Swahili na Waswahili

Swahili na Waswahili
Waswahili na Mswahili Rachel Siwa...Pamoja Daima!!

Wednesday 19 May 2021

Kikombe Cha Asubuhi; Kitabu cha 2Timotheo....3


Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?

Tumshukuru Mungu katika yote....

Mungu wetu Baba yetu,Muumba wetu Muumba wa Mbingu na Nchi
Muumba wa vyote vilivyomo vinavyoonekana na visivyoonekana
Mungu wa walio hai,Mungu  mwenye huruma,Mungu wa upendo
Mungu wa Abrahamu,Isaka na Yakobo...
Asante kwa wema na fadhili zako kwetu
Asante kwa ulinzi wako kwetu wakati wote
Asante kwa kutuchagua tena na kutupa
kibali cha kuendelea kuiona leo hii
Asante kwa pumzi/uzima,afya na kuwatayari kwa majukumu yetu

Neema yako yatutosha ee Mungu wetu...


Alipotukanwa yeye hakujibu kwa tukano; alipoteseka yeye hakutoa vitisho, bali aliyaweka matumaini yake kwa Mungu, hakimu mwenye haki.

1 Petro 2:23

Baba wa Mbinguni tunakuja mbele zako,
Tukijinyenyekeza,tukijiachilia mikononi mwako
Mungu wetu tunamomba utusamehe dhambi zetu
Baba wa Mbinguni nasi tunaomba ukatupe neema
 ya kuweza kuwasamehe wale wote waliotukosea

Usitutie majaribuni Mungu wetu tunaomba utuepushe
na yule mwovu na kazi zake zote
Jehovah ututakase miili yetu na akili zetu
Baba wa Mbinguni tunaomba utufunike kwa Damu
ya Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo wa Nazareti
yeye aliteseka kwanza ili sisi tupate kupona....

Yeye mwenyewe alizibeba dhambi zetu katika mwili wake juu ya msalaba, tupate kufa kuhusu dhambi, na kuishi kwa ajili ya uadilifu. Kwa majeraha yake, nyinyi mmeponywa.

1 Petro 2:24

Mungu wetu tunaomba ukabariki kazi za mikono yetu
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe ubunifu na maarifa katika utendaji
Jehovah nasi tukatende sawasawa na mapenzi yako
Yahweh tunaomba ukabariki ridhiki zetu ziingiazo/zitokazo
Mungu wetu nasi tunaomna ukatupe neema ya kuweza kuwabariki wenye kuhitaji
Tusipungukiwe katika mahitaji yetu
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe kama inavyokupendeza wewe...


Yahweh tunayaweka maisha yetu mikononi mwako
Mungu wetu tunaomba ukabariki nyumba/ndoa zetu,
Jehovah tunaomba ulinzi wako kwetu na kwa vyote tunavyovimiliki
Yahweh tunaomba ukatubariki tuingiapo/tutokapo
Mungu wetu tunaomba ukavibariki vyote tunavyoenda kugusa/kutumia
Baba wa Mbinguni ukavitakase kwa Damu ya Bwana wetu Yesu Kristo
Mungu wetu ukatamalaki na kutuatamia
Baba wa Mbinguni tukawe salama rohoni
Yahwe ukatupe akili ya kutambua mema na mabaya
Mfalme wa amani amani yako ikatawale katika maisha yetu
Mungu wetu ukatupe macho ya kuona,masikio ya kusikia sauti yako na kuitii..
Baba wa Mbinguni  tunaomba ukatupe neema ya kufuata
njia zako,tukasimamie Neno lako,amri na sheria zako
siku zote za maisha yetu...
Ukatuguse kwa mkono wako wenye nguvu,ukatufanye chombo chema
ee Mungu wetu nasi tukatumike kama inavyokupendeza wewe
Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi....

Nyinyi mlikuwa kama kondoo waliokuwa wamepotea; lakini sasa mmemrudia Mchungaji na Mlinzi wa roho zenu.

1 Petro 2:25

Tazama watoto wako wenye shida/tabu,wote wanaopitia magumu/majaribu mbalimbali
Mungu wetu tunaomba ukawaguse kwa mkono wako wenye nguvu
kila mmoja na mahitaji yake
Mungu wetu tunaomba ukawasamehe pale walipo kwenda kinyume nawe
Yahweh tunaomba ukawape neema ya kuweza kujiombea,kufuata njia zako nazo zikawaweke huru...
Baba wa Mbinguni tunayaweka haya yote mikononi mwako
Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele...
Amina...!!


Asanteni sana wapendwa katika Kristo Yesu kwakuwa nami,
Baba wa Mbinguni aendelee kuwatendea sawasawa na mapenzi yake...
Nawapenda. Siku ya mwisho

1Kumbuka kwamba, katika siku za mwisho kutakuwa na nyakati za taabu. 2Watu watakuwa na ubinafsi, wenye tamaa ya fedha, wenye majivuno, wenye kujiona, wenye kumtukana Mungu, wasiowatii wazazi wao, wasio na shukrani na waovu; 3watatokea watu wasio na upendo moyoni, wasio na huruma, wachongezi, walafi na wakali; watachukia chochote kilicho chema; 4watakuwa wahaini, wakaidi na waliojaa kiburi; watapenda anasa kuliko kumpenda Mungu. 5Kwa nje wataonekana kama watu wenye kumcha Mungu, lakini wataikana nguvu yake. Jiepushe kabisa na watu wa namna hiyo. 6Baadhi yao huenda katika nyumba za watu na huwateka wanawake dhaifu waliolemewa mizigo ya dhambi na ambao wanaongozwa na tamaa za kila aina; 7wanawake ambao wanajaribu daima kujifunza lakini hawawezi kuufikia ujuzi wa huo ukweli. 8Watu hao huupinga ukweli kama vile Yane na Yambre walivyompinga Mose. Hao ni watu wa akili potovu na imani ya uongo. 9Lakini hawataweza kuendelea zaidi kwa maana upumbavu wao utaonekana wazi kwa wote. Ndivyo ilivyokuwa kwa akina Yane na Yambre.
Maagizo ya Mwisho
10Wewe, lakini, umeyafuata mafundisho yangu, mwenendo wangu, makusudi yangu katika maisha, imani yangu, uvumilivu wangu, upendo wangu, subira yangu, 11udhalimu na mateso. Unayajua mambo yaliyonipata huko Antiokia, Ikonio na Lustra. Nilivumilia udhalimu mkubwa mno! Lakini Bwana aliniokoa katika mambo hayo yote. 12Kila mtu anayetaka kuishi maisha ya kumcha Mungu katika kuungana na Kristo Yesu lazima adhulumiwe. 13Watu waovu na wadanganyifu wataendelea kuwa wabaya, wakidanganya wengine, na wao wenyewe wakidanganywa. 14Lakini wewe dumu katika ukweli ule uliofundishwa ukaukubali kabisa. Wawajua wale waliokuwa waalimu wako, 15wakumbuka kwamba tangu utoto wako umejua Maandiko Matakatifu ambayo yaweza kukupatia hekima iletayo wokovu kwa njia ya imani kwa Kristo Yesu. 16Maandiko yote Matakatifu yameandikwa kwa uongozi wa Mungu, na yanafaa katika kufundishia ukweli, kuonya, kusahihisha makosa, na kuwaongoza watu waishi maisha adili, 17ili mtu wa Mungu awe mkamilifu, na tayari kabisa kufanya kila kazi njema.
2Timotheo3;1-17
Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)
"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe

No comments: