Swahili na Waswahili

Swahili na Waswahili
Waswahili na Mswahili Rachel Siwa...Pamoja Daima!!

Monday 19 April 2021

Kikombe Cha Asubuhi;Kitabu cha Wafilipi....3


Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?

Haleluyah ni siku/wiki nyingine tena Mungu wetu ametuchagua

na kutupa kibali cha kuendelea kuiona leo hii
Si kwamba sisi tumetenda mema sana wala si kwa nguvu zetu
si kwa utashi wetu wala si kwa akili zetu si kwamba sisi
ni wazuri mno si kwa uwezo wetu sisi kuwa hivi tulivyo leo hii
Ni kwa rehema/neema zake ni kwa mapenzi yake Mungu wetu....

Tumshukuru Mungu wetu katika yote...

Asante Mungu wetu kwa wema na fadhili zako kwetu
Asante kwa ulinzi wako kwetu wakati wote
Asante kwa pumzi/uzima,afya na kuwa tayari kwa majukumu yetu
Sifa na Utukufu tunakurudshia Mungu wetu....!!


Jumuiya yote ya waumini ilikuwa na moyo mmoja na roho moja. Hakuna hata mmoja aliyekuwa na kitu chochote akakiweka kuwa mali yake binafsi, ila waligawana vyote walivyokuwa navyo. Mitume walishuhudia kwa nguvu nyingi kufufuka kwa Bwana Yesu, naye Mungu akawapa baraka nyingi.

Matendo 4:32-33

Tazama jana imepita ee Mungu wetu leo ni siku mpya na kesho ni siku nyingine
Jehovah tunakuja mbele zako tukijinyenyekeza,
tukijishusha na kujiachilia mikononi mwako
 Mungu wetu tunaomba utusamehe dhambi zetu zote tulizozifanya kwakuwaza,kwakunena,kwakutenda,kwakujua/kutojua
Baba wa Mbinguni nasi tunaomba utupe neema ya kuweza kuwasamehe wale wote waliotukosea
Jehovah usitutie majaribuni Mungu wetu tunaomba utuepushe na yule mwovu na kazi zake zote
Yahweh tunaomba ututakase miili yetu na akili zetu
Baba wa Mbinguni utufunike kwa Damu ya Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo wa Nazareti
yeye aliteseka kwanza ili sisi tupate kupona

Kwakupigwa kwake sisi tumepata kupona....


Hakuna mtu yeyote aliyetindikiwa kitu, maana waliokuwa na mashamba au nyumba walikuwa wanaviuza na kuwakabidhi mitume fedha hizo, zikagawiwa kila mmoja kadiri ya mahitaji yake.

Matendo 4:34-35

Yahweh tunaomba ukabariki kazi za mikono yetu

Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe ubunifu na maarifa 
katika utendaji
Jehovah nasi tukatende sawasawa na mapenzi yako
Baba wa Mbinguni tunaomba ukabariki ridhiki zetu
ziingiazo/zitokazo
Mungu wetu nasi tunaomba ukatupe neema ya kuweza
kuwabariki wenye kuhitaji
Yahweh tusipungukiwe katika mahitaji yetu
Mungu wetu ukatupe kama inavyokupendeza wewe

Baba wa Mbinguni tunayaweka maisha yetu mikononi mwako
Mungu wetu tunaomba ukabariki nyumba/ndoa zetu,
watoto,wazazi wetu,familia/ndugu na wote wanaotuzunguka
Jehovah tunaomba ulinzi wako kwetu na kwa vyote tunavyo vimiliki
Yahweh tunaomba ukatubariki tuingiapo/tutokapo
Mungu wetu tunaomba ukavibariki vyote tunavyoenda kugusa/kutumia
Baba wa Mbinguni ukavitakase kwa Damu ya Bwana wetu Yesu Kristo
Mungu wetu ukatamalaki na kutuatamia
Baba wa Mbinguni tukawe salama rohoni
Mfalme wa amani amani yako ikatawale katika maisha yetu
Mungu wetu ukatupe macho ya kuona na masikio ya kusikia 
sauti yako na kuitii
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe neema ya kufuata njia zako
Yahweh tukasimamie Neno lako amri na sheria zako siku zote 
za maisha yetu
Mungu wetu ukaonekane katika maisha yetu
Neema zako zikawe nasi Nuru yako ikaangaze katika maisha yetu
ukatuguse kwa mkono wako wenye nguvu
Ukatufanye chombo chema ee Mungu wetu nasi tukatumike kama
inavyokupendeza wewe
Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi...


Kulikuwa na Mlawi mmoja, mzaliwa wa Kupro, jina lake Yosefu, ambaye mitume walimwita Barnaba (maana yake, “Mtu mwenye kutia moyo”). Yeye pia alikuwa na shamba lake, akaliuza; akazichukua zile fedha, akawakabidhi mitume.

Matendo 4:36-37

Mungu wetu tunawaweka mikononi mwako wenye shida/tabu,wote wanaopitia magumu/majaribu mbalimbali
Mungu wetu tunaomba ukawaguse kwa mkono wako wenye nguvu
 kila mmoja na mahitaji yake 
Mungu wetu tunaomba ukawasamehe pale walipokwenda kinyume nawe
Baba wa Mbinguni ukawape neema ya kujiombea,kufuata njia zako
wakasimamie Neno lako nalo likawaweke huru
Mungu wetu tunaomba ukasikie kuomba kwetu
Mungu wetu ukawatendee sawasawa na mapenzi yako
Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele
Amina...!!


Asanteni sana wapendwa katika Kristo Yesu kwakuwa nami
Mungu Baba aendelee kuwabariki na kuwatendea 
kama inavyompendeza yeye....
Nawapenda.


 
Uadilifu wa kweli

1Hatimaye, ndugu zangu, furahini katika kuungana na Bwana. Sichoki kurudia yale niliyokwisha andika pale awali, maana yatawaongezeeni usalama. 2Jihadharini na hao watendao maovu, hao mbwa, watu wanaosisitiza kujikata mwilini. 3Watu waliotahiriwa kikweli ni sisi, si wao; kwani sisi twamwabudu Mungu kwa njia ya Roho wake, na kuona fahari katika kuungana na Kristo Yesu. Mambo ya nje tu hatuyathamini. 4Mimi pia ningeweza kuyathamini hayo mambo ya nje; na kama yupo mtu anayefikiri kwamba anaweza kuyathamini hayo mambo ya nje, mimi ninayo sababu kubwa zaidi ya kufikiri hivyo: 5Mimi nilitahiriwa siku ya nane baada ya kuzaliwa kwangu; mimi ni wa taifa la Israeli, kabila la Benyamini, Mwebrania halisi. Kuhusu kuizingatia sheria mimi nilikuwa Mfarisayo, 6na nilikuwa na bidii sana hata nikalidhulumu kanisa. Kuhusu uadilifu unaopatikana kwa kuitii sheria, mimi nilikuwa bila hatia yoyote. 7Lakini hayo yote ambayo ningeweza kuyafikiria kuwa ni faida, nimeyaona kuwa ni hasara, kwa ajili ya Kristo. 8Naam, wala si hayo tu; ila naona kila kitu kuwa ni hasara tupu, kwa ajili ya jambo bora zaidi, yaani kumjua Kristo Yesu Bwana wangu. Kwa ajili yake nimekubali kutupilia mbali kila kitu; nimeyaona hayo yote kuwa ni takataka, ili nimpate Kristo 9na kuunganishwa naye kabisa. Mimi sitaki tena uadilifu unaotokana na kuitii sheria. Sasa ninao ule uadilifu unaopatikana katika kumwamini Kristo; uadilifu utokao kwa Mungu na ambao unategemea imani. 10Ninachotaka tu ni kumjua Kristo na kuiona nguvu ya ufufuo wake, kushiriki mateso yake na kufanana naye katika kifo chake, 11nikitumaini kwamba nami pia nitafufuliwa kutoka kwa wafu.
Mbioni kuelekea lengo letu
12Sijidai kwamba nimekwisha faulu au nimekwisha kuwa mkamilifu. Naendelea kujitahidi kupata lile tuzo ambalo kwalo Kristo amekwisha nipata mimi. 13Ama kweli, ndugu zangu, sidhani kuwa nimekwisha pata tuzo hilo; lakini jambo moja nafanya: Nayasahau yale yaliyopita na kufanya bidii kuyazingatia yale yaliyo mbele. 14Basi, nimo mbioni kuelekea lengo langu, ili nipate lile tuzo, ambalo ni mwito wa Mungu kwa maisha ya juu kwa njia ya Kristo Yesu. 15Sisi sote tuliokomaa tunapaswa kuwa na msimamo huohuo. Lakini kama baadhi yenu wanafikiri vingine, basi, Mungu atawadhihirishieni jambo hilo. 16Kwa vyovyote, tusonge mbele katika njia hiyohiyo ambayo tumeifuata mpaka hivi sasa.
17Ndugu zangu, fuateni mfano wangu. Tumewapeni mfano mwema, na hivyo wasikilizeni wale wanaofuata mfano huo. 18Nimekwisha waambieni jambo hili mara nyingi, na sasa narudia tena kwa machozi: Watu wengi wanaishi kama maadui wa msalaba wa Kristo. 19Mwisho wao ni kuangamia, kwani tumbo lao ndilo mungu wao; wanaona fahari juu ya mambo yao ya aibu, hufikiria tu mambo ya kidunia. 20Lakini sisi ni raia wa mbinguni, na twatazamia kwa hamu kubwa Mwokozi aje kutoka mbinguni, Bwana Yesu Kristo. 21Yeye ataibadili miili yetu dhaifu na kuifanya ifanane na mwili wake mtukufu, kwa nguvu ile ambayo kwayo anaweza kuviweka vitu vyote chini ya utawala wake.
Wafilipi3;1-21
Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)
"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe

No comments: