Swahili na Waswahili

Swahili na Waswahili
Waswahili na Mswahili Rachel Siwa...Pamoja Daima!!

Wednesday, 26 May 2021

Kikombe Cha Asubuhi; Tunamshukuru Mungu kwa kumaliza Kitabu cha Tito Leo Tunaanza Kitabu cha Filemoni....1

 Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?

Tunamshukuru Mungu kwa kutupa kibali cha
 kupitia kitabu cha "Tito
"
Ni matumaini yangu kuna mengi tumejifunza/kufaidika
na kutupa mwanga/kuelewa kwenye kitabu hiki...

Leo tunapokwenda anza kupitia Kitabu cha"Filemoni"
tunamuomba Mungu wetu akatupe kibali,macho ya rohoni
 na akili ya kuelewa katika kujifunza NENO lake...
Ee Mungu  tunaomba ukatuongoze...!!
Tumshukuru Mungu wetu katika yote...

Mungu wetu Baba yetu,Muumba wetu Muumba wa Mbingu na Nchi
Muumba wa vyote vilivyomo vinavyoonekana na visivyoonekana
Mungu wa walio hai,Mungu  mwenye huruma,Mungu wa upendo
Mungu wa Abrahamu,Isaka na Yakobo...


Asante kwa wema na fadhili zako kwetu
Asante kwa ulinzi wako kwetu wakati wote
Asante kwa kutuchagua tena na kutupa
kibali cha kuendelea kuiona leo hii
Asante kwa pumzi/uzima,afya na kuwatayari kwa majukumu yetu

Neema yako yatutosha ee Mungu wetu....!!

Mbinguni, nani awezaye kunisaidia ila wewe? Na duniani hamna ninachotamani ila wewe!

Zaburi 73:25

Baba wa Mbinguni tunakuja mbele zako,
Tukijinyenyekeza,tukijiachilia mikononi mwako
Mungu wetu tunamomba utusamehe dhambi zetu
Baba wa Mbinguni nasi tunaomba ukatupe neema
 ya kuweza kuwasamehe wale wote waliotukosea

Usitutie majaribuni Mungu wetu tunaomba utuepushe
na yule mwovu na kazi zake zote
Jehovah ututakase miili yetu na akili zetu
Baba wa Mbinguni tunaomba utufunike kwa Damu
ya Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo wa Nazareti
yeye aliteseka kwanza ili sisi tupate kupona...

Hata nikikosa nguvu mwilini na rohoni, wewe, ee Mungu, u mwamba wangu; riziki yangu kuu ni wewe milele. Anayejitenga nawe, hakika ataangamia. Anayekukana, utamwangamiza.

Zaburi 73:26-27

Yahweh tunayaweka maisha yetu mikononi mwako
Mungu wetu tunaomba ukabariki nyumba/ndoa zetu,
Jehovah tunaomba ulinzi wako kwetu na kwa vyote tunavyovimiliki
Yahweh tunaomba ukatubariki tuingiapo/tutokapo
Mungu wetu tunaomba ukavibariki vyote tunavyoenda kugusa/kutumia
Baba wa Mbinguni ukavitakase kwa Damu ya Bwana wetu Yesu Kristo
Mungu wetu ukatamalaki na kutuatamia
Baba wa Mbinguni tukawe salama rohoni
Yahwe ukatupe akili ya kutambua mema na mabaya
Mfalme wa amani amani yako ikatawale katika maisha yetu
Mungu wetu ukatupe macho ya kuona,masikio ya kusikia sauti yako na kuitii..
Baba wa Mbinguni  tunaomba ukatupe neema ya kufuata
njia zako,tukasimamie Neno lako,amri na sheria zako
siku zote za maisha yetu...
Ukatuguse kwa mkono wako wenye nguvu,ukatufanye chombo chema
ee Mungu wetu nasi tukatumike kama inavyokupendeza wewe
Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi....

Lakini, kwangu ni vema kuwa karibu na Mungu, wewe Bwana Mwenyezi-Mungu ndiwe usalama wangu. Nitatangaza mambo yote uliyotenda!

Zaburi 73:28

Tazama watoto wako wenye shida/tabu,wote wanaopitia magumu/majaribu mbalimbali
Mungu wetu tunaomba ukawaguse kwa mkono wako wenye nguvu
kila mmoja na mahitaji yake
Mungu wetu tunaomba ukawasamehe pale walipo kwenda kinyume nawe
Yahweh tunaomba ukawape neema ya kuweza kujiombea,kufuata njia zako nazo zikawaweke huru...
Baba wa Mbinguni tunayaweka haya yote mikononi mwako
Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele...
Amina...!!


Asanteni sana wapendwa katika Kristo Yesu kwakuwa nami,
Baba wa Mbinguni aendelee kuwatendea sawasawa na mapenzi yake...
Nawapenda.


1Mimi Paulo, mfungwa kwa ajili ya Kristo Yesu, na ndugu Timotheo, ninakuandikia wewe Filemoni mpendwa, mfanyakazi mwenzetu, 2na kanisa linalokutana nyumbani kwako, na wewe dada Afia, na askari mwenzetu Arkipo.

3Tunawatakieni neema na amani kutoka kwa Mungu Baba yetu, na kwa Bwana Yesu Kristo.
Upendo na imani ya Filemoni
4Kila wakati ninaposali, nakukumbuka wewe Filemoni, na kumshukuru Mungu, 5maana nasikia habari za imani yako kwa Bwana Yesu na upendo wako kwa watu wote wa Mungu. 6Naomba ili imani hiyo unayoshiriki pamoja nasi ikuwezeshe kuwa na ujuzi mkamilifu zaidi wa baraka zote tunazopata katika kuungana kwetu na Kristo. 7Ndugu, upendo wako umeniletea furaha kubwa na kunipa moyo sana! Nawe umeichangamsha mioyo ya watu wa Mungu.
Ombi kwa ajili ya Onesimo
8Kwa sababu hiyo, ningeweza, kwa uhodari kabisa, nikiwa ndugu yako katika kuungana na Kristo, kukuamuru ufanye unachopaswa kufanya. 9Lakini kwa sababu ya upendo, ni afadhali zaidi nikuombe. Nafanya hivi ingawa mimi ni Paulo, balozi wa Kristo Yesu, na sasa pia mfungwa kwa ajili yake. 10Basi, ninalo ombi moja kwako kuhusu mwanangu Onesimo, ambaye ni mwanangu katika Kristo kwani nimekuwa baba yake nikiwa kifungoni. 11Ni Onesimo yuleyule ambaye wakati mmoja alikuwa hakufai kitu, lakini sasa ananifaa mimi na wewe pia.
12Sasa namrudisha kwako, naye ni kama moyo wangu mimi mwenyewe. 13Ningependa akae nami hapa anisaidie badala yako wakati niwapo kifungoni kwa sababu ya Injili. 14Lakini sitafanya chochote bila kibali chako. Sipendi kukulazimisha unisaidie, kwani wema wako unapaswa kutokana na hiari yako wewe mwenyewe na si kwa kulazimika.
15Labda Onesimo aliondoka kwako kwa kitambo tu, kusudi uweze tena kuwa naye daima. 16Na sasa yeye si mtumwa wa kawaida, ila ni bora zaidi ya mtumwa: Yeye ni ndugu yetu mpenzi. Ni wa maana sana kwangu mimi, na kwako atakuwa wa maana zaidi, kama mtumwa na kama ndugu katika Bwana.
17Basi, ikiwa wanitambua mimi kuwa mwenzako, mpokee tena kama vile ungenipokea mimi mwenyewe. 18Kama alikuwa amekukosea kitu, au alikuwa na deni lako, basi, unidai mimi. 19Naandika jambo hili kwa mkono wangu mwenyewe: Mimi Paulo nitalipa! (Tena sina haja ya kusema kwamba wewe unalo deni kwangu la nafsi yako). 20Naam, ndugu yangu, nifanyie jambo hilo kwa ajili ya jina la Bwana; burudisha moyo wangu kama ndugu katika Kristo.
21Naandika nikitumaini kwamba utanikubalia ombi langu; tena najua kwamba utafanya hata zaidi ya haya ninayokuomba. 22Pamoja na hayo, nitayarishie chumba kwani natumaini kwamba kwa sala zenu, Mungu atanijalia niwatembeleeni.
Salamu za mwisho
23Epafra, mfungwa mwenzangu kwa ajili ya Kristo Yesu, anakusalimu. 24Nao akina Marko, Aristarko, Dema na Luka, wafanyakazi wenzangu, wanakusalimu.
25Nawatakieni nyinyi nyote neema ya Bwana Yesu Kristo.
Filemoni1;1-25
Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)
"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe

No comments: