Swahili na Waswahili

Swahili na Waswahili
Waswahili na Mswahili Rachel Siwa...Pamoja Daima!!

Thursday 15 April 2021

Kikombe Cha Asubuhi; Tunamshukuru Mungu kwa kumaliza Kitabu cha Waefeso,Leo Tunaanza Kitabu cha Wafilipi....1

 


Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?

Tunamshukuru Mungu kwa kutupa kibali cha
 kupitia kitabu cha "Waefeso
"
Ni matumaini yangu kuna mengi tumejifunza/kufaidika
na kutupa mwanga/kuelewa kwenye kitabu hiki...

Leo tunapokwenda anza kupitia Kitabu cha"Wafilipi"
tunamuomba Mungu wetu akatupe kibali,macho ya rohoni
 na akili ya kuelewa katika kujifunza NENO lake...
Ee Mungu  tunaomba ukatuongoze...!!
Tumshukuru Mungu wetu katika yote...

Mungu wetu Baba yetu,Muumba wetu Muumba wa Mbingu na Nchi
Muumba wa vyote vilivyomo vinavyoonekana na visivyoonekana
Mungu wa walio hai,Mungu  mwenye huruma,Mungu wa upendo
Mungu wa Abrahamu,Isaka na Yakobo...


Asante kwa wema na fadhili zako kwetu
Asante kwa ulinzi wako kwetu wakati wote
Asante kwa kutuchagua tena na kutupa
kibali cha kuendelea kuiona leo hii
Asante kwa pumzi/uzima,afya na kuwatayari kwa majukumu yetu

Neema yako yatutosha ee Mungu wetu....!!

Mara tu walipoachwa huru, Petro na Yohane walirudi kwa wenzao, wakawaeleza yale waliyoambiwa na makuhani wakuu na wazee.

Matendo 4:23

Baba wa Mbinguni tunakuja mbele zako,
Tukijinyenyekeza,tukijiachilia mikononi mwako
Mungu wetu tunamomba utusamehe dhambi zetu
Baba wa Mbinguni nasi tunaomba ukatupe neema
 ya kuweza kuwasamehe wale wote waliotukosea

Usitutie majaribuni Mungu wetu tunaomba utuepushe
na yule mwovu na kazi zake zote
Jehovah ututakase miili yetu na akili zetu
Baba wa Mbinguni tunaomba utufunike kwa Damu
ya Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo wa Nazareti
yeye aliteseka kwanza ili sisi tupate kupona....


Nao waliposikia habari hizo waliungana pamoja katika kumwomba Mungu wakisema, “Bwana, wewe ni Muumba wa mbingu na dunia, bahari na vyote vilivyomo!

Matendo 4:24

Mungu wetu tunaomba ukabariki kazi za mikono yetu
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe ubunifu na maarifa katika utendaji
Jehovah nasi tukatende sawasawa na mapenzi yako
Yahweh tunaomba ukabariki ridhiki zetu ziingiazo/zitokazo
Mungu wetu nasi tunaomna ukatupe neema ya kuweza kuwabariki wenye kuhitaji
Tusipungukiwe katika mahitaji yetu
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe kama inavyokupendeza wewe...


Yahweh tunayaweka maisha yetu mikononi mwako
Mungu wetu tunaomba ukabariki nyumba/ndoa zetu,
Jehovah tunaomba ulinzi wako kwetu na kwa vyote tunavyovimiliki
Yahweh tunaomba ukatubariki tuingiapo/tutokapo
Mungu wetu tunaomba ukavibariki vyote tunavyoenda kugusa/kutumia
Baba wa Mbinguni ukavitakase kwa Damu ya Bwana wetu Yesu Kristo
Mungu wetu ukatamalaki na kutuatamia
Baba wa Mbinguni tukawe salama rohoni
Yahwe ukatupe akili ya kutambua mema na mabaya
Mfalme wa amani amani yako ikatawale katika maisha yetu
Mungu wetu ukatupe macho ya kuona,masikio ya kusikia sauti yako na kuitii..
Baba wa Mbinguni  tunaomba ukatupe neema ya kufuata
njia zako,tukasimamie Neno lako,amri na sheria zako
siku zote za maisha yetu...
Ukatuguse kwa mkono wako wenye nguvu,ukatufanye chombo chema
ee Mungu wetu nasi tukatumike kama inavyokupendeza wewe
Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi....


Ndiwe uliyemfanya mtumishi wako, baba yetu Daudi, aseme kwa nguvu ya Roho Mtakatifu: ‘Kwa nini mataifa yameghadhibika? Mbona watu wamefanya mipango ya bure?

Matendo 4:25

Tazama watoto wako wenye shida/tabu,wote wanaopitia magumu/majaribu mbalimbali
Mungu wetu tunaomba ukawaguse kwa mkono wako wenye nguvu
kila mmoja na mahitaji yake
Mungu wetu tunaomba ukawasamehe pale walipo kwenda kinyume nawe
Yahweh tunaomba ukawape neema ya kuweza kujiombea,kufuata njia zako nazo zikawaweke huru...
Baba wa Mbinguni tunayaweka haya yote mikononi mwako
Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele...
Amina...!!


Asanteni sana wapendwa katika Kristo Yesu kwakuwa nami,
Baba wa Mbinguni aendelee kuwatendea sawasawa na mapenzi yake...
Nawapenda.


1Mimi Paulo na Timotheo, watumishi wa Yesu Kristo, tunawaandikia nyinyi watu wa Mungu huko Filipi ambao mmeunganishwa na Kristo Yesu, pamoja na viongozi

1:1 viongozi: Au Maaskofu. na wasaidizi wa kanisa. 2Tunawatakieni neema na amani kutoka kwa Mungu Baba yetu na kutoka kwa Bwana Yesu Kristo.
Sala kwa ajili ya Wafilipi
3Namshukuru Mungu wangu kila ninapowakumbukeni; 4na kila ninapowaombeeni nyote, nasali kwa furaha, 5kwa sababu ya jinsi mlivyonisaidia katika kazi ya Injili tangu siku ile ya kwanza mpaka leo. 6Basi, nina hakika kwamba Mungu aliyeanza kazi hii njema ndani yenu, ataiendeleza mpaka ikamilike katika siku ile ya Kristo Yesu. 7Hivyo ndivyo ninavyopaswa kuwafikirieni, kwani nawakumbukeni daima moyoni mwangu. Kwa maana nyinyi nyote mmeshiriki katika fadhili aliyonijalia Mungu ya kutetea na kuithibitisha Injili, sasa niwapo kifungoni na pia pale awali nilipokuwa huru. 8Mungu anajua kuwa ninasema ukweli ninaposisitiza kwamba, kwa upendo uleule wa Yesu Kristo, natamani sana kuwaoneni.
9Sala yangu ni hii: Naomba upendo wenu uzidi kuongezeka zaidi na zaidi pamoja na ujuzi wa kweli na busara ya kila namna, 10ili muweze kuchagua jambo lililo bora. Hapo ndipo mtakuwa safi na bila lawama yoyote ile katika siku ile ya Kristo. 11Maisha yenu yatajazwa mambo yote yaliyo kweli bora, ambayo Yesu Kristo mwenyewe anaweza kuwajalieni, kwa ajili ya utukufu na sifa ya Mungu.
Kuishi ni Kristo
12Ndugu zangu, napenda mfahamu kwamba mambo yote yaliyonipata yamesaidia sana kuieneza Injili. 13Kutokana na hayo, walinzi wote wa ikulu pamoja na wengine wote hapa wanafahamu kwamba niko kifungoni kwa sababu mimi namtumikia Kristo. 14Na huku kuweko kwangu kifungoni kumewafanya ndugu wengi kuwa na imani kwa Bwana, hata wanazidi kuwa hodari katika kuutangaza ujumbe wa Mungu bila hofu. 15Kweli, baadhi yao wanamhubiri Kristo kwa sababu wana wivu na ni watu wagomvi; lakini wengine wanamhubiri Kristo kwa nia nzuri. 16Hawa wanafanya hivyo kwa upendo, kwani wanajua kwamba Mungu amenipa jukumu hili la kuitetea Injili. 17Hao wengine wanamtangaza Kristo kwa mashindano na si kwa moyo mnyofu, wakidhani kwamba wataniongezea mateso yangu kifungoni.
18Haidhuru! Mimi nafurahi ikiwa tu watu wanamhubiri Kristo kwa kila njia, iwe ni kwa nia nzuri au kwa nia mbaya. Tena nitaendelea kufurahi, 19kwani najua kwamba kwa sala zenu na kwa msaada wa Roho wa Yesu Kristo, nitakombolewa. 20Hamu yangu kubwa na tumaini langu ni kwamba kwa vyovyote sitashindwa katika kutimiza wajibu wangu, bali nitakuwa na moyo thabiti kila wakati na hasa wakati huu, ili kwa maisha yangu yote, niwapo hai au nikifa, nimpatie Kristo heshima. 21Kwangu, kuishi ni Kristo, na kufa ni faida zaidi. 22Lakini, kama kwa kuishi nitaweza kufanya kazi yenye faida zaidi, basi, sijui nichague lipi! 23Nakabiliwa na haya mawili yaliyo sawa. Natamani kuyaacha maisha haya nikakae pamoja na Kristo, jambo ambalo ni bora zaidi; 24lakini ni jambo la maana zaidi kwenu kama nikiendelea kuishi. 25Nina hakika ya jambo hili, na hivyo najua kwamba nitaendelea kuishi pamoja nanyi nyote, ili nipate kuongeza maendeleo yenu na furaha katika imani. 26Basi, nitakapokuwa nanyi tena mtakuwa na sababu ya kuona fahari juu yangu katika kuungana na Kristo Yesu.
27Basi, jambo muhimu ni kwamba mwenendo wenu uambatane na matakwa ya Injili ya Kristo, ili kama nikiweza kuja kwenu au nisipoweza, nipate walau kusikia kwamba mnasimama imara mkiwa na lengo moja, na kwamba mnapigana vita kwa pamoja na mnayo nia moja kwa ajili ya imani ya Injili. 28Msiwaogope maadui zenu, bali muwe hodari daima, na hiyo itawathibitishia kwamba wao watashindwa, nanyi mtashinda kwani Mungu mwenyewe ndiye anayewapeni ushindi. 29Maana nyinyi mmepewa fadhili ya kumtumikia Kristo si tu kwa kumwamini bali pia kwa kuteswa kwa ajili yake. 30Sasa mwaweza kushirikiana nami katika kupigana vita. Vita hivi ni vile mlivyoona nikipigana pale awali na ambavyo bado napigana sasa kama mnavyosikia.
Wafilipi1;1-30
Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)
"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe

No comments: