kesho yake, hao watu watatu wakiwa bado safarini, lakini karibu kufika Yopa, Petro alipanda juu ya paa la nyumba yapata saa sita mchana ili kusali. 10Aliona njaa, akatamani kupata chakula. Chakula kilipokuwa kinatayarishwa, akaota ndoto. 11Aliona mbingu zimefunguliwa na kitu kama shuka kubwa inateremshwa chini ikiwa imeshikwa pembe zake nne. 12Ndani ya shuka hiyo kulikuwa na kila aina ya wanyama: Wanyama wenye miguu minne, wanyama watambaao na ndege wa angani. 13Akasikia sauti ikimwambia: “Petro, amka uchinje, ule!” 14Petro akajibu, “La, Bwana; mimi sijaonja kamwe chochote ambacho ni najisi au kichafu.”
15Ile sauti ikasikika tena ikimwambia: “Usiviite najisi vitu ambavyo Mungu amevitakasa!” 16Jambo hili lilifanyika mara tatu, kisha ile shuka ikarudishwa juu mbinguni.
17Petro alipokuwa bado anashangaa juu ya maana ya hayo maono aliyokuwa ameyaona, wale watu waliotumwa na Kornelio, baada ya kuigundua nyumba ya Simoni, walifika mlangoni, 18wakaita kwa sauti: “Je, kuna mgeni humu aitwaye Simoni Petro?”
19Petro alikuwa bado anajaribu kuelewa yale maono, na hapo Roho akamwambia, “Sikiliza! Kuna watu watatu hapa, wanakutafuta. 20Shuka upesi na wala usisite kwenda pamoja nao kwa maana ni mimi niliyewatuma.” 21Basi, Petro akateremka chini, akawaambia hao watu, “Mimi ndiye mnayemtafuta. Kwa nini mmekuja?” 22Wao wakamjibu, “Jemadari Kornelio ambaye ni mtu mwema, mcha Mungu na mwenye kuheshimika mbele ya Wayahudi wote, ametutuma. Aliambiwa na malaika mtakatifu akualike nyumbani kwake ili asikilize chochote ulicho nacho cha kusema.” 23Petro akawakaribisha ndani, akawapa mahali pa kulala usiku ule.
Kesho yake, Petro alianza safari pamoja nao, na baadhi ya ndugu wa huko Yopa walifuatana naye. 24Siku ya pili yake walifika Kaisarea na huko Kornelio alikuwa anawangojea pamoja na jamaa na marafiki aliokuwa amewaalika. 25Petro alipokuwa anaingia, Kornelio alitoka nje kumlaki, akapiga magoti mbele yake na kuinama chini kabisa. 26Lakini Petro alimwinua, akamwambia, “Simama, kwa maana mimi ni binadamu tu.” 27Petro aliendelea kuongea na Kornelio wakiwa wanaingia nyumbani ambamo aliwakuta watu wengi wamekusanyika. 28Petro akawaambia, “Nyinyi wenyewe mnajua kwamba Myahudi yeyote amekatazwa na sheria yake ya dini kushirikiana na watu wa mataifa mengine. Lakini Mungu amenijulisha nisimfikirie mtu yeyote kuwa najisi au mchafu. 29Kwa sababu hiyo, mliponiita nimekuja bila kusita. Basi, nawaulizeni: Kwa nini mmeniita?” 30Kornelio akasema, “Siku tatu zilizopita saa kama hii, saa tisa alasiri, nilikuwa nikisali chumbani mwangu. Ghafla, mtu aliyekuwa amevaa mavazi yenye kungaa alisimama mbele yangu, 31akasema: ‘Kornelio! Sala yako na sadaka zako kwa maskini zimekubaliwa na Mungu. 32Mtume mtu Yopa akamwite mtu mmoja aitwaye Simoni, kwa jina lingine Petro; yuko nyumbani kwa Simoni mtengenezaji wa ngozi karibu na bahari.’ 33Kwa hiyo nilikutumia ujumbe bila kuchelewa, nawe umefanya vyema kuja. Sasa, sisi tuko mbele ya Mungu, kusikiliza chochote ambacho Bwana amekuamuru kusema.”
Hotuba ya Petro
34Hapo Petro akaanza kusema: “Sasa nimetambua kwamba hakika Mungu hana ubaguzi. 35Mtu wa taifa lolote anayemcha Mungu na kutenda yaliyo sawa anapokelewa naye. 36Huu ndio ule ujumbe Mungu alioupeleka kwa watu wa Israeli, akitangaza Habari Njema iletayo amani kwa njia ya Yesu Kristo ambaye ni Bwana wa wote. 37Nyinyi mnajua jambo lililotukia katika nchi yote ya Wayahudi kuanzia Galilaya baada ya ule ubatizo aliohubiri Yohane. 38Mnamjua Yesu wa Nazareti na jinsi Mungu alivyomteua kwa kummiminia Roho Mtakatifu na nguvu. Mungu alikuwa pamoja naye; yeye alikwenda huko na huko akitenda mema na kuwaponya wote waliokuwa wamevamiwa na Ibilisi. 39Sisi ni mashahidi wa mambo yote aliyotenda katika nchi ya Wayahudi na katika Yerusalemu. Walimuua kwa kumtundika msalabani; 40lakini Mungu alimfufua siku ya tatu, akamfanya aonekane, 41si kwa watu wote, ila kwa wale Mungu aliokwisha wachagua wawe mashahidi wake, yaani sisi tuliokula na kunywa pamoja naye baada ya kufufuka kwake kutoka kwa wafu. 42Alituamuru kuihubiri Habari Njema kwa watu wote na kushuhudia kwamba yeye ndiye aliyeteuliwa na Mungu awe Mwamuzi wa walio hai na wafu. 43Manabii wote waliongea juu yake kwamba kila mtu atakayemwamini atasamehewa dhambi zake zote kwa jina lake.”
Kornelio na jamaa yake wanampokea Roho Mtakatifu
44Wakati Petro alipokuwa bado anasema maneno hayo, Roho Mtakatifu aliwashukia wote waliokuwa wanasikiliza ujumbe huo. 45Wale Wayahudi waumini waliokuja pamoja na Petro kutoka Yopa walishangaa kuona kuwa Mungu aliwamiminia kipawa cha Roho Mtakatifu watu wa mataifa mengine pia; 46maana waliwasikia wakiongea kwa lugha mbalimbali wakimtukuza Mungu. Hapo Petro akasema, 47“Watu hawa wamempokea Roho Mtakatifu kama sisi wenyewe tulivyompokea. Je, kuna yeyote atakayeweza kuwazuia wasibatizwe kwa maji?” 48Basi, akaamuru wabatizwe kwa jina la Yesu Kristo. Kisha wakamwomba akae nao kwa siku chache.

Matendo10;1-48
Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)
"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe

No comments: