Swahili na Waswahili

Swahili na Waswahili
Waswahili na Mswahili Rachel Siwa...Pamoja Daima!!

Wednesday 8 March 2017

Kikombe Cha Asubuhi;Mwanzo35....


Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje Wapendwa/Waungwana?
Mtakatifu Mtakatifu Baba wa Mbinguni, Muumba Mbingu na Nchi, Muumba wetu, Muweza wa yote,Mungu wetu na Baba Yetu,Mwokozi na Mponyaji wetu..Tunasema asante Baba kwa kibali chako ulichotupa cha kuendelea kuiona siku hii..Shukrani na utufu ni kwako Baba, Mfalme wa Amani ukatawale siku hii na maisha yetu yawe juu yako,Ukatuongoze tuingiapo/Tutokapo,Hatua zetu ziwe nawe,Ukabariki Kazi zetu,Biashara,Masomo na vyote tunavyoenda kutumia/kugusa Baba ukavitakase na damu ya Mwokozi wetu Bwana wetu Yesu Kristo iliyomwagika kwa ajili yetu..
Ukatusamehe pale tulipoenda kinyume nawe Baba..
Nasi ukatupe kuweza kuwasamehe waliotukosea...
Ukatupe sawasawa na mapenzi yako...
Tukatumike kama chombo chako na kutuongoza katika Kunena/kutenda..

Wema wako ,Fadhili zako, Upendo na Neema/Rehema zisipungue..
Kwakuwa Ufalme ni Wako,Nguvu na Utukufu ni wako Baba..

Wema wa Mungu
5Fadhili zako ee Mwenyezi-Mungu zaenea hata mbinguni;
uaminifu wako wafika mawinguni.
6Uadilifu wako ni kama milima mikubwa,
hukumu zako ni kama vilindi vya bahari.
Wewe, ee Mwenyezi-Mungu, wawalinda wanadamu na wanyama
7Jinsi gani zilivyo bora fadhili zako!
Wanadamu hukimbilia kivulini mwa mabawa yako.
8Wawashibisha kwa utajiri wa nyumba yako;
wawanywesha kutoka mto wa wema wako.
9Wewe ndiwe asili ya uhai;
kwa mwanga wako twaona mwanga.
10Uendelee kuwafadhili wale wanaokutambua;
uzidi kuwa mwema kwa wanyofu wa moyo.
11Usikubali wenye majivuno wanivamie,
wala watu waovu wanikimbize.
12Kumbe watendao maovu wameanguka;
wameangushwa chini, hawawezi kuinuka.
                   [Zaburi 36:5-12]
Tunashukuru na kukusifu..Tunajiachilia mikononi mwako Baba wa mbinguni, Tukishukuru na kuamini wewe ni Bwana na Mwokozi wetu..
Amina....!!!!

Yakobo anahamia Betheli

1Siku moja, Mungu alimwambia Yakobo, “Anza safari, uende kuishi Betheli na kunijengea humo mahali pa kunitambikia mimi Mungu niliyekutokea wakati ulipomkimbia kaka yako Esau.” 2Basi, Yakobo akawaambia jamaa yake na wote aliokuwa nao, “Tupilieni mbali sanamu za miungu ya kigeni mlizo nazo, mjitakase na kubadili mavazi yenu. 3Kisha, tutakwenda Betheli ili nimjengee mahali pa kumtambikia Mungu aliyenisaidia siku ya taabu, Mungu ambaye amekuwa nami popote nilipokwenda.” 4Basi, wakampa Yakobo sanamu zote za miungu ya kigeni walizokuwa nazo pamoja na vipuli walivyokuwa wamevaa masikioni; naye akavifukia chini ya mwaloni uliokuwa karibu na Shekemu.
5Yakobo na wanawe walipokuwa wanasafiri, Mungu aliwatia hofu wenyeji wa miji yote ya jirani hata hawakuthubutu kuwafuatia. 6Basi, Yakobo akawasili Luzu yaani Betheli katika nchi ya Kanaani, pamoja na watu wote aliokuwa nao. 7Akajenga hapo madhabahu na kupaita El-betheli kwani hapo ndipo mahali Mungu alipojionesha kwake wakati alipokuwa akimkimbia kaka yake. 8Debora, mlezi wa Rebeka, alifariki, akazikwa chini ya mwaloni upande wa kusini wa Betheli. Kwa hiyo Yakobo akauita mji huo Alon-bakuthi.
9Baada ya Yakobo kurudi kutoka Padan-aramu, Mungu alimtokea tena na kumbariki. 10Mungu alimwambia, “Jina lako ni Yakobo, lakini hutaitwa hivyo tena, bali sasa jina lako litakuwa Israeli.” Kwa hiyo Yakobo akaitwa Israeli. 11Tena Mungu akamwambia, “Mimi ndimi Mungu mwenye nguvu. Ujaliwe wazawa wengi; kwako wewe kutatokea taifa, mataifa na wafalme. 12Nchi niliyowapa Abrahamu na Isaka, nitakupa wewe na wazawa wako.” 13Basi, baada ya kuongea na Yakobo, Mungu akamwacha na kupanda juu. 14Yakobo akasimika nguzo ya jiwe la ukumbusho mahali hapo Mungu alipozungumza naye, akaiweka wakfu kwa kuimiminia tambiko ya kinywaji na mafuta. 15Basi, Yakobo akapaita mahali hapo alipozungumza na Mungu Betheli.

Kuzaliwa kwa Benyamini na kifo cha Raheli

16Yakobo na jamaa yake yote waliendelea na safari yao kutoka Betheli. Walipokuwa umbali fulani kabla ya kufika Efratha, Raheli akashikwa na uchungu mkali wa kuzaa. 17Naye alipokuwa katika uchungu huo, mkunga akamwambia, “Usiogope, umepata mtoto mwingine wa kiume.” 18Raheli huku akikata roho, akampa huyo mtoto jina Ben-oni. Lakini baba yake akamwita mtoto huyo Benyamini. 19Basi, Raheli akafariki na kuzikwa kando ya njia iendayo Efratha (yaani Bethlehemu). 20Yakobo akasimika nguzo ya kumbukumbu juu ya kaburi la Raheli ambayo ipo mpaka leo. 21Israeli akaendelea na safari yake na kupiga kambi yake baada ya kuupita mnara wa Ederi.
22Wakati Israeli alipokuwa anakaa nchini humo, mwanawe Reubeni, alilala na Bilha, suria wa baba yake; naye Israeli akasikia habari hizo.

Wana wa Yakobo

(1Nya 2:1-2)

Yakobo alikuwa na watoto wa kiume kumi na wawili. 23Wana wa Lea walikuwa Reubeni, mzaliwa wa kwanza wa Yakobo, Simeoni, Lawi, Yuda, Isakari na Zebuluni. 24Watoto wa kiume wa Raheli walikuwa Yosefu na Benyamini. 25Watoto wa kiume waliozaliwa na Bilha, mjakazi wa Raheli, walikuwa Dani na Naftali. 26Na watoto wa kiume waliozaliwa na Zilpa, mjakazi wa Lea, walikuwa Gadi na Asheri. Hao ndio watoto wa kiume wa Yakobo, aliowazaa alipokuwa kule Padan-aramu.

Kifo cha Isaka

27Yakobo aliondoka akaenda Mamre kwa baba yake Isaka, huko Kiriath-arba, yaani Hebroni, mahali ambapo Abrahamu na Isaka walikaa kama wageni. 28Isaka alikuwa na miaka 180 29akafariki akiwa mzee wa miaka mingi. Watoto wake, Esau na Yakobo wakamzika.
Mwanzo35;1-29
Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN):
Jifunze zaidi

"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.

No comments: