Swahili na Waswahili

Swahili na Waswahili
Waswahili na Mswahili Rachel Siwa...Pamoja Daima!!

Monday 10 April 2017

Kikombe Cha Asubuhi;Kutoka 8...

Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje Wapendwa/Waungwana?
Tumshukuru Mungu katika roho na kweli..
Mtakatifu , Mtakatifu, Mtakatifu...!! Baba wa mbinguni, Baba yetu Mungu wetu, Muumba wetu,Muumba Mbingu na nchi na Vyote vilivyomo ni mali yako, Hata sisi Baba ni mali yako..Mungu wa Abrahamu,Isaka na Yakobo, Muweza wa yote,wewe ni mwanzo na wewe ni mwisho...Alfa na Omega...
Yahweh..!!!!!Jehovah..!!
Tunashukuru Baba kwa kutupa Kibali hiki cha kutuchagua na kuendelea kuiona Leo..Baba si kwamba wajuzi sana, wenye nguvu sana, wema na wazuri mno.. Hapa ni kwa Neema/Rehema yako tuu Mfalme wa Amani...
Baba tunaomba ukaibariki siku hii ikawe njema na yenye Amani, Furaha, wema na Fadhili,Ukatubariki tuingiapo/tutokapo,vyombo vya usafiri, tutembeapo hatua zetu ziwe nawe Baba...
Baba ukabariki  kazi zetu,Biashara,Masomo na vyote tunavyoenda kugusa/kutumia ukavitakase kwa Damu ya Bwana wetu na Mwokozi wetu Yesu Kristo wa Nazareti..Yeye aliteseka pale Msalabani ili sisi tupate kupona..Ukatutakase Akili na miili yetu..Roho Mtakatifu akatuongoze kwenye kunena/kutenda, kutambua/kujitambua..
Baba utusamehe pale tulipokwenda kinyume nawe kwa kuwaza,kutenda, kwakujua/kutojua..Baba wa Mbinguni nasi tunaomba utupe Neema ya kuweza kuwasamehe waliotukosea..
Mfalme wa Amani ukawaguse na kuwaponya wote wanaopitia magumu/majaribu,shida/tabu,wagonjwa,wafiwa ukawe mfariji wao,waliovivfungoni baba ukawafungue na kuwaponya kimwili na kiroho pia..
Baba ukatamalaki katika nchi hii tunayoishi.. Ukaibariki na kutubariki wote tunaoishi hapa..ukatulinde na adui yeyote anayepanga kwenda kinyume nawe..Ukatuatamie Jehovah..!!

Mfalme wa Amani Tanzania tunaiweka mikononi mwako na watanzania wote popote walipo,Ukaibariki na kutubariki katika kila lililojema na ukatulinde na uovu wowote unaondelea na kunaopangwa kufanyika..mikononi mwako yote yanawezekena..
Afrika ikawe nawe Baba wa mbinguni ..Dunia yote ukawe mtawala na Amani iliyo juu yako ikatawale..
Ukawabariki na kuwaongoza wote wanaotuongoza wakatuongoze katika haki na kweli..


2“Hakuna aliye mtakatifu kama Mwenyezi-Mungu;
hakuna yeyote aliye kama yeye;

hakuna aliye mwamba kama Mungu wetu.[1 Samueli 2:2]
 20Hakuna mwingine kama wewe, ee Mwenyezi-Mungu, na yote tunayoyasikia yanathibitisha kwamba hakuna Mungu mwingine ila wewe.[1 Mambo ya Nyakati 17:20]
Tunayaweka haya yote mikononi mwako, Tukijinyeyekeza, kukusifu,Tunashukuru na kuamini wewe ni Mungu wetu na hakuna mwingine kama wewe na hatokuwepo..Milele na Milele..
Amina..!!!!! 





Pigo la pili: Vyura

1Kisha Mwenyezi-Mungu akamwambia Mose, “Nenda kwa Farao ukamwambie Mwenyezi-Mungu asema hivi: Waache watu wangu waondoke ili wanitumikie. 2Lakini ukikataa kuwaacha waondoke, basi, nitaipiga nchi yako yote kwa kuiletea vyura. 3Mto Nili utafurika vyura, nao wataingia mpaka ndani ya nyumba yako, chumba chako cha kulala, kitandani mwako, na katika nyumba za watumishi wako na watu wako. Vyura hao wataingia katika majiko yenu na vyombo vyenu vya kukandia unga. 4Vyura watapanda juu ya mwili wako, miili ya watu wako na watumishi wenu!”
5Mwenyezi-Mungu akamwambia Mose, “Mwambie Aroni anyoshe mkono wake na fimbo yake juu ya mito, juu ya mifereji na madimbwi, nao vyura watatokea na kuenea kila mahali nchini Misri.”8:5 katika makala ya Kiebrania ni 8:1. 6Basi, Aroni akanyosha fimbo yake juu ya maji yote, vyura wakatokea na kuifunika nchi nzima ya Misri. 7Lakini wachawi wa Misri kwa uchawi wao pia wakaleta vyura nchini Misri.
8Kisha Farao akamwita Mose na Aroni, akamwambia, “Msihi Mwenyezi-Mungu, ili aniondolee mimi na watu wangu vyura hawa, nami nitawaacha Waisraeli waende zao na kumtambikia Mwenyezi-Mungu.” 9Mose akamjibu Farao, “Haya! Waweza kutaja wakati unaotaka nikuombee kwa Mungu, niwaombee maofisa wako na watu wako; nitamwomba awaangamize vyura hawa waliomo katika nyumba zenu; watabaki tu mtoni Nili!”
10Farao akamwambia, “Kesho.” Mose akasema, “Nitafanya kama unavyosema, ili ujue kwamba hakuna yeyote anayelingana na Mwenyezi-Mungu, Mungu wetu. 11Vyura wataondoka kwako, na kwenye nyumba zenu, kwa maofisa wako na kwa watu wako; watabaki tu katika mto Nili.”
12Basi, Mose na Aroni wakaondoka nyumbani kwa Farao, na Mose akamlilia Mwenyezi-Mungu amwondolee Farao uvamizi wa vyura hao aliomletea. 13Mwenyezi-Mungu akafanya kama Mose alivyomwomba: Vyura wakafa majumbani, viwanjani na kwenye kumbi za nyumba na katika mashamba. 14Watu wakawakusanya vyura hao marundo marundo; nchi nzima ikanuka. 15Lakini Farao alipoona kwamba nchi imepata nafuu, akawa mkaidi tena, wala hakuwasikiliza Mose na Aroni, kama Mwenyezi-Mungu alivyokuwa amesema.

Pigo la tatu: Viroboto

16Kisha, Mwenyezi-Mungu akamwambia Mose, “Mwambie Aroni anyoshe fimbo yake na kuyapiga mavumbi, nayo yatageuka kuwa viroboto kote nchini Misri.” 17Mose na Aroni wakafanya hivyo. Aroni alinyosha fimbo yake na kuyapiga mavumbi, nayo yakageuka kuwa viroboto na kuwaparamia watu na wanyama. Mavumbi yote nchini kote Misri yakageuka kuwa viroboto. 18Wachawi wa Misri, kwa uchawi wao, wakajaribu kuyageuza mavumbi yawe viroboto, lakini hawakufaulu. Viroboto hao wakaenea juu ya watu na wanyama. 19Taz Luka 11:20 Wale wachawi wakamwambia Farao, “Hii ni kazi ya mkono wa Mungu.”8:19 au Hii ni nguvu ya kimungu Kiebrania, neno kwa neno: “Ni kidole cha Mungu”. Lakini moyo wa Farao ukaendelea kuwa mgumu; wala hakuwasikiliza Mose na Aroni. Ikawa kama Mwenyezi-Mungu alivyokuwa amesema.

Pigo la nne: Nzi

20Kisha Mwenyezi-Mungu akamwambia Mose, “Kesho amka asubuhi mapema umwendee Farao wakati anapokwenda mtoni umwambie, ‘Mwenyezi-Mungu asema hivi: Waache watu wangu waondoke ili wanitumikie. 21Kama ukikataa kuwaacha waondoke, basi, nitakuletea makundi ya nzi, wewe, maofisa wako na watu wako wote. Wataingia kwenye nyumba zenu na nyumba zote za Wamisri zitajaa makundi ya nzi, kadhalika na ardhi yote ya Misri. 22Lakini siku hiyo sehemu ya Gosheni wanakoishi watu wangu nitaikinga: Humo nzi hao hawatakuwamo. Hapo ndipo utakapotambua kwamba mimi Mwenyezi-Mungu natenda mambo nchini mwako. 23Nitawakinga watu wangu na mambo yatakayowapata watu wako. Mambo hayo yatafanyika kesho.’” 24Mwenyezi-Mungu akafanya kama alivyosema: Makundi makubwa ya nzi yakaivamia nyumba ya Farao, nyumba za maofisa wake na nchi nzima ya Misri. Nchi nzima ya Misri ikaharibiwa na nzi hao.
25Ndipo Farao akawaita Mose na Aroni, akasema, “Mnaweza kwenda kumtambikia Mungu wenu, lakini iwe humuhumu nchini Misri.” 26Lakini Mose akamjibu, “La! Haifai kufanya hivyo, maana tambiko tutakazomtolea Mwenyezi-Mungu, Mungu wetu, zitawachukiza Wamisri. Je, Wamisri wakituona tukitoa tambiko ambazo ni chukizo kwao, si watatupiga mawe? 27Ni lazima tusafiri mwendo wa siku tatu jangwani tukamtambikie Mwenyezi-Mungu, Mungu wetu, kama atakavyotuamuru.”
28Basi, Farao akasema, “Nitawaacha mwende zenu kumtambikia Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, jangwani. Walakini msiende mbali mno. Niombeeni na mimi.” 29Mose akamjibu, “Mara tu nitakapokuacha, nitamwomba Mwenyezi-Mungu makundi haya ya nzi yatoweke kwako wewe Farao, maofisa wako na watu wako, kesho. Lakini wewe usitudanganye tena kwa kukataa kuwaacha watu kwenda kumtambikia Mwenyezi-Mungu.”
30Basi, Mose akaondoka nyumbani kwa Farao, akamwomba Mwenyezi-Mungu. 31Mwenyezi-Mungu akafanya kama Mose alivyomwomba, wale nzi wakatoweka kutoka kwa Farao, maofisa wake na watu wake, wala hakusalia hata mmoja. 32Lakini hata safari hii Farao alikuwa mkaidi, wala hakuwaruhusu Waisraeli kuondoka.Kutoka8;1-32

Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)
"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.

No comments: