Swahili na Waswahili

Swahili na Waswahili
Waswahili na Mswahili Rachel Siwa...Pamoja Daima!!

Monday 4 December 2017

Kikombe Cha Asubuhi ;Waamuzi 16...



Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?
Haleluyah..!!Mungu wetu yu mwema sana..
Ni siku/wiki nyingine tena Mungu wetu ametuchagua na kutupa
kibali cha kuendelea kuiona leo hii...
Si kwa nguvu zetu wala si kwa utashi wetu,si kwamba sisi 
tumetenda mema sana,si kwa ujuaji wetu wala si kwa akili zetu
sisi kuwa hivi tulivyo leo hii..
Ni kwa neema/rehema zake Mungu wetu/ni kwa mapenzi yake Baba
wa Mbinguni...
Basi tuitumie nafasi hii vyema wapendwa/waungwana..
Tumshukuru Mungu wetu katika yote..


Kwa hiyo tunapaswa kuzingatia kwa makini yote tuliyosikia, tusije tukayakosa. Ujumbe ule waliopewa wazee wetu na malaika ulioneshwa kuwa kweli, hata mtu yeyote ambaye hakuufuata au hakuutii aliadhibiwa kama alivyostahili. Basi, sisi tutaokokaje kama hatuujali wokovu mkuu kama huu? Kwanza Bwana mwenyewe aliutangaza wokovu huu, na wale waliomsikia walituthibitishia kwamba ni kweli. Mungu pia aliongeza hapo ushahidi wake kwa kufanya kila namna ya miujiza na maajabu, na kwa kuwagawia watu vipaji vya Roho Mtakatifu kadiri ya mapenzi yake.

Mtakatifu Baba wa Mbinguni,Mungu wetu,Muumba wetu,Muumba wa 
Nchi na Mbingu,Muumba wa vyote vilivyomo,vinavyoonekana na 
visivyooneka,Mungu wa Abrahamu,Isaka na Yakobo..!
Muweza wa yote,Utukuzwe ee Mungu wetu,Unastahili sifa Jehovah..!
Unastahili kuabudiwa Baba wa Mbinguni,Unastahili kuhimidiwa Yahweh
Unastahili ee Mungu wetu..!
Matendo yako ni makuu mno,Matendo yako
ni ya ajabu,Unatosha Baba wa Mbinguni,Hakuna kama wewe..!!
Sifa na Utukufu tunakurudishia ee Mungu wetu..!!

Tazama jana imepita Baba wa Mbinguni Leo ni siku mpya Yahweh
na Kesho ni siku nyingine Jehovah..
Mungu wetu tunakuja mbele zako tukijinyenyekeza,tukijishusha na 
kujiachilia mikononi mwako Yahweh..
Baba wa Mbinguni tunaomba utusamehe dhambi zetu zote tulizo zifanya
kwakuwaza,kwakunena,kwakutenda,kwakujua/kutojua..
Mungu wetu nasi tunaomba utupe neema ya kuweza kuwasamehe wale
wote waliotukosea..
Yahweh tunaomba utuepushe katika majaribu Mungu wetu utuokoe na
yule mwovu na kazi zake zote..
Jehovah tunaomba ututakase miili yetu na akili zetu Yahweh tunaomba
utufunike kwa Damu ya Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo wa Nazareti
yeye aliteseka kwanza ili sisi tupate kupona..




Mungu hakuwaweka malaika wautawale ulimwengu ujao, yaani ulimwengu ule tunaoongea habari zake. Tena yasemwa mahali fulani katika Maandiko: “Mtu ni nini, hata umfikirie; mwanadamu ni nini hata umjali? Ulimfanya tu kidogo kuwa chini ya malaika; umemvika taji ya utukufu na heshima, ukaweka kila kitu chini ya miguu yake.” Yasemwa kwamba Mungu alimweka mtu kuwa mtawala wa vitu vyote, yaani bila kuacha hata kimoja. Hata hivyo, hatuoni bado mtu akivitawala vitu vyote sasa. Lakini twamwona Yesu ambaye alifanywa kwa kitambo kidogo kuwa chini kuliko malaika, ili kwa neema ya Mungu afe kwa ajili ya watu wote. Sasa tunamwona ametawazwa kwa utukufu na heshima kwa sababu ya kifo alichoteseka. Ilikuwa haki tupu kwamba Mungu, ambaye huumba na kutegemeza vitu vyote, alimfanya Yesu kuwa mkamilifu kabisa kwa njia ya mateso, ili awalete watoto wengi waushiriki utukufu wake. Maana Yesu ndiye anayewaongoza kwenye wokovu. Yeye anawatakasa watu dhambi zao, naye pamoja na wale waliotakaswa, wote wanaye Baba mmoja. Ndiyo maana Yesu haoni aibu kuwaita hao, ndugu zake;

Yahweh tunaomba ukabariki kazi za mikono yetu BABA tunaomba
ukatupe ubunifu,maarifa katika ufanyaji na utendaji Mungu wetu
tukatende sawasawa na mapenzi yako..
Baba wa Mbinguni tunaomba ukabariki ridhiki zetu ziingiazo/zitokazo
Yahweh nasi tunaomba utupe neema ya kuweza kuwabariki wenye kuhitaji
Jehovah tunaomba tusipungukiwe katika mahitaji yetu Baba wa Mbinguni
tunaomba ukatupe kama inavyokupendeza wewe..

Mfalme wa Amani tunayaweka maisha yetu mikononi mwako..
Jehovah tunaomba ukabariki nyumba/ndoa zetu,watoto,wazazi wetu,familia/ndugu na wote wanaotuzunguka..
Yahweh tunaomba ulinzi wako kwetu na kwa vyote tunavyo vimiliki
Mungu wetu tunaomba ukatupe neema ya kufuata njia zako,kusimamia
Neno lako amri na sheria zako siku zote za maisha yetu..
Baba wa Mbinguni utuokoe na kiburi,majivuno,makwazo na yote
yanayokwenda kinyume nawe,Mungu wetu tunaomba upendo kati yetu
udumu,amani ya moyo,furaha,utuwema,msamaha,tuchukuliane,
tuonyane/tuelimishane kwa amani na upendo,Mungu wetu ukatupe
macho ya rohoni na masikio ya kusikia sauti yako na kutii..
Baba wa Mbinguni ukatufanye chombo chema Yahweh nasi tukatumike
kama inavyokupendeza wewe..
Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi..




kama asemavyo: “Ee Mungu, nitawasimulia ndugu zangu matendo yako. Nitakusifu katika kusanyiko lao.” Tena asema: “Nitamwekea Mungu tumaini langu.” Na tena: “Mimi niko hapa pamoja na watoto alionipa Mungu.” Basi, kwa vile watoto hao, kama awaitavyo, ni watu wenye mwili na damu, Yesu mwenyewe akawa kama wao na kushiriki ubinadamu wao. Alifanya hivyo ili, kwa njia ya kifo chake, amwangamize Ibilisi ambaye ana mamlaka juu ya kifo, na hivyo awaokoe wale waliokuwa watumwa maisha yao yote kwa sababu ya hofu yao ya kifo. Maana ni wazi kwamba yeye hakuja kuwasaidia malaika, bali kama yasemavyo Maandiko: “Anawasaidia wazawa wa Abrahamu.” Ndiyo maana ilimbidi awe kama ndugu zake kwa kila namna, ili awe Kuhani Mkuu wao aliye mwaminifu na mwenye huruma katika kumtumikia Mungu, ili dhambi za watu ziondolewe. Na, anaweza sasa kuwasaidia wale wanaojaribiwa na kuteswa.


Tazama wenye shida/tabu,wagonjwa,wenye njaa,wanaopitia 
magumu/majaribu mbalimbali,waliokatika vifungo vya yule
mwovu,waliokata tamaa na waliokataliwa,walioanguka/walio
kwenda kinyume nawe na wote wasumbukao na kuelemewa na
mizigo..Mungu wetu tunaomba ukawaguse kwa mkono wako wenye
nguvu,Baba ukawape uponyaji wa mwili na roho,Yahweh
ukaonekane katika mapito yao,Mungu wetu ukawasamehe
na kuwasimamisha tena,Jehovah tunaomba ukawape neema
ya kujiombea,kufuata njia zako nazo ziwaweka huru..
Baba wa mbinguni ukabariki mashamba yao wapate chakula
cha kutosha na kuweka akiba..Ee Mungu wetu ukawafungue
na kuwaokoa,Nuru yako ikaangaze katika maisha yao..
Jehovah tunaomba usikie na upokee maombi/sala zetu..

Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele..
Amina..!
Wapendwa katika Kristo Yesu asanteni sana kwakuwa nami..
Mungu aendelee kuwabariki na msipungukiwe katika mahitaji yenu
Baba wa Mbinguni akawape kama inavyompendeza yeye..
Amani ya Bwana wetu Yesu Kristo iwe nayi daima..
Nawapenda.

Samsoni huko Gaza

1Siku moja Samsoni alikwenda mjini Gaza, akakutana na malaya mmoja akalala naye. 2Watu wa Gaza walipoambiwa kuwa Samsoni yuko huko, walilizingira eneo hilo na kumvizia kwenye lango la mji usiku kucha. Wakakaa kimya huko langoni usiku wote wakifikiri kwamba wanaweza kungojea mpaka mapambazuko wapate kumuua. 3Lakini Samsoni akabaki mjini mpaka usiku wa manane. Wakati wa usiku wa manane akaamka akashika miimo miwili ya malango, akaingoa pamoja na makomeo yake akaibeba na kwenda nayo mpaka karibu na Hebroni.

Delila anamsaliti Samsoni

4Baada ya hayo, Samsoni alimpenda mwanamke mmoja aitwaye Delila ambaye aliishi katika bonde la Soreki. 5Wakuu wa Wafilisti wakamjia Delila, wakamwambia, “Mbembeleze Samsoni ili ujue asili ya nguvu zake nyingi ili tuweze kumkamata na kumfunga. Ukifanya hivyo, kila mmoja wetu atakupa vipande thelathini vya fedha.” 6Delila akamwambia Samsoni, “Tafadhali, niambie asili ya nguvu zako, na jinsi gani mtu anaweza kukushinda na kukufunga.” 7Samsoni akamjibu, “Wakinifunga kwa kamba saba mbichi za upinde, nitakuwa dhaifu kama mtu yeyote.” 8Wakuu wa Wafilisti wakamletea Delila kamba hizo saba mbichi za upinde, naye akamfunga Samsoni kwa kamba hizo. 9Delila alikuwa ameweka watu wamvizie katika chumba cha ndani. Kisha, akamwambia Samsoni kwa sauti kubwa, “Samsoni, Wafilisti wamekujia kukushambulia.” Samsoni akazikata kamba hizo kama nyuzi za kitani zinapogusa moto. Hivyo hakuna aliyegundua siri ya nguvu zake.
10Delila akamwambia Samsoni, “Wewe umenidhihaki. Umenidanganya. Tafadhali niambie jinsi unavyoweza kufungwa.” 11Samsoni akamjibu, “Wakinifunga kwa kamba mpya ambazo hazijatumiwa, nitakuwa dhaifu kama mtu yeyote.” 12Basi, Delila akachukua kamba mpya, akamfunga nazo. Kisha akamwambia Samsoni kwa sauti kubwa, “Samsoni! Wafilisti wamekuja kukushambulia!” Wakati huo kulikuwa na watu chumbani wakimvizia. Samsoni akazikata kamba hizo kama uzi.
13Delila akamwambia Samsoni, “Mpaka sasa bado unanidhihaki. Umenidanganya. Niambie unavyoweza kufungwa.” Samsoni akamwambia, “Ukivisuka vishungi vyangu saba vya nywele zangu katika mtandio wa nguo na kuvikaza kabisa kwa kigingi, nitakuwa dhaifu kama mtu yeyote.” 14Wakati Samsoni alipokuwa analala Delila akavisuka pamoja vishungi saba vya nywele za Samsoni akavifunga kwa mtandio wa nguo na kuvikaza kabisa kwa kigingi. Kisha akamwambia Samsoni, “Samsoni! Wafilisti wanakuja kukushambulia.” Samsoni akaamka kutoka usingizini akakingoa kile kigingi na kuutatua ule mtandio wa nguo.
15Delila akamwambia Samsoni, “Unawezaje kusema kuwa unanipenda na moyo wako hauko pamoja nami? Umenidhihaki sasa mara tatu. Hujaniambia asili ya nguvu zako iko wapi.” 16Delila alipoendelea kumbana sana Samsoni kwa maneno, siku baada ya siku na kumkera hata akachoka rohoni karibu kufa, 17hakuweza kuvumilia, akamfunulia siri yake, akisema, “Nywele zangu kamwe hazijapata kunyolewa. Mimi nimewekwa wakfu kwa Mungu tangu tumboni mwa mama yangu. Kama nikinyolewa nguvu zangu zitanitoka, nami nitakuwa dhaifu kama mtu yeyote.”
18Basi, Delila alipoona kwamba Samsoni amemwambia siri yake yote, akawaita wakuu wa Wafilisti, akawaambia, “Njoni safari hii moja tu maana Samsoni ameniambia siri yake yote.” Wakuu wa Wafilisti wakamwendea Delila huku wamemletea fedha walizomwahidi. 19Naye Delila akamfanya Samsoni alale usingizi magotini mwake, akamwita mtu amnyoe vile vishungi vyake saba. Kisha Delila akaanza kumtesa Samsoni kwa kuwa sasa nguvu zilikuwa zimemtoka. 20Delila akamwambia Samsoni, “Samsoni! Wafilisti wanakuja kukushambulia!” Samsoni akaamka usingizini huku akifikiri kwamba atatoka na kujiokoa kama hapo awali. Kumbe hakujua kwamba Mwenyezi-Mungu alikuwa amemwacha. 21Wafilisti walimkamata, wakamngoa macho, wakampeleka Gaza, wakamfunga kwa pingu za shaba, na kumlazimisha kufanya kazi ya kusaga unga huko gerezani. 22Lakini nywele zake zikaanza kukua tena baada ya kunyolewa.

Kifo cha Samsoni

23Wakuu wa Wafilisti walikusanyika ili kusherehekea na kumtolea tambiko mungu wao aitwaye Dagoni. Basi, wakawa wanaimba, “Mungu wetu amemtia mikononi mwetu adui yetu Samsoni.” 24Watu walipomwona Samsoni wakamsifu mungu wao na kusema, “Mungu wetu amemtia mikononi mwetu adui yetu ambaye amekuwa akiharibu nchi yetu na kuwaua wengi wetu.” 25Walipojawa na furaha sana mioyoni mwao, wakasema, “Mleteni Samsoni atutumbuize.” Basi wakamtoa Samsoni gerezani, wakamleta naye akawatumbuiza. Wakamweka katikati ya nguzo. 26Samsoni akamwambia kijana aliyekuwa anamwongoza, “Niruhusu nizipapase nguzo zinazotegemeza jumba hili ili nami niziegemee.” 27Jumba hilo lilikuwa limejaa watu: Wakuu wote wa Wafilisti walikuwapo na kwenye paa kulikuwa na watu 3,000 wanaume na wanawake, wakimtazama Samsoni akiwatumbuiza.
28Hapo Samsoni akamwomba Mwenyezi-Mungu: “Bwana Mwenyezi-Mungu nakuomba unikumbuke. Nitie nguvu, mara hii moja tu, ee Mungu, ili niwalipize kisasi mara moja hii tu Wafilisti ambao waliyangoa macho yangu mawili.” 29Samsoni akazishika nguzo mbili za katikati ambazo zilitegemeza uzito wote wa jumba hilo, mkono mmoja nguzo hii na mkono mwingine nguzo ya pili. 30Kisha akasema, “Na nife pamoja na Wafilisti.” Akasukuma kwa nguvu zake zote. Jumba likawaangukia wakuu hao wote wa Wafilisti waliokuwamo humo ndani. Wale waliouawa wakati wa kifo chake walikuwa wengi kuliko wale aliowaua wakati wa uhai wake. 31Ndugu zake na jamaa yake yote wakaja kumchukua; wakamzika katikati ya mji wa Sora na mji wa Eshtaoli katika kaburi la Manoa, baba yake. Samsoni alikuwa mwamuzi wa Israeli kwa miaka ishirini.


Waamuzi 16;1-31

Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)

"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.


Friday 1 December 2017

Kikombe Cha Asubuhi ;Waamuzi 15...



Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?
Tumshukuru Mungu wetu katika yote..
Mtakatifu Baba wa Mbinguni,Mungu wetu, Muumba wetu
Muumba wa Mbingu na Nchi,Mungu mwenye nguvu,Mungu wa
Abrahamu,Isaka na Yakobo,Baba wa upendo,Baba wa Baraka
Mponyaji wetu,Kimbilio letu,Muweza wa yote,Jehovah Nissi,
Jehovah Jireh,Jehovah Raah,Jehovah Rapha,Jehovah Shammah,
Jehovah Shalom....!Emanuel-Mungu pamoja nasi..!

Asante kwa wema na fadhili zako kwetu Mungu wetu..
Asante kwa ulinzi wako wakati wote kwetu..
Asante kwa pumzi/uzima,afya na tukiwa tayari katika majukumu yetu..
Asante kwakutuchagua tena na kutupa kibali cha kuendelea kuiona Leo hii
Si kwa nguvu zetu wala si kwa utashi wetu,si kwamba sisi tumetenda mema sana,si kwa uwezo wetu wala si kwa akili zetu Jehovah ni kwa 
neema/rehema zako,ni kwa mapenzi yako Mungu wetu sisi kuwa hivi tulivyo leo hii..

Yahweh tunakuja mbele zako tukijinyenyekeza,tukijishusha na 
tukijiachilia mikononi mwako Mungu wetu..
Baba wa Mbinguni tunaomba utusamehe dhambi zetu zote tulizozifanya
kwakuwaza,kwakunena,kwakutenda,kwakujua/kutojua..
Mungu wetu nasi tunaomba utupe neema ya kuweza kuwasamehe
wale wote waliotukosea..
Baba wa mbinguni tunaomba utuepushe katika majaribu Yahweh tunaomba utuokoe na yule mwovu na kazi zake zote..
Jehovah tunaomba ututakase miili yetu na akili zetu kwa Damu ya 
Bwana wetu na Mwokozi wetu Yesu Kristo wa Nazareti..
Yeye aliteseka kwanza ili sisi tupate kupona..




Maana tunajua kwamba hema hii ambamo tunaishi sasa hapa duniani yaani mwili wetu, itakapongolewa, Mungu atatupa makao mengine mbinguni, nyumba ya milele isiyotengenezwa kwa mikono. Na sasa, katika hali hii, tunaugua tukitazamia kwa hamu kubwa kuvikwa makao yetu yaliyo mbinguni. Naam, tunapaswa kuvikwa namna hiyo ili tusije tukasimama mbele ya Mungu bila vazi. Tukiwa bado katika hema hii ya duniani, tunalia kwa kukandamizwa; si kwamba tunataka kuuvua mwili huu wa kufa, ila tuna hamu ya kuvalishwa ule usiokufa, ili kile chenye kufa kimezwe kabisa na uhai. Mungu mwenyewe alitutayarishia mabadiliko hayo, naye ametupa Roho wake awe dhamana ya yote aliyotuwekea. Tuko imara daima. Tunajua kwamba kuishi katika mwili huu tu ni kukaa mbali na Bwana. Maana tunaishi kwa imani, na si kwa kuona. Lakini tuko imara na tungependelea hata kuyahama makao haya, tukahamie kwa Bwana. Lakini jambo la maana zaidi, tunataka kumpendeza, iwe tunaishi hapa duniani au huko. Maana sote ni lazima tusimame mbele ya kiti cha hukumu cha Kristo, ili kila mmoja apokee anayostahili kwa matendo aliyoyafanya wakati alipokuwa anaishi duniani, mema au mabaya.


Baba wa Mbinguni tunaomba ukabariki kazi za mikono yetu
Yahweh tunaomba utupe ubunifu,maarifa katika ufanyaji/utendaji
Mungu wetu tukatende sawasawa na mapenzi yako..
Jehovah tunaomba ukabariki ridhiki zetu ziingiazo/zitokazo
Mungu wetu nasi tunaomba utupe neema ya kuweza kuwabariki
wenye kuhitaji..Yahweh tusipungukiwe katika mahitaji yetu
Mungu Baba ukatupe kama inavyokupendeza wewe..

Mfalme wa Amani tunayaweka maisha yetu mikononi mwako
Yahweh tunaomba ukabariki nyumba/ndoa zetu,watoto,wazazi wetu
familia/ndugu na wote wanaotuzunguka...
Yahweh tunaomba ulinzi wako kwetu na kwa vyote tunavyovimiliki
Mungu wetu ukatamalaki na kutuatamia Yahweh ukatupe neema
ya kufuata njia zako,kusimamia Neno lako amri na sheria zako
siku zote za maisha yetu,Mungu wetu ukaonekane popote
tupitapo na Ukatufanye chombo chema nasi tukatumike kama inavyokupendeza wewe..
Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi..




Basi, sisi tunajua umuhimu wa kumcha Bwana, na hivyo tunajitahidi kuwavuta watu. Mungu anatujua waziwazi, nami natumaini kwamba nanyi pia mnatujua kinaganaga. Si kwamba tunajaribu tena kujipendekeza kwenu, ila tunataka kuwapa nyinyi sababu zetu za kuona fahari juu yenu, ili mpate kuwajibu wale wanaojivunia hali yao ya nje zaidi kuliko jinsi walivyo moyoni. Ikiwa tumeonekana kuwa wendawazimu, hiyo ni kwa ajili ya Mungu; na ikiwa tunazo akili zetu timamu, hiyo ni kwa faida yenu. Maana mapendo ya Kristo yanatumiliki sisi ambao tunatambua ya kwamba mtu mmoja tu amekufa kwa ajili ya wote, na hiyo ina maana kwamba wote wanashiriki kifo chake. Alikufa kwa ajili ya watu wote, ili wanaoishi wasiishi kwa ajili yao wenyewe, bali kwa ajili yake yeye aliyekufa, akafufuliwa kwa ajili yao. Basi, tangu sasa, sisi hatumpimi mtu yeyote kibinadamu. Hata kama kwa wakati mmoja tulimpima Kristo kibinadamu, sasa si hivyo tena. Mtu yeyote akiungana na Kristo huwa kiumbe kipya, mambo ya kale yamepita, hali mpya imefika. Yote ni kazi ya Mungu mwenye kutupatanisha sisi naye kwa njia ya Kristo, na kutupa jukumu la kuwapatanisha watu naye. Ndiyo kusema: Mungu, amekuwa akiupatanisha ulimwengu naye kwa njia ya Kristo, bila kutia maanani dhambi zao binadamu. Yeye ametupa ujumbe kuhusu kuwapatanisha watu naye. Basi, sisi tunamwakilisha Kristo, naye Mungu mwenyewe anatutumia sisi kuwasihi nyinyi. Tunawaombeni kwa niaba ya Kristo, mpatanishwe na Mungu. Kristo hakuwa na dhambi, lakini Mungu alimfanya ahusike na dhambi kwa ajili yetu, ili sisi kwa kuungana naye, tupate kuushiriki uadilifu wake Mungu.

Yahweh tunaomba ukawaguse kwa mkono wako wenye nguvu wote
wanaopitia magumu/majaribu mbalimbali,Mungu wetu tunaomba
ukawaponye wagonjwa,Baba wa Mbinguni tunaomba ukawapatie
chakula wenye njaa,Jehovah ukaguse wenye shida/tabu,Yahweh
ukawafungue wale wote walio katika vifungo vya yule mwovu
Baba wa Mbinguni ukawape tumaini wale wote waliokata tamaa,
Mungu wetu ukawatue wote wenye kuelemewa na mizigo,Yahweh
tunaomba ukawasamehe wale wote waliokwenda kinyume nawe
Mungu wetu tunaomba ukawaponye kimwili na kiroho pia,Baba 
ukawape neema ya kujiombea,kufuata njia zako na Nuru yako
ikaangaze katika maisha yao..Jehovah ukawafariji wafiwa..
Ee Baba tunayaweka haya yote miononi mwako,Tukiamini na 
kukushukuru daima..
Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele..
Amina..!
Asanteni sana wapendwa katika Bwana kwa kuwa nami
Mungu mwenye neema/rehema aendelee kuwabariki
Amani  ya Kristo Yesu iwe nanyi wakati wote..
Nawapenda..



1Baada ya muda fulani, wakati wa mavuno ya ngano, Samsoni alichukua mwanambuzi, akaenda kumtembelea mkewe. Akamwambia baba mkwe wake kwamba anataka kumwona mke wake chumbani mwake. Lakini baba mkwe hakumruhusu, 2akamwambia, “Mimi nilidhani ulimchukia kabisa. Kwa hiyo nilimwoza rafiki yako. Hata hivyo, dada yake mdogo ni mzuri kuliko yeye. Tafadhali, umwoe huyo badala yake.” 3Samsoni akamwambia, “Safari hii sitakuwa na lawama kwa yale nitakayowatendea Wafilisti.” 4Basi, Samsoni akaenda, akawakamata mbweha 300 na akawafunga mikia yao pamoja wawiliwawili. Kisha akaweka mwenge katika kila jozi ya mbweha. 5Halafu akaiwasha hiyo mienge na kuwaachilia hao mbweha ambao waliingia kwenye mashamba ya Wafilisti na kuteketeza miganda ya ngano na pia ngano iliyokuwa bado haijavunwa hata na mashamba ya mizeituni. 6Wafilisti walipotaka kujua aliyefanya hayo, waliambiwa, “Ni huyo Samsoni, mkwewe Mtimna, amefanya hivyo kwa sababu huyo baba mkwe wake amemchukua mke wake na kumwoza kwa kijana mmoja aliyekuwa mdhamini wake mwenyewe Samsoni katika harusi.” Basi Wafilisti wakaenda kumchoma moto yule mwanamke pamoja na baba yake.
7Samsoni akawaambia hao Wafilisti, “Kama hayo ndiyo mliyoyafanya, naapa kwamba sitaondoka mpaka nimelipiza kisasi.” 8Basi, akawashambulia vikali na kuwaua wengi. Kisha akaenda kuishi katika pango la mwamba wa Etamu.

Samsoni awashinda Wafilisti

9Wafilisti wakaja, wakapiga kambi yao nchini Yuda na kuushambulia mji wa Lehi. 10Watu wa Yuda wakawauliza, “Kwa nini mmekuja kutushambulia?” Nao wakawajibu, “Tumekuja ili tumfunge Samsoni na kumtendea kama alivyotutendea.”
11Basi, watu 3,000 wa Yuda wakamwendea Samsoni pangoni mwa mwamba wa Etamu wakamwambia, “Je, hujui kwamba Wafilisti wanatawala juu yetu? Tazama basi, mkosi uliotutendea!” Samsoni akawajibu, “Kama walivyonitendea ndivyo nilivyowatendea.” 12Wakamwambia, “Tumekuja kukufunga ili tukutie mikononi mwao.” Samsoni akawaambia, “Niapieni kwamba nyinyi wenyewe hamtaniua.” 13Nao wakamwambia, “Sisi hatutakuua ila tutakufunga tu na kukutia mikononi mwao.” Basi, wakamfunga kwa kamba mbili mpya na kumtoa humo pangoni.
14Alipofika Lehi, Wafilisti walimwendea mbio huku wakipiga kelele. Ghafla roho ya Mwenyezi-Mungu ikamjia Samsoni kwa nguvu na zile kamba walizomfunga mikononi mwake zikakatika kama kitani kilichoshika moto, navyo vifungo vikaanguka chini. 15Samsoni akapata utaya mbichi wa punda, akautumia kuwaua watu 1,000. 16Kisha Samsoni akasema,
“Kwa utaya wa punda,
nimeua watu elfu moja.
Kwa utaya wa punda,
nimekusanya marundo ya maiti.”
17Alipomaliza kusema, akatupa utaya huo. Mahali hapo pakaitwa Ramath-lehi, yaani mlima wa utaya.
18Kisha Samsoni akashikwa na kiu sana. Basi, akamwomba Mwenyezi-Mungu, akisema, “Ee Mungu, wewe ndiwe uliyeleta ukombozi huu, kwa kunitumia mimi mtumishi wako. Je, sasa utaniacha nife kwa kiu na kutekwa na Wafilisti hawa wasiotahiriwa?” 19Mungu akafungua mahali palipokuwa na shimo huko Leki, akatiririsha maji. Samsoni akanywa maji hayo na nguvu zake zikamrudia. Chemchemi hiyo ikaitwa En-hakore; nayo iko huko Lehi mpaka leo.
20Samsoni alikuwa mwamuzi wa Waisraeli kwa miaka ishirini, nyakati za Wafilisti.


Waamuzi 15;1-20

Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)

"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.

Thursday 30 November 2017

Kikombe Cha Asubuhi ;Waamuzi 14...




Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?
Tumshukuru Mungu wetu katika yote...
Asante Mungu wetu kwa wema na fadhili zako kwetu..
Asante kwa ulinzi wako kwetu wakati wote..
Asante kwa pumzi/uzima,afya na kuwa tayari kwa majukumu yetu..
Asante kwakutuchagua tena na kutupa kibali cha kuiona leo hii..
Si kwa akili zetu,wala si kwa nguvu/utashi wetu,si kwamba 
tumetenda mema sana zaidi ya wengine walikuotangulia/kufa,
wengine wapo hoi vitandani wanatamani hata kutubu na kuita
jina la Mungu lakini hawana kauli,wengine hawajitambui...

Ni kwa Neema/rehema zako,Ni kwa mapenzi yako Baba wa Mbinguni sisi kuwa hivi tulivyo  leo hii..
Wapendwa tuitumie vyema nafasi hii,tumtangulize Mungu katika
yote,yeye ndiye Mungu wa uponyaji,Mungu wetu anaweza..
Mungu wetu ana nguvu,Mungu wetu anaponya,Mungu wetu anabariki,
Mungu wetu anatenda,anasikia,anajibu,anaokoa,kwakwe yeye hakuna
lisilowezakana,yeye ni mwanzo na yeye ni mwisho,Alfa na Omega..!!


Mimi Paulo, mfungwa kwa ajili ya Kristo Yesu, na ndugu Timotheo, ninakuandikia wewe Filemoni mpendwa, mfanyakazi mwenzetu, na kanisa linalokutana nyumbani kwako, na wewe dada Afia, na askari mwenzetu Arkipo. Tunawatakieni neema na amani kutoka kwa Mungu Baba yetu, na kwa Bwana Yesu Kristo. Kila wakati ninaposali, nakukumbuka wewe Filemoni, na kumshukuru Mungu, maana nasikia habari za imani yako kwa Bwana Yesu na upendo wako kwa watu wote wa Mungu. Naomba ili imani hiyo unayoshiriki pamoja nasi ikuwezeshe kuwa na ujuzi mkamilifu zaidi wa baraka zote tunazopata katika kuungana kwetu na Kristo. Ndugu, upendo wako umeniletea furaha kubwa na kunipa moyo sana! Nawe umeichangamsha mioyo ya watu wa Mungu.


Baba wa Mbinguni tunakuja mbele zako tukijinyenyekeza,tukijishusha
na kujiachilia mikononi mwako..
 Jehovah tunaomba utesamehe makosa yetu yote tuliyoyafanya
kwakuwaza,kwakunena,kwakutenda,kwakujua/kutojua..
Yahweh nasi tunaomba utupe neema ya kuweza kuwasamehe wale wote
waliotukosea,Mungu wetu tunaomba utuepushe katika majaribu
Yahweh tunaomba utuokoe na yule mwovu na kazi zake zote..
Baba wa Mbinguni tunaomba ututakase miili yetu na akili zetu..
Mungu wetu tunaomba utufunike kwa Damu ya Bwana na Mwokozi
wetu Yesu Kristo wa Nazareti,yeye aliteseka kwanza ili sisi tupate
kupona...

Baba wa Mbinguni tunaomba ukabariki kazi za mikono yetu
Yahweh ukatupe ubunifu,maarifa katika ufanyaji/utendaji
Mungu wetu tukatende sawasawa na mapenzi yako
Yahweh tunaomba ukabariki ridhiki zetu ziingiazo/zitokazo
Mungu wetu nasi tunaomba utupe neema ya kuweza kuwabariki
wenye kuhuitaji...
Yahweh tusipungikiwe katika mahitaji yetu Mungu wetu ukatupe kama inavyokupendeza wewe..

Mfalme wa Amani tunayaweka maisha yetu mikononi mwako

Baba wa Mbinguni tunaomba baraka zako katika nyumba/ndoa
zetu,watoto,wazazi wetu,familia/ndugu na wote wanaotuzunguka
Yahweh tunaomba ulinzi wako kwetu na kwa vyote tunavyovimiliki
Mungu wetu tunaomba ukatamalaki na kutuatamia,Baba wa Mbinguni
ukatupe neema ya kufuata njia zako,tukasimamie Neno lako Amri na sheria zako siku zote za maisha yetu..
Yahweh ukatupe neema ya subira,amani,fadhili,utuwema,busara,Hekima,upendo
ukatawale kati yetu,tuchukuliane na kusameheana..
Tuonyane/tuelimishane kwa upendo..

Mungu wetu ukaonekane popote tupitapo,tukanene yaliyo yako,tukapate kutambua/kujitambua..

Ukatufanye chombo chema Yahweh nasi tukatumike kama inavyokupendeza wewe..
Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi..



Kwa sababu hiyo, ningeweza, kwa uhodari kabisa, nikiwa ndugu yako katika kuungana na Kristo, kukuamuru ufanye unachopaswa kufanya. Lakini kwa sababu ya upendo, ni afadhali zaidi nikuombe. Nafanya hivi ingawa mimi ni Paulo, balozi wa Kristo Yesu, na sasa pia mfungwa kwa ajili yake. Basi, ninalo ombi moja kwako kuhusu mwanangu Onesimo, ambaye ni mwanangu katika Kristo kwani nimekuwa baba yake nikiwa kifungoni. Ni Onesimo yuleyule ambaye wakati mmoja alikuwa hakufai kitu, lakini sasa ananifaa mimi na wewe pia. Sasa namrudisha kwako, naye ni kama moyo wangu mimi mwenyewe. Ningependa akae nami hapa anisaidie badala yako wakati niwapo kifungoni kwa sababu ya Injili. Lakini sitafanya chochote bila kibali chako. Sipendi kukulazimisha unisaidie, kwani wema wako unapaswa kutokana na hiari yako wewe mwenyewe na si kwa kulazimika. Labda Onesimo aliondoka kwako kwa kitambo tu, kusudi uweze tena kuwa naye daima. Na sasa yeye si mtumwa wa kawaida, ila ni bora zaidi ya mtumwa: Yeye ni ndugu yetu mpenzi. Ni wa maana sana kwangu mimi, na kwako atakuwa wa maana zaidi, kama mtumwa na kama ndugu katika Bwana. Basi, ikiwa wanitambua mimi kuwa mwenzako, mpokee tena kama vile ungenipokea mimi mwenyewe. Kama alikuwa amekukosea kitu, au alikuwa na deni lako, basi, unidai mimi. Naandika jambo hili kwa mkono wangu mwenyewe: Mimi Paulo nitalipa! (Tena sina haja ya kusema kwamba wewe unalo deni kwangu la nafsi yako). Naam, ndugu yangu, nifanyie jambo hilo kwa ajili ya jina la Bwana; burudisha moyo wangu kama ndugu katika Kristo. Naandika nikitumaini kwamba utanikubalia ombi langu; tena najua kwamba utafanya hata zaidi ya haya ninayokuomba. Pamoja na hayo, nitayarishie chumba kwani natumaini kwamba kwa sala zenu, Mungu atanijalia niwatembeleeni.

Mungu wetu tunawaweka ndugu zetu wanaopitia magumu/majaribu
mbali mbali Baba tunaomba ukawaguse kwa mkono wako wenye nguvu
Mungu wetu tunaomba uponyaji wako kwa wagonjwa,Yahweh tunaomba
ukawapatie chakula na ukabariki mashamba yao wote wenye njaa..
Jehovah tunaomba ukawaguse wenye shida/tabu,waliokata tamaa,
walio na hofu,mashaka Baba ukawe tumaini lao..
Mungu wetu ukawafungue wote waliokatika vifungo vya yule mwovu..
Baba tunaomba ukawasamehe wale wote waliokwenda kinyume nawe
Mungu wetu tunaomba ukawape neema ya kujiombea na kufuata njia zako
Baba tunaomba ukasikie kilio cha watoto wako wanaokuomba kwa 
bidii na imani,Wafiwa ukawe mfariji wao..
Ee Mungu wetu tunaomba upokee sala/maombi yetu..
Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hat Milele..
Amina..!



Epafra, mfungwa mwenzangu kwa ajili ya Kristo Yesu, anakusalimu. Nao akina Marko, Aristarko, Dema na Luka, wafanyakazi wenzangu, wanakusalimu. Nawatakieni nyinyi nyote neema ya Bwana Yesu Kristo.


Asanteni sana wapendwa katika Kristo Yesu kwa kuwa nami
Mungu mwenyezi akawaguse kwa mkono wake wenye nguvu
akawabariki na kuwatendea kama inavyompendeza yeye..
Nawapenda.

Matendo ya kwanza ya ushujaa ya Samsoni


1Siku moja, Samsoni aliteremka na kwenda Timna ambako alimwona msichana mmoja Mfilisti. 2Aliporudi nyumbani akawaambia wazazi wake, “Nimemwona msichana mmoja Mfilisti huko Timna. Niozeni msichana huyo.” 3Lakini wazazi wake wakamwambia, “Je, hakuna msichana yeyote miongoni mwa ndugu zako au kati ya watu wetu hata uende kuoa kwa Wafilisti wasiotahiriwa?” Lakini Samsoni akamwambia baba yake, “Niozeni msichana huyo, maana ananipendeza sana.”
4Wazazi wake hawakujua kwamba huo ulikuwa mpango wa Mwenyezi-Mungu ambaye alikuwa anatafuta kisa cha kuchukua hatua dhidi ya Wafilisti. Wakati huo, Wafilisti waliwatawala Waisraeli.
5Samsoni na wazazi wake waliondoka kwenda Timna. Walipofika huko kwenye mashamba ya mizabibu, mwanasimba mmoja akatokea akamngurumia Samsoni. 6Basi, roho ya Mwenyezi-Mungu ikamwingia Samsoni kwa nguvu, akamrarua simba huyo kama mtu araruavyo mwanambuzi. Naye Samsoni hakuwaambia wazazi wake kisa hicho. 7Kisha akateremka akaenda kuzungumza na yule msichana; huyo msichana alimpendeza sana Samsoni. 8Baada ya siku chache alirudi huko Timna kumchukua huyo msichana. Alipokuwa njiani akageuka pembeni kuuona mzoga wa yule simba, na kumbe kulikuwa na nyuki ndani ya mzoga na asali. 9Basi, akapakua asali kwa mikono yake akawa anakula huku akiendelea na safari yake. Aliporudi kwa wazazi wake, akawapa asali kidogo nao wakala. Lakini hakuwaambia kwamba alitoa asali hiyo ndani ya mzoga wa simba.
10Baba yake akaenda nyumbani kwa yule msichana, naye Samsoni akafanya karamu huko, kama walivyofanya vijana wakati huo. 11Wafilisti walipomwona Samsoni wakamletea vijana thelathini wakae naye. 12Samsoni akawaambia, “Nitatega kitendawili. Kama mkiweza kutegua kitendawili hicho kwa muda wa siku saba za sherehe za harusi, basi, nitawapa mavazi thelathini ya kitani na mavazi thelathini ya sikukuu. 13Lakini msipoweza kukitegua, nyinyi mtanipa mavazi thelathini ya kitani na mavazi thelathini ya sikukuu.” 14Nao wakamwambia, “Haya tega tusikie.” Samsoni akawaambia,
“Kwa mla kukatoka mlo
kwa mwenye nguvu, utamu.”
Baada ya siku tatu hao vijana walikuwa bado hawajaweza kutegua hicho kitendawili.
15Basi siku ya saba14:15 siku ya saba: Hati nyingine za kale: Siku ya nne. wakamwambia mke wa Samsoni, “Mbembeleze mumeo ili atuambie maana ya kitendawili hicho, la sivyo tutakuteketeza kwa moto wewe pamoja na nyumba ya baba yako. Je, mlitualika hapa kuja kutunyanganya mali zetu?” 16Mke wa Samsoni akamwendea Samsoni, huku machozi yanamtiririka, akamwambia, “Kwa kweli unanichukia; hunipendi hata kidogo. Umewategea kitendawili watu wangu na hukuniambia maana yake.”
Samsoni akamjibu, “Mimi sijawaeleza hata wazazi wangu. Sasa nitawezaje kukuambia wewe?” 17Lakini aliendelea kulia katika muda wao wote wa siku saba za sherehe za harusi. Siku ya saba Samsoni akamwambia mkewe kile kitendawili kwani alimbana sana. Mkewe akaenda haraka akawaambia watu wake. 18Siku hiyo ya saba, kabla ya jua kutua, wakamwambia Samsoni,
“Ni kitu gani kitamu kuliko asali?
Ni nani mwenye nguvu kuliko simba?”
Samsoni akawajibu, “Kama hamngejishughulisha na mtamba wangu hamngeweza kukitegua kitendawili changu.”
19Hapo roho ya Mwenyezi-Mungu ikamjia Samsoni kwa nguvu, naye akaenda mjini Ashkeloni, akawaua watu thelathini, kisha akachukua mavazi yao ya sikukuu, akawapa wale waliotegua kitendawili chake. Halafu akaondoka, akaenda nyumbani kwa wazazi wake akiwa na hasira kali. 20Basi, wakamwoza mwanamke wake kwa kijana mmoja ambaye alikuwa mdhamini wa Samsoni katika harusi.

Waamuzi 14;1-20

Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)

"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.


Wednesday 29 November 2017

Kikombe Cha Asubuhi ;Waamuzi 13...



Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?
Tumshukuru Mungu wetu katika yote..
Mtakatifu..!Mtakatifu..!Mtakatifu..!Baba wa Mbinguni..
Mungu wetu,Muumba wetu,Mungu wa Abrahamu,Isaka na Yakobo.
Wewe si Mungu wa wafu bali ni Mungu wa walio hai,Mungu wa majeshi
Mungu mwokozi,si Mungu wa fujo ni Mungu wa amani..
Unatosha Baba wa Mbinguni,Matendo yako ni makuu mno,Matendo yako
ni ya ajabu,hakuna kama wewe,wewe ni mwanzo na wewe ni mwisho..!



Ee Mungu, sisi tumesikia kwa masikio yetu, wazee wetu wametusimulia mambo uliyotenda nyakati zao, naam, mambo uliyotenda hapo kale: Kwa mkono wako mwenyewe uliyafukuza mataifa mengine, na mahali pao ukawakalisha watu wako; uliyaadhibu mataifa mengine, na kuwafanikisha watu wako. Watu wako hawakuitwaa nchi kwa silaha zao, wala hawakupata ushindi kwa nguvu zao; ila uliwasalimisha kwa mkono wako mwenyewe, kwa kuwaangazia uso wako, kwani wewe uliwapenda. Wewe ni mfalme wangu na Mungu wangu! Wawajalia ushindi wazawa wa Yakobo. Kwa nguvu yako twawashinda maadui zetu, kwa jina lako twawakanyaga wanaotushambulia. Mimi siutegemei upinde wangu, wala upanga wangu hauwezi kuniokoa. Wewe ndiwe uliyetuokoa na maadui zetu; uliwavuruga wale waliotuchukia. Daima tutaona fahari juu yako, ee Mungu; tutakutolea shukrani milele.

Asante Mungu wetu kwa wema na fadhili zako kwetu..
Asante kwakutuchagua tena na kutupa kibali cha kuendelea
kuiona leo hii..
Asante kwa ulinzi wako kwetu..
Asante kwa pumzi/uzima,afya na kuwa tayari kwa majukumu yetu..



Ole wenye majivuno na walevi wa Efraimu, fahari yake inatoweka kama ua linalonyauka! Naam, fahari iliyotawala bondeni kwenye rutubarutuba; na vichwani kwao walio watu walevi kupindukia! Bwana amejichagulia mtu wake shujaa na mwenye nguvu, ambaye ni kama mvua ya mawe na dhoruba kali, kama tufani ya mafuriko makubwa; kwa mkono wake atawatupa chini ardhini. Majivuno na fahari ya walevi wa Efraimu yatakanyagwakanyagwa ardhini, fahari yake inatoweka kama ua linalonyauka; fahari iliyotawala bondeni kwenye rutuba itakuwa kama tini za mwanzo kabla ya kiangazi; mtu akiziona huzichuma na kuzila mara moja. Siku ile Mwenyezi-Mungu wa majeshi atakuwa taji tukufu, kama kilemba kizuri kwa watu wake watakaobaki hai. Waamuzi mahakamani atawaongoza kutenda haki, nao walinzi wa mji atawapa nguvu.
Yahweh tunakuja mbele zako tukijinyenyekeza,tukijishusha na 
kujiachilia mikononi mwako Baba wa Mbinguni..
Jehovah tunaomba utusamehe makosa yetu yote tuliyoyafanya
kwakuwaza,kwakunena,kwakutenda,kwakujua/kutojua..
Mungu wetu nasi tunaomba utupe neema ya kuweza kuwasamehe
wale wote waliotukosea..
Yahweh tunaomba utuepushe katika majaribu Mungu wetu utuokoe na
yule mwovu na kazi zake zote..
Baba wa Mbinguni tunaomba ututakase miili yetu na akili zetu
Yahweh tunaomba utufunike kwa Damu ya Bwana na Mwokozi
wetu Yesu Kristo wa Nazareti,yeye aliteseka kwanza ili sisi tupate kupona..




Lakini wako wengine waliolewa divai na kuyumbayumba kwa sababu ya pombe; naam, makuhani na manabii wamelewa mvinyo, wamevurugika kwa divai. Wanayumbayumba kwa pombe kali; maono yao yamepotoka, wanapepesuka katika kutoa hukumu. Meza zote zimetapakaa matapishi, hakuna mahali popote palipo safi. Wao wananidhihaki na kuuliza: “Huyu nabii ataka kumfundisha nani? Je, anadhani atatueleza sisi ujumbe wake? Je, sisi ni watoto wachanga walioachishwa kunyonya juzijuzi? Anatufundisha kama watoto wadogo: Sheria baada ya sheria, mstari baada ya mstari; mara hiki, mara kile!” Haya basi! Mwenyezi-Mungu ataongea na watu hawa kwa njia ya watu wa lugha tofauti wanaoongea lugha ngeni. Hata hivyo yeye alikuwa amewaahidi: “Nitawaonesheni pumziko, nitawapeni pumziko enyi mliochoka. Hapa ni mahali pa pumziko.” Lakini wao hawakutaka kunisikiliza. Kwa hiyo kwao neno la Mwenyezi-Mungu litakuwa tu: Sheria sheria, mstari mstari; mara hiki, mara kile! Nao watalazimika kukimbia lakini wataanguka nyuma; watavunjika, watanaswa na kutekwa.

Mungu wetu tunaomba ukabariki kazi za mikono yetu..
Yahweh tunaomba ukatupe ubunifu,maarifa katika ufanyaji/utendaji
Jehovah nasi tukatende sawasawa na mapenzi yako..
Mungu wetu tunaomba ukabariki ridhiki zetu ziingiazo/zitokazo
Jehovah nasi tunaomba utupe neema ya kuweza kuwabariki wenye kuhitaji..
Baba wa Mbinguni tusipungukiwe katika mahitaji yetu Baba ukatupe
sawasawa na mapenzi yako...


Basi, sikilizeni neno la Mwenyezi-Mungu, enyi wenye madharau mnaotawala watu wa Yerusalemu, “Nyinyi mnajidai mmefanya mkataba na kifo, mmefanya mapatano na Kuzimu! Nyinyi mwasema eti balaa lijapo halitawapata, kwa sababu mmefanya uongo kuwa tegemeo lenu, na udanganyifu kuwa kinga yenu!” Basi, hivi ndivyo asemavyo Mwenyezi-Mungu: “Tazama! Naweka mjini Siyoni jiwe la msingi, jiwe ambalo limethibitika. Jiwe la pembeni, la thamani, jiwe ambalo ni la msingi thabiti; jiwe lililo na maandishi haya: ‘Anayeamini hatatishika.’ Nitatumia haki kama kipimo changu, nitatumia uadilifu kupimia.” Mvua ya mawe itaufagilia mbali uongo mnaoutegemea, na mafuriko yataharibu kinga yenu. Hapo mkataba wenu na kifo utabatilishwa, na mapatano yenu na Kuzimu yatafutwa. Janga lile kuu litakapokuja litawaangusheni chini. Kila litakapopitia kwenu litawakumba; nalo litapita kila asubuhi, mchana na usiku. Kusikia ujumbe huu tu kutakuwa kitisho. Kwenu itakuwa kama ajinyoshaye juu ya kitanda kifupi mno, au kujifunika kwa blanketi lililo dogo mno! Maana Mwenyezi-Mungu atainuka kama kule mlimani Perazimu; atawaka hasira kama kule bondeni Gibeoni. Atatekeleza mpango wake wa ajabu; atatenda kazi yake ya kustaajabisha. Basi, nyinyi msiwe na madharau vifungo vyenu visije vikakazwa zaidi. Maana nimesikia kuwa Mwenyezi-Mungu wa majeshi ameazimia kuiangamiza nchi yote.

Mfalme wa Amani tunayaweka maisha yetu mikononi mwako

Yahweh tunaomba ukabariki nyumba/ndoa zetu,watoto,wazazi wetu,
familia/ndugu na wote wanaotuzunguka..
Mungu wetu tunaomba ulinzi wako kwetu na kwa vyote tunavyovimiliki
Yahweh ukatamalaki na kutuatamia,Mungu wetu ukatuepushe na roho za 
dharau,masengenyo,kuumizana,kukwazana,kiburi na vyote vinavyokwenda kinyume nawe..
Jehovah ukatupe neema ya kufuata njia zako,tukasimamie
Neno lako amri na sheria zako siku zote za maisha yetu..
Baba wa Mbinguni ukatufanye chombo chema nasi tukatumike kama inavyokupendeza wewe..
Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi..


Tegeni sikio msikilize ninayowaambieni; sikilizeni kwa makini hotuba yangu. Je, alimaye ili kupanda hulima tu? Je, huendelea kulima na kusawazisha shamba lake? La! Akisha lisawazisha shamba lake, hupanda mbegu za bizari na jira, akapanda ngano na shayiri katika safu, na mipakani mwa shamba mimea mingineyo. Mtu huyo huwa anajua la kufanya, kwa sababu Mungu wake humfundisha. Bizari haipurwi kwa mtarimbo wala jira kwa gari la ng'ombe! Ila bizari hupurwa kwa kijiti na jira kwa fimbo. Mkulima apurapo ngano yake, haendelei kuipura mpaka kuvunja punje zake. Anajua jinsi ya kuipura kwa gurudumu, bila kuziharibu punje za ngano. Ujuzi huu nao watoka kwa Mwenyezi-Mungu wa majeshi. Mipango yake Mungu ni ya ajabu, hekima yake ni kamilifu kabisa.

Tazama wenye shida/tabu,wagonjwa,wenye njaa,wanaopitia
magumu/majaribu mbalimbali,waliokatika vifungo vya yule mwovu
waliokata tamaa,waliokataliwa,wenye hofu na mashaka na wote
walioanguka/potea Mungu wetu tunaomba ukawaguse na mkono wako
wenye nguvu,Yahweh tunaomba ukawaponye kiroho na kimwili pia
Mungu wetu ukawavushe salama,Baba ukawaokoe na kuwasimamisha tena,Yahweh ukawasamehe pale walipokwenda kinyume nawe
Mungu wetu ukawafunike kwa Damu ya Mwokozi wetu Yesu Kristo
Baba ukawape neema ya kujiombea,kufuata njia zako na Nuru ikaangaze
katika maisha yao..
Mungu wetu tunaomba upokee sala/maombi yetu..
Ee Baba tunayaweka haya yote mikononi mwako,kwa imani
tunashukuru na kukusifu daima..
Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele..
Amina..!

Asanteni sana wapendwa katika Kristo Yesu kwakuwa nami
Mungu aendelee kuwabariki na kuwatendea kama inavyompendeza yeye
Nawapenda.


Kuzaliwa kwa Samsoni

1Waisraeli walitenda tena uovu mbele ya Mwenyezi-Mungu, naye akawaacha watawaliwe na Wafilisti kwa miaka arubaini.
2Kulikuwa na mtu mmoja huko Sora, wa kabila la Dani, jina lake Manoa. Mke wake alikuwa tasa. 3Siku moja, malaika wa Mwenyezi-Mungu akamtokea huyo mwanamke, akamwambia, “Wewe ni tasa, huna watoto. Lakini utapata mimba na kumzaa mtoto wa kiume. 4Kwa hiyo uwe mwangalifu, usinywe divai au kileo wala usile kitu chochote kilicho najisi, 5kwa maana utachukua mimba na kuzaa mtoto wa kiume. Nywele za mtoto huyo kamwe zisinyolewe, maana atakuwa amewekwa wakfu kwa Mungu tangu kuzaliwa kwake.13:5 Masharti na majukumu yanayotajwa hapa (taz 4-5) kwa kawaida yahusu mtu aliyewekwa wakfu kwa Mungu kwa nadhiri fulani (taz Hes 6:1-8). Naye ataanza kuwakomboa Waisraeli mikononi mwa Wafilisti.” 6Mwanamke huyo akaenda kumwambia mume wake, “Mtu wa Mungu ambaye sura yake ilikuwa kama ya malaika wa Mungu alinijia. Sikumwuliza alikotoka wala hakuniambia jina lake. 7Lakini aliniambia kwamba nitachukua mimba na kuzaa mtoto wa kiume. Aliniamuru nisinywe divai au kileo wala kula chochote kilicho najisi, maana mtoto huyo atakuwa amewekwa wakfu kwa Mungu tangu kuzaliwa kwake mpaka atakapokufa.”
8Kisha Manoa akamwomba Mwenyezi-Mungu, akisema, “Nakuomba ee Mwenyezi-Mungu, umtume tena yule mtu wako uliyemtuma ili atufundishe mambo tunayopaswa kumtendea huyo mtoto atakayezaliwa.” 9Mwenyezi-Mungu akalisikia ombi la Manoa, na yule malaika wa Mungu akamwendea tena yule mwanamke alipokuwa ameketi shambani. Lakini mumewe, Manoa, hakuwa pamoja naye. 10Mwanamke akakimbia upesi, akamwambia mumewe, “Tazama! Yule mtu aliyenijia siku ile amenitokea tena.” 11Manoa akafuatana naye mpaka kwa mtu huyo, akamwuliza, “Je, wewe ni yule mtu aliyezungumza na mwanamke huyu?” Yule mtu akamjibu, “Ni mimi.” 12Kisha Manoa akasema, “Sasa maneno yako yatakapotimia ni mambo gani tutakayofuata kwa ajili ya huyo mtoto? Tutafanya nini kwa ajili yake?” 13Malaika wa Mwenyezi-Mungu akamwambia Manoa, “Mkeo atapaswa kushika yote niliyomwambia: 14Asionje mazao yoyote ya mzabibu, wala asinywe divai au kileo wala kula chochote kilicho najisi. Yote niliyomwamuru, ayafuate.”
15Manoa akamwambia huyo malaika wa Mwenyezi-Mungu, “Tafadhali, ukae kidogo tukutayarishie mwanambuzi.” 16Yule malaika wa Mwenyezi-Mungu akamwambia Manoa, “Hata kama mkinilazimisha kukaa sitakula chakula chenu. Lakini kama ukipenda, tayarisha sadaka ya kuteketezwa, mtolee Mwenyezi-Mungu.” Manoa hakujua kuwa huyo alikuwa malaika wa Mwenyezi-Mungu. 17Basi, Manoa akamwambia huyo malaika wa Mwenyezi-Mungu, “Tuambie jina lako ili tukuheshimu wakati maneno yako yatakapotimia.” 18Malaika wa Mwenyezi-Mungu akamjibu, “Kwa nini unataka kujua jina langu, kwa kuwa jina langu ni la ajabu?” 19Hapo Manoa akatayarisha mwanambuzi na tambiko, akaviweka juu ya mwamba amtolee Mwenyezi-Mungu afanyaye maajabu. 20Basi, wakati Manoa na mkewe walipokuwa wanatazama miali ya moto ikipanda juu mbinguni kutoka madhabahuni, walimwona malaika katika miali hiyo akipanda kwenda mbinguni. Basi Manoa na mkewe wakasujudu. 21Manoa akajua kuwa huyo alikuwa malaika wa Mwenyezi-Mungu. Malaika hakumtokea tena Manoa na mkewe.
22Basi, Manoa akamwambia mkewe, “Hakika tutakufa, maana tumemwona Mungu.” 23Lakini mkewe akamjibu, “Kama Mwenyezi-Mungu angetaka kutuua hangepokea sadaka yetu ya kuteketezwa na ya nafaka; wala hangetuonesha mambo hayo wala kutuambia maagizo.”
24Kisha mkewe Manoa akajifungua mtoto wa kiume, naye Manoa akampa jina Samsoni. Mtoto huyo akakua naye Mwenyezi-Mungu akambariki. 25Roho ya Mwenyezi-Mungu ikaanza kumsukuma akiwa huko Mahane-dani, kati ya Sora na Eshtaoli.



Waamuzi 13;1-25

Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)

"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.