Swahili na Waswahili

Swahili na Waswahili
Waswahili na Mswahili Rachel Siwa...Pamoja Daima!!

Monday 27 August 2018

Kikombe Cha Asubuhi ; Nehemia 3...


Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?

Haleluyah ni siku/wiki nyingine tena Mungu wetu ametuchagua
na kutupa kibali cha kuendelea kuiona leo hii
Si kwamba sisi tumetenda mema sana wala si kwa nguvu zetu
si kwa utashi wetu wala si kwa akili zetu si kwamba sisi
ni wazuri mno si kwa uwezo wetu sisi kuwa hivi tulivyo leo hii
Ni kwa rehema/neema zake ni kwa mapenzi yake Mungu wetu....

Tumshukuru Mungu wetu katika yote...

Asante Mungu wetu kwa wema na fadhili zako kwetu
Asante kwa ulinzi wako kwetu wakati wote
Asante kwa pumzi/uzima,afya na kuwa tayari kwa majukumu yetu
Sifa na Utukufu tunakurudshia Mungu wetu....!!



Mikono yako iliniumba na kuniunda; unijalie akili nijifunze amri zako. Wakuchao wataniona na kufurahi, maana tumaini langu liko katika neno lako. Najua hukumu zako ni adili, ee Mwenyezi-Mungu, na kwamba umeniadhibu kwani wewe ni mwaminifu. Fadhili zako na zinipe faraja, kama ulivyoniahidi mimi mtumishi wako. Unionee huruma nipate kuishi, maana sheria yako ni furaha yangu. Wenye kiburi waaibike kwa maana wamenifanyia hila, lakini mimi nitazitafakari kanuni zako. Wote wakuchao na waje kwangu, wapate kuyajua maamuzi yako. Moyo wangu na uzingatie masharti yako, nisije nikaaibishwa.



Tazama jana imepita ee Mungu wetu leo ni siku mpya na kesho ni siku nyingine
Jehovah tunakuja mbele zako tukijinyenyekeza,tukijishusha na kujiachilia mikononi mwako
 Mungu wetu tunaomba utusamehe dhambi zetu zote tulizozifanya kwakuwaza,kwakunena,kwakutenda,kwakujua/kutojua
Baba wa Mbinguni nasi tunaomba utupe neema ya kuweza kuwasamehe wale wote waliotukosea
Jehovah usitutie majaribu Mungu wetu tunaomba utuepushe na yule mwovu na kazi zake zote
Yahweh tunaomba ututakase miili yetu na akili zetu
Baba wa Mbinguni utufunike kwa Damu ya Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo wa Nazareti
yeye aliteseka kwanza ili sisi tupate kupona
Kwakupigwa kwake sisi tumepata kupona...

Niko hoi kwa kukungojea uniokoe; naweka tumaini langu katika neno lako. Macho yangu yanafifia nikingojea ulichoahidi. Nauliza: “Utakuja lini kunifariji?” Nimekunjamana kama kiriba katika moshi, hata hivyo sijasahau masharti yako. Mimi mtumishi wako nitasubiri mpaka lini? Utawaadhibu lini wale wanaonidhulumu? Wenye kiburi wamenichimbia mashimo, watu ambao hawafuati sheria yako. Amri zako zote ni za kuaminika; watu wananitesa bila haki; unisaidie! Karibu wangefaulu kuniangamiza, lakini mimi sijavunja kanuni zako. Unisalimishe kadiri ya fadhili zako, nipate kuzingatia maamuzi uliyotamka.


Yahweh tunaomba ukabariki kazi za mikono yetu
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe ubunifu na maarifa 
katika utendaji
Jehovah nasi tukatende sawasawa na mapenzi yako
Baba wa Mbinguni tunaomba ukabariki ridhiki zetu
ziingiazo/zitokazo
Mungu wetu nasi tunaomba ukatupe neema ya kuweza
kuwabariki wenye kuhitaji
Yahweh tusipungukiwe katika mahitaji yetu
Mungu wetu ukatupe kama inavyokupendeza wewe

Baba wa Mbinguni tunayaweka maisha yetu mikononi mwako
Mungu wetu tunaomba ukabariki nyumba/ndoa zetu,
watoto,wazazi wetu,familia/ndugu na wote wanaotuzunguka
Jehovah tunaomba ulinzi wako kwetu na kwa vyote tunavyo vimiliki
Yahweh tunaomba ukatubariki tuingiapo/tutokapo
Mungu wetu tunaomba ukavibariki vyote tunavyoenda kugusa/kutumia
Baba wa Mbinguni ukavitakase kwa Damu ya Bwana wetu Yesu Kristo
Mungu wetu ukatamalaki na kutuatamia
Baba wa Mbinguni tukawe salama rohoni
Mfalme wa amani amani yako ikatawale katika maisha yetu
Mungu wetu ukatupe macho ya kuona na masikio ya kusikia 
sauti yako na kuitii
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe neema ya kufuata njia zako
Yahweh tukasimamie Neno lako amri na sheria zako siku zote 
za maisha yetu
Mungu wetu ukaonekane katika maisha yetu
Neema zako zikawe nasi Nuru yako ikaangaze katika maisha yetu
ukatuguse kwa mkono wako wenye nguvu
Ukatufanye chombo chema ee Mungu wetu nasi tukatumike kama
inavyokupendeza wewe
Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi...



Neno lako, ee Mwenyezi-Mungu, ladumu milele; limethibitika juu mbinguni. Uaminifu wako wadumu vizazi vyote, umeiweka dunia mahali pake nayo yadumu. Kwa amri yako viumbe vyote vipo leo, maana vitu vyote ni watumishi wako. Kama sheria yako isingekuwa furaha yangu, ningalikwisha angamia kwa taabu zangu. Sitasahau kamwe kanuni zako, maana kwa hizo umenipa uhai. Mimi ni wako, uniokoe, maana nimejitahidi kuzishika kanuni zako. Waovu wanivizia wapate kuniua; lakini mimi natafakari masharti yako. Nimetambua kila kitu hufikia kikomo, lakini amri yako ni kamilifu.


Mungu wetu tunawaweka mikononi mwako wenye shida/tabu,wote wanaopotia magumu/majaribu mbalimbali
watoto wako wanaokuomba kwa bidii na imani
Mungu wetu tunaomba ukawaguse kwa mkono wako wenye nguvu
 kila mmoja na mahitaji yake 
Yahweh tunaomba ukaonekane katika maisha yao
Jehovah tunaomba ukawaokoe,ukawavushe salama na  kuwalinda
Mungu wetu tunaomba ukawasamehe pale walipokwenda kinyume nawe
Baba wa Mbinguni ukawape neema ya kujiombea,kufuata njia zako
wakasimaie Neno lako nalo likaweke huru
Mungu wetu tunaomba ukasikie kuomba kwetu
Baba wa Mbinguni ukapokee sala/maombi yetu
Mungu wetu ukawatendee sawasawa na mapenzi yako
Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele
Amina...!!

Asanteni sana wapendwa katika Kristo Yesu kwakuwa nami
Mungu Baba aendelee kuwabariki na kuwatendea 
kama inavyompendeza yeye....
Nawapenda.

Ukuta wa Yerusalemu unajengwa upya

1Basi Lango la Kondoo lilijengwa upya na Eliashibu, kuhani mkuu, pamoja na ndugu zake waliokuwa makuhani. Waliliweka wakfu na kutia milango yake; wakaliweka wakfu tangu Mnara wa Mia Moja hadi Mnara wa Hananeli.
2Sehemu iliyofuata ilijengwa upya na watu wa mji wa Yeriko. Baada ya hayo akafuata Zakuri mwana wa Imri kujenga ukuta.
3Lango la Samaki lilijengwa upya na ukoo wa Hasena, wakatia miimo yake, milango, bawaba na makomeo yake. 4Sehemu inayofuata ilijengwa upya na Meremothi, mwana wa Uria, mwana wa Hakosi. Sehemu inayofuata ilijengwa upya na Meshulamu, mwana wa Berekia, mwana wa Meshezabeli. Sehemu inayofuata ilijengwa upya na Sadoki, mwana wa Baana. 5Sehemu inayofuata ilijengwa na watu kutoka mji wa Tekoa. Lakini viongozi wa mji wakakataa kufanya kazi ya mikono waliyoagizwa kufanya na wasimamizi.
6Lango la Zamani lilijengwa upya na Yoyada, mwana wa Pasea, pamoja na Meshulamu, mwana wa Besodeya, wakatia miimo yake, milango, bawaba na makomeo yake. 7Waliowafuata hao katika kazi hiyo ya kujenga upya walikuwa Melatia, Mgibeoni; Yadoni, Mmeronothi pamoja na watu wa mji wa Gibeoni na Mizpa waliokuwa chini ya uongozi wa mtawala wa mkoa wa magharibi ya mto Eufrate. 8Sehemu inayofuata, ilijengwa upya na Uzieli, mwana wa Harkaya, mfua dhahabu. Sehemu inayofuata hadi Ukuta Mpana ilijengwa upya na Hanania, mtengenezaji wa marashi. 9Sehemu inayofuata ilijengwa upya na Refaya, mwana wa Huri, mkuu wa nusu ya wilaya ya Yerusalemu. 10Sehemu inayofuata, inayokabiliana na nyumba yake ilijengwa upya na Yedaya, mwana wa Harumafu. Sehemu inayofuata ilijengwa upya na Hatushi, mwana wa Hashabneya. 11Sehemu inayofuata pamoja na Mnara wa Tanuri vilijengwa upya na Malkiya, mwana wa Harimu akishirikiana na Hashubu, mwana wa Pahath-moabu.
12Sehemu inayofuata ilijengwa upya na Shalumu, mwana wa Haloheshi, mtawala wa nusu nyingine ya wilaya ya Yerusalemu. Alisaidiana na binti zake katika ujenzi huo.
13Lango la Bondeni lilijengwa upya na Hanuni pamoja na wakazi wa mji wa Zanoa. Wakayaweka malango mahali pake, wakatia bawaba na makomeo yake. Waliujenga upya ukuta ukiwa na urefu wa mita 400 hivi hadi Lango la Samadi.
14Lango la Samadi lilijengwa upya na Malkiya, mwana wa Rekabu, mkuu wa wilaya ya Beth-hakeremu. Akaliweka lango mahali pake, akatia bawaba na makomeo yake.
15Lango la Chemchemi lilijengwa upya na Shalumu, mwana wa Kolhoze, mkuu wa wilaya ya Mizpa. Akalifunika, akaliweka lango mahali pake, akatia bawabu na makomeo yake. Kwenye Bwawa la Shela akajenga ukuta ulio karibu na bustani ya kifalme hadi ngazi zinazoshuka toka mji wa mfalme Daudi. 16Sehemu inayofuata hadi kwenye makaburi ya Daudi, bwawa na majengo ya jeshi ilijengwa upya na Nehemia, mwana wa Azbuki, mkuu wa nusu ya wilaya ya Beth-suri.

Walawi waliojenga ukuta

17Baada ya hao, Walawi waliendeleza ujenzi mpya wa ukuta. Sehemu inayofuata ilijengwa upya na Rehumu, mwana wa Bani, na Hashabia, mkuu wa nusu ya wilaya ya Keila, alijenga upya sehemu inayohusu wilaya yake. 18Baada ya huyo, sehemu zinazofuata zilijengwa upya na ndugu zao. Sehemu inayofuata ilijengwa upya na Bavai, mwana wa Henadadi, mkuu wa nusu ya wilaya ya Keila. 19Sehemu inayofuata inayoelekeana na ghala ya silaha kwenye pembe ya ukuta ilijengwa upya na Ezeri, mwana wa Yeshua, mkuu wa Mizpa. 20Sehemu inayofuata tangu pembeni hadi kwenye mlango wa Eliashibu, kuhani mkuu, ilijengwa upya na Baruku, mwana wa Zabai. 21Sehemu inayofuata tangu mlangoni mwa nyumba ya Eliashibu, kuhani mkuu, hadi mwisho wa nyumba hiyo, ilijengwa upya na Meremothi, mwana wa Uria, mwana wa Hakosi.

Makuhani waliojenga ukuta

22Sehemu inayofuata ilijengwa upya na makuhani waliokaa katika sehemu tambarare. 23Benyamini na Hashubu walijenga upya sehemu inayokabiliana na nyumba yake. Azaria, mwana wa Maaseya, mwana wa Anania, alijenga upya sehemu inayokabiliana na nyumba yao. 24Kuanzia kwenye nyumba ya Azaria hadi pembeni mwa ukuta ilijengwa upya na Binui, mwana wa Henadadi. 25Sehemu inayofuata, tokea pembeni mwa ukuta na mnara wa ikulu ya juu karibu na uwanda wa ulinzi ilijengwa upya na Palali, mwana wa Uzai. Pedaia, mwana wa Paroshi, 26akishirikiana na watumishi wa hekalu waliokaa Ofeli, walijenga upya sehemu inayokabiliana na Lango la Maji, upande wa mashariki na mnara mrefu.

Wajenzi wengine

27Sehemu nyingine inayofuata, ikitokea kwenye mnara mrefu hadi ukuta wa Ofeli ilijengwa upya na wakazi wa mji wa Tekoa. 28Juu ya Lango la Farasi palijawa na makuhani, kila mmoja alijenga sehemu inayokabiliana na nyumba yake. 29Sadoki, mwana wa Imeri alijenga upya sehemu inayokabiliana na nyumba yake. Sehemu inayofuata, ilijengwa upya na Shemaya, mwana wa Shekania, mlinzi wa Lango la Mashariki. 30Sehemu inayofuata ikiwa ni sehemu yao ya pili ilijengwa upya na Hanania mwana wa Shelemia, akishirikiana na Hanuni, mwana wa sita wa Zalafu. Meshulamu, mwana wa Berekia, alijenga upya sehemu inayokabiliana na chumba chake. 31Sehemu inayofuata, toka nyumba waliyoitumia wafanyakazi wa hekalu na wafanyabiashara iliyokuwa inaelekeana na Lango la Gereza,3:31 Lango la Gereza: Au Lango la Mifkadi. karibu na chumba cha juu kwenye pembe upande wa kaskazini-mashariki ilijengwa upya na Malkiya, mfua dhahabu.
32Sehemu ya mwisho kutoka chumba kwenye pembe hadi Lango la Kondoo ilijengwa upya na wafua dhahabu na wafanyabiashara.


Nehemia3;1-32

Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)

"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.

No comments: