Swahili na Waswahili

Swahili na Waswahili
Waswahili na Mswahili Rachel Siwa...Pamoja Daima!!

Wednesday 20 September 2017

Kikombe Cha Asubuhi Kumbukumbu la Sheria 21 (Kumbukumbu la Torati katika tafsiri nyingine)



Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?

Haleluyah..!Mungu wetu yu mwema sana..
Tumshukuru Mungu wetu katika yote..
Mungu wetu Baba yetu,Muumba wetu Muumba wa Mbingu na Nchi..
Baba wa Upendo,Baba wa Baraka,Baba wa Yatima,Mume wa Wajane..
Mungu wa Abrahamu,Isaka na Yakobo,Alfa na Omega..
Muweza wa yote,Unatosha Baba wa Mbinguni..
Unastahili sifa,Unastahili kuabudiwa...

Utukuzwe Mungu wetu,Uhimidiwe Jehovah..
Hakuna kama wewe Yahweh..!!

Kisha mfalme Daudi akaingia ndani na kuketi mbele ya Mwenyezi-Mungu; halafu akaomba, “Mimi ni nani ee Bwana Mungu, na jamaa yangu ni nini hata ukaniinua mpaka hapa nilipo leo! Tena jambo hili lilikuwa dogo machoni pako, Bwana Mungu; zaidi ya hayo umeiahidi jamaa yangu mambo makubwa katika miaka mingi ijayo; na kwamba umenijalia kuona hayo, Ee Bwana Mungu. Nikuambie nini zaidi, mimi Daudi, mtumishi wako? Kwani wewe unanijua mimi mtumishi wako, ee Bwana Mungu! Kutokana na ahadi yako na kulingana na moyo wako, umetenda makuu hayo yote ili unijulishe mimi mtumishi wako. Kutokana na yale tuliyosikia, wewe Mwenyezi-Mungu ni mkuu; hakuna aliye kama wewe, na hakuna Mungu mwingine ila wewe. Tena ni watu gani duniani ambao wanaweza kufananishwa na watu wako wa Israeli, ambao Mungu wake alikwenda kuwakomboa ili wawe watu wake? Wewe ee Mungu ulijifanyia jina na kujitendea mambo makubwa na ya ajabu kwa ajili ya nchi yako mbele ya watu wako ambao kwa ajili yako mwenyewe uliwaokoa kutoka Misri, ukayafukuza mataifa na miungu yake mbele yao? Hata umewaimarisha watu wako wa Israeli kwa ajili yako mwenyewe, ili wawe watu wako milele; nawe ee Mwenyezi-Mungu umekuwa Mungu wao. Basi, sasa, ee Mwenyezi-Mungu, ikamilishe ile ahadi uliyosema kuhusu mimi mtumishi wako na kuhusu jamaa yangu kama ulivyoahidi. Nalo jina lako litatukuzwa milele, nao watu watasema, ‘Mwenyezi-Mungu wa majeshi ni Mungu juu ya Israeli!’ Na jamaa yangu, mimi Daudi mtumishi wako, itaimarika mbele yako. Maana wewe, ee Mwenyezi-Mungu wa majeshi, Mungu wa Israeli, umenifunulia mimi mtumishi wako, ukisema ‘Nitakujengea nyumba;’ ndio maana nina ujasiri kutoa ombi hili mbele yako. Sasa, ee Bwana Mungu, wewe ndiwe Mungu, na maneno yako ni kweli na umeniahidi mimi mtumishi wako jambo hili jema; kwa hiyo, nakuomba nyumba yangu mimi mtumishi wako ipate kudumu milele mbele yako; kwani wewe umesema hivyo, pia kwa baraka zako nyumba yangu itabarikiwa milele.”


Asante Baba wa Mbinguni kwa wema na fadhili zako kwetu...
Asante kwa ulinzi wako wakati wote.
Asante kwakutuchagua tena na kutupa kibali cha kuendelea kuiona leo hii..
Yahweh tunakuja mbele zako tukijinyenyekeza,tukijishusha na kujiachilia mikononi mwako..
Jehovah tunaomba utusamehe dhambi zetu zote tulizozifanya..
Kwakuwaza,kwakunena,kwakutenda,kwakujua/kutojua..
Mfalme wa Amani nasi tunaomba utupe neema ya kuweza kuwasamehe wale wote waliotukosea..
Yahweh tunaomba utuepushe katika majaribu Mungu wetu utuokoe na yule mwovu na kazi zake zote..
Jehovah tunaomba ututakase miili yetu na akili zetu Yahweh utufunike kwa Damu ya Bwana wetu Yesu Kristo wa Nazareti..



Kuwa na imani ni kuwa na hakika ya mambo tunayotumainia; kusadiki kabisa mambo tusiyoyaona. Maana wazee wa kale walipata kibali cha Mungu kwa sababu ya imani yao. Kwa imani sisi tunafahamu kwamba ulimwengu uliumbwa kwa neno la Mungu; vitu vinavyoonekana kutoka vitu visivyoonekana. Kwa imani Abeli alimtolea Mungu tambiko iliyokuwa bora kuliko ile ya Kaini. Kwa imani yake alikubaliwa na Mungu kuwa mwadilifu; Mungu mwenyewe alizikubali sadaka zake. Kwa imani yake ingawa alikufa, bado ananena. Kwa imani Henoki alichukuliwa na Mungu, asipate kufa. Hakuonekana tena kwa sababu Mungu alikuwa amemchukua. Maandiko yasema kwamba kabla ya kuchukuliwa kwake, yeye alikuwa amempendeza Mungu. Basi, pasipo imani haiwezekani kumpendeza Mungu. Kwa maana kila mtu anayemwendea Mungu ni lazima aamini kwamba Mungu yuko, na kwamba huwatuza wale wanaomtafuta.



Mungu wetu tunaomba utubariki na ukabariki kazi za mikono yetu..
Ukabariki ridhiki zetu ziingiazo/zitokazo..
Yahweh nasi tunaomba utupe neema ya kuweza kuwabariki wenye kuhitaji..
Tusipungukiwe katika mahitaji yetu Mungu wetu ukatupoe sawasawa na mapenzi yako..


Baba wa Mbinguni tunayaweka maisha yetu mikononi mwako..
Ukabariki Nyumba/Ndoa zetu,watoto,wazazi/wazee wetu,

Familia/Ndugu na wote wanaotuzunguka..
Mungu wetu ukawe mlizi mkuu,Ukatamalaki na kutuatamia..
Ukatupe neema ya kusimamia Neno lako
Imani yetu kwako Mungu ikakue na tukafuate Amri na Sheria zako.




Kwa imani Noa alionywa na Mungu juu ya mambo ya baadaye ambayo hayakuwa yameonekana bado. Alimtii Mungu, akajenga ile safina ambamo aliokolewa yeye pamoja na jamaa yake. Kutokana na hayo ulimwengu ulihukumiwa, naye Noa akapokea uadilifu unaotokana na imani. Kwa imani Abrahamu alimtii Mungu alipoitwa aende katika nchi ambayo Mungu angempa iwe yake. Ingawa hakujua alikokuwa anakwenda, Abrahamu alihama. Kwa imani aliishi kama mgeni katika nchi aliyoahidiwa na Mungu. Aliishi huko katika hema kama walivyoishi Isaka na Yakobo, ambao pia walishiriki ahadi ileile. Maana Abrahamu alikuwa akingojea mji wenye misingi imara, mji ambao Mungu mwenyewe ndiye fundi aliyeubuni na kuujenga. Kwa imani hata Sara aliamini kwamba Mungu hutimiza ahadi zake, kwa hiyo akajaliwa kuchukua mimba ingawaje alikuwa amepita umri. Kwa hiyo, kutoka katika mtu huyo mmoja, Abrahamu, ambaye alikuwa kama amekufa, walitokea watu wengi wasiohesabika kama vile nyota za mbinguni na mchanga wa pwani. Watu hawa wote walikufa wakiwa na imani. Walikufa kabla ya kupokea mambo ambayo Mungu alikuwa ameahidi, lakini kwa mbali waliyaona, wakashangilia, na kukiri wazi kwamba wao walikuwa wageni na wakimbizi duniani. Watu wanaosema mambo kama hayo, huonesha wazi kwamba wanaitafuta nchi yao wenyewe. Kama wangalikuwa wanaifikiria nchi walikotoka zamani, wangalipata nafasi ya kurudi huko. Lakini sasa wanataka nchi iliyo bora zaidi, yaani nchi ya mbinguni. Ndio maana Mungu haoni haya wakimwita yeye Mungu wao, kwa sababu yeye mwenyewe amekwisha watayarishia mji. Kwa imani Abrahamu alimtoa tambiko mwanawe Isaka wakati Mungu alipomjaribu. Huyo Abrahamu ndiye aliyekuwa amepokea ahadi ya Mungu, lakini, hata hivyo, alikubali kumtoa tambiko mwanawe wa pekee, ingawa Mungu alikuwa amemwambia: “Wazawa wako watatokana na Isaka.” Abrahamu aliamini kwamba Mungu anaweza kuwafufua wafu; na kwa namna fulani kweli Abrahamu alimpata tena mwanawe kutoka kwa wafu. Kwa imani Isaka aliwabariki Yakobo na Esau, wapate baraka zitakazokuja baadaye. Kwa imani Yakobo alipokuwa karibu kufa, aliwabariki kila mmoja wa wana wa Yosefu, akamwabudu Mungu akiegemea kichwa cha ile fimbo yake. Kwa imani Yosefu alipokuwa karibu kufa, alinena juu ya kutoka kwa Waisraeli katika nchi ya Misri, na pia akawaachia maagizo kuhusu mifupa yake.

Ukatufanye chombo chema Mungu wetu nasi tukatumike kama
inavyokupendeza wewe..
Kwa Imani Baba wa Mbinguni tunaomba ukawaponye na kuwaokoa wote wanaotaabika,waliokatatamaa,waliokataliwa,wagonjwa,wenye shida/tabu na wote waliokatika vifungo mbalimbali vya yule mwovu,
Wanopitia magumu/majaribu mbalimbali..
Mungu wetu ukawaguse kwa mkono wako wenye nguvu..
wakapate uponyaji wa mwili na roho pia,Ukawape Neema ya kusimamia Neno lako na kufuata njia zako nazo zikawaweke huru..
Imani yao ikakue na wakawe na shauku ya kukujua wewe zaidi..

Kwa imani wazazi wa Mose walimficha huyo mtoto kwa muda wa miezi mitatu baada ya kuzaliwa kwake. Walimwona kuwa ni mtoto mzuri, wala hawakuiogopa amri ya mfalme. Kwa imani Mose alipokuwa mtu mzima, alikataa kuitwa mwana wa binti Farao. Aliona ni afadhali kuteseka pamoja na watu wa Mungu kuliko kufurahia raha ya dhambi kwa kitambo kidogo. Alitambua kwamba kuteseka kwa ajili ya Kristo kuna faida kubwa kuliko utajiri wote wa nchi ya Misri, maana alikuwa anatazamia tuzo la baadaye. Kwa imani Mose alihama kutoka nchi ya Misri bila kuogopa hasira ya mfalme; na wala hakurudi nyuma, kwani alikuwa kama mtu aliyemwona yule Mungu asiyeonekana. Kwa imani aliadhimisha siku ya Pasaka, akaamuru damu inyunyizwe juu ya milango, ili yule Malaika Mwangamizi asiwaue wazaliwa wa kwanza wa Israeli. Kwa imani watu wa Israeli walivuka bahari ya Shamu kana kwamba ilikuwa nchi kavu; lakini Wamisri walipojaribu kufanya hivyo walikufa maji. Kwa imani kuta za mji wa Yeriko zilianguka watu wa Israeli walipokwisha zunguka kuta hizo kwa siku saba. Kwa imani Rahabu aliyekuwa malaya hakuangamia pamoja na wale waliomwasi Mungu, kwa sababu aliwakaribisha wale wapelelezi. Basi, niseme nini zaidi? Wakati hauniruhusu kueleza juu ya Gideoni, Baraki, Samsoni, Yeftha, Daudi, Samueli na manabii. Kwa imani hawa wote walipigana vita na wafalme, wakashinda. Walitenda mambo adili, wakapokea yale aliyoahidi Mungu. Walifunga vinywa vya simba, walizima mioto mikali, waliepuka kuuawa kwa upanga, walikuwa dhaifu lakini walipata nguvu. Walikuwa hodari katika vita, wakashinda majeshi ya kigeni. Na, wanawake walioamini walirudishiwa wafu wao wakiwa wamefufuliwa. Baadhi yao walikataa kufunguliwa, wakateswa mpaka kufa ili wapate kufufuliwa na kuingia katika maisha bora zaidi. Wengine walidhihakiwa na kupigwa mijeledi, na wengine walifungwa minyororo na kutupwa gerezani. Walipigwa mawe, walipasuliwa vipandevipande, waliuawa kwa upanga. Walizungukazunguka wakiwa wamevaa ngozi za kondoo na ngozi za mbuzi; walikuwa watu maskini, walioteswa na kudhulumiwa. Ulimwengu haukustahili kuwa na watu hao. Walitangatanga jangwani na milimani, wakaishi katika mashimo na mapango ya ardhi. Watu hawa wote walionekana kuwa mashujaa kwa sababu ya imani yao. Hata hivyo, hawakupokea yale ambayo Mungu aliwaahidi, maana Mungu alikuwa ameazimia mpango ulio bora zaidi kwa ajili yetu; yaani wao wangeufikia ukamilifu wakiwa pamoja nasi.

Asante Mungu wetu tunakushukuru na kukusifu Daima..
Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele..
Amina..!

Asanteni sana wapendwa/waungwana kwakuwa nami..
Mungu muweza wa yote aendelee kuwabariki..
Akaonekane katika maisha yenu na akajibu sala/maombi yenu..
Nawapenda.

Kuhusu mauaji yenye utata

1“Mtu akipatikana ameuawa mbugani katika nchi ambayo Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, anawapeni muimiliki, nanyi hamjui ni nani aliyemuua, 2wazee na waamuzi wenu watajitokeza na kupima umbali wa kutoka mahali maiti ilipo hadi miji ya karibu. 3Kisha, wazee wa mji ule ulio karibu zaidi na ile maiti watachukua ndama ambaye hajatumiwa kufanya kazi yoyote ile wala kutiwa nira. 4Nao watamteremsha ndama bondeni kwenye kijito ambacho hakikauki, na bonde hilo halilimwi au kupandwa; huko watamvunja huyo ndama shingo. 5Nao makuhani wa ukoo wa Lawi sharti wawepo hapo. Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, aliwachagua wamhudumie na kubariki watu kwa jina lake. Wao pia ndio wenye mamlaka kuhusu kila tukio na utumiaji wa nguvu. 6Yule ndama atakapovunjwa shingo, wazee wote wa mji huo ulio karibu na mtu huyo aliyeuawa, watanawa mikono yao kwa maji juu ya ndama 7na kusema, ‘Hatuna hatia kuhusu kifo hiki, wala hatumjui aliyemuua. 8Ee Mwenyezi-Mungu, uwasamehe watu wako wa Israeli ambao umewakomboa, usiwawekee watu wako Israeli hatia ya mauaji ya mtu asiye na hatia, ila uwasamehe hatia hiyo.’ 9Hivyo damu hiyo iliyomwagwa haitakuwa tena sababu ya lawama kwenu, maana mmefanya yale Mwenyezi-Mungu aliyotaka myafanye.
10“Mkienda kupigana vita na adui, naye Mwenyezi-Mungu akawapeni ushindi, mkawachukua mateka, 11kama mmoja wenu akiona miongoni mwa mateka mwanamke mzuri, akamtamani na kutaka kumwoa, 12basi, wewe mwanamume mhusika utamchukua nyumbani kwako, naye atanyoa kichwa chake, akakate kucha zake, 13na kubadili nguo zake za mateka. Atakaa muda wa mwezi mzima kumwombolezea baba yake na mama yake; kisha waweza kumwoa uwe mume wake, naye awe mke wako. 14Kama baadaye hupendezwi naye, utamwacha huru aende zake; usimwuze kwa fedha, wala usimfanye kama mtumwa, kwa sababu ulimnyenyekesha.
15“Ikiwa mwanamume fulani ana wake wawili naye anampenda mmoja kuliko mwingine. Nao wanawake hao wamemzalia watoto wa kiume, na mtoto wa kwanza kuzaliwa ni wa yule mama asiyempenda, 16ikafika siku ya kuwapa hao wanawe urithi, huyo baba haruhusiwi kamwe kumtendea mtoto wa yule mke anayempenda kama kwamba ni mtoto mzaliwa wa kwanza, badala ya yule mtoto wa mama asiyependwa ambaye ndiye aliye mzaliwa wa kwanza. 17Lazima amkubali yule mzaliwa wa kwanza, mtoto wa yule mwanamke asiyependwa, na kumpa haki yake: Sehemu ya mali zake mara mbili.
18“Kama mtu ana mtoto mkaidi na mtundu, asiyemtii baba yake au mama yake wanapompa nidhamu, 19basi, mama na baba yake huyo mtoto watamchukua mlangoni mwa nyumba anamoishi na kumpeleka kwa wazee katika lango la mji. 20Wazazi hao watawaambia wazee wa mji: ‘Mtoto wetu ni mkaidi na mtundu, hataki kutusikiliza, ni mlafi na mlevi.’ 21Hapo watu wa mji huo watampiga mawe mtoto huyo mpaka afe. Ndivyo mtakavyokomesha ubaya huo miongoni mwenu. Kila mtu katika Israeli atasikia tukio hilo na kuogopa.

Sheria mbalimbali

22“Kama mtu amefanya kosa la jinai linalompasa auawe na akauawa kwa kutundikwa mtini, 23maiti yake isiachwe mtini usiku wote, bali mtaizika siku hiyohiyo. Maana mtu aliyenyongwa amelaaniwa na Mungu nanyi hamtaitia najisi nchi yenu mliyopewa na Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, iwe mali yenu.


Kumbukumbu la Sheria 21:1-23

Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)

"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.

No comments: