Swahili na Waswahili

Swahili na Waswahili
Waswahili na Mswahili Rachel Siwa...Pamoja Daima!!

Friday 1 December 2017

Kikombe Cha Asubuhi ;Waamuzi 15...



Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?
Tumshukuru Mungu wetu katika yote..
Mtakatifu Baba wa Mbinguni,Mungu wetu, Muumba wetu
Muumba wa Mbingu na Nchi,Mungu mwenye nguvu,Mungu wa
Abrahamu,Isaka na Yakobo,Baba wa upendo,Baba wa Baraka
Mponyaji wetu,Kimbilio letu,Muweza wa yote,Jehovah Nissi,
Jehovah Jireh,Jehovah Raah,Jehovah Rapha,Jehovah Shammah,
Jehovah Shalom....!Emanuel-Mungu pamoja nasi..!

Asante kwa wema na fadhili zako kwetu Mungu wetu..
Asante kwa ulinzi wako wakati wote kwetu..
Asante kwa pumzi/uzima,afya na tukiwa tayari katika majukumu yetu..
Asante kwakutuchagua tena na kutupa kibali cha kuendelea kuiona Leo hii
Si kwa nguvu zetu wala si kwa utashi wetu,si kwamba sisi tumetenda mema sana,si kwa uwezo wetu wala si kwa akili zetu Jehovah ni kwa 
neema/rehema zako,ni kwa mapenzi yako Mungu wetu sisi kuwa hivi tulivyo leo hii..

Yahweh tunakuja mbele zako tukijinyenyekeza,tukijishusha na 
tukijiachilia mikononi mwako Mungu wetu..
Baba wa Mbinguni tunaomba utusamehe dhambi zetu zote tulizozifanya
kwakuwaza,kwakunena,kwakutenda,kwakujua/kutojua..
Mungu wetu nasi tunaomba utupe neema ya kuweza kuwasamehe
wale wote waliotukosea..
Baba wa mbinguni tunaomba utuepushe katika majaribu Yahweh tunaomba utuokoe na yule mwovu na kazi zake zote..
Jehovah tunaomba ututakase miili yetu na akili zetu kwa Damu ya 
Bwana wetu na Mwokozi wetu Yesu Kristo wa Nazareti..
Yeye aliteseka kwanza ili sisi tupate kupona..




Maana tunajua kwamba hema hii ambamo tunaishi sasa hapa duniani yaani mwili wetu, itakapongolewa, Mungu atatupa makao mengine mbinguni, nyumba ya milele isiyotengenezwa kwa mikono. Na sasa, katika hali hii, tunaugua tukitazamia kwa hamu kubwa kuvikwa makao yetu yaliyo mbinguni. Naam, tunapaswa kuvikwa namna hiyo ili tusije tukasimama mbele ya Mungu bila vazi. Tukiwa bado katika hema hii ya duniani, tunalia kwa kukandamizwa; si kwamba tunataka kuuvua mwili huu wa kufa, ila tuna hamu ya kuvalishwa ule usiokufa, ili kile chenye kufa kimezwe kabisa na uhai. Mungu mwenyewe alitutayarishia mabadiliko hayo, naye ametupa Roho wake awe dhamana ya yote aliyotuwekea. Tuko imara daima. Tunajua kwamba kuishi katika mwili huu tu ni kukaa mbali na Bwana. Maana tunaishi kwa imani, na si kwa kuona. Lakini tuko imara na tungependelea hata kuyahama makao haya, tukahamie kwa Bwana. Lakini jambo la maana zaidi, tunataka kumpendeza, iwe tunaishi hapa duniani au huko. Maana sote ni lazima tusimame mbele ya kiti cha hukumu cha Kristo, ili kila mmoja apokee anayostahili kwa matendo aliyoyafanya wakati alipokuwa anaishi duniani, mema au mabaya.


Baba wa Mbinguni tunaomba ukabariki kazi za mikono yetu
Yahweh tunaomba utupe ubunifu,maarifa katika ufanyaji/utendaji
Mungu wetu tukatende sawasawa na mapenzi yako..
Jehovah tunaomba ukabariki ridhiki zetu ziingiazo/zitokazo
Mungu wetu nasi tunaomba utupe neema ya kuweza kuwabariki
wenye kuhitaji..Yahweh tusipungukiwe katika mahitaji yetu
Mungu Baba ukatupe kama inavyokupendeza wewe..

Mfalme wa Amani tunayaweka maisha yetu mikononi mwako
Yahweh tunaomba ukabariki nyumba/ndoa zetu,watoto,wazazi wetu
familia/ndugu na wote wanaotuzunguka...
Yahweh tunaomba ulinzi wako kwetu na kwa vyote tunavyovimiliki
Mungu wetu ukatamalaki na kutuatamia Yahweh ukatupe neema
ya kufuata njia zako,kusimamia Neno lako amri na sheria zako
siku zote za maisha yetu,Mungu wetu ukaonekane popote
tupitapo na Ukatufanye chombo chema nasi tukatumike kama inavyokupendeza wewe..
Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi..




Basi, sisi tunajua umuhimu wa kumcha Bwana, na hivyo tunajitahidi kuwavuta watu. Mungu anatujua waziwazi, nami natumaini kwamba nanyi pia mnatujua kinaganaga. Si kwamba tunajaribu tena kujipendekeza kwenu, ila tunataka kuwapa nyinyi sababu zetu za kuona fahari juu yenu, ili mpate kuwajibu wale wanaojivunia hali yao ya nje zaidi kuliko jinsi walivyo moyoni. Ikiwa tumeonekana kuwa wendawazimu, hiyo ni kwa ajili ya Mungu; na ikiwa tunazo akili zetu timamu, hiyo ni kwa faida yenu. Maana mapendo ya Kristo yanatumiliki sisi ambao tunatambua ya kwamba mtu mmoja tu amekufa kwa ajili ya wote, na hiyo ina maana kwamba wote wanashiriki kifo chake. Alikufa kwa ajili ya watu wote, ili wanaoishi wasiishi kwa ajili yao wenyewe, bali kwa ajili yake yeye aliyekufa, akafufuliwa kwa ajili yao. Basi, tangu sasa, sisi hatumpimi mtu yeyote kibinadamu. Hata kama kwa wakati mmoja tulimpima Kristo kibinadamu, sasa si hivyo tena. Mtu yeyote akiungana na Kristo huwa kiumbe kipya, mambo ya kale yamepita, hali mpya imefika. Yote ni kazi ya Mungu mwenye kutupatanisha sisi naye kwa njia ya Kristo, na kutupa jukumu la kuwapatanisha watu naye. Ndiyo kusema: Mungu, amekuwa akiupatanisha ulimwengu naye kwa njia ya Kristo, bila kutia maanani dhambi zao binadamu. Yeye ametupa ujumbe kuhusu kuwapatanisha watu naye. Basi, sisi tunamwakilisha Kristo, naye Mungu mwenyewe anatutumia sisi kuwasihi nyinyi. Tunawaombeni kwa niaba ya Kristo, mpatanishwe na Mungu. Kristo hakuwa na dhambi, lakini Mungu alimfanya ahusike na dhambi kwa ajili yetu, ili sisi kwa kuungana naye, tupate kuushiriki uadilifu wake Mungu.

Yahweh tunaomba ukawaguse kwa mkono wako wenye nguvu wote
wanaopitia magumu/majaribu mbalimbali,Mungu wetu tunaomba
ukawaponye wagonjwa,Baba wa Mbinguni tunaomba ukawapatie
chakula wenye njaa,Jehovah ukaguse wenye shida/tabu,Yahweh
ukawafungue wale wote walio katika vifungo vya yule mwovu
Baba wa Mbinguni ukawape tumaini wale wote waliokata tamaa,
Mungu wetu ukawatue wote wenye kuelemewa na mizigo,Yahweh
tunaomba ukawasamehe wale wote waliokwenda kinyume nawe
Mungu wetu tunaomba ukawaponye kimwili na kiroho pia,Baba 
ukawape neema ya kujiombea,kufuata njia zako na Nuru yako
ikaangaze katika maisha yao..Jehovah ukawafariji wafiwa..
Ee Baba tunayaweka haya yote miononi mwako,Tukiamini na 
kukushukuru daima..
Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele..
Amina..!
Asanteni sana wapendwa katika Bwana kwa kuwa nami
Mungu mwenye neema/rehema aendelee kuwabariki
Amani  ya Kristo Yesu iwe nanyi wakati wote..
Nawapenda..



1Baada ya muda fulani, wakati wa mavuno ya ngano, Samsoni alichukua mwanambuzi, akaenda kumtembelea mkewe. Akamwambia baba mkwe wake kwamba anataka kumwona mke wake chumbani mwake. Lakini baba mkwe hakumruhusu, 2akamwambia, “Mimi nilidhani ulimchukia kabisa. Kwa hiyo nilimwoza rafiki yako. Hata hivyo, dada yake mdogo ni mzuri kuliko yeye. Tafadhali, umwoe huyo badala yake.” 3Samsoni akamwambia, “Safari hii sitakuwa na lawama kwa yale nitakayowatendea Wafilisti.” 4Basi, Samsoni akaenda, akawakamata mbweha 300 na akawafunga mikia yao pamoja wawiliwawili. Kisha akaweka mwenge katika kila jozi ya mbweha. 5Halafu akaiwasha hiyo mienge na kuwaachilia hao mbweha ambao waliingia kwenye mashamba ya Wafilisti na kuteketeza miganda ya ngano na pia ngano iliyokuwa bado haijavunwa hata na mashamba ya mizeituni. 6Wafilisti walipotaka kujua aliyefanya hayo, waliambiwa, “Ni huyo Samsoni, mkwewe Mtimna, amefanya hivyo kwa sababu huyo baba mkwe wake amemchukua mke wake na kumwoza kwa kijana mmoja aliyekuwa mdhamini wake mwenyewe Samsoni katika harusi.” Basi Wafilisti wakaenda kumchoma moto yule mwanamke pamoja na baba yake.
7Samsoni akawaambia hao Wafilisti, “Kama hayo ndiyo mliyoyafanya, naapa kwamba sitaondoka mpaka nimelipiza kisasi.” 8Basi, akawashambulia vikali na kuwaua wengi. Kisha akaenda kuishi katika pango la mwamba wa Etamu.

Samsoni awashinda Wafilisti

9Wafilisti wakaja, wakapiga kambi yao nchini Yuda na kuushambulia mji wa Lehi. 10Watu wa Yuda wakawauliza, “Kwa nini mmekuja kutushambulia?” Nao wakawajibu, “Tumekuja ili tumfunge Samsoni na kumtendea kama alivyotutendea.”
11Basi, watu 3,000 wa Yuda wakamwendea Samsoni pangoni mwa mwamba wa Etamu wakamwambia, “Je, hujui kwamba Wafilisti wanatawala juu yetu? Tazama basi, mkosi uliotutendea!” Samsoni akawajibu, “Kama walivyonitendea ndivyo nilivyowatendea.” 12Wakamwambia, “Tumekuja kukufunga ili tukutie mikononi mwao.” Samsoni akawaambia, “Niapieni kwamba nyinyi wenyewe hamtaniua.” 13Nao wakamwambia, “Sisi hatutakuua ila tutakufunga tu na kukutia mikononi mwao.” Basi, wakamfunga kwa kamba mbili mpya na kumtoa humo pangoni.
14Alipofika Lehi, Wafilisti walimwendea mbio huku wakipiga kelele. Ghafla roho ya Mwenyezi-Mungu ikamjia Samsoni kwa nguvu na zile kamba walizomfunga mikononi mwake zikakatika kama kitani kilichoshika moto, navyo vifungo vikaanguka chini. 15Samsoni akapata utaya mbichi wa punda, akautumia kuwaua watu 1,000. 16Kisha Samsoni akasema,
“Kwa utaya wa punda,
nimeua watu elfu moja.
Kwa utaya wa punda,
nimekusanya marundo ya maiti.”
17Alipomaliza kusema, akatupa utaya huo. Mahali hapo pakaitwa Ramath-lehi, yaani mlima wa utaya.
18Kisha Samsoni akashikwa na kiu sana. Basi, akamwomba Mwenyezi-Mungu, akisema, “Ee Mungu, wewe ndiwe uliyeleta ukombozi huu, kwa kunitumia mimi mtumishi wako. Je, sasa utaniacha nife kwa kiu na kutekwa na Wafilisti hawa wasiotahiriwa?” 19Mungu akafungua mahali palipokuwa na shimo huko Leki, akatiririsha maji. Samsoni akanywa maji hayo na nguvu zake zikamrudia. Chemchemi hiyo ikaitwa En-hakore; nayo iko huko Lehi mpaka leo.
20Samsoni alikuwa mwamuzi wa Waisraeli kwa miaka ishirini, nyakati za Wafilisti.


Waamuzi 15;1-20

Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)

"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.

No comments: