Swahili na Waswahili

Swahili na Waswahili
Waswahili na Mswahili Rachel Siwa...Pamoja Daima!!

Thursday 16 August 2018

Kikombe Cha Asubuhi ; Ezra 6...


Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?


Tumshukuru Mungu wetu katika yote...

Asante kwa wema na fadhili zako kwetu
Asante kwa ulinzi wako kwetu wakati wote
Asante kwa kutuchagua tena na kutupa
kibali cha kuendelea kuiona leo hii
Asante kwa pumzi/uzima,afya na kuwatayari kwa majukumu yetu


Utukuzwe ee Mungu wetu,usifiwe Baba wa Mbinguni

Jehovah  Jireh..!Jehovah Nissi..!Jehovah Raah..!
Jehovah Rapha..!Jehovah Shammah..!Jehovah Shamlom..!
Emanuel-Mungu pamohja nasi..!!
Neema yako yatutosha Baba wa Mbinguni..!



Sasa, yahusu ule mchango kwa ajili ya watu wa Mungu: Fanyeni kama nilivyoyaagiza makanisa ya Galatia. Kila Jumapili kila mmoja wenu atenge kiasi cha fedha kadiri ya mapato yake, ili kusiwe na haja ya kufanya mchango wakati nitakapokuja. Wakati nitakapokuja kwenu, nitawatuma wale mtakaowachagua miongoni mwenu wapeleke barua na zawadi zenu Yerusalemu. Kama itafaa nami niende, basi, watakwenda pamoja nami.


Baba wa Mbinguni tunakuja mbele zako tukijinyenyekeza,tukijishusha
na kujiachilia mikononi mwako
Mungu wetu tunaomba utusamehe dhambi zetu zote tulizo zifanya
Kwakuwaza,kwakunena,kwakutenda,kwakujua/kutojua
Baba wa Mbinguni nasi tunaomba ukatupe neema
ya kuweza kuwasamehe wale wote waliotukosea
Usitutie majaribu Mungu wetu tunaomba utuepushe
na yule mwovu na kazi zake zote
Jehovah ututakase miili yetu na akili zetu
Baba wa Mbinguni tunaomba utufunike kwa Damu
ya Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo wa Nazareti
yeye aliteseka kwanza ili sisi tupate kupona...



Nitakuja kwenu baada ya kupitia Makedonia – maana nataraji kupitia Makedonia. Labda nitakaa kwenu kwa muda fulani, au huenda nitakaa pamoja nanyi wakati wote wa baridi, ili mpate kunisaidia niendelee na safari yangu kokote nitakakokwenda. Sipendi kupita kwenu harakaharaka na kuendelea na safari. Natumaini kukaa kwenu kwa kitambo fulani, Bwana akiniruhusu. Lakini nitabaki hapa Efeso mpaka siku ya Pentekoste. Mlango uko wazi kabisa kwa ajili ya kazi yangu muhimu hapa, ingawa wapinzani nao ni wengi. Timotheo akija, angalieni asiwe na hofu yoyote wakati yupo kati yenu, kwani anafanya kazi ya Bwana kama mimi. Kwa hiyo mtu yeyote asimdharau, ila msaidieni aendelee na safari yake kwa amani ili aweze kurudi kwangu, maana mimi namngojea pamoja na ndugu zetu. Kuhusu ndugu Apolo, nimemsihi sana aje kwenu pamoja na ndugu wengine, lakini hapendelei kabisa kuja sasa ila atakuja mara itakapowezekana.


Mungu wetu tunaomba ukabariki kazi za mikono yetu
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe ubunifu na maarifa 
katika utendaji
Jehovah nasi tukatende sawasawa na mapenzi yako
Baba wa Mbinguni tunaomba ukabariki ridhiki zetu
ziingiazo/zitokazo
Mungu wetu nasi tunaomba ukatupe neema ya kuweza
kuwabariki wenye kuhitaji
Yahweh tusipungukiwe katika mahitaji yetu
Mungu wetu ukatupe kama inavyokupendeza wewe



Jehovah tunayaweka maisha yetu mikononi mwako
Baba wa Mbinguni tunaomba ukabariki nyumba/ndoa zetu,
watoto,wazazi wetu,familia/ndugu na wote wanaotuzunguka
Jehovah tunaomba ulinzi wako kwetu na kwa vyote tunavyo vimiliki
Yahweh tunaomba ukatubariki tuingiapo/tutokapo
Mungu wetu tunaomba ukavibariki vyote tunavyoenda kugusa/kutumia
Baba wa Mbinguni ukavitakase kwa Damu ya Bwana wetu Yesu Kristo
Mungu wetu ukatamalaki na kutuatamia
Baba wa Mbinguni tukawe salama rohoni
Mfalme wa amani amani yako ikatawale katika maisha yetu
Mungu wetu ukatupe macho ya kuona na masikio ya kusikia 
sauti yako na kuitii
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe neema ya kufuata njia zako
Yahweh tukasimamie Neno lako amri na sheria zako siku zote 
za maisha yetu

Mungu wetu tunaomba ukatupe akili ya kutambua mema na mabaya Baba wa Mbinguni ukaonekane katika maisha yetu popote tupitapo na ikajulikane kwamba upo Mungu wetu

Neema zako zikawe nasi Nuru yako ikaangaze katika maisha yetu
ukatuguse kwa mkono wako wenye nguvu
Ukatufanye barua njema ee Mungu wetu nasi tukasomeke kama
inavyokupendeza wewe
Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi...



Kesheni, simameni imara katika imani, muwe hodari na wenye nguvu. Kila mfanyacho kifanyike kwa upendo. Ndugu, mnaifahamu jamaa ya Stefana; wao ni watu wa kwanza kabisa kuipokea imani ya Kikristo katika Akaya, na wamejitolea kuwatumikia watu wa Mungu. Ninawasihi nyinyi ndugu zangu, muufuate uongozi wa watu kama hao, na uongozi wa kila mtu afanyaye kazi na kutumika pamoja nao. Nafurahi sana kwamba Stefana, Fortunato na Akaiko wamefika; wamelijaza pengo lililokuwako kwa kutokuwako kwenu. Wameiburudisha roho yangu na yenu pia. Kwa hiyo inafaa kuwakumbuka watu wa namna hii. Makanisa yote ya Asia yanawasalimuni. Akula na Priska pamoja na watu wote wa Mungu walio nyumbani mwao wanawasalimuni sana katika kuungana na Bwana. Ndugu wote wanawasalimuni. Nanyi salimianeni kwa ishara ya mapendo ya Mungu. Mimi Paulo nawasalimuni, nikiandika kwa mkono wangu mwenyewe. Yeyote asiyempenda Bwana, na alaaniwe. MARANATHA – BWANA, NJOO! Neema ya Bwana Yesu iwe nanyi. Upendo wangu uwe kwenu katika kuungana na Kristo Yesu.


Tazama wenye shida/tabu,watoto wako wanaokutafuta kwa bidii na imani
Mungu wetu tunaomba ukawaguse kwa mkono wako wenye nguvu
Yahweh tunaomba  ukawaguse kila mmoja na mahitaji yake
Mungu wetu  unajua haja za mioyo ya kila mmoja
Baba wa Mbinguni tunaomba ukawasamehe pale walipokwenda
kinyume nawe
Mungu wetu ukawape neema ya kujiombea,macho ya rohoni,masikio yakusikia sauti yako,wakafuate njia zako nazo zikawaweke huru
Mungu wetu tunaomba ukasikie kulia kwao
Baba wa Mbinguni tunomba ukawafute machozi yao
Jehovah ukaonekane katika maisha yao
Nuru yako ikaangaze katika maisha yao
Mungu wetu tunaomba ukawatendee sawasawa na mapenzi yako
Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele
Amina....!!!


Wapendwa katika Kristo Yesu asanteni sana
kwakuwanami/kunisoma

Mungu Baba aendelee kuwabariki na kuwatendea
kama inavyompendeza yeye
Amani ya Bwana wetu Yesu Kristo na upendo wa Mungu Baba
ukae nanyi daima....
Nawapenda.



Amri ya Koreshi yapatikana

1Mfalme Dario alitoa amri na uchunguzi ulifanywa mjini Babuloni katika nyumba ya kumbukumbu za kifalme. 2Lakini kitabu kilipatikana mjini Ekbatana katika mkoa wa Media, nacho kilikuwa na maagizo yafuatayo:
3“Mnamo mwaka wa kwanza wa utawala wake, mfalme Koreshi alitoa amri nyumba ya Mungu ijengwe upya mjini Yerusalemu, na iwe mahali pa kutolea tambiko na sadaka za kuteketezwa. Kimo chake kitakuwa mita 27 na upana wake mita 27. 4Kuta zake zitajengwa kwa safu moja ya miti juu ya kila safu tatu za mawe makubwa. Gharama zote zilipwe kutoka katika hazina ya mfalme. 5Pia, vyombo vyote vya dhahabu na fedha ambavyo mfalme Nebukadneza alivileta Babuloni kutoka katika hekalu la Yerusalemu, vitarudishwa na kuwekwa kila kimoja mahali pake katika nyumba ya Mungu.”

Dario aamuru kazi iendelee

6Ndipo Dario akapeleka ujumbe ufuatao:
“Kwa Tatenai, mtawala wa mkoa wa magharibi ya Eufrate, Shethar-bozenai na maofisa wenzako mkoani. ‘Msiende huko kwenye hekalu, 7na acheni kazi ya ujenzi wa nyumba hii ya Mungu iendelee. Mwacheni mtawala wa Yuda na viongozi wa Wayahudi waijenge nyumba ya Mungu mahali pake. 8Zaidi ya hayo, natoa amri kwamba nyinyi mtawasaidia katika kazi hiyo. Gharama zao zote zitalipwa bila kuchelewa kutoka katika hazina ya mfalme inayotokana na kodi kutoka katika mkoa wa magharibi wa mto Eufrate. 9Kila siku, tena bila kukosa, mtawapa makuhani wa Yerusalemu kila kitu watakachohitaji; iwe ni fahali wachanga, kondoo dume au wanakondoo wa sadaka za kuteketezwa kwa Mungu wa mbinguni, au ngano, chumvi, divai au mafuta. 10Haya yote yatatendeka ili waweze kumtolea Mungu wa mbinguni tambiko zinazompendeza na waombee maisha yangu mimi mfalme na watoto wangu. 11Naamuru pia kwamba mtu yeyote ambaye hatatii amri hii, boriti ingolewe kutoka katika nyumba yake, na atumbuliwe kwayo. Tena, nyumba yake na ifanywe kuwa rundo la mavi. 12Mungu aliyeuchagua mji wa Yerusalemu kuwa mahali pake pa kuabudiwa na amwangushe mfalme au taifa lolote litakalopinga amri hii au kutaka kuiharibu nyumba hii ya Mungu iliyoko mjini Yerusalemu. Mimi Dario nimetoa amri hii. Ni lazima ifuatwe.’”

Hekalu lawekwa wakfu

13Basi, Tatenai, mtawala wa mkoa wa magharibi ya mto Eufrate, Shethar-bozenai, na maofisa wenzao, wakafanya bidii kutekeleza maagizo ya mfalme. 14Taz Hag 1:2; Zek 1:1 Viongozi wa Wayahudi waliendelea vizuri sana na kazi ya ujenzi wa hekalu, wakitiwa moyo kwa mahubiri ya nabii Hagai na Zekaria, mwana wa Ido. Walimaliza ujenzi wa hekalu kama walivyoamriwa na Mungu wa Israeli, na kama walivyoagizwa na mfalme Koreshi, mfalme Dario na mfalme Artashasta, wa Persia. 15Ujenzi wa nyumba hiyo ulimalizika mnamo siku ya tatu ya mwezi wa Adari, katika mwaka wa sita wa utawala wa mfalme Dario. 16Basi, watu wa Israeli, makuhani, Walawi na watu wengine waliokuwa wamerudi kutoka uhamishoni waliiweka wakfu nyumba ya Mwenyezi-Mungu kwa shangwe kuu. 17Wakati wa kuiweka wakfu nyumba ya Mungu, walitoa mafahali 100, kondoo madume 200, wanakondoo 800 na mbuzi madume 12 kwa ajili ya sadaka ya kuondoa dhambi, mbuzi mmoja kwa kila kabila la Israeli. 18Pia, kwa ajili ya huduma ya Mungu katika Yerusalemu, waliwapanga makuhani katika makundi yao ya Walawi katika zamu zao kufuatana na maagizo yaliyoandikwa katika kitabu cha Mose.

Pasaka

19Mnamo siku ya kumi na nne ya mwezi wa kwanza, watu waliokuwa wamerudi kutoka uhamishoni walisherehekea Pasaka. 20Makuhani na Walawi walikuwa wamejitakasa, wote walikuwa safi kabisa. Walichinja mwanakondoo wa Pasaka kwa ajili ya watu wote waliorudi kutoka uhamishoni, ndugu zao makuhani na kwa ajili yao wenyewe. 21Waliokula mwanakondoo wa Pasaka walikuwa Waisraeli wote waliorudi kutoka uhamishoni pamoja na watu wengine wote ambao walikuwa wameziacha njia za mataifa mengine ili kumwabudu Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli. 22Kwa muda wa siku saba watu walisherehekea kwa furaha sikukuu ya mikate isiyotiwa chachu, kwa sababu Mwenyezi-Mungu aliwajalia furaha na kumpa mfalme wa Ashuru moyo wa upendo kwao, akawasaidia katika kazi za ujenzi wa nyumba ya Mungu wa Israeli.



Ezra6;1-22

Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)

"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.

No comments: