Swahili na Waswahili

Swahili na Waswahili
Waswahili na Mswahili Rachel Siwa...Pamoja Daima!!

Tuesday 25 July 2017

KWA SIMU TOKA LONDON- Mitaani na muziki wa Kizungu




IJUE PIANO – NA MANUFAA YAKE
Na Freddy Macha

Piano (au kinanda) ni chombo mahsusi cha Wazungu.
Kitaaluma muziki maana yake ni vitu vitatu : melodi (unayoisikia bila hata kujua maneno na kuipigia uluzi), ridhimu (mapigo), na mpangilio wa sauti (“harmony”). Kipengele cha tatu ndiyo kigumu zaidi....
Kati ya vyombo muhimu vya kitengo cha utunzi na upangaji (“harmony”) wa muziki ni Piano na Gitaa.
Ila Piano inaongoza Uzunguni.
Ndiyo maana kila utakapokwenda, makanisani, mabaa, mashuleni, majumbani na hata vituo vya usafiri hukosi Piano. Kihistoria, watunzi mashuhuri wa muziki ulimwenguni wametumia Piano kupanga vibao vyao vilivyofahamika na kupendwa miaka mingi zaidi.
Mifano michache ni George Gershwin (“Summertime”- 1934), Stevie Wonder (“Superstition”, 1973 ), Billy Joel (“I love You Just the Way You are”- 1977) , Herbie Hancock (“Watermelon Man”, 1962), Paul McCartney ( “Nyimbo za Beatles, “Let it Be”, “Long Winding Road”, “Yesterday”, nk), Prince (”When Doves Cry”, 1984), Gill Scott Heron (Mtunzi mashuhuri wa Mashairi aliyefariki 2011), na Alicia Keys , binti , kijana anayewika sasa.
Hata wanamuziki waimbaji walipiga piano, ingawa si sana hadharani. Prince, Michael Jackson, James Brown, nk.
Afrika yetu tunao marehem Fela Kuti na Abdullah Ibrahim (Afrika Kusini) anayeheshimika kama mmoja wa wapiga piano wakubwa duniani wa Jazz. Watanzania marehemu Patrick Balisidja na Kassim Magati (Sunburst) vile vile. Miaka yake ya mwisho marehem Balisidja alipiga Piano akiwa na King Kiki.
Kimuziki Piano ni kama kamusi. Ni muhimu kuijua kuelewa nini kinatendeka katika moyo, ngozi na mifupa ya muziki.
Kiafya upigaji Piano huoanisha pande mbili za Ubongo na kuzuia kuchakaa kwake. Hivyo kwa Wazee na watu wa makamo ni kinga maradhi ya kusinyaa na kulemaa Ubongo mathalan “Dementia” na “Alzheimer”...
Hii ni sababu mkono mmoja hufanya tendo tofauti na mwingine, unapotwanga Piano.
Kufuatana na maelezo ya mwanasayansi wa Kimarekani, Roger Sperry (aliyeshinda tuzo la Nobel 1981) upande wa kushoto wa Ubongo hufikiri, na kulia mambo ya hisia na utunzi. Bw Sperry alifikia ugunduzi huo akifanya utafiti wa kiini cha Kifafa.
Ni vizuri pia kwa watoto wadogo na huwasaidia kufanya vyema katika masomo yote. Ndiyo maana muziki na Sanaa (kijumla) huzingatiwa sana mashuleni Uzunguni.
Mwafrika jifunze Piano hata kama unaanza kuzeeka, itakufaa. Na wasisitize wanao kufanya muziki na sanaa, utawajenga kiakili katika hesabu na sayansi pia.

https://www.youtube.com/watch?v=lPZODRiP36A&t=88s
Rick Schmull akionesha vitu, mitaani London



https://www.youtube.com/watch?v=Oi06SqJW84g
Mdau nikionja embe.


https://www.youtube.com/watch?v=E-ItFW11Qsg
Mpiga piano, Billy Joel akiimba wimbo wake maarufu wa mapenzi duniani, kimaudhui na kimuziki.

https://www.youtube.com/watch?v=tJWM5FmZyqU
Wimbo huo ulifanywa maarufu zaidi na marehemu Barry White. Ulidunda sana madisko na redio za Afrika Mashariki enzi zake


https://www.youtube.com/watch?v=p52uF5qVDdA
Mpiga Piano maarufu wa Afrika Kusini, Abdullah Ibrahim. Gwiji wa Jazz



1 comment:

Anonymous said...

Really clear website, thanks for this post.