Swahili na Waswahili

Swahili na Waswahili
Waswahili na Mswahili Rachel Siwa...Pamoja Daima!!

Friday 24 August 2018

Kikombe Cha Asubuhi ; Nehemia 2...


Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?

Tumshukuru Mungu wetu katika yote...

Asante kwa wema na fadhili zako kwetu
Asante kwa ulinzi wako kwetu wakati wote
Asante kwa kutuchagua tena na kutupa
kibali cha kuendelea kuiona leo hii
Asante kwa pumzi/uzima,afya na kuwatayari kwa majukumu yetu


Utukuzwe ee Mungu wetu,usifiwe Baba wa Mbinguni

Jehovah  Jireh..!Jehovah Nissi..!Jehovah Raah..!
Jehovah Rapha..!Jehovah Shammah..!Jehovah Shamlom..!
Emanuel-Mungu pamohja nasi..!!
Neema yako yatutosha Baba wa Mbinguni..!



Ukumbuke ahadi yako kwangu mimi mtumishi wako, ahadi ambayo imenipa matumaini. Hata niwapo taabuni napata kitulizo, maana ahadi yako yanipa uhai. Wasiomjali Mungu hunidharau daima, lakini mimi sikiuki sheria yako. Ninapoyakumbuka maagizo yako ya tangu kale, nafarijika, ee Mwenyezi-Mungu. Nashikwa na hasira kali, nionapo waovu wakivunja sheria yako. Masharti yako yamekuwa wimbo wangu, nikiwa huku ugenini. Usiku ninakukumbuka, ee Mwenyezi-Mungu, na kushika sheria yako. Hii ni baraka kubwa kwangu, kwamba nazishika kanuni zako.


Baba wa Mbinguni tunakuja mbele zako tukijinyenyekeza,tukijishusha
na kujiachilia mikononi mwako
Mungu wetu tunaomba utusamehe dhambi zetu zote tulizo zifanya
Kwakuwaza,kwakunena,kwakutenda,kwakujua/kutojua
Baba wa Mbinguni nasi tunaomba ukatupe neema
ya kuweza kuwasamehe wale wote waliotukosea
Usitutie majaribu Mungu wetu tunaomba utuepushe
na yule mwovu na kazi zake zote
Jehovah ututakase miili yetu na akili zetu
Baba wa Mbinguni tunaomba utufunike kwa Damu
ya Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo wa Nazareti
yeye aliteseka kwanza ili sisi tupate kupona...



Wewe, ee Mwenyezi-Mungu, ndiwe riziki yangu kuu; naahidi kushika maneno yako. Naomba radhi yako kwa moyo wangu wote; unionee huruma kama ulivyoahidi! Nimeufikiria mwenendo wangu, na nimerudi nifuate maamuzi yako. Bila kukawia nafanya haraka kuzishika amri zako. Waovu wametega mitego waninase, lakini mimi sisahau sheria yako. Usiku wa manane naamka kukusifu, kwa sababu ya maagizo yako maadilifu. Mimi ni rafiki ya wote wakuchao, rafiki yao wanaozitii kanuni zako. Dunia imejaa fadhili zako, ee Mwenyezi-Mungu, unifundishe masharti yako.


Mungu wetu tunaomba ukabariki kazi za mikono yetu
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe ubunifu na maarifa 
katika utendaji
Jehovah nasi tukatende sawasawa na mapenzi yako
Baba wa Mbinguni tunaomba ukabariki ridhiki zetu
ziingiazo/zitokazo
Mungu wetu nasi tunaomba ukatupe neema ya kuweza
kuwabariki wenye kuhitaji
Yahweh tusipungukiwe katika mahitaji yetu
Mungu wetu ukatupe kama inavyokupendeza wewe



Jehovah tunayaweka maisha yetu mikononi mwako
Baba wa Mbinguni tunaomba ukabariki nyumba/ndoa zetu,
watoto,wazazi wetu,familia/ndugu na wote wanaotuzunguka
Jehovah tunaomba ulinzi wako kwetu na kwa vyote tunavyo vimiliki
Yahweh tunaomba ukatubariki tuingiapo/tutokapo
Mungu wetu tunaomba ukavibariki vyote tunavyoenda kugusa/kutumia
Baba wa Mbinguni ukavitakase kwa Damu ya Bwana wetu Yesu Kristo
Mungu wetu ukatamalaki na kutuatamia
Baba wa Mbinguni tukawe salama rohoni
Mfalme wa amani amani yako ikatawale katika maisha yetu
Mungu wetu ukatupe macho ya kuona na masikio ya kusikia 
sauti yako na kuitii
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe neema ya kufuata njia zako
Yahweh tukasimamie Neno lako amri na sheria zako siku zote 
za maisha yetu

Mungu wetu tunaomba ukatupe akili ya kutambua mema na mabaya Baba wa Mbinguni ukaonekane katika maisha yetu popote tupitapo na ikajulikane kwamba upo Mungu wetu

Neema zako zikawe nasi Nuru yako ikaangaze katika maisha yetu
ukatuguse kwa mkono wako wenye nguvu
Ukatufanye barua njema ee Mungu wetu nasi tukasomeke kama
inavyokupendeza wewe
Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi...



Umenitendea vema mimi mtumishi wako, kama ulivyoahidi, ee Mwenyezi-Mungu. Unifundishe akili na maarifa, maana nina imani sana na amri zako. Kabla ya kuniadhibu nilikuwa nikikosea, lakini sasa nashika neno lako. Wewe ni mwema na mfadhili; unifundishe masharti yako. Wenye kiburi wanasema uongo juu yangu, lakini mimi nashika kanuni zako kwa moyo wote. Mioyo yao imejaa upumbavu, lakini mimi nafurahia sheria yako. Nimefaidika kutokana na taabu yangu, maana imenifanya nijifunze masharti yako. Sheria uliyoweka ni bora kwangu, kuliko mali zote za dunia.


Tazama wenye shida/tabu,watoto wako wanaokutafuta kwa bidii na imani
Mungu wetu tunaomba ukawaguse kwa mkono wako wenye nguvu
Yahweh tunaomba  ukawaguse kila mmoja na mahitaji yake
Mungu wetu  unajua haja za mioyo ya kila mmoja
Baba wa Mbinguni tunaomba ukawasamehe pale walipokwenda
kinyume nawe
Mungu wetu ukawape neema ya kujiombea,macho ya rohoni,masikio yakusikia sauti yako,wakafuate njia zako nazo zikawaweke huru
Mungu wetu tunaomba ukasikie kulia kwao
Baba wa Mbinguni tunomba ukawafute machozi yao
Jehovah ukaonekane katika maisha yao
Nuru yako ikaangaze katika maisha yao
Mungu wetu tunaomba ukawatendee sawasawa na mapenzi yako
Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele
Amina....!!!


Wapendwa katika Kristo Yesu asanteni sana
kwakuwanami/kunisoma

Mungu Baba aendelee kuwabariki na kuwatendea
kama inavyompendeza yeye
Amani ya Bwana wetu Yesu Kristo na upendo wa Mungu Baba
ukae nanyi daima....
Nawapenda.


Nehemia anakwenda Yerusalemu

1Katika mwezi wa Nisani, katika mwaka wa ishirini wa utawala wa mfalme Artashasta, wakati divai ilipokuwa mbele yake, nilichukua divai na kumpelekea mkononi mwake. Kamwe sikuwahi kuwa mwenye huzuni mbele yake. 2Mfalme Artashasta akaniuliza, “Je, mbona unaonekana kuwa mwenye huzuni, ingawa huonekani kuwa mgonjwa? Naona una huzuni sana moyoni mwako!” Ndipo nilipoogopa sana. 3Nikamjibu, “Ee mfalme, udumu milele! Kwa nini nisiwe mwenye huzuni wakati mji wa Yerusalemu yalimo makaburi ya babu zangu uko tupu na malango yake yameteketezwa kwa moto?” 4Ndipo mfalme Artashasta akanijibu, “Sasa unaomba nini?” Nikamwomba Mungu wa mbinguni. 5Halafu nikamwambia mfalme, “Ee mfalme, ikiwa unapendezwa nami na ikiwa nimepata upendeleo mbele yako, nakuomba unitume Yuda ili niende kuujenga upya mji ambamo yamo makaburi ya babu zangu.” 6Mfalme akaniuliza (malkia akiwa karibu naye), “Utakuwa huko kwa muda gani na utarudi lini hapa?” Ombi langu akalikubali nami nikamjulisha wakati nitakaporudi. 7Nikamjibu, “Ee mfalme ikiwa unapendezwa nami, naomba nipewe barua ili nizipeleke kwa watawala wa mkoa wa magharibi ya mto Eufrate ili waniruhusu nipite hadi nchini Yuda. 8Pia nakuomba barua iandikwe kwa Asafu mtunzaji wa msitu wa kifalme ili anipatie mbao za kutengenezea miimo ya malango ya ngome ya hekalu, ukuta wa mji na nyumba yangu nitakamokaa.” Mfalme akakubali ombi langu kwa kuwa Mungu, kwa wema wake, alikuwa pamoja nami.
9Nilipowafikia wakuu wa mkoa wa magharibi ya mto Eufrate, niliwapa barua za mfalme. Mfalme alikuwa amenituma pamoja na maofisa wa jeshi na wapandafarasi. 10Lakini Sanbalati, Mhoroni, na Tobia, Mwamoni, mtumishi wake, waliposikia kuwa nimekuja ili kushughulikia hali njema ya watu wa Israeli, hawakufurahia kabisa jambo hilo.
11Hivyo nikafika Yerusalemu, nikakaa huko kwa siku tatu. 12Kisha niliondoka usiku, mimi pamoja na watu wachache; sikumwambia mtu yeyote yale ambayo Mungu alikuwa ameyaweka moyoni mwangu kwa ajili ya mji wa Yerusalemu. Lakini siku moja usiku, niliondoka na kuwachukua watu wachache tu. Sikuchukua mnyama yeyote isipokuwa punda niliyempanda mimi mwenyewe. 13Nikatoka nikipitia Lango la Bondeni katika njia ielekeayo kwenye Kisima cha Joka na Lango la Mavi; nikazikagua kuta za mji wa Yerusalemu ambazo zilikuwa zimebomolewa pamoja na malango yake ambayo yalikuwa yameteketezwa kwa moto. 14Halafu, nikaenda kwenye Lango la Chemchemi na kwenye Bwawa la Mfalme. Lakini yule punda niliyempanda hakuweza kupita.
15Wakati huo wa usiku, nikapitia bondeni na kukagua ukuta wa mji. Nilirudi nikapitia Lango la Bondeni. 16Maofisa hawakujua mahali nilipokuwa nimekwenda wala nimefanya nini. Tena nilikuwa sijawaambia Wayahudi, makuhani, viongozi, wakuu wala wale watu ambao wangeifanya kazi ya kuujenga upya mji.
17Kisha nikawaambia, “Bila shaka mnaliona tatizo letu kuwa mji wa Yerusalemu ni magofu na malango yake yameteketezwa kwa moto. Basi, na tuujenge tena ukuta wa Yerusalemu ili tusiaibishwe zaidi.” 18Nikawaeleza jinsi Mungu alivyokuwa pamoja nami akinitendea kwa wema wake. Nikawaeleza pia maneno ambayo mfalme alikuwa ameniambia. Wao walipoyasikia hayo, wakasema, “Haya, na tuanze kazi ya ujenzi.” Hivyo wakajiandaa kwa kazi hiyo njema.
19Lakini Sanbalati, Mhoroni, Tobia, Mwamoni mtumishi wake, na Geshemu, Mwarabu, waliposikia, wakatucheka na kutuzomea wakisema, “Ni kitu gani hiki mnachotenda? Je, mnataka kumwasi mfalme?” 20Nikawajibu, “Mungu wa mbinguni atatufanikisha katika kazi hii, nasi tulio watumishi wake tutaanza ujenzi. Lakini nyinyi hamna fungu wala haki wala kumbukumbu katika mji wa Yerusalemu.”


Nehemia2;1-20

Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)

"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.

No comments: