Swahili na Waswahili

Swahili na Waswahili
Waswahili na Mswahili Rachel Siwa...Pamoja Daima!!

Tuesday 22 May 2018

Kikombe Cha Asubuhi ; 1Mambo ya Nyakati 9...




Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?

Haleluyah Mungu wetu yu mwema sana
Tumshukuru Mungu katika yote......

Mungu wetu Baba yetu,Muumba wetu Muumba wa Mbingu na Nchi
Muumba wa vyote vilivyomo,vinavyoonekana na visivyooneka
Mungu mwenye nguvu,Mungu mwenye huruma,Mungu wa walio hai
Mungu wa Abrahamu,Isaka na Yakobo....
Muweza wa yote ,Mfalme wa amani,Baba wa Baraka,Baba wa Upendo
Wewe ni mwanzo na wewe ni mwisho,Alfa na Omega...!!

Asante kwa wema na fadhili zako kwetu
Asante kwa ukinzi wako kwetu wakati wote
Asante kwa kutuchagua tena na kutupa kibali
cha kuendelea kuiona leo hii
Asante kwa pumzi/uzima,afya na kuwatayari kwa majukumu yetu
Sifa na Utukufu tunakurudishia Mungu wetu...!!




Lakini sasa namwendea yule aliyenituma; na hakuna hata mmoja wenu anayeniuliza: ‘Unakwenda wapi?’ Kwa kuwa nimewaambieni mambo hayo mmejaa huzuni mioyoni mwenu. Lakini, nawaambieni ukweli: Afadhali kwenu mimi niende zangu, maana nisipokwenda Msaidizi hatakuja kwenu. Lakini nikienda, basi, nitamtuma kwenu. Naye atakapokuja atawathibitishia walimwengu kwamba wamekosea kuhusu dhambi, uadilifu na hukumu ya Mungu. Wamekosea kuhusu dhambi kwa sababu hawaniamini; kuhusu uadilifu, kwa sababu nakwenda zangu kwa Baba, nanyi hamtaniona tena; kuhusu hukumu, kwa sababu mkuu wa ulimwengu huu amekwisha hukumiwa. “Ninayo bado mengi ya kuwaambieni, ila kwa sasa hamwezi kuyastahimili. Lakini atakapokuja huyo Roho wa ukweli atawaongoza kwenye ukweli wote; maana hatasema kwa mamlaka yake mwenyewe, bali atasema atakayoyasikia na kuwajulisheni yatakayokuja. Yeye atanitukuza mimi kwa kuwa atawajulisheni yale atakayopata kutoka kwangu. Vyote alivyo navyo Baba ni vyangu; ndiyo maana nimesema kwamba huyo Roho atawajulisheni yale atakayopata kutoka kwangu.

Baba wa Mbinguni tunakuja mbele zako tukijinyenyekeza,
tukijishusha na kujiachilia mikononi mwako
Mungu wetu tunaomba utusamehe dhambi zetu zote tulizozifanya
Kwakuwaza,kwakunena,kwakutenda,kwakujua/kutojua
Yahweh nasi tunaomba utupe neema ya kuweza kuwasamehe
wale wote waliotukosea
Jehovah tunaomba  utuepushe katika majaribu
Mungu wetu utuokoe na yule mwovu na kazi zake zote
Baba wa Mbinguni ututakase miili yetu na akili zetu
Yahweh utufunike kwa Damu ya Bwana na Mwokozi wetu
Yesu Kristo wa Nazareti yeye aliteseka kwanza ili sisi tupate kupona.....




“Bado kitambo kidogo nanyi hamtaniona; na baada ya kitambo kidogo tena mtaniona!” Hapo baadhi ya wanafunzi wake wakaulizana, “Ana maana gani anapotuambia: ‘Bado kitambo kidogo nanyi hamtaniona; na baada ya kitambo kidogo tena mtaniona?’ Tena anasema: ‘Kwa kuwa ninakwenda kwa Baba!’” Basi, wakawa wanaulizana, “Ana maana gani anaposema: ‘Bado kitambo kidogo?’ Hatuelewi anasema nini.” Yesu alijua kwamba walitaka kumwuliza, basi akawaambia, “Je, mnaulizana juu ya yale niliyosema: ‘Bado kitambo kidogo nanyi hamtaniona; na baada ya kitambo kidogo tena mtaniona?’ Nawaambieni kweli, nyinyi mtalia na kuomboleza, lakini ulimwengu utafurahi; mtaona huzuni lakini huzuni yenu itageuka kuwa furaha. Wakati mama anapojifungua huona huzuni kwa sababu saa ya maumivu imefika; lakini akisha jifungua hayakumbuki tena maumivu hayo kwa sababu ya furaha kwamba mtu amezaliwa duniani. Nyinyi pia mna huzuni sasa; lakini nitawajieni tena, nanyi mtajaa furaha mioyoni mwenu, na furaha hiyo hakuna mtu atakayeiondoa kwenu. Siku hiyo hamtaniomba chochote. Kweli nawaambieni, chochote mtakachomwomba Baba kwa jina langu, atawapeni. Mpaka sasa hamjaomba chochote kwa jina langu. Ombeni nanyi mtapata ili furaha yenu ikamilike.

Mungu wetu tunaomba ukabariki kazi za mikono yetu
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe ubunifu na maarifa katika utendaji
Jehovah nasi tukatende sawasawa na mapenzi yako
Yahweh tunaomba ukabariki ridhiki zetu ziingiazo/zitokazo
Mungu wetu nasi tunaomba ukatupe neema ya kuweza 
kuwabariki wenye kuhitaji 
Tusipungukiwe katika mahitaji yetu Baba wa Mbinguni ukatupe
kama inavyokupendeza wewe.....

Mfalme wa amani tunayaweka maisha yetu mikononi mwako
Tunaomba amani yako ikatawale katika maisha yetu
Mungu wetu tunaomba ukabariki nyumba/ndoa zetu,watoto,wazazi wetu
Familia/ndugu na wote wanaotuzunguka
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatubariki tuingiapo/tutokapo
Mungu wetu tunaomba ukavibariki vyote tunavyoenda kugusa/kutumia
Yahweh ukavitakase na kuvifunika kwa Damu ya Bwana wetu Yesu Kristo
Jehovah tunaomba ulinzi wako kwetu na kwa vyote tunavyo vimiliki
Mungu wetu tukawe salama rohoni
Baba wa Mbinguni ukatamalaki na kutuatamia
Mungu wetu ukatupe macho ya kuona na masikio ya kusikia
sauti yako na kuitii
Yahweh ukaonekane katika maisha yetu
Neema zako zikawe nasi Nuru yako ikaangaze katika maisha yetu
Ukatufanye barua njema Mungu wetu nasi tukasomeke
kama inavyo kupendeza wewe
Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi.....



“Nimewaambieni mambo hayo kwa mafumbo. Lakini wakati utakuja ambapo sitasema tena nanyi kwa mafumbo, bali nitawaambieni waziwazi juu ya Baba. Siku hiyo mtaomba kwa jina langu, na siwaambii kwamba nitamwomba Baba kwa niaba yenu; maana yeye mwenyewe anawapenda nyinyi, kwa sababu nyinyi mmenipenda mimi na mmeamini kwamba nimetoka kwa Mungu. Mimi nilitoka kwa Baba, nikaja ulimwenguni; na sasa nauacha ulimwengu na kurudi kwa Baba.” Basi, wanafunzi wake wakamwambia, “Ahaa! Sasa unasema waziwazi kabisa bila kutumia mafumbo. Sasa tunajua kwamba wewe unajua kila kitu, na huna haja ya kuulizwa maswali na mtu yeyote; kwa hiyo tunaamini kwamba umetoka kwa Mungu.” Yesu akawajibu, “Je, mnaamini sasa? Wakati unakuja, tena umekwisha fika, ambapo nyinyi nyote mtatawanywa kila mtu kwake, nami nitaachwa peke yangu. Kumbe, lakini mimi siko peke yangu, maana Baba yu pamoja nami. Nimewaambieni mambo haya ili mpate kuwa na amani katika kuungana nami. Ulimwenguni mtapata masumbuko; lakini jipeni moyo! Mimi nimeushinda ulimwengu!”

Yahweh tazama watoto wako wanaokutafuta kwa bidii na imani
Mungu wetu tunaomba ukawaguse kila mmoja na mahitaji yake
Baba wa Mbinguni ukaonekane katika maisha yao
Jehovah ukawaguse kwa mkono wako wenye nguvu
Yahweh ukawasamehe pale walipokwenda kinyume nawe
Mungu wetu tunaomba ukawape macho ya rohoni na masikio
ya kusikia sauti yako na kuitii
Baba wa Mbinguni ukawape neema ya kujiombea
wakafuate njia zako nazo ziwaweke huru
Mungu wetu tunaomba ukasikie kuomba kwetu
Baba wa Mbinguni tunaomba ukapokee sala/maombi yetu
Mungu wetu ukawatendee sawasawa na mapenzi yako
Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele
Amina...!!

Asanteni sana wapendwa katika Kristo Yesu kwa kuwa nami
Mungu Baba aendelee kuwabariki na kuwatendea kama
inavyompendeza yeye
Amani ya Bwana wetu Yesu Kristo na upendo wa Mungu Baba
Ukae nanyi daima...
Nawapenda.

Watu waliorudi toka uhamishoni

1Hivyo, watu wote wa Israeli waliandikishwa katika nasaba, na orodha hiyo imeandikwa katika Kitabu cha Wafalme wa Israeli. Watu wa Yuda walikuwa wamechukuliwa mateka hadi Babuloni kwa sababu ya kutokuwa waaminifu. 2Watu wa kwanza kuyarudia makazi yao katika miji yao walikuwa raia wa kawaida, makuhani, Walawi na watumishi wa hekaluni. 3Baadhi ya watu wa makabila ya Yuda, Benyamini, Efraimu na Manase walikwenda kuishi mjini Yerusalemu: 4Uthai mwana wa Amihudi, mwana wa Omri, mwana wa Imri, mwana wa Bani, wa wana wa Peresi, mwana wa Yuda. 5Na wazawa wa Shilo, Asaya mzaliwa wa kwanza, kiongozi na wanawe. 6Na wazawa wa Zera, Yeueli, na ndugu zao; watu 690. 7Na wa wazawa wa Benyamini: Salu mwana wa Meshulamu, mwana wa Hodavia, mwana wa Hasenua; 8na Ibneya mwana wa Yerohamu, Ela, mwana wa Uzi, mwana wa Mikri; na Meshulamu, mwana wa Shefatia, mwana wa Reueli, mwana wa Ibniya; 9na ndugu zao, sawasawa na vizazi vyao; watu956. Watu hao wote ndio waliokuwa wakuu wa koo za baba zao, kwa kadiri ya koo za baba zao.

Makuhani walioishi Yerusalemu

10Makuhani wafuatao waliishi Yerusalemu: Yedaya, Yehoyaribu na Yakini, 11na Azaria mwana wa Hilkia, mwana wa Meshulamu, mwana wa Sadoki, mwana wa Merayothi, mwana wa Ahitubu, mkuu wa nyumba ya Mungu; 12na Adaya, mwana wa Yerohamu, mwana wa Pashuri, mwana wa Malkiya; na Maasai, mwana wa Adieli, mwana wa Yazera, mwana wa Meshulamu, mwana wa Meshilemithi, mwana wa Imeri; 13wakuu wa koo za baba zao; pamoja na ndugu zao; jumla watu 1,760. Walikuwa wakuu wenye uwezo mkubwa katika huduma yote ya nyumba ya Mungu.

Walawi walioishi Yerusalemu

14Walawi wafuatao waliishi Yerusalemu: Shemaya, mwana wa Hashubu, mwana wa Azrikamu, mwana wa Hashabia, wa wana wa Merari; 15na Bakbakari, na Hereshi, na Galali, Matania, mwana wa Mika, mwana wa Zikri, mwana wa Asafu; 16na Obadia, mwana wa Shemaya, mwana wa Galali, mwana wa Yeduthuni; na Berekia, mwana wa Asa, mwana wa Elkana; waliokuwa wakiishi katika vijiji vya Wanetofathi.

Walinzi wa hekalu waliokuwa wakiishi Yerusalemu

17Walinzi wa hekalu wafuatao pia waliishi katika Yerusalemu: Shalumu, Akubu, Talmoni na Ahimani na ndugu zao. Shalumu alikuwa mkuu wao. 18Hadi kufikia wakati huo, walinzi kutoka katika koo zao ndio waliolinda Lango la mfalme9:18 Lango la mfalme: Lango la mashariki alilopitia mfalme. la upande wa mashariki. Hapo awali, walikuwa walinzi wa maingilio ya makambi ya Walawi.
19Shalumu, mwana wa Kore, mwana wa Ebiasafu, pamoja na ndugu zake wa ukoo wa Kora, walikuwa na wajibu wa kuyatunza maingilio ya hema la mkutano, kama vile walivyokuwa babu zake wakati wa ulinzi wa kambi ya Mwenyezi-Mungu. 20Finehasi, mwana wa Eleazari, alikuwa msimamizi wao, hapo awali, naye Mwenyezi-Mungu alikuwa pamoja naye. 21Zekaria mwana wa Meshelemia, pia alikuwa mlinzi wa maingilio ya hema la mkutano. 22Jumla, watu 212 walichaguliwa kuwa walinzi wa maingilio ya hekalu. Waliandikishwa kulingana na vijiji walimoishi. Mfalme Daudi na Samueli mwonaji ndio waliowathibitisha katika wadhifa huu muhimu. 23Basi, watu hao na wazawa wao, waliendelea kuyalinda malango ya nyumba ya Mwenyezi-Mungu. 24Kila upande, yaani mashariki, magharibi, kaskazini na kusini, palikuwa na lango lililokuwa na walinzi. 25Walinzi hawa walisaidiwa na ndugu zao waliokuwa wakiishi vijijini, ambao walilazimika kushika zamu ya ulinzi kwa muda wa siku saba, mara kwa mara, 26kwa maana wale walinzi wakuu wanne, ambao walikuwa Walawi, walikuwa na wajibu wa kusimamia vyumba na hazina ya nyumba ya Mungu. 27Wao waliishi karibu na nyumba ya Mungu kwa sababu ilikuwa ni wajibu wao kuyalinda na kuyafungua malango yake kila siku asubuhi.

Walawi wengineo

28Baadhi ya Walawi walisimamia vyombo vilivyotumika wakati wa ibada. Walihitajika kuvihesabu wakati vilipotolewa na wakati viliporudishwa. 29Wengine walichaguliwa kuvisimamia vifaa vya hekalu, na vyombo vyote vitakatifu, na unga safi, divai, mafuta ya zeituni, ubani na manukato. 30Lakini kazi ya kutayarisha manukato ilifanywa na makuhani.
31Metithia, mmoja wa Walawi aliyekuwa mzaliwa wa kwanza wa Shalumu, wa ukoo wa Kora, alisimamia utengenezaji wa tambiko ya mikate myembamba. 32Nao ndugu zao wengine wa ukoo wa Kohathi walikuwa na wajibu wa kutayarisha mikate ya wonyesho kwa ajili ya hekalu kila Sabato. 33Jamaa nyingine za Walawi zilisimamia huduma ya nyimbo hekaluni. Waliishi katika baadhi ya majengo ya nyumba ya Mungu na hawakuhitajika kufanya kazi nyingine yoyote kwa maana walikuwa kazini usiku na mchana.
34Watu wote hawa waliotajwa walikuwa viongozi wa kabila la Walawi, kulingana na koo zao. Wao ndio viongozi walioishi Yerusalemu.

Babu na wazawa wa mfalme Shauli

(8:29-38)

35Yeieli alikuwa mwanzilishi wa mji wa Gibeoni ambamo aliishi yeye pamoja na mkewe, jina lake Maaka. 36Mzaliwa wake wa kwanza alikuwa Abdoni, naye alifuatiwa na Zuri, Kishi, Baali, Neri, Nadabu, 37Gedori, Ahio, Zekaria na Miklothi. 38Miklothi alimzaa Shimeamu. Wazawa wao waliishi Yerusalemu karibu na jamaa nyingine za koo zao.
39Neri alimzaa Kishi, naye Kishi akamzaa Shauli. Shauli alikuwa na wana wanne: Yonathani, Malki-shua, Abinadabu na Eshbaali. 40Yonathani alimzaa Merib-baali, Merib-baali akamzaa Mika. 41Mika alikuwa na wana wanne: Pithoni, Meleki, Tarea na Ahazi.9:41 Ahazi: Kiebrania hakina Ahazi (taz 8:35). 42Ahazi alimzaa Yara, Yara akawazaa Alemethi, Azmawethi na Zimri, naye Zimri akamzaa Mosa, 43Mosa akamzaa Binea, Binea akamzaa Refaya, Refaya akamzaa Eleasa, naye Eleasa akamzaa Aseli.
44Aseli alikuwa na wana sita: Azrikamu, Bokeru, Ishmaeli, Shearia, Obadia na Hamani. Hawa wote walikuwa wana wa Aseli.



1Mambo ya Nyakati9;1-44


Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)

"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.

No comments: