Swahili na Waswahili

Swahili na Waswahili
Waswahili na Mswahili Rachel Siwa...Pamoja Daima!!

Monday 3 July 2017

Kikombe Cha Asubuhi;Mambo Ya Walawi..27...Mwisho wa Kitabu cha Walawi

Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?

Ni siku/wiki nyingine tena Mungu wetu,Baba yetu,Muumba wetu,Muumba Mbingu na Nchi na vyote vilivyomo,Mungu wa Abrahamu,Isaka na Yakobo..!

Asante Baba wa Mbinguni kwakutuchagua tena na kutupa kibali cha kuendelea kuiona siku hii..
Tazama jana imepita Mungu Baba Leo ni siku mpya na kesho ni siku nyingine..
Asante kwa wema na fadhili zako kwetu..
Asante kwakutulinda na kutuamsha salama wenye Afya na kuendelea kwa majukumu yetu..
Si kwamba sisi ni wema sana au ni wazuri mno hapana ni kwa neema/rehema zako tuu Mungu wetu..


Tunakuja mbele zako Jehovah..!Tunaomba utusamehe dhambi zetu zote..

Tilizozifanya kwakuwaza,kwakunena,kwakutenda,kwakujua/kutojua..
Mungu wetu nasi ukatupe neema ya kuweza kuwasamehe wale waliotukosea..
Yahweh tunaomba utuepushe na majaribu na utuokoe na mwovu na kazi zake zote..

Ututakase Miili yetu na Akili zetu Mungu  Baba na utufunike kwa Damau  ya mwanano Mpendwa Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo wa Nazareti..
yeye aliteseka kwanza ilisisi tupate kupona..



Kwa vile sheria ni kivuli tu cha mambo mema yatakayokuja na si picha kamili ya mambo yale halisi, tambiko zilezile za sheria zinazotolewa mwaka hata mwaka, haziwezi kamwe kuwafanya wale wanaoabudu wawe wakamilifu! Kama hao watu wanaomwabudu Mungu wangekuwa wametakaswa dhambi zao kweli, hawangejisikia tena kuwa na dhambi, na tambiko hizo zote zingekoma. Lakini tambiko hizo hufanyika kila mwaka kuwakumbusha watu dhambi zao. Maana damu ya fahali na mbuzi haiwezi kamwe kuondoa dhambi. Ndiyo maana Kristo alipokuwa anakuja ulimwenguni, alimwambia Mungu: “Hukutaka tambiko wala sadaka, lakini umenitayarishia mwili. Sadaka za kuteketezwa au za kuondoa dhambi hazikupendezi. Hapo nikasema: ‘Niko hapa, ee Mungu, kutimiza matakwa yako kama ilivyoandikwa juu yangu katika kitabu cha sheria.’” Kwanza alisema: “Hutaki wala hupendezwi na tambiko, sadaka za kuteketezwa na za kuondoa dhambi.” Alisema hivyo ingawa sadaka hizi zote hutolewa kufuatana na sheria. Kisha akasema: “Niko hapa, ee Mungu, tayari kufanya matakwa yako.” Hivyo Mungu alibatilisha tambiko za zamani na mahali pake akaweka tambiko nyingine moja. Kwa kuwa Yesu Kristo alitimiza matakwa ya Mungu, sisi tunatakaswa dhambi zetu kwa ile tambiko ya mwili wake aliyotoa mara moja tu, ikatosha. Kila kuhani Myahudi hutoa huduma yake ya ibada ya kila siku na kutoa tambiko zilezile mara nyingi, tambiko ambazo haziwezi kuondoa dhambi. Lakini Kristo alitoa tambiko moja kwa ajili ya dhambi, tambiko ifaayo milele, kisha, akaketi upande wa kulia wa Mungu, anangoja maadui zake wafanywe kama kibao chini ya miguu yake. Basi, kwa tambiko yake moja, amewafanya kuwa wakamilifu milele wote wale wanaotakaswa dhambi zao. Naye Roho Mtakatifu anatupa ushahidi wake. Kwanza anasema: “Hili ndilo agano nitakalofanya nao, siku zijazo, asema Bwana: Nitaweka sheria zangu mioyoni mwao, na kuziandika akilini mwao.” Kisha akaongeza kusema: “Sitakumbuka tena dhambi zao, wala vitendo vyao vya uhalifu.” Basi, dhambi zikisha ondolewa, hakutakuwa na haja tena ya kutoa tambiko za kuondoa dhambi.


Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi..
Mungu wetu ukatupe neema ya kusimamia Neno lako na kufuata sheria na Amri zako..
Kwa moyo  mnyofu na imani timilifu tuzingatie tumaini na ahadi zako kwani wewe ni mwaminifu na wakuabudiwa..
Ukatufanye Chombo chema na tukatumike sawasawa na mapenzi yako..
Ukatubariki tuingiapo/tutokapo na ukabariki kazi zetu na vyote tunavyoenda kutenda/kufanya Mungu wetu tukatende kama inavyokupendeza wewe..
Tusipungukiwe katika mahitaji yetu na ukatupe sawasawa na mapenzi yako..
Ukabariki ridhiki zetu ziingiazo/zitokazo nasi ukatupe neema ya kuwabariki wenye kuhitaji..
Tazama Yatima na wajane Mungu ukawabariki na wasipungukiwe katika mahitaji yao..
Wenye shida/tabu,wagonjwa na wote wanaopita magumu/majaribu,waliokatika vifungo mbalimbali Mungu wetu ukawaguse na mkono wako wenye nguvu,ukawape neema ya kukujua wewe na kufuata njia zako,waijue kweli yako nayo ikawaweke huru..Ukawaponye na kuwaokoa..

wafiwa ukawe mfariji wao na ukawape nguvu na uvumilivu...

Mungu wetu tunashukuru hata kwakumaliza/kupitia/kusoma na kujifunza katika kitabu hiki..leo tumefikia mwisho lakini ikawe ndiyo mwanzo wa kujituma zaidi na  utupe neema ya kujifunza zaidi na kurudia kila wakati ili tuishi kwa sheria na misingi yako..
tupate pia shauku ya kupenda kusoma na kujifunza na kuendelea kusoma Neno lako kila wakati..
si kwa uwezo wetu bali ni kwa neema  yako Mungu..

Tunayaweka haya yote mikononi mwako Mungu wetu..
Tukiami na kushukuru daima..

kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele...
Amina..!!
Asanteni sana wapendwa/waungwana kwakuwa pamoja..
Leo tumefikia mwisho wa kitabu hiki lakini usiwe mwisho wakuendela kujifunza na kusoma vitabu vingine na pia tuwe tunarudia ili kuhifadhi na kujifunza zaidi..
Ninawashukuru sana na sina neno zuri zaidi ya kusema..
Nawapenda na Mungu aendelee kutuongoza.

Sheria kuhusu matoleo

1Mwenyezi-Mungu alimwambia Mose, 2“Waambie Waisraeli hivi: Mtu akiweka nadhiri ya kumtolea Mwenyezi-Mungu binadamu, mtu huyo anaweza kuondoa nadhiri yake kwa kulipa kiasi cha fedha kinachokadiriwa kama ifuatavyo: 3Mwanamume wa miaka ishirini hadi miaka sitini atakombolewa kwa fedha shekeli 50 kulingana na kipimo cha mahali patakatifu. 4Kama ni mwanamke, atakombolewa kwa fedha shekeli 30. 5Kama mtu huyo ni wa miaka kati ya mitano na 20 atakombolewa kwa fedha shekeli 20 kama ni mvulana na shekeli 10 za fedha kama ni msichana. 6Ikiwa ni mtoto wa umri wa kati ya mwezi mmoja na miaka mitano atakombolewa kwa shekeli 5 za fedha kama ni mvulana na shekeli 3 za fedha kama ni msichana. 7Ikiwa mtu huyo umri wake ni zaidi ya miaka sitini, thamani yake itakuwa ni shekeli 15 za fedha kama ni mwanamume na shekeli 10 za fedha kama ni mwanamke. 8Lakini ikiwa mtu huyo ni maskini na hawezi kulipa gharama yake, basi, mtu huyo atapelekwa kwa kuhani. Kuhani atampima thamani yake kulingana na uwezo wa huyo aliyeweka nadhiri.
9“Ikiwa nadhiri yenyewe inahusu mnyama wa namna ambayo watu humtolea Mwenyezi-Mungu sadaka, basi mnyama huyo huwa kitu kitakatifu. 10Hairuhusiwi kumbadilisha mnyama huyo kwa mwingine awaye yeyote, mzuri kwa mbaya au mbaya kwa mzuri. Kama akimbadilisha kwa mnyama mwingine, wote wawili watakuwa watakatifu.
11“Kama nadhiri hiyo yahusu mnyama najisi, wa aina ambayo si halali kumtolea Mwenyezi-Mungu, basi, mtu aliyemtoa, atamleta kwa kuhani, 12naye kuhani ataamua thamani yake kulingana na uzuri au ubaya wake. Jinsi atakavyoamua kuhani, ndivyo itakavyokuwa. 13Lakini ikiwa mwenyewe anataka kumkomboa, basi, ataongeza asilimia ishirini ya thamani ya mnyama huyo.
14“Mtu akiiweka wakfu nyumba yake kuwa takatifu kwa Mwenyezi-Mungu, kuhani ataamua thamani yake kulingana na uzuri au ubaya wake. Jinsi atakavyoamua, ndivyo itakavyokuwa. 15Kama huyo mtu aliyeiweka wakfu akitaka kuikomboa hiyo nyumba, basi, ataongeza asilimia ishirini ya thamani yake, nayo itakuwa mali yake.
16“Mtu akiiweka ardhi yake, ambayo ni urithi wake, wakfu kwa Mwenyezi-Mungu basi, thamani yake itapimwa kulingana na mbegu zinazotumika kulipanda shamba hilo; kwa kila kilo ishirini za shayiri thamani yake itakuwa shekeli hamsini za fedha. 17Kama akiliweka wakfu shamba lake katika mwaka wa kuadhimisha miaka hamsini, thamani yake ni lazima ilingane na vipimo vyenu. 18Lakini kama akiliweka wakfu baada ya mwaka huo, basi, kuhani ataamua thamani yake kulingana na miaka iliyobaki kufikia mwaka wa ukumbusho wa miaka hamsini na thamani yake ipunguzwe. 19Kama mwenyewe akitaka kulikomboa, basi, ni lazima aongeze asilimia ishirini ya thamani ya shamba hilo, na kisha litakuwa mali yake. 20Lakini kama hataki kulikomboa au amemwuzia mtu mwingine, basi, shamba hilo lisikombolewe tena. 21Katika mwaka wa ukumbusho wa miaka hamsini shamba hilo litaachiliwa na kuwa lake Mwenyezi-Mungu milele. Kuhani ndiye atakayelimiliki.
22“Kama mtu akiweka wakfu shamba alilonunua, yaani sio lake kwa urithi, 23kuhani ataamua thamani ya shamba hilo kwa kulingana na miaka iliyobaki kufikia mwaka wa ukumbusho wa miaka hamsini na mtu huyo atalazimika kulipa thamani yake kama ni kitu kitakatifu kwa Mwenyezi-Mungu. 24Lakini katika mwaka wa ukumbusho wa miaka hamsini, shamba hilo ni lazima arudishiwe yule mtu aliyeliuza. 25Kila thamani itapimwa kwa kipimo cha uzito cha shekeli kulingana na kipimo cha mahali patakatifu: Uzito wa gera 20 ni sawa na uzito wa shekeli moja.
26“Hairuhusiwi kumweka wakfu mzaliwa wa kwanza wa wanyama; kisheria huyo ni wake Mwenyezi-Mungu; awe ni ng'ombe au kondoo. 27Kama anayehusika ni mnyama najisi, mwenyewe atamnunua kwa kulingana na mnavyompima na ataongeza asilimia ishirini ya thamani ya mnyama huyo. Kama hakombolewi, basi, atauzwa kulingana na vipimo vyenu.
28 # Taz Hes 18:14 “Lakini kitu chochote kilichowekwa wakfu kwa Mwenyezi-Mungu, kiwe ni mtu au mnyama au kitu kilichopatikana kwa urithi, hakitauzwa wala kukombolewa. Chochote kilichowekwa wakfu kwa Mwenyezi-Mungu ni kitakatifu kabisa. 29Mtu yeyote aliyewekwa wakfu kwa Mwenyezi-Mungu ili aangamizwe, asikombolewe; sharti auawe.
30 # Taz Hes 18:21; Kumb 14:22-29 “Zaka za mazao iwe ni nafaka au matunda ya miti, yote ni mali ya Mwenyezi-Mungu; ni takatifu kwa Mwenyezi-Mungu. 31Kama mtu akitaka kuikomboa zaka yake, atalipa thamani yake na kuongeza asilimia ishirini ya thamani ya zaka hiyo. 32Kuhusu mifugo, inapohesabiwa, kila mnyama wa kumi ni mtakatifu kwa Mwenyezi-Mungu. 33Mtu yeyote hana ruhusa kuuliza kama mnyama huyo ni mzuri au mbaya wala mnyama huyo kamwe hatabadilishwa kwa mwingine. Kama akibadilishwa kwa mwingine, wanyama wote wawili watakuwa watakatifu; hawatakombolewa.”
34Hizo ndizo amri ambazo Mwenyezi-Mungu alimwamuru Mose ili awaambie Waisraeli, mlimani Sinai.

Mambo Ya Walawi27;1-34


Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)

"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.

No comments: