Swahili na Waswahili

Swahili na Waswahili
Waswahili na Mswahili Rachel Siwa...Pamoja Daima!!

Thursday 7 December 2017

Kikombe Cha Asubuhi ;Waamuzi 19...



Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?

Tumshukuru Mungu wetu katika yote..

Mtakatifu..!Mtakatifu..!Mtakatifu..!Baba wa Mbinguni..
Mungu wetu,Muumba wetu,Mwokozi wetu,Mungu wa Abrahamu,
Isaka na Yakobo,Mungu mwenye nguvu,Baba wa Yatima,Mume wa wajane
Muweza wa Yote,Jehovah..!Yahweh..!El shaddai..!El Qanna..!Elo Him..!El Elyon..!El Olam..!Emanueli-Mungu pamoja nasi...!Mungu wa walio hai..!
Unatosha Baba wa Mbinguni,Hakuna kama wewe Mungu wetu..!!

Asante kwa wema na fadhili zako kwetu..
Asante kwa ulinzi wako kwetu wakati wote..
Asante kwa pumzi/uzima,afya na tukiwa tayari kwa majukumu yetu..
Asante kwa kutuchagua tena na kutupa kibali cha kuendelea kuiona leo hii..


Basi, mimi niliye mfungwa kwa kuwa namtumikia Bwana, nawasihi muishi maisha yanayostahili wito mlioitiwa. Muwe daima wanyenyekevu, wapole na wenye saburi; vumilianeni nyinyi kwa nyinyi kwa mapendo. Fanyeni bidii ya kuhifadhi umoja uletwao na Roho kwa kuzingatia amani iliyo kati yenu. Kuna mwili mmoja na Roho mmoja, kama vile tumaini mliloitiwa na Mungu ni moja.
Tazama jana imepita Mungu wetu Leo ni siku mpya na Kesho ni siku nyingine Baba wa Mbinguni..
Yahweh tunakuja mbele zako tukijinyenyekeza,tukijishusha na kujiachilia mikononi mwako Mungu wetu..
Jehovah tunaomba utusamehe dhambi zetu zote tulizo zifanya
kwakuwaza,kwakunena,kwakutenda,kwakujua/kutojua..
Yahweh nasi tunaomba utupe neema ya kuweza kuwasamehe wale
wote waliotukosea..
Mungu wetu tunaomba utuepushe katika majaribu Yahweh utuokoe 
na yule mwovu na kazi zake zote..
Nguvu za giza,nguvu za mapepo,nguvu za mizimu,nguvu za mpinga Kristo
zishindwe katika jina lililo kuu jina la Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo..
Mungu wetu tunaomba ututakase miili yetu na akili zetu Jehovah tunaomba utufunike kwa Damu ya Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo
wa Nazareti yeye aliseka kwanza ili sisi tupate kupona..


Kama yasemavyo Maandiko: “Alipopaa mbinguni juu kabisa, alichukua mateka; aliwapa watu zawadi.” Basi, inaposemwa: “Alipaa juu,” ina maana gani? Maana yake ni kwamba, kwanza alishuka mpaka chini kabisa duniani. Basi, huyo aliyeshuka hapa duniani ndiye aliyepaa juu ya mbingu zote apate kuujaza ulimwengu. Ndiye aliyewapa watu zawadi: Wengine aliwajalia wawe mitume, wengine manabii, wengine wawe waeneza Injili, wengine wachungaji na waalimu. Alifanya hivyo apate kuwatayarisha watu wote wa Mungu kwa ajili ya kazi ya huduma ya Kikristo ili kuujenga mwili wa Kristo, na hivyo sote tuufikie umoja wa imani na kumjua Mwana wa Mungu; tuwe watu waliokomaa na kuufikia utimilifu wake Kristo mwenyewe. Basi, hatutakuwa tena kama watoto, tukitupwa na kupeperushwa huko na huko kwa kila upepo wa mafundisho wanayozua watu wadanganyifu ili wawapotoshe wengine kwa hila. Kama tukiuzingatia ukweli kwa moyo wa mapendo tutakua katika kila jambo kulingana na Kristo ambaye ndiye kichwa; chini ya uongozi wake, viungo vyote vya mwili hushikamana pamoja, na mwili wote hutegemezwa kwa msaada wa viungo vyake. Basi, kila kiungo kikitekeleza kazi yake ipasavyo, mwili wote hukua na kujijenga katika upendo.


Baba wa Mbinguni tunaomba ukabariki kazi za mikono yetu..
Yahweh tunaomba ukatupe ubunifu,maarifa katika ufanyaji/utendaji
Mungu wetu tukatende sawasawa na mapenzi yako..
Jehovah tunaomba ukabariki ridhiki zetu ziingiazo/zitokazo Yahweh
nasi tunaomba utupe neema ya kuweza kuwabariki wenye kuhitaji
Mungu wetu tusipungukiwe katika mahitaji yetu Jehovah tunaomba ukatupe kama inavyokupendeza wewe..

Mfalme wa Amani tunayaweka maisha yetu mikononi mwako
Baba wa Mbinguni tunaomba amani yako ikatawale na ukabariki
Nyumba/ndoa zetu,watoto,wazazi wetu,familia/ndugu na wote wanaotuzunguka,Mungu wetu tunaomba ulinzi wako kwetu na kwavyote tunavyovimiliki,Yahweh tunaomba ukatamalaki na kutuatamia,Mungu wetu ukaonekane katika maisha yetu na popote tupitapo na ijulikane kwamba upo Baba wa Mbinguni..
Yahweh ukatupe neema ya kufuata njia zako,kusimamia Neno lako
amri na sheria zako siku zote za maisha yetu,tukanene yaliyo yako,ukatupe macho ya rohoni,masikio ya kusikia
sauti yako na kutii..
Mungu Baba ukatufanye barua njema Jehovah nasi tukasomeke
kama inavyokupendeza wewe..
Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi..




Basi, kwa jina la Bwana, nawaonyeni: Msiishi tena kama watu wasiomjua Mungu, ambao fikira zao zimekuwa upuuzi mtupu, na akili zao zimo gizani. Wako mbali na uhai wa Mungu kwa sababu ya upumbavu ulio ndani yao na ukaidi wao. Wamepotoka na hawana aibu, wamejitosa katika ufisadi; hufanya kwa pupa kila aina ya mambo ya aibu. Lakini nyinyi hamkujifunza hivyo juu ya Kristo. Ni dhahiri kwamba mlisikia barabara habari zake, na mkiwa wafuasi wake mkafundishwa ukweli ulivyo katika Yesu. Basi, acheni mwenendo wenu wa awali, yaani ule utu wenu wa kale uliokuwa unaangamizwa kwa tamaa zake danganyifu. Jirekebisheni upya rohoni na katika fikira zenu. Vaeni hali mpya ya utu ambayo imeumbwa kwa mfano wa Mungu na ambayo hujionesha katika maisha ya kweli ya uadilifu na utakatifu. Kwa hiyo, acheni uongo. Kila mmoja anapaswa kumwambia mwenzake ukweli, maana kila mmoja wetu ni kiungo cha mwili wa Kristo. Kama mkikasirika, msikubali hasira yenu iwafanye mtende dhambi, na wala msikae na hasira kutwa nzima. Msimpe Ibilisi nafasi. Aliyekuwa akiiba, asiibe tena, bali na aanze kufanya kazi njema kwa mikono yake, apate kuwa na kitu cha kumsaidia mtu aliye maskini. Maneno mabaya hata yasisikike kamwe miongoni mwenu; kila mara maneno yenu yawe ya kufaa na ambayo hujenga na kuwasaidia wengine, ili yawaneemeshe wasikilizaji wenu. Msimhuzunishe Roho Mtakatifu wa Mungu, maana Roho huyo ni alama ya Mungu kwenu kwamba nyinyi ni watu wake, na thibitisho kwamba siku itakuja ambapo Mungu atawakomboeni. Basi, achaneni na uhasama, chuki, hasira, kelele na matusi. Acheni kila uovu! Muwe na moyo mwema na wenye kuhurumiana; kila mmoja na amsamehe mwenzake kama naye Mungu alivyowasamehe nyinyi kwa njia ya Kristo.


Baba wa Mbinguni ukawaguse kwa mkono wako wenye nguvu wote
wanaopitia magumu/majaribu,Yahweh tunaomba ukawaponye wagonjwa
Mungu wetu ukawatendee na kuwalinda Yatima na Wajane,Mungu mwenye nguvu tunaomba ukawafungue wale wote waliokatika vifungo vya yule mwovu,Mungu wetu tunaomba ukawapatie chakula wenye njaa,Baba wa Mbinguni tunaomba ukawafariji wafiwa,Yahweh usiwaaache waliopotea/anguka Mungu wetu ukawasamehe wale wote waliokwenda kinyume nawe,Jehovah ukawe tumaini kwa wote waliokata tamaa,Yahweh
ukawakumbatie waliokataliwa,Mfalme wa Amani ukawaguse wenye hofu na mashaka,Mungu wetu ukawaponye kimwili na kiroho pia,Yahweh ukawape neema ya kujiombea,kufuata njia zako,amani ikatawale Nuru ikaangaze katika maisha yao,Baba ukasikie kuomba kwetu,Yahweh ukapokee sala/maombi ya watoto wako wanaokutafuta kwa bidii na kuomba kwa imani Ee Baba ukawafute machozi ya watoto wako..
Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele..
Amina..!
Wapendwa/waungwana asanteni sana kwakuwa nami
Mungu wetu muweza wa yote akatamalaki na kuwaatamia
Amani ya Kristo Yesu iwe nanyi daima..
Nawapenda..

Mlawi na suria wake

1Wakati huo ambapo hapakuwepo na mfalme katika Israeli, kulikuwa na Mlawi fulani aliyeishi kama mgeni mbali katika eneo la milima ya Efraimu. Mtu huyo alichukua suria kutoka Bethlehemu nchini Yuda. 2Lakini suria huyo akamkasirikia;19:2 akamkasirikia: Makala ya Kiebrania; tafsiri nyingine: Akamvunjia uaminifu. huyo Mlawi, akamwacha na kurudi nyumbani kwa baba yake huko Bethlehemu, akakaa kwa muda wa miezi minne. 3Siku moja, mumewe alikwenda kumtafuta; alikusudia kuongea naye vizuri na kumrudisha nyumbani kwake. Basi huyo mwanamume alikwenda pamoja na mtumishi wake na punda wawili. Basi yule mwanamke akampeleka ndani kwa baba yake, naye baba mkwe19:3 mkwe: Makala ya Kiebrania: Akampeleka kwa baba yake. wake alipomwona akampokea kwa furaha. 4Baba mkwe wake akamkaribisha, naye akakaa huko kwa muda wa siku tatu; huyo Mlawi na mtumishi wake wakala, wakanywa na kulala huko. 5Siku ya nne, wakaamka asubuhi na mapema, wakajitayarisha kuondoka; lakini baba wa yule mwanamke akamwambia, “Kwanza kula chakula kidogo upate nguvu, kisha uondoke.” 6Basi hao watu wawili wakakaa, wakala na kunywa pamoja. Kisha baba mkwe wake akamwambia, “Tafadhali ulale hapa usiku huu na kufurahi.” 7Yule mtu aliposimama akitaka kuondoka, baba mkwe wake akamhimiza abaki, naye akabaki. 8Siku ya tano huyo mtu aliamka asubuhi, akitaka kuondoka. Lakini baba yake yule mwanamke akamwambia, “Kwanza upate nguvu kwa kula, ungoje alasiri, halafu uondoke.” Basi wote wawili wakala pamoja.
9Huyo Mlawi na suria wake pamoja na mtumishi wake walipoinuka kwenda zao, baba mkwe wake akamwambia huyo Mlawi, “Sasa mchana umekwisha na jioni imekaribia. Ulale hapa, na kufurahi. Kesho asubuhi utaamka mapema kuanza safari yako ya kurudi nyumbani.” 10Lakini huyo mtu alikataa kulala huko usiku huo. Basi, akainuka, akaondoka akafika karibu na mji wa Yebusi (yaani Yerusalemu). Alikuwa na wale punda wake wawili waliotandikwa tayari, pamoja na suria wake. 11Walipokuwa wamekaribia mjini Yebusi, siku ilikuwa karibu imekwisha; naye mtumishi akamwambia bwana wake, “Sasa heri tuingie katika mji huu wa Wayebusi tulale humo usiku huu.” 12Bwana wake akamjibu, “Hatutageuka na kuingia katika mji wa wageni ambao si Waisraeli. Tutaendelea na safari mpaka Gibea. 13Twende tukaribie sehemu hizo na kulala huko Gibea au Rama.” 14Basi, wakaendelea na safari yao mpaka jua likatua wakiwa karibu na mji wa Gibea ambao ni mji wa kabila la Benyamini. 15Wakaingia mjini wapate kulala humo usiku. Walipoingia mjini wakaenda kukaa kwenye uwanja wa wazi wa mji, kwani hakuna mtu aliyewakaribisha nyumbani kwake. 16Walipokuwa huko mzee mmoja akafika kutoka shambani kwake. Mzee huyo alikuwa mwenyeji wa nchi ya milima ya Efraimu na alikuwa akiishi huko Gibea kama mgeni. Wakazi wa mji wa Gibea walikuwa wa kabila la Benyamini. 17Mzee huyo alipotazama na kumwona huyo msafiri akiwa huko uwanjani, alimwuliza, “Umetoka wapi na unakwenda wapi?” 18Naye akamjibu, “Tumetoka Bethlehemu nchini Yuda na tunaelekea sehemu za mbali za eneo la milima ya Efraimu. Huko ndiko ninakoishi na sasa ninarudi safarini huko Bethlehemu katika Yuda na kurejea nyumbani;19:18 kurejea nyumbani: Kulingana na tafsiri ya Kigiriki; makala ya Kiebrania ina: Nakwenda katika nyumba ya Mwenyezi-Mungu, msemo ambao hauafiki. hakuna mtu hapa aliyetukaribisha nyumbani kwake. 19Lakini sisi watumishi wako tuna nyasi na malisho kwa ajili ya punda wetu. Pia nina mkate na divai; hivyo vinanitosha mimi, suria wangu na mtumishi wangu. Hatupungukiwi kitu chochote.”
20Huyo mzee akamwambia, “Amani iwe nanyi! Nitawapa mahitaji yote. Ila msilale huku uwanjani.” 21Hivyo akawapeleka nyumbani kwake na kuwapa punda wao malisho. Hao wasafiri wakanawa miguu yao, wakala na kunywa.
22Walipokuwa wanajifurahisha, kumbe wanaume mabaradhuli wa mji huo wakaja wakaizingira hiyo nyumba na kugonga mlangoni. Wakamwambia mzee mwenye nyumba, “Mtoe nje yule mwanamume aliyekuja kwako, tulale naye.” 23Lakini huyo mzee mwenye nyumba akatoka nje, akawaambia “Sivyo ndugu zangu; nawasihi msitende uovu huo. Huyu ni mgeni wangu, hivyo msimtendee ubaya huo. 24Ninaye bado binti yangu ambaye ni bikira na yupo pia yule suria wa mgeni wangu. Niruhusuni niwatoe nje, muwachukue na kuwatendea kama mnavyotamani; lakini mtu huyu msimtendee jambo hilo la kipumbavu.” 25Lakini wanaume hao hawakumsikiliza. Kwa hiyo Mlawi yule akamchukua suria wake na kumtoa kwao huko nje. Nao wakamchukua na kumnajisi usiku kucha mpaka asubuhi. Karibu na mapambazuko, wakamwacha aende zake. 26Asubuhi, yule mwanamke akaja mpaka mlangoni mwa nyumba alimokuwa bwana wake, akaanguka chini hapo mlangoni na kukaa hapo mpaka kulipopambazuka kabisa.
27Bwana wa mwanamke huyo alipoamka asubuhi, alifungua milango ya nyumba, akatoka nje ili aendelee na safari. Ghafla akamkuta suria wake amelala chini mlangoni, mikono yake ikishika kizingiti cha mlango. 28Akamwambia, “Simama twende.” Lakini yeye hakujibu kitu. Akamchukua, akamweka juu ya punda wake na kumpeleka mpaka nyumbani kwake. 29Alipofika nyumbani kwake akachukua kisu na kumkatakata yule suria vipande kumi na viwili. Kisha akavipeleka vipande hivyo katika maeneo yote ya nchi ya Israeli. 30Wale wote walioona jambo hilo wakasema, “Jambo kama hili halijawahi kutukia wala kuonekana tangu siku ile Waisraeli walipotoka nchini Misri mpaka leo. Tulifikirie, tushauriane na kuamua.”


Waamuzi 19;1-30

Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)

"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.

Wednesday 6 December 2017

Kikombe Cha Asubuhi ;Waamuzi 18...




Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?

Mungu wetu yu mwema sana tumshukuru katika yote..
Asante Baba wa Mbinguni kwa wema na fadhili zako kwetu..
Asante kwa ulinzi wako kwetu wakati wote..
Asante kwa pumzi/uzima,afya na kuwa tayari kwa majukumu yetu..
Asante kwakutuchagua tena na kutupa kibali cha kuiona leo hii..
Utukuzwe ee Mungu wetu,Usifiwe Baba wa Mbinguni,Uhimidiwe Yahweh
Uabudiwe daima Jehovah Jireh..!Unatosha Jehovah Nissi..!Hakuna kama wewe Jehovah Shammah..!Matendo yako ni makuu mno Jehovah Rapha..!
Matendo yako ni ya ajabu Jehovah Raah..!Utukufu una wewe Jehovah
Shalom,Asante Emanuel-Mungu pamoja nasi...!!


Kwake Mwenyezi-Mungu nakimbilia usalama; mnawezaje basi kuniambia: “Ruka kama ndege, mpaka milimani, maana waovu wanavuta pinde; wameweka mishale tayari juu ya uta, wawapige mshale watu wema gizani! Kama misingi ikiharibiwa, mtu mwadilifu atafanya nini?” Mwenyezi-Mungu yumo katika hekalu lake takatifu; kiti cha enzi cha Mwenyezi-Mungu kiko mbinguni. Kwa macho yake huwachungulia wanadamu, na kujua kila kitu wanachofanya. Mwenyezi-Mungu huwapima waadilifu na waovu; huwachukia kabisa watu wakatili. Atawanyeshea waovu makaa ya moto na madini ya kiberiti; upepo wa hari utakuwa ndio adhabu yao. Mwenyezi-Mungu ni mwadilifu na apenda uadilifu; watu wanyofu watakaa pamoja naye.


Tunakuja mbele zako Mungu wetu tukijinyenyekeza,tukijishusha na 
kujiachilia mikononi mwako Baba wa Mbinguni..
Yahweh tunaomba utusamehe dhambi zetu zote tulizozifanya kwakuwaza,
kwakunena,kwakutenda,kwakujua/kutojua..
Mungu wetu nasi tunaomba utupe neema ya kuweza kuwasamehe wale
wote waliotukosea..
Baba wa Mbinguni tunaomba utuepushe katika majaribu Yahweh tunaomba utuokoe na yule mwovu na kazi zake zote..
Jehovah tunaomba ututakase miili yetu na akili zetu Baba utufunike
kwa Damu ya Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo wa Nazareti
yeye aliteseka kwanza ili sisi tupate kupona..




Nani ee Mwenyezi-Mungu atakayekaa hemani mwako? Nani atakayeishi juu ya mlima wako mtakatifu? Ni mtu aishiye bila lawama, atendaye daima yaliyo mema, asemaye ukweli kutoka moyoni; ni mtu asiyesengenya watu, asiyemtendea uovu rafiki yake, wala kumfitini jirani yake; ni mtu anayewadharau wafisadi, lakini huwaheshimu wamchao Mwenyezi-Mungu; ni mtu asiyegeuza kiapo chake hata kikimtia hasara; asiyekopesha fedha yake kwa riba, wala kupokea rushwa kumdhulumu asiye na hatia. Mtu atendaye hayo, kamwe hatatikisika.

Yahweh tunaomba ukabariki kazi za mikono yetu Mungu wetu tunaomba
ukatupe ubunifu,maarifa katika ufanyaji/utendaji Jehovah tukatende
kama inavyokupendeza wewe..
Mungu wetu tunaomba ukabariki ridhiki zetu ziingiazo/zitokazo Yahweh
nasi tunaomba utupe neema ya kuweza kuwabariki wenye kuhitaji..
Baba wa Mbinguni tunaomba tusipungukiwe katika mahitaji yetu
Jehovah ukatupe sawasawa na mapenzi yako..

Mfalme wa Amani tuyaweka maisha yetu mikononi mwako Baba wa Mbinguni tunaomba ukabariki nyumba/ndoa zetu,watoto ,wazazi 
wetu,familia/ndugu na wote wanaotuzunguka..
Yahweh tunaomba amani yako ikatawale Baba wa Mbinguni tunaomba
Ulinzi wako kwetu na kwa vyote tunavyovimiliki,Mungu wetu tunaomba
ukatamalaki na kutuatamia Jehovah ukatuguse kwa mkono wako wenye nguvu Yahweh ukatupe uponyaji moyoni,tukanene yaliyoyako,tukapate
kutambua/kujitambua BABA tunaomba ukatupe neema ya kufuata njia
zako,kusimamia Neno lako amri na sheria zako siku zote za maisha yetu
Baba wa Mbinguni ukaonekane katika maisha yetu na popote tupitapo
na ijulikane kama Upo Mungu wetu..
Yahweh ukatufanye chombo chema nasi tukatumike kama inavyokupendeza wewe..
Roho matakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi..


Unilinde ee Mungu; maana kwako nakimbilia usalama. Namwambia Mungu: “Wewe u Bwana wangu; sina jema lolote ila wewe.” Ni bora sana hao watakatifu walioko nchini, kukaa nao ndiyo furaha yangu. Lakini wanaoabudu miungu mingine, watapata mateso mengi. Tambiko ya damu sitaitolea kamwe, na majina ya miungu hiyo sitayataja. Wewe ee Mwenyezi-Mungu ndiwe riziki yangu kuu, majaliwa yangu yamo mikononi mwako. Umenipimia sehemu nzuri sana; naam, urithi wangu ni wa kupendeza. Namsifu Mwenyezi-Mungu kwa kuniongoza, usiku dhamiri yangu yanionya. Namweka Mwenyezi-Mungu mbele yangu daima; yuko pamoja nami, wala sitatikisika. Kwa hiyo nitafurahi kwa moyo wote na kushangilia, nami nitakaa salama salimini. Naam wewe hutaiacha nafsi yangu kuzimu, hutaniacha mimi mwaminifu wako nipate kuoza. Wanionesha njia ya kufikia uhai; kuwako kwako kwanijaza furaha kamili, katika mkono wako wa nguvu mna mema ya milele.

Mungu wetu tazama wenye shida/tabu,wagonjwa,wenye njaa,wanaotaabika na kuelemewa na mizigo,wanaopitia magumu/majaribu mbalimbali,waliokatika vifungo vya yule mwovu,
waliokata tamaa,waliokataliwa,wenye hofu na mashaka,waliopoteza
matumaini,wajane,yatima,Mungu wetu tunaomba ukawaguse kwa mkono wako wenye nguvu,Yahweh ukawaponye kimwili na kiroho pia,Mungu wetu ukawafungue na kuwaweka huru,Jehovah ukawavushe salama na amani
yako ikawe nao,Baba wa Mbinguni ukawapatie chakula na ukabariki mashamba,kazi zao,Yahweh ukawasamehe wale wote waliokwenda kinyume nawe Mungu wetu ukaonekane katika maisha yao,Baba wa Mbinguni ukawape neema ya kujiombea,kufuata njia zako..
Yahweh Nuru yako ikaangaze katika maisha yao..
Mungu wetu tunaomba ukasikie,ukapokee na ukajibu sala/maombi yetu
Mungu wetu tunaomba ukawatendee sawasawa na mapenzi yako..
Wafiwa ukawe mfariji wao..



Lakini wewe wawaona wenye dhiki na shida; nawe daima uko tayari kuwasaidia. Mnyonge anakutegemea wewe, ee Mungu, wewe umekuwa daima msaada wa yatima. Uzivunje nguvu za mtu mwovu; ukomeshe uovu wake wote, usiwepo tena. Mwenyezi-Mungu ni mfalme milele na milele! Mataifa yasiyomjua yatatoweka nchini mwake. Ee Mwenyezi-Mungu, wapokea dua za mnyonge; wampa moyo na kumtegea sikio. Utawatendea haki yatima na wanaodhulumiwa, binadamu aliye udongo asiweze tena kuleta hofu.
Sifa na Utukufu tunakurudishia Mungu Baba..
Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele..
Amina..!

Asanteni sana wapendwa katika Bwana kwakuwa nami
Mungu aendelee kuwabariki,amani ya Kristo Yesu iwe nanyi daima
Baba wa Mbinguni akawatendee kama inavyompendeza yeye..
Nawapenda.

Mika na kabila la Dani

1Siku hizo hakukuwa na mfalme katika Israeli. Basi kabila la Dani lilikuwa linatafuta eneo lake lenyewe la kuishi humo, kwani mpaka wakati huo, halikuwa limegawiwa sehemu yake lenyewe miongoni mwa makabila ya Israeli. 2Hivyo watu wa kabila la Dani walichagua miongoni mwao watu hodari wakawatuma kutoka huko Eshtaoli na Sora wakawaamuru waende kuipeleleza nchi. Basi watu hao wakafika katika nchi ya milima ya Efraimu, nyumbani kwa Mika, wakakaa humo. 3Walipokuwa nyumbani kwa Mika, waliitambua sauti ya yule kijana Mlawi. Wakamgeukia na kumwuliza, “Nani amekuleta huku? Una shughuli gani hapa?” 4Yeye akawajibu, “Mika amefanya nami mpango; ameniajiri nami nimekuwa kuhani wake.” 5Nao wakamwambia, “Tafadhali utuulizie kwa Mwenyezi-Mungu kama tutafanikiwa katika safari yetu.” 6Yule kuhani akawaambia, “Nendeni kwa amani. Mwenyezi-Mungu anaichunga safari yenu.”
7Basi, watu hao watano wakaondoka, wakaenda Laishi. Waliwaona watu walioishi huko, na jinsi walivyokaa kwa usalama kama vile watu wa Sidoni. Walikuwa watu watulivu wasio na wasiwasi na hawakupungukiwa18:7 hawakupungukiwa: Linganisha na 18:10; maana katika Kiebrania si dhahiri. mahitaji yoyote nchini. Walikuwa mbali na watu wa Sidoni, na hawakuwa na shughuli yoyote na watu wengine.
8Basi hao wapelelezi walirudi kwa ndugu zao huko Sora na Eshtaoli, nao wakawauliza, “Mmetuletea taarifa gani?” 9Wao wakasema, “Inukeni twende na kuishambulia nchi hiyo. Tumeiona nchi hiyo, na kweli ni nchi yenye rutuba. Je, mtakaa hapa tu bila kufanya kitu? Msikawie kwenda kuimiliki nchi hiyo. 10Mtakapofika huko mtakuta watu wasio na wasiwasi wowote. Nchi hiyo ni kubwa, haikupungukiwa chochote na Mungu ameitia mikononi mwetu.”
11Basi, watu 600 wa kabila la Dani wakiwa na silaha zao za vita wakaondoka kutoka Sora na Eshtaoli 12wakaenda kupiga kambi yao huko Kiriath-yearimu katika nchi ya Yuda. Ndiyo maana mahali hapo, upande wa magharibi wa Kiriath-yearimu pameitwa Mahane-dani18:12 Mahane-dani: Maana yake ni Kambi ya Dani. mpaka leo. 13Kutoka huko wakaelekea nchi ya milima ya Efraimu, wakafika nyumbani kwa Mika.
14Watu wale watano waliokwenda kuipeleleza nchi ya Laishi wakawaambia ndugu zao, “Je, mnajua kwamba katika nyumba mojawapo ya hizi kuna kizibao, kinyago na sanamu ya kusubu? Basi, fikirini namna ya kufanya.” 15Basi wale wapelelezi wakaelekea kwenye nyumba ya Mika, wakaingia ndani na kumwuliza habari zake yule kijana Mlawi. 16Wakati huo, wale watu 600 wa kabila la Dani wakiwa na silaha zao za vita walisimama mlangoni. 17Wale watu watano waliokwenda kuipeleleza nchi waliingia ndani, wakachukua ile sanamu mungu ya kusubu, kile kizibao na kinyago cha ibada. Wakati huo yule kuhani alikuwa amesimama mlangoni pamoja na wale watu 600 wenye silaha. Basi, alipowaona wale wapelelezi 18wameingia nyumbani mwa Mika wakachukua sanamu ya kuchonga, kifuko cha kauli, kinyago na sanamu ile ya kusubu, akawauliza, “Mnafanya nini?” 19Nao wakamwambia, “Nyamaza, funga mdomo wako, uje pamoja nasi, uwe kuhani wetu na kama baba yetu. Au waonaje? Je, yafaa kwako zaidi kuwa kuhani wa mtu mmoja ama kuwa kuhani wa kabila moja la Israeli?” 20Yule kuhani akafurahi sana akachukua kile kifuko, kile kinyago cha ibada, na ile sanamu ya mungu ya kusubu, akafuatana nao.
21Basi, wakaanza safari yao, huku wametanguliwa na watoto wao na mifugo na mali zao. 22Walipokuwa wamefika mbali na nyumbani kwa Mika, watu waliokuwa jirani na Mika wakaitwa, wakawafuatia watu wa kabila la Dani wakawafikia. 23Kisha wakawapigia kelele, nao watu wa kabila la Dani wakageuka, wakamwuliza Mika, “Una shida gani hata umetufuatia pamoja na kundi hili lote?”
24Mika akasema, “Nyinyi mmechukua miungu yangu niliyojitengenezea, mkamchukua na kuhani wangu, mkaniacha bila chochote. Mnawezaje basi kuniuliza nina shida gani?” 25Watu wa kabila la Dani wakamwambia, “Afadhali uache kelele zako, la sivyo wengine wetu wenye hasira wanaweza wakakuvamia, nawe ukapoteza maisha yako na maisha ya jamaa yako.” 26Mika alipoona kwamba wamemzidi nguvu, akageuka, akarudi nyumbani; nao watu wa kabila la Dani wakaenda zao.
27Hao watu wa kabila la Dani walivichukua vitu vile ambavyo Mika alikuwa amevitengeneza, wakamchukua na yule kuhani aliyemhudumia. Basi wakaenda kushambulia Laishi wakawaua wakazi wake ambao waliishi humo kwa utulivu na bila wasiwasi, wakauteketeza mji huo. 28Wakazi wa mji huo hawakuwa na mtu wa kuwaokoa kwa sababu walikuwa mbali na mji wa Sidoni, tena hawakuwa na uhusiano na watu wengine. Mji huo ulikuwa kwenye bonde la Beth-rehobu. Watu wa kabila la Dani wakaujenga upya, wakaishi humo. 29Walibadilisha jina la mji huo, wakauita Dani, kufuata jina la babu yao aliyekuwa mwana wa Israeli. Lakini mji huo hapo awali uliitwa Laishi. 30Watu wa kabila la Dani wakaisimika ile sanamu ya kuchonga, naye Yonathani, mwana wa Gershomu, mwana wa Mose, akawa kuhani wao. Wazawa wake pia walikuwa makuhani wa kabila la Dani mpaka wananchi wa nchi hiyo walipopelekwa uhamishoni. 31Wakati wote nyumba ya Mungu ilipokuwa huko Shilo, watu wa kabila la Dani waliiabudu sanamu ya kuchonga ambayo Mika aliitengeneza.


Waamuzi 18;1-31


Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)

"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.

Tuesday 5 December 2017

Mahojiano Saidi Kanda - sehemu ya 2- NGOMA



Kwa Simu Toka London- Na Freddy Macha 
Kwa kuanzia kama hujawahi kumsikia  Saidi Kanda sikiliza wimbo maarufu "Nasikitika " wa Remmy Ongala. Hizo ngoma kali zinapigwa na nguli huyu mzawa wa Bagamoyo.
Mwezi huu, Desemba 2017,  Saidi Kanda yuko safarini Kenya na Tanzania kushughulikia muziki yake.
 Anahesabiwa kati ya wapiga ngoma stadi ulimwenguni.  Alitunukiwa tuzo ya kwanza ya shirika maarufu la  WOMAD - mwaka 1989. 
Sehemu ya pili ya mazungumzo na Mwanamuziki huyu wa Jadi- Mpiga ngoma mkali - Saidi Kanda- mkazi Uingereza- anazungumzia THAMANI ya Ngoma na vyombo vyetu asilia.




zaidi ingia;
Kwa Simu Toka London- Na Freddy Macha

Kikombe Cha Asubuhi ;Waamuzi 17...



Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?

Tumshukuru Mungu wetu katika yote..

Mtakatifu Baba wa Mbinguni,Mungu wetu,Muumba wetu,
Muumba wa nchi na Mbingu,Mungu wa Abarahamu,Isaka na Yakobo
Baba wa Upendo,Mungu mwenye nguvu,Baba wa Yatima,Mume wa
wajane,Baba wa baraka,Muweza wa yote,Alfa na Omega,Hakuna
kama wewe,unatosha Mungu wetu...
Unastahili sifa,unasthahili kuabudiwa,unasthahili kuhimidiwa
Utukufu ni wako Mungu wetu..!!

Mfalme wa amani tunakuja mbele zako tukijinyenyekeza,
tukijishusha na kujiachilia mikononi mwako Yahweh..
Baba wa Mbinguni tunaomba utusamehe makosa yetu yote 
tuliyoyafanya kwakuwaza,kwakunena,kwakutenda,kwakujua/kutojua
Jehovah nasi tunaomba utupe neema ya kuweza kuwasamehe wale
wote waliotukosea..
Mungu wetu tunaomba utuepushe katika majaribu Yahweh tunaomba
utuokoe na yule mwovu na kazi zake zote..
Jehovah tunaomba ututakase miili yetu na akili zetu Yahweh utufunike
kwa Damu ya Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo wa Nazareti
Yeye aliteseka kwanza ili sisi tupate kupona..


Mungu wetu tunaomba ukabariki kazi za mikono yetu
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe ubunifu,maarifa katika
ufanyaji/utendaji Yahweh nasi tukatende sawasawa na mapenzi yako
Jehovah tunaomba ukabariki ridhiki zetu ziingiazo/zitokazo Yahweh
nasi tunaomba utupe neema ya kuweza kuwabariki wenye kuhitaji
Mungu wetu tusipungukiwe katika mahitaji yetu Baba ukatupe
kama inavyokupendeza wewe..


Mfalme wa Amani tuyaweka maisha yetu mikononi mwako
Yahweh tunaomba ukabariki nyumba/ndoa zetu,watoto,wazazi
wetu,familia/ndugu na wote wanaotuzunguka...
Mungu wetu tunaomba ulinzi wako kwetu na kwavyote tunavyo
vimiliki,Baba wa Mbinguni tunaomba ukatamalaki na kutuatamia..Yahweh ukatupe neema ya kufuata njia zako,kusimamia Neno lako amri na sheria zako siku zote za maisha yetu..
Baba ukatupe neema ya kusaidiana,kuchukuliana,kusameheana,utu wema
fadhili,upendo wa kweli,kuhurumiana na yote yanayokupendeza wewe..
Nuru yako ikaangaze katika maisha yetu,Amani ikatawale,furaha na
shangwe zisipungue,Mungu wetu ukaonekane popote tupitapo na tukanene
yaliyo yako..



Kwa hiyo, ndugu zangu, maadamu Mungu ni mwenye huruma nyingi, nawasihi kwa moyo wote: Mtoleeni Mungu miili yenu kama tambiko iliyo hai, takatifu na yenye kupendeza. Hii ndiyo njia yenu halisi ya kumwabudu. Msiige mitindo ya ulimwengu huu, bali Mungu afanye mabadiliko ndani yenu kwa kuzigeuza fikira zenu. Hapo ndipo mtakapoweza kuyajua mapenzi ya Mungu na kutambua jambo lililo jema, linalompendeza na kamilifu. Kutokana na neema aliyonijalia Mungu, nawaambieni nyinyi nyote: Msijione kuwa ni kitu zaidi kuliko mnavyopaswa kuwa. Fikira zenu na ziwe na kiasi kadiri ya kipimo cha imani Mungu aliyomgawia kila mmoja. Mwili una viungo vingi, kila kimoja na kazi yake. Hali kadhalika ingawa sisi ni wengi, tu mwili mmoja kwa kuungana na Kristo, na kila mmoja ni kiungo cha mwenzake. Basi, tunavyo vipaji mbalimbali kadiri ya neema tuliyopewa. Mwenye kipaji cha unabii na akitumie kadiri ya imani yake. Mwenye kipaji cha utumishi na atumikie. Mwenye kipaji cha kufundisha na afundishe. Mwenye kipaji cha kuwafariji wengine na afanye hivyo. Mwenye kumgawia mwenzake alicho nacho na afanye hivyo kwa ukarimu. Msimamizi na asimamie kwa bidii; naye mwenye kutenda jambo la huruma na afanye hivyo kwa furaha.

Ukatufanye chombo chema Yahweh nasi tukatumike kama inavyokupendeza wewe..
Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi..

Mungu wetu tazama watoto wadodo walio yatima,wanao lelewa  na mzazi mmoja[single parent]sababu ya Ndoa kuvunjika/kutoelewana kwa wazazi,watoto walioterekezwa wazazi wao
wapo lakini hawawajali,watoto wanaopenda kusoma lakini hawana uwezo,watoto walio wagonjwa,wasiojiweza,wenye njaa,wanaopitia magumu/majaribu mbalimbali,waliokatika vifungo vya yule mwovu,
waliokata tamaa,wenye shida/tabu..Mungu wetu tunaomba ukawaguse kwa mkono wako wenye nguvu,
Yahweh tunaomba ukawaokoe na ukawaponye kimwilina kiroho pia,
Mungu wetu tunaomba ukaguse maisha ya hawa watoto,
Baba ukaguse hizi ndoa,Baba ukawaguse na walezi wao..
Mungu wetu tunaomba ukaonekane katika maisha ya watoto hawa
Baba wa Mbinguni ukawatendee sawasawa na mapenzi yako..
Furaha ikawe nao,Amani isipotee,Baba wakapate tumaini,Yahweh
ukawafariji,ukawape ubunifu/maarifa walezi wao,
Jehovah tunaomba upokee sala/maombi yetu Baba wa Mbinguni 
usikie kilio chetu na ukafute machozi ya hawa watoto,wazazi,walezi
 na wote wanaowaangalia/walea..
Mungu wetu nasi tunaomba utupe neema ya kuweza kuwasaidia
kwa chochote kitakacho kupendeza wewe,iwe sala/maombi,ikawe
kulipia ada,chakula,mavazi,sabuni,kuwatia moyo,kufurahi pamoja nao,
Ee Mungu wetu tunaomba ukatuongoze katika yote...!!


Mapendo yenu na yawe bila unafiki wowote. Chukieni jambo lolote ovu, zingatieni jema. Pendaneni kindugu; kila mmoja amfikirie kwanza mwenzake kwa heshima. Msilegee katika bidii, ila muwe wachangamfu rohoni katika kumtumikia Bwana. Tumaini lenu liwaweke daima wenye furaha; muwe na saburi katika shida, na kusali daima. Wasaidieni watu wa Mungu katika mahitaji yao; wapokeeni wageni kwa ukarimu. Watakieni baraka wote wanaowadhulumu nyinyi; naam, watakieni baraka na wala msiwalaani. Furahini pamoja na wenye kufurahi, lieni pamoja na wenye kulia. Ishini kwa kupatana vema nyinyi kwa nyinyi. Msijitakie makuu, bali jishughulisheni na madogo. Msijione kuwa wenye hekima sana. Msilipe ovu kwa ovu. Zingatieni mambo mema mbele ya wote. Kadiri inavyowezekana kwa upande wenu, muwe na amani na watu wote. Wapenzi wangu, msilipize kisasi, bali mwachieni Mungu jambo hilo; maana Maandiko Matakatifu yasema: “Kulipiza kisasi ni shauri langu; mimi nitalipiza, asema Bwana.” Zaidi ya hayo, Maandiko yasema: “Adui yako akiwa na njaa, mpe chakula; akiwa na kiu, mpe kinywaji. Maana kwa kufanya hivyo utamfanya apate aibu kali kama makaa ya moto juu ya kichwa chake.” Usikubali kushindwa na ubaya, bali ushinde ubaya kwa wema.
Sifa na Utukufu tunakurudishia Mungu wetu..
Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele..
Amina..!

Asanteni sana wapendwa katika Bwana kwa kuwa nami
Baba wa Mbinguni awe nanyi daima..
Nawapenda.


Sanamu za Mika

1Kulikuwa na mtu mmoja huko katika milima ya Efraimu, jina lake Mika. 2Siku moja alimwambia mama yake, “Vile vipande 1,100 vya fedha ulivyoibiwa, nawe ukamlaani aliyekuibia nikisikia, mimi ninavyo. Mimi ndiye niliyevichukua.” Mama yake akasema, “Mwanangu, ubarikiwe na Mwenyezi-Mungu.” 3Mika akamrudishia mama yake hivyo vipande 1,100 vya fedha. Mama yake akasema, “Ili laana niliyotoa isikupate, fedha hii naiweka wakfu kwa Mwenyezi-Mungu, ili kutengenezea sanamu ya kuchonga na ya kusubu. Sasa ninakurudishia vipande hivyo vya fedha.” 4Mika alipomrudishia mama yake hiyo fedha, mama yake akachukua vipande 200 vya fedha, akampa mfua fedha, naye akafua sanamu ya kuchonga na ya kusubu. Sanamu hiyo ikawekwa ndani ya nyumba ya Mika. 5Mtu huyo, Mika, alikuwa na mahali pake pa ibada. Alitengeneza kizibao cha kuhani na kinyago, kisha akamfanya mmoja wa watoto wake kuwa kuhani wake. 6Siku hizo hapakuwepo na mfalme katika Israeli. Kila mtu alifanya chochote alichoona ni chema.
7Wakati huo kulikuwa na kijana mmoja Mlawi mjini Bethlehemu nchini Yuda. 8Kijana huyo akaondoka Bethlehemu nchini Yuda, akaenda kutafuta mahali pengine pa kuishi. Katika safari yake akafika nyumbani kwa Mika katika nchi ya milima ya Efraimu. 9Mika akamwuliza, “Umetoka wapi?” Naye akamjibu, “Mimi ni Mlawi, kutoka mjini Bethlehemu nchini Yuda. Nitakaa popote nitakapopata nafasi ya kukaa kama mgeni.” 10Mika akamwambia, “Kaa pamoja nami, uwe kwangu kama baba na kuhani wangu. Nitakulipa vipande kumi vya fedha kila mwaka na mavazi pamoja na mahitaji yako.” 11Huyo Mlawi akaingia akakubali, akakaa huko na kuwa kama mmoja wa wana wa Mika. 12Naye Mika akamfanya kijana huyo Mlawi kuwa kuhani wake huko nyumbani kwake. 13Kisha akasema, “Sasa najua kwamba Mwenyezi-Mungu atanifanikisha kwani nina kijana huyu Mlawi kama kuhani wangu.”


Waamuzi 17;1-13

Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)

"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.


Monday 4 December 2017

Kikombe Cha Asubuhi ;Waamuzi 16...



Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?
Haleluyah..!!Mungu wetu yu mwema sana..
Ni siku/wiki nyingine tena Mungu wetu ametuchagua na kutupa
kibali cha kuendelea kuiona leo hii...
Si kwa nguvu zetu wala si kwa utashi wetu,si kwamba sisi 
tumetenda mema sana,si kwa ujuaji wetu wala si kwa akili zetu
sisi kuwa hivi tulivyo leo hii..
Ni kwa neema/rehema zake Mungu wetu/ni kwa mapenzi yake Baba
wa Mbinguni...
Basi tuitumie nafasi hii vyema wapendwa/waungwana..
Tumshukuru Mungu wetu katika yote..


Kwa hiyo tunapaswa kuzingatia kwa makini yote tuliyosikia, tusije tukayakosa. Ujumbe ule waliopewa wazee wetu na malaika ulioneshwa kuwa kweli, hata mtu yeyote ambaye hakuufuata au hakuutii aliadhibiwa kama alivyostahili. Basi, sisi tutaokokaje kama hatuujali wokovu mkuu kama huu? Kwanza Bwana mwenyewe aliutangaza wokovu huu, na wale waliomsikia walituthibitishia kwamba ni kweli. Mungu pia aliongeza hapo ushahidi wake kwa kufanya kila namna ya miujiza na maajabu, na kwa kuwagawia watu vipaji vya Roho Mtakatifu kadiri ya mapenzi yake.

Mtakatifu Baba wa Mbinguni,Mungu wetu,Muumba wetu,Muumba wa 
Nchi na Mbingu,Muumba wa vyote vilivyomo,vinavyoonekana na 
visivyooneka,Mungu wa Abrahamu,Isaka na Yakobo..!
Muweza wa yote,Utukuzwe ee Mungu wetu,Unastahili sifa Jehovah..!
Unastahili kuabudiwa Baba wa Mbinguni,Unastahili kuhimidiwa Yahweh
Unastahili ee Mungu wetu..!
Matendo yako ni makuu mno,Matendo yako
ni ya ajabu,Unatosha Baba wa Mbinguni,Hakuna kama wewe..!!
Sifa na Utukufu tunakurudishia ee Mungu wetu..!!

Tazama jana imepita Baba wa Mbinguni Leo ni siku mpya Yahweh
na Kesho ni siku nyingine Jehovah..
Mungu wetu tunakuja mbele zako tukijinyenyekeza,tukijishusha na 
kujiachilia mikononi mwako Yahweh..
Baba wa Mbinguni tunaomba utusamehe dhambi zetu zote tulizo zifanya
kwakuwaza,kwakunena,kwakutenda,kwakujua/kutojua..
Mungu wetu nasi tunaomba utupe neema ya kuweza kuwasamehe wale
wote waliotukosea..
Yahweh tunaomba utuepushe katika majaribu Mungu wetu utuokoe na
yule mwovu na kazi zake zote..
Jehovah tunaomba ututakase miili yetu na akili zetu Yahweh tunaomba
utufunike kwa Damu ya Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo wa Nazareti
yeye aliteseka kwanza ili sisi tupate kupona..




Mungu hakuwaweka malaika wautawale ulimwengu ujao, yaani ulimwengu ule tunaoongea habari zake. Tena yasemwa mahali fulani katika Maandiko: “Mtu ni nini, hata umfikirie; mwanadamu ni nini hata umjali? Ulimfanya tu kidogo kuwa chini ya malaika; umemvika taji ya utukufu na heshima, ukaweka kila kitu chini ya miguu yake.” Yasemwa kwamba Mungu alimweka mtu kuwa mtawala wa vitu vyote, yaani bila kuacha hata kimoja. Hata hivyo, hatuoni bado mtu akivitawala vitu vyote sasa. Lakini twamwona Yesu ambaye alifanywa kwa kitambo kidogo kuwa chini kuliko malaika, ili kwa neema ya Mungu afe kwa ajili ya watu wote. Sasa tunamwona ametawazwa kwa utukufu na heshima kwa sababu ya kifo alichoteseka. Ilikuwa haki tupu kwamba Mungu, ambaye huumba na kutegemeza vitu vyote, alimfanya Yesu kuwa mkamilifu kabisa kwa njia ya mateso, ili awalete watoto wengi waushiriki utukufu wake. Maana Yesu ndiye anayewaongoza kwenye wokovu. Yeye anawatakasa watu dhambi zao, naye pamoja na wale waliotakaswa, wote wanaye Baba mmoja. Ndiyo maana Yesu haoni aibu kuwaita hao, ndugu zake;

Yahweh tunaomba ukabariki kazi za mikono yetu BABA tunaomba
ukatupe ubunifu,maarifa katika ufanyaji na utendaji Mungu wetu
tukatende sawasawa na mapenzi yako..
Baba wa Mbinguni tunaomba ukabariki ridhiki zetu ziingiazo/zitokazo
Yahweh nasi tunaomba utupe neema ya kuweza kuwabariki wenye kuhitaji
Jehovah tunaomba tusipungukiwe katika mahitaji yetu Baba wa Mbinguni
tunaomba ukatupe kama inavyokupendeza wewe..

Mfalme wa Amani tunayaweka maisha yetu mikononi mwako..
Jehovah tunaomba ukabariki nyumba/ndoa zetu,watoto,wazazi wetu,familia/ndugu na wote wanaotuzunguka..
Yahweh tunaomba ulinzi wako kwetu na kwa vyote tunavyo vimiliki
Mungu wetu tunaomba ukatupe neema ya kufuata njia zako,kusimamia
Neno lako amri na sheria zako siku zote za maisha yetu..
Baba wa Mbinguni utuokoe na kiburi,majivuno,makwazo na yote
yanayokwenda kinyume nawe,Mungu wetu tunaomba upendo kati yetu
udumu,amani ya moyo,furaha,utuwema,msamaha,tuchukuliane,
tuonyane/tuelimishane kwa amani na upendo,Mungu wetu ukatupe
macho ya rohoni na masikio ya kusikia sauti yako na kutii..
Baba wa Mbinguni ukatufanye chombo chema Yahweh nasi tukatumike
kama inavyokupendeza wewe..
Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi..




kama asemavyo: “Ee Mungu, nitawasimulia ndugu zangu matendo yako. Nitakusifu katika kusanyiko lao.” Tena asema: “Nitamwekea Mungu tumaini langu.” Na tena: “Mimi niko hapa pamoja na watoto alionipa Mungu.” Basi, kwa vile watoto hao, kama awaitavyo, ni watu wenye mwili na damu, Yesu mwenyewe akawa kama wao na kushiriki ubinadamu wao. Alifanya hivyo ili, kwa njia ya kifo chake, amwangamize Ibilisi ambaye ana mamlaka juu ya kifo, na hivyo awaokoe wale waliokuwa watumwa maisha yao yote kwa sababu ya hofu yao ya kifo. Maana ni wazi kwamba yeye hakuja kuwasaidia malaika, bali kama yasemavyo Maandiko: “Anawasaidia wazawa wa Abrahamu.” Ndiyo maana ilimbidi awe kama ndugu zake kwa kila namna, ili awe Kuhani Mkuu wao aliye mwaminifu na mwenye huruma katika kumtumikia Mungu, ili dhambi za watu ziondolewe. Na, anaweza sasa kuwasaidia wale wanaojaribiwa na kuteswa.


Tazama wenye shida/tabu,wagonjwa,wenye njaa,wanaopitia 
magumu/majaribu mbalimbali,waliokatika vifungo vya yule
mwovu,waliokata tamaa na waliokataliwa,walioanguka/walio
kwenda kinyume nawe na wote wasumbukao na kuelemewa na
mizigo..Mungu wetu tunaomba ukawaguse kwa mkono wako wenye
nguvu,Baba ukawape uponyaji wa mwili na roho,Yahweh
ukaonekane katika mapito yao,Mungu wetu ukawasamehe
na kuwasimamisha tena,Jehovah tunaomba ukawape neema
ya kujiombea,kufuata njia zako nazo ziwaweka huru..
Baba wa mbinguni ukabariki mashamba yao wapate chakula
cha kutosha na kuweka akiba..Ee Mungu wetu ukawafungue
na kuwaokoa,Nuru yako ikaangaze katika maisha yao..
Jehovah tunaomba usikie na upokee maombi/sala zetu..

Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele..
Amina..!
Wapendwa katika Kristo Yesu asanteni sana kwakuwa nami..
Mungu aendelee kuwabariki na msipungukiwe katika mahitaji yenu
Baba wa Mbinguni akawape kama inavyompendeza yeye..
Amani ya Bwana wetu Yesu Kristo iwe nayi daima..
Nawapenda.

Samsoni huko Gaza

1Siku moja Samsoni alikwenda mjini Gaza, akakutana na malaya mmoja akalala naye. 2Watu wa Gaza walipoambiwa kuwa Samsoni yuko huko, walilizingira eneo hilo na kumvizia kwenye lango la mji usiku kucha. Wakakaa kimya huko langoni usiku wote wakifikiri kwamba wanaweza kungojea mpaka mapambazuko wapate kumuua. 3Lakini Samsoni akabaki mjini mpaka usiku wa manane. Wakati wa usiku wa manane akaamka akashika miimo miwili ya malango, akaingoa pamoja na makomeo yake akaibeba na kwenda nayo mpaka karibu na Hebroni.

Delila anamsaliti Samsoni

4Baada ya hayo, Samsoni alimpenda mwanamke mmoja aitwaye Delila ambaye aliishi katika bonde la Soreki. 5Wakuu wa Wafilisti wakamjia Delila, wakamwambia, “Mbembeleze Samsoni ili ujue asili ya nguvu zake nyingi ili tuweze kumkamata na kumfunga. Ukifanya hivyo, kila mmoja wetu atakupa vipande thelathini vya fedha.” 6Delila akamwambia Samsoni, “Tafadhali, niambie asili ya nguvu zako, na jinsi gani mtu anaweza kukushinda na kukufunga.” 7Samsoni akamjibu, “Wakinifunga kwa kamba saba mbichi za upinde, nitakuwa dhaifu kama mtu yeyote.” 8Wakuu wa Wafilisti wakamletea Delila kamba hizo saba mbichi za upinde, naye akamfunga Samsoni kwa kamba hizo. 9Delila alikuwa ameweka watu wamvizie katika chumba cha ndani. Kisha, akamwambia Samsoni kwa sauti kubwa, “Samsoni, Wafilisti wamekujia kukushambulia.” Samsoni akazikata kamba hizo kama nyuzi za kitani zinapogusa moto. Hivyo hakuna aliyegundua siri ya nguvu zake.
10Delila akamwambia Samsoni, “Wewe umenidhihaki. Umenidanganya. Tafadhali niambie jinsi unavyoweza kufungwa.” 11Samsoni akamjibu, “Wakinifunga kwa kamba mpya ambazo hazijatumiwa, nitakuwa dhaifu kama mtu yeyote.” 12Basi, Delila akachukua kamba mpya, akamfunga nazo. Kisha akamwambia Samsoni kwa sauti kubwa, “Samsoni! Wafilisti wamekuja kukushambulia!” Wakati huo kulikuwa na watu chumbani wakimvizia. Samsoni akazikata kamba hizo kama uzi.
13Delila akamwambia Samsoni, “Mpaka sasa bado unanidhihaki. Umenidanganya. Niambie unavyoweza kufungwa.” Samsoni akamwambia, “Ukivisuka vishungi vyangu saba vya nywele zangu katika mtandio wa nguo na kuvikaza kabisa kwa kigingi, nitakuwa dhaifu kama mtu yeyote.” 14Wakati Samsoni alipokuwa analala Delila akavisuka pamoja vishungi saba vya nywele za Samsoni akavifunga kwa mtandio wa nguo na kuvikaza kabisa kwa kigingi. Kisha akamwambia Samsoni, “Samsoni! Wafilisti wanakuja kukushambulia.” Samsoni akaamka kutoka usingizini akakingoa kile kigingi na kuutatua ule mtandio wa nguo.
15Delila akamwambia Samsoni, “Unawezaje kusema kuwa unanipenda na moyo wako hauko pamoja nami? Umenidhihaki sasa mara tatu. Hujaniambia asili ya nguvu zako iko wapi.” 16Delila alipoendelea kumbana sana Samsoni kwa maneno, siku baada ya siku na kumkera hata akachoka rohoni karibu kufa, 17hakuweza kuvumilia, akamfunulia siri yake, akisema, “Nywele zangu kamwe hazijapata kunyolewa. Mimi nimewekwa wakfu kwa Mungu tangu tumboni mwa mama yangu. Kama nikinyolewa nguvu zangu zitanitoka, nami nitakuwa dhaifu kama mtu yeyote.”
18Basi, Delila alipoona kwamba Samsoni amemwambia siri yake yote, akawaita wakuu wa Wafilisti, akawaambia, “Njoni safari hii moja tu maana Samsoni ameniambia siri yake yote.” Wakuu wa Wafilisti wakamwendea Delila huku wamemletea fedha walizomwahidi. 19Naye Delila akamfanya Samsoni alale usingizi magotini mwake, akamwita mtu amnyoe vile vishungi vyake saba. Kisha Delila akaanza kumtesa Samsoni kwa kuwa sasa nguvu zilikuwa zimemtoka. 20Delila akamwambia Samsoni, “Samsoni! Wafilisti wanakuja kukushambulia!” Samsoni akaamka usingizini huku akifikiri kwamba atatoka na kujiokoa kama hapo awali. Kumbe hakujua kwamba Mwenyezi-Mungu alikuwa amemwacha. 21Wafilisti walimkamata, wakamngoa macho, wakampeleka Gaza, wakamfunga kwa pingu za shaba, na kumlazimisha kufanya kazi ya kusaga unga huko gerezani. 22Lakini nywele zake zikaanza kukua tena baada ya kunyolewa.

Kifo cha Samsoni

23Wakuu wa Wafilisti walikusanyika ili kusherehekea na kumtolea tambiko mungu wao aitwaye Dagoni. Basi, wakawa wanaimba, “Mungu wetu amemtia mikononi mwetu adui yetu Samsoni.” 24Watu walipomwona Samsoni wakamsifu mungu wao na kusema, “Mungu wetu amemtia mikononi mwetu adui yetu ambaye amekuwa akiharibu nchi yetu na kuwaua wengi wetu.” 25Walipojawa na furaha sana mioyoni mwao, wakasema, “Mleteni Samsoni atutumbuize.” Basi wakamtoa Samsoni gerezani, wakamleta naye akawatumbuiza. Wakamweka katikati ya nguzo. 26Samsoni akamwambia kijana aliyekuwa anamwongoza, “Niruhusu nizipapase nguzo zinazotegemeza jumba hili ili nami niziegemee.” 27Jumba hilo lilikuwa limejaa watu: Wakuu wote wa Wafilisti walikuwapo na kwenye paa kulikuwa na watu 3,000 wanaume na wanawake, wakimtazama Samsoni akiwatumbuiza.
28Hapo Samsoni akamwomba Mwenyezi-Mungu: “Bwana Mwenyezi-Mungu nakuomba unikumbuke. Nitie nguvu, mara hii moja tu, ee Mungu, ili niwalipize kisasi mara moja hii tu Wafilisti ambao waliyangoa macho yangu mawili.” 29Samsoni akazishika nguzo mbili za katikati ambazo zilitegemeza uzito wote wa jumba hilo, mkono mmoja nguzo hii na mkono mwingine nguzo ya pili. 30Kisha akasema, “Na nife pamoja na Wafilisti.” Akasukuma kwa nguvu zake zote. Jumba likawaangukia wakuu hao wote wa Wafilisti waliokuwamo humo ndani. Wale waliouawa wakati wa kifo chake walikuwa wengi kuliko wale aliowaua wakati wa uhai wake. 31Ndugu zake na jamaa yake yote wakaja kumchukua; wakamzika katikati ya mji wa Sora na mji wa Eshtaoli katika kaburi la Manoa, baba yake. Samsoni alikuwa mwamuzi wa Israeli kwa miaka ishirini.


Waamuzi 16;1-31

Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)

"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.