Swahili na Waswahili

Swahili na Waswahili
Waswahili na Mswahili Rachel Siwa...Pamoja Daima!!

Wednesday 5 April 2017

Kikombe Cha Asubuhi; Kutoka 5...

Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje Wapendwa/Waungwana?
Tumshukuru Mungu kwa yote...
Mtakatifu Mtakatifu Mtakatifu...!!!!!!! Baba wa Mbinguni, Mungu wetu na Mwokozi wetu,Muumba wetu na Muumba mbingu,Nchi na vyote vilivyomo ni mali yake.Hata sisi Baba ni mali yako..Tunashukuru na kukusifu Daima..Asante Baba kwa wema,Fadhili,Ridhiki na yote..Asante kwakutuchagua tena na kutupa kibali cha kuendelea kuona leo hii..
Ikawe siku njema na yenye Baraka..Utubariki tuingiapo/tutokapo,vyombo vya usafiri,tutembeapo Baba hatua zetu ziwe nawe.. Baba wa Mbinguni Ukabariki Kazi zetu,Biashara,Masomo na vyote tunavyoenda kugusa/kutumia Baba ukavitakase na ukatutakase kwa Damu ya mwanao Bwana wetu na Mwokozi wetu aliteseka pale msalabani ili sisi tupate kupona Yesu Kristo wa Nazareti..
Baba ukatamalaki  kwenye maisha yetu,Baba na  Uatamie watoto wetu na familia zetu..ukawalinde watoto wetu na kuwaongoza katika ujana wao,Masomo yao na wapate kuelewa na kukumbuka yote wanayofundishwa..wawe na kiu ya kutaka kukujua Mungu zaidi..
Mfalme wa Amani tunaomba utusamehe pale tulipoenda kinyume nawe..Tunajinyenyekeza mbele zako Baba wa Mbinguni..nasi utupe Neema ya kuweza kuwasamehe waliotukosea..
Yahweh..!!Tunaomba ukawaguse/kuwaponya wote wanaopitia Magumu/Majaribu, Wenye Shida/Tabu,Wagonjwa,Wafiwa wakawemfariji wao..Ukawafungue waliokuwa katika vifungo mbalimbali na wapate kupona kimwili na kiroho..

Baba utajaalie Hekima,Busara na Roho Mtakatifu akatuongoze kwenye kunena/kutenda,kuamua,kutambua/kujitambua..tukawe barua njema na tusomeke..ukatufanye chombo chako na tukatumike sawasawa na mapenzi yako..


Asante kwa yote Jehovah...!!Tunayaweka maisha yetu mikononi mwako..Tunashukuru na kukusifu,Tukiamini wewe ni Mungu wetu na Mlinzi wetu..Leo na hata milele..
Amina.Mungu wa amani awakamilishe katika kila tendo jema ili mtekeleze matakwa yake; yeye na afanye ndani yetu kwa njia ya Kristo yale yanayompendeza mwenyewe. Utukufu uwe kwake, milele na milele! Amina.[Waebrania 13:21]

Mose na Aroni mbele ya Farao

1Baadaye, Mose na Aroni walimwendea Farao, wakamwambia, “Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli anasema hivi, ‘Waache watu wangu waondoke, wakanifanyie sikukuu jangwani.’” 2Lakini Farao akawauliza, “Ni nani huyo Mwenyezi-Mungu, hata nimsikilize na kuwaacha Waisraeli waondoke? Mimi simtambui huyo Mwenyezi-Mungu, wala sitawaruhusu Waisraeli waondoke.” 3Mose na Aroni wakamwambia, “Mungu wa Waebrania amekutana nasi. Tunakusihi utuache twende zetu jangwani mwendo wa siku tatu tukamtambikie Mwenyezi-Mungu, Mungu wetu. La sivyo, yeye atatuua kwa maradhi mabaya au vita.” 4Lakini mfalme wa Misri akawajibu, “Enyi Mose na Aroni, kwa nini mnajaribu kuwatoa watu kazini mwao? Rudini kazini mwenu.” 5Tena Farao akasema, “Hawa watu wenu ni wengi kuliko wananchi; mnataka waache kufanya kazi!”
6Siku hiyohiyo Farao aliwaamuru wanyapara pamoja na wasimamizi, akasema, 7“Tangu leo msiwape watu hawa nyasi za kutengenezea matofali kama ilivyo kawaida. Wao wenyewe watakwenda kujitafutia. 8Lakini idadi ya matofali yanayotengenezwa kila siku iwe ileile, wala lisipungue hata tofali moja, kwa kuwa watu hawa ni wavivu ndio maana wanapiga kelele: ‘Tuache twende tukamtambikie Mungu wetu.’ 9Wazidishieni watu hawa kazi ngumu ili waitolee jasho na kuacha kusema maneno ya uongo.”
10Basi, wanyapara na wasimamizi wa watu wakatoka na kuwaambia watu, “Farao anasema hivi, ‘Sitawapeni nyasi. 11Nendeni nyinyi wenyewe mkatafute popote mtakapoweza kuzipata, na wala kazi yenu haitapunguzwa hata kidogo.’” 12Basi, watu wote wakatawanyika kila mahali nchini Misri wakitafuta nyasi za kutengenezea matofali. 13Nao Wanyapara wakakazana wakisema, “Timizeni kazi yenu ya kila siku kama hapo awali mlipoletewa nyasi.” 14Wanyapara Wamisri wakawapiga wasimamizi wa Waisraeli waliochaguliwa kusimamia kazi wakisema, “Kwa nini hamtimizi kazi yenu na kufikisha idadi ileile ya matofali kama awali?”
15Ndipo wasimamizi wa Waisraeli walipomwendea Farao, wakamlilia wakisema, “Kwa nini unatutenda hivi sisi watumishi wako? 16Hatupewi tena nyasi zozote na huku tunalazimishwa kufyatua matofali. Tena sisi watumishi wako tunapigwa, hali kosa ni la watu wako.” 17Lakini Farao akasema, “Wavivu nyinyi; nyinyi ni wavivu, ndio maana mnasema, ‘Tuache twende tukamtambikie Mwenyezi-Mungu’. 18Nendeni sasa mkafanye kazi; maana hamtapewa nyasi zozote na mtafyatua idadi ileile ya matofali.” 19Basi, hao wasimamizi wa Waisraeli sasa walijiona kuwa wako taabuni, kwani waliambiwa, “Hamtaipunguza kamwe idadi ya matofali ya kila siku.”
20Walipoondoka kwa Farao, walikutana na Mose na Aroni ambao walikuwa wanawangojea. 21Basi, wakawaambia Mose na Aroni, “Mwenyezi-Mungu na aone jambo hili na kuwahukumu nyinyi kwa sababu mmetufanya sisi kuwa chukizo kwa Farao na maofisa wake; nyinyi mmewapa sababu ya kutuua.”

Mose anamlalamikia Mwenyezi-Mungu

22Kisha Mose akamgeukia tena Mwenyezi-Mungu, akasema, “Ee Mwenyezi-Mungu, kwa nini unawatendea watu hawa uovu? Kwa nini hata ulinituma? 23Tangu nilipokwenda na kuongea na Farao kwa jina lako, yeye amewatendea uovu watu hawa. Wewe hujafanya lolote kuwakomboa watu wako.”

Kutoka5;1-23

Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)
"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.

No comments: