Swahili na Waswahili

Swahili na Waswahili
Waswahili na Mswahili Rachel Siwa...Pamoja Daima!!

Tuesday, 4 December 2018

Kikombe Cha Asubuhi ;Zaburi 9...


Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?

Tumshukuru Mungu katika yote....

Mungu wetu Baba yetu,Muumba wetu Muumba wa Mbingu na Nchi
Muumba wa vyote vilivyomo vinavyoonekana na visivyoonekana
Mungu wa walio hai,Mungu  mwenye huruma,Mungu wa upendo
Mungu wa Abrahamu,Isaka na Yakobo..
Yahweh..!Jehovah..! Adonai..!Elohim..!El Olam..!El Qanna..!
El Elyon..!El shaddai..!Emanueli...!-Mungu pamoja nasi...
Unastahili sifa Mungu wetu,Unastahili kuabudiwa Jehovah,
Unastahili kuhimidiwa Yahweh,Unastahili Kutukuzwa Baba wa Mbinguni....!Asante kwa wema na fadhili zako kwetu
Asante kwa ulinzi wako kwetu wakati wote
Asante kwa kutuchagua tena na kutupa
kibali cha kuendelea kuiona leo hii
Asante kwa pumzi/uzima,afya na kuwatayari kwa majukumu yetu

Neema yako yatutosha ee Mungu wetu....!!

Mungu alifanya miujiza ya ajabu kwa mikono ya Paulo. Watu walikuwa wakichukua leso na nguo nyingine za kazi ambazo Paulo alikuwa amezitumia, wakazipeleka kwa wagonjwa, nao wakaponywa magonjwa yao; na wale waliokuwa na pepo wabaya wakatokwa na pepo hao. Wayahudi kadhaa wenye kupunga pepo wabaya walisafiri huko na huko wakijaribu kulitumia jina la Bwana Yesu kwa wale waliokuwa wamepagawa na pepo wabaya. Walikuwa wakisema: “Ninawaamuru kwa jina la Yesu ambaye Paulo anamhubiri.”

Baba wa Mbinguni tunakuja mbele zako tukijinyenyekeza,tukijishusha na kujiachilia mikononi mwako
Mungu wetu tunaomba utusamehe dhambi zetu zote tulizo zifanya
Kwakuwaza,kwakunena,kwakutenda,kwakujua/kutojua
Baba wa Mbinguni nasi tunaomba ukatupe neema
ya kuweza kuwasamehe wale wote waliotukosea
Usitutie majaribu Mungu wetu tunaomba utuepushe
na yule mwovu na kazi zake zote
Jehovah ututakase miili yetu na akili zetu
Baba wa Mbinguni tunaomba utufunike kwa Damu
ya Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo wa Nazaretiyeye aliteseka kwanza ili sisi tupate kupona....

Watoto saba wa Skewa, kuhani mkuu wa Kiyahudi, walikuwa miongoni mwa hao waliokuwa wanafanya hivyo. Lakini pepo mbaya aliwajibu, “Ninamfahamu Yesu, ninamjua pia Paulo, lakini nyinyi ni nani?” Kisha yule mtu aliyepagawa aliwarukia wote kwa kishindo, akawashinda nguvu. Na hao watoto wa Skewa wakakimbia kutoka ile nyumba wakiwa uchi na wamejaa majeraha. Kila mtu huko Efeso, Myahudi na asiye Myahudi, alisikia juu ya tukio hilo. Wote waliingiwa na hofu, wakalitukuza jina la Bwana Yesu.

Mungu wetu tunaomba ukabariki kazi za mikono yetu
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe ubunifu na maarifa katika utendaji

Jehovah nasi tukatende sawasawa na mapenzi yako
Yahweh tunaomba ukabariki ridhiki zetu ziingiazo/zitokazo
Mungu wetu nasi tunaomba ukatupe neema ya kuweza
kuwabariki wenye kuhitaji
Tusipungukiwe katika mahitaji yetu Baba wa Mbinguni
tunaomba ukatupe kama inavyokupendeza wewe....Yahweh  tunayaweka maisha yetu mikononi mwako
Mungu wetu tunaomba ukabariki nyumba/ndoa zetu,
watoto,wazazi wetu,familia/ndugu na wote wanaotuzunguka
Jehovah tunaomba ulinzi wako kwetu na kwa vyote tunavyo vimiliki
Yahweh tunaomba ukatubariki tuingiapo/tutokapo
Mungu wetu tunaomba ukavibariki vyote tunavyoenda kugusa/kutumia
Baba wa Mbinguni ukavitakase kwa Damu ya Bwana wetu Yesu Kristo
Mungu wetu ukatamalaki na kutuatamia
Baba wa Mbinguni tukawe salama rohoni

Yahweh ukatupe akili ya kutambua mema na mabaya
Mfalme wa amani amani yako ikatawale katika maisha yetu
Mungu wetu ukatupe macho ya kuona na masikio ya kusikia 
sauti yako na kuitii
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe neema ya kufuata njia zako
Yahweh tukasimamie Neno lako amri na sheria zako siku zote 
za maisha yetu
Mungu wetu ukaonekane katika maisha yetu
Baba wa Mbinguni tukanene yaliyo yako
Neema zako zikawe nasi Nuru yako ikaangaze katika maisha yetu
ukatuguse kwa mkono wako wenye nguvu
Ukatufanye chombo chema ee Mungu wetu nasi tukatumike kama
inavyokupendeza wewe
Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi...

Waumini wengi walijitokeza wakakiri hadharani mambo waliyokuwa wametenda. Wengine waliokuwa wameshughulikia mambo ya uchawi hapo awali, walikusanya vitabu vyao, wakavichoma mbele ya wote. Walikisia gharama ya vitabu hivyo, wakaona yafikia vipande 50,000 vya fedha. Kwa namna hiyo, neno la Bwana lilizidi kuenea na kuwa na nguvu zaidi.

Tazama watoto wako wanaokutafuta/kukuomba kwa bidii na imani, Mungu wetu tunawaweka mikononi mwako wenye shida/tabu,
wote wanaopitia magumu/majaribu mbalimbali
Mungu wetu tunaomba ukawaguse kwa mkono wako wenye nguvu
kila mmoja na mahitaji yake
Baba wa Mbinguni tunaomba ukaonekane katika maisha yao
Mungu wetu tunaomba ukawasamehe pale walipokwenda
kinyume nawe Yahweh tunaomba ukawape neema ya kujiombea
Kufuata njia zako nazo zikawaweke huru
Ukawape macho ya rohoni ee Mungu wetu na masikio ya kusikia
sauti yako,Ukawaokoe na kuwalinda,ukawaponye kimwili na kiroho
Nuru yako ikaangaze katika maisha yao,Amani ikatawale katika maisha yao,Upendo ukadumu kati yao
 

Baba wa Mbinguni tunayaweke haya yote mikono mwako
tukiamini Mungu wetu utawatendea sawasawa na mapenzi yako
Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele
Amina...!!Asanteni sana wapendwa katika Kristo Yesu
kwakuwanami/kunisoma Mungu Baba aendelee
kuwabariki na kuwatendea kama inavyompendeza yeye
Amani ya Bwana wetu Yesu Kristo na Upendo wa Mungu Baba
ukae nanyi daima
Nawapenda. 

Shukrani kwa Mungu

(Kwa Mwimbishaji: Mtindo wa Muth-labeni. Zaburi ya Daudi)
1Nitakushukuru Mungu kwa moyo wangu wote;
nitayasimulia matendo yako yote ya ajabu.
2Nitafurahi na kushangilia kwa sababu yako;
nitaliimbia sifa jina lako, ewe Mungu Mkuu.
3Wakati ulipotokea, maadui zangu walirudi nyuma,
walijikwaa na kuangamia.
4Umenitetea kuhusu kisa changu cha haki;
umeketi katika kiti chako cha enzi,
ukatoa hukumu iliyo sawa.
5Umeyakemea mataifa,
umewaangamiza waovu;
majina yao umeyafutilia mbali milele.
6Maadui wameangamia milele;
umeingolea mbali miji yao,
kumbukumbu lao limetoweka.
7Lakini Mwenyezi-Mungu anatawala milele;
ameweka kiti chake cha enzi apate kuhukumu.
8Anauhukumu ulimwengu kwa haki;
anayaamua mataifa kwa unyofu.
9Mwenyezi-Mungu ni ngome ya watu wanaoonewa;
yeye ni ngome nyakati za taabu.
10Wanaokujua wewe, ee Mungu hukutegemea,
wewe Mwenyezi-Mungu huwatupi wakutafutao.
11Mwimbieni sifa Mwenyezi-Mungu akaaye Siyoni.
Yatangazieni mataifa mambo aliyotenda!
12Mungu hulipiza kisasi kwa umwagaji damu;
kamwe hasahau kilio cha wanaoonewa.
13Unirehemu, ee Mwenyezi-Mungu!
Ona mateso ninayoteswa na wanaonichukia;
wewe waninyakua kutoka nguvu za kifo,
14nisimulie sifa zako mbele ya watu wa Siyoni,
nipate kushangilia kwa sababu umeniokoa.
15Watu wa mataifa wametumbukia katika shimo walilochimba,
wamenaswa miguu katika wavu waliouficha.
16Mwenyezi-Mungu amejionesha alivyo;
ametekeleza hukumu.
Watu waovu wamenaswa kwa matendo yao wenyewe.
17Waovu wataishia kuzimu;
naam, mataifa yote yanayomsahau Mungu.
18Lakini fukara hawatasahauliwa daima;
tumaini la maskini halitapotea milele.
19Inuka, ee Mwenyezi-Mungu!
Usimwache binadamu ashinde.
Uyakusanye mataifa mbele yako, uyahukumu.
20Uyatie hofu, ee Mwenyezi-Mungu,
watu wa mataifa watambue kuwa wao ni watu tu!Zaburi9;1-20

Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)

"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.

No comments: