Swahili na Waswahili

Swahili na Waswahili
Waswahili na Mswahili Rachel Siwa...Pamoja Daima!!

Thursday 25 October 2018

Kikombe Cha Asubuhi ;Yobu 23...



Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?

Haleluyah Mungu wetu yu mwema sana..
Tumshukuru Mungu wetu katika yote....

Mungu wetu Baba yetu,Muumba wetu Muumba wa Mbingu na Nchi
Baba wa Upendo,Baba wa faraja,Baba wa huruma,Baba wa Baraka
Mungu mwenye nguvu,Mungu mwenye kuponya
Mungu wa Abrahamu,Isaka na Yakobo,Muweza wa yote
Wewe ni mwanzo na wewe ni mwisho,Alfa na Omega...!!


Asante kwa wema na fadhili zako kwetu
Asante kwa ulinzi wako kwetu wakati wote
Asante kwa kutuchagua tena na kutupa
kibali cha kuendelea kuiona leo hii
Asante kwa pumzi/uzima,afya na kuwatayari kwa majukumu yetu

Sifa na Utukufu tunakurudishia wewe ee Mungu wetu....!!

“Halafu atamchinja yule beberu wa sadaka ya kuondoa dhambi kwa ajili ya watu wote. Damu ya mbuzi huyo ataileta ndani mahali patakatifu sana na kufanya kama alivyofanya na damu ya yule fahali; atainyunyiza juu ya kiti cha rehema, upande wake wa mbele. Hivyo atafanya ibada ya upatanisho kwa ajili ya mahali patakatifu kwa sababu ya unajisi, makosa na dhambi zote za Waisraeli. Ndivyo atakavyofanya pia kwa ajili ya hema la mkutano lililo miongoni mwa watu hao walio najisi. Wakati Aroni anafanya ibada ya upatanisho kwa ajili yake mwenyewe, jamaa yake na jamii nzima ya Israeli, kamwe asiwepo mtu yeyote ndani ya hema la mkutano hadi atakapokuwa amemaliza na kutoka nje. Kisha atatoka na kwenda kwenye madhabahu iliyo mbele ya Mwenyezi-Mungu na kuifanyia ibada ya upatanisho. Atachukua kiasi cha damu ya yule fahali na ya yule mbuzi na kuzipaka pembe za madhabahu pande zote. Atainyunyizia madhabahu hiyo damu kwa kidole chake mara saba na hivyo kuiweka wakfu na kuitakasa unajisi wote wa watu wa Israeli.

Tazama Jana imepita ee Mungu wetu Leo ni siku mpya na kesho ni siku nyingineJehovah...
Yahweh tunakuja mbele zako tukijinyenyekeza,tukijishusha

na kujiachilia mikononi mwako
Mungu wetu tunaomba utusamehe dhambi zetu zote tulizo zifanya
Kwakuwaza,kwakunena,kwakutenda,kwakujua/kutojua
Baba wa Mbinguni nasi tunaomba ukatupe neema
ya kuweza kuwasamehe wale wote waliotukosea
Usitutie majaribu Mungu wetu tunaomba utuepushe
na yule mwovu na kazi zake zote
Jehovah ututakase miili yetu na akili zetu
Baba wa Mbinguni tunaomba utufunike kwa Damu
ya Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo wa Nazareti

yeye aliteseka kwanza ili sisi tupate kupona





“Baada ya Aroni kumaliza kupatakasa mahali patakatifu, hema la mkutano na madhabahu, ndipo atamtoa yule beberu kwa ajili ya Azazeli, akiwa hai. Aroni ataweka mikono yake juu ya kichwa cha huyo beberu hai na kuuungama juu yake dhambi zote za watu wa Israeli, makosa yao yote na dhambi zao zote, ili kumwajibisha huyo. Kisha atamwacha huyo beberu aende jangwani akipelekwa huko na mtu yeyote anayejitoa kwa hiari. Atamwacha huyo beberu aende jangwani, mahali pasipokuwa na watu, akiwa ameyachukua maovu yao yote. “Kisha Aroni atarudi ndani ya hema la mkutano, atavua yale mavazi aliyovaa alipoingia mahali patakatifu sana na kuyaacha humo. Ataoga humo ndani katika mahali patakatifu na kuvaa mavazi yake. Atatoka na kutoa sadaka yake ya kuteketezwa, na sadaka ya kuteketezwa ya watu wa Israeli, ili kufanya ibada ya upatanisho kwa ajili yake mwenyewe na kwa ajili ya watu wote. Mafuta ya sadaka ya kuondoa dhambi atayateketeza juu ya madhabahu. Yule mtu aliyempeleka yule beberu kwa Azazeli kwanza atayafua mavazi yake na kuoga ndipo atakapoweza kuingia kambini. Yule fahali na mbuzi waliotolewa sadaka ya kuondoa dhambi ambao damu yao ilipelekwa mahali patakatifu sana ili kufanya ibada ya upatanisho, watapelekwa nje ya kambi na kuteketezwa. Ngozi zao, nyama na mavi yao, vyote vitateketezwa. Yule mtu atakayewateketeza atayafua mavazi yake na kuoga, ndipo atakapoweza kuingia kambini.


Mungu wetu tunaomba ukabariki kazi za mikono yetu
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe ubunifu na maarifa katika utendaji
Jehovah nasi tukatende sawasawa na mapenzi yako
Yahweh tunaomba ukabariki ridhiki zetu ziingiazo/zitokazo
Mungu wetu nasi tunaomba ukatupe neema ya kuweza
kuwabariki wenye kuhitaji
Tusipungukiwe katika mahitaji yetu Baba wa Mbinguni
tunaomba ukatupe kama inavyokupendeza wewe....



Baba wa Mbinguni tunayaweka maisha yetu mikononi mwako
Mungu wetu tunaomba ukabariki nyumba/ndoa zetu,
watoto,wazazi wetu,familia/ndugu na wote wanaotuzunguka
Jehovah tunaomba ulinzi wako kwetu na kwa vyote tunavyo vimiliki
Yahweh tunaomba ukatubariki tuingiapo/tutokapo
Mungu wetu tunaomba ukavibariki vyote tunavyoenda kugusa/kutumia
Baba wa Mbinguni ukavitakase kwa Damu ya Bwana wetu Yesu Kristo
Mungu wetu ukatamalaki na kutuatamia
Baba wa Mbinguni tukawe salama rohoni
Mfalme wa amani amani yako ikatawale katika maisha yetu
Mungu wetu ukatupe macho ya kuona na masikio ya kusikia 
sauti yako na kuitii

 Mungu wetu ukatupe akili ya kutambua mema na mabaya
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe neema ya kufuata njia zako
Yahweh tukasimamie Neno lako amri na sheria zako siku zote 
za maisha yetu

Mungu wetu ukaonekane katika maisha yetu

Baba wa Mbinguni tukanene yaliyo yako
Neema zako zikawe nasi Nuru yako ikaangaze katika maisha yetu
ukatuguse kwa mkono wako wenye nguvu
Tukawe barua njema  ee Mungu wetu nasi tukasomeke kama
inavyokupendeza wewe
Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi...

“Hili ni sharti ambalo mnapaswa kulifuata milele: Siku ya kumi ya mwezi wa saba, nyinyi wenyewe na hata wageni wanaoishi miongoni mwenu, ni lazima mfunge siku hiyo na kuacha kufanya kazi. Mtafanya hivyo kwa sababu siku hiyo ndiyo siku ambayo mtafanyiwa ibada ya upatanisho, msafishwe dhambi zenu, nanyi mtakuwa safi mbele ya Mwenyezi-Mungu. Siku hiyo ni siku ya mapumziko kamili nanyi mtafunga. Kanuni hiyo ni ya kudumu milele. Kuhani aliyepakwa mafuta na kuwekwa wakfu ashike nafasi ya baba yake, ndiye atakayefanya ibada ya upatanisho akiwa amevaa mavazi matakatifu ya kitani. Atafanya ibada ya upatanisho kwa ajili ya mahali patakatifu sana, kwa ajili ya hema la mkutano, madhabahu, makuhani na kwa ajili ya jumuiya nzima ya Israeli. Hili, basi ni sharti la kudumu milele; ni lazima mlifuate ili kufanya ibada ya upatanisho kwa ajili ya watu wa Israeli mara moja kila mwaka na kusamehewa dhambi zao.” Mose akafanya yote kama alivyoamriwa na Mwenyezi-Mungu.

Mungu Baba tunawaweka mikononi mwako wenye shida/tabuwote wanaopotia magumu/majaribu mbalimbali
watoto wako wanaokuomba kwa bidii na imani
Mungu wetu tunaomba ukawaguse kwa mkono wako wenye nguvu
 kila mmoja na mahitaji yake 
Yahweh tunaomba ukaonekane katika maisha yao
Jehovah tunaomba ukawaokoe,ukawavushe salama na  kuwalinda
Mungu wetu tunaomba ukawasamehe pale walipokwenda kinyume nawe
Baba wa Mbinguni ukawape neema ya kujiombea,kufuata njia zako
wakasimaie Neno lako nalo likaweke huru
Mungu wetu tunaomba ukasikie kuomba kwetu
Baba wa Mbinguni ukapokee sala/maombi yetu
Mungu wetu ukawatendee sawasawa na mapenzi yako
Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele
Amina...!!

Asanteni sana wapendwa katika Kristo Yesu kwakuwa nami
Mungu Baba aendelee kuwabariki na kuwatendea 
kama inavyompendeza yeye....
Nawapenda.

Jibu la Yobu

1Kisha Yobu akajibu:
2“Leo pia lalamiko langu ni chungu.
Napata maumivu na kusononeka.
3Laiti ningejua mahali nitakapompata Mungu!
Ningeweza kwenda hata karibu naye.
4Ningeleta kesi yangu mbele yake,
na kumtolea hoja yangu.
5Ningeweza kujua atakachonijibu,
na kuelewa atakachoniambia.
6Je, angeshindana nami kwa nguvu zake zote?
La! Bila shaka angenisikiliza.
7Yeye aweza kuzungumza na mtu mnyofu,
Mungu, hakimu wangu angeamua kuwa sina hatia milele.
8“Tazama, nakwenda mbele, lakini simpati,
narudi nyuma, lakini siwezi kumwona.
9Namtafuta upande wa kushoto lakini simwoni;
nageukia kulia, lakini siwezi kumwona.
10Lakini yeye anajua njia ninayofuata;
atakapomaliza kunijaribu
nitatoka humo safi kama dhahabu.
11Nafuata nyayo zake kwa uaminifu
njia yake nimeishikilia wala sikupinda.
12Kamwe sijaacha kushika amri yake,
maneno yake nimeyatunza moyoni mwangu.
13Lakini yeye habadiliki, nani awezaye kumgeuza?
Analotaka, ndilo analofanya!
14Atanijulisha yote aliyonipangia;
na mengi kama hayo yamo akilini mwake.
15Hivyo, natetemeka kwa hofu mbele yake;
hata nikifikiria tu napatwa na woga.
16Mungu ameufanya moyo wangu ufifie,
Mungu Mwenye Nguvu amenitia hofu.
17Maana nimekumbwa na giza,
na giza nene limetanda usoni mwangu.



Yobu23;1-17

Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)

"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.

No comments: