Katika maisha haya, unaweza ukakutwa na majanga na kufikia hata kukufuru, ukizania wewe tu ndiye unayeonewa, lakini ugumu na matatizo ya kimaisha yapo katika watu wengi, ila ni kwasababu tu hujawahi kusikia au kukutana na watu kama hao. Nalisema hili pale nilipokumbuka kisa cha huyu mwanadada ambaye nilimkuta akiwa kainama upembezoni mwa nyumba huku kashika shavu na michirizi miwili ya machozi ikiwa imeshajichora mashavuni.
Niliingiwa na huruma nilipoona ule ukaaji aliokuwa kaka huyo binti, hasa kwa binti mkubwa kama yule, na ile nguo nyepesi aliyovaa asubuhi kama ile licha ya baridi kali. Pembeni yake kulikuwa na ndoo ya maji, iliyo tupu. Niliingiwa na moyo wa huruma nikamsogelea kwa tahadhari, kwani dunia hii haina wema, unaweza ukajitia una huruma, na huruma hiyo ikakutokea puani.
Wakati namsogelea kwa tahadhari,nilikumbuka kisa cha jamaa yetu mmoja, ambaye alienda kusota jela, baada ya kujifanya msamarai mwema, kwa kumoenea huruma binti kama huyu. Yeye alimkuta huyo binti njiani, akiwa analia, na hali aliyomkuta nayo, ilikuwa ya kusikitisha, kwani kama alivyodai, ana siku mbili , kula hali, anachoambulia ni makombo. Yule jamaa yangu alipomuona kwenye hiyo hali akamchukua kwake, lakini kabla hajatahamaki polisi hawa wapo mlangoni pake.
‘Tumeskilia wewe umemchukua msichana wa watu, umemficha hapa kwako , yupo wapi?’ akaulizwa.
‘Afande, mimi nimemuona huyu binti njiani, akiwa analia, nikajaribu kumuuliza ana tatizo gani, akawa hanijibu, lakini kwa hali aliyokuwa nayo ilionyesha dhahiri kuwa ana njaa, nikaona nimchukue kwangu, ili anywe chai, halafu atanielekeza kwao, au polisi ikibidi, kwani hali aliyokuwa nayo hata wewe ungelimuonea huruma, inaonyesha wazi ana njaa, na pia mahala kama pale nilipomkuta hapana usalama’akajitetea huyo jamaa yangu.
Wale maaskari wakaangua kicheko, na kusema;
‘Hivi wewe kweli una akili, ukutane na binti wa watu,tena msichana, badala ya kwenda naye polsi unampeleka kwako, kwanza wewe una mke, au ndio ulitaka awe mkeo wa muda baadaye umeshamuharibia maisha yake unamtelekeza!’ akasema yule askari huku akiangalia huku na kule kama ataona mke wa jamaa yangu huyo.
‘Mimi ninaye mke, na kwasasa hayupo kaenda kwao, hivi sasa nipo peke yangu, alikwenda kwao kusalimia.’akajitetea jamaa yangu huyo
‘Kwahiyo ukaona uchukue mwanya huo, kutorosha mabinti za watu,wewe huoni hilo ni kosa kubwa, linalinganishwana kuteka nyara. Na wewe hujui kuwa utakuwa na mtoto kama huyo siku za baadaye?
’akasema yule askari huku akitikisa kichwa na mwenzake akatikisa kichwa kukubaliana naye.
‘Jamani, huyu binti wala sijamtorosha, sivyo kabisa mnavyozania nyie, kwanza yupo hapo ndani anakunywa chai, hebu ingieni mumuhoji wenyewe‘akasema na wale maaskari wakaingia ili kuhakikisha, na wakamkuta yule binti akiwa anakunywa chai, na alipowaona wale maaskari, akakurupuka pale mezani akitaka kukimbia, wakamshika.
‘Wewe ulikuwa wapi muda wote huo, ulikuwa na huyu muhuni, ndiyo yeye anayekuhadaa kila siku ehe, utatumabie vyema?’akasema yule askari huku kamkazia macho yule binti.
Inaendelea....Kusoma zaidi ingia;http://www.miram3.blogspot.com
Kwa Visa vya kusisimua na kufundisha, Ungana na EMU-Three... Na;
Diary Yangu.
Yakeeeee!!!!!!!!!
"Swahili NA Wswahili" Pamoja Daima