Swahili na Waswahili

Swahili na Waswahili
Waswahili na Mswahili Rachel Siwa...Pamoja Daima!!

Thursday 22 October 2020

Kikombe Cha Asubuhi; Luka 6...



Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?

Tumshukuru Mungu katika yote....

Mungu wetu Baba yetu,Muumba wetu Muumba wa Mbingu na Nchi
Muumba wa vyote vilivyomo vinavyoonekana na visivyoonekana
Mungu wa walio hai,Mungu  mwenye huruma,Mungu wa upendo
Mungu wa Abrahamu,Isaka na Yakobo...
Asante kwa wema na fadhili zako kwetu
Asante kwa ulinzi wako kwetu wakati wote
Asante kwa kutuchagua tena na kutupa
kibali cha kuendelea kuiona leo hii
Asante kwa pumzi/uzima,afya na kuwatayari kwa majukumu yetu

Neema yako yatutosha ee Mungu wetu....!!



Tazama! Adui anakuja kama mawingu. Magari yake ya vita ni kama kimbunga, na farasi wake waenda kasi kuliko tai. Ole wetu! Tumeangamia! Yerusalemu, yasafishe maovu moyoni mwako, ili upate kuokolewa. Mpaka lini utaendelea kuwaza maovu?

Yeremia 4:13-14

Baba wa Mbinguni tunakuja mbele zako,
Tukijinyenyekeza,tukijiachilia mikononi mwako
Mungu wetu tunamomba utusamehe dhambi zetu
Baba wa Mbinguni nasi tunaomba ukatupe neema
 ya kuweza kuwasamehe wale wote waliotukosea

Usitutie majaribuni Mungu wetu tunaomba utuepushe
na yule mwovu na kazi zake zote
Jehovah ututakase miili yetu na akili zetu
Baba wa Mbinguni tunaomba utufunike kwa Damu
ya Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo wa Nazareti
yeye aliteseka kwanza ili sisi tupate kupona....



Sauti kutoka Dani inatoa taarifa; inatangaza maafa kutoka vilima vya Efraimu. Inayaonya mataifa, inaitangazia Yerusalemu: “Wavamizi waja kutoka nchi ya mbali, wanaitisha miji ya Yuda,

Yeremia 4:15-16

Mungu wetu tunaomba ukabariki kazi za mikono yetu
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe ubunifu na maarifa katika utendaji
Jehovah nasi tukatende sawasawa na mapenzi yako
Yahweh tunaomba ukabariki ridhiki zetu ziingiazo/zitokazo
Mungu wetu nasi tunaomna ukatupe neema ya kuweza kuwabariki wenye kuhitaji
Tusipungukiwe katika mahitaji yetu
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe kama inavyokupendeza wewe...


Yahweh tunayaweka maisha yetu mikononi mwako
Mungu wetu tunaomba ukabariki nyumba/ndoa zetu,
Jehovah tunaomba ulinzi wako kwetu na kwa vyote tunavyovimiliki
Yahweh tunaomba ukatubariki tuingiapo/tutokapo
Mungu wetu tunaomba ukavibariki vyote tunavyoenda kugusa/kutumia
Baba wa Mbinguni ukavitakase kwa Damu ya Bwana wetu Yesu Kristo
Mungu wetu ukatamalaki na kutuatamia
Baba wa Mbinguni tukawe salama rohoni
Yahwe ukatupe akili ya kutambua mema na mabaya
Mfalme wa amani amani yako ikatawale katika maisha yetu
Mungu wetu ukatupe macho ya kuona,masikio ya kusikia sauti yako na kuitii..
Baba wa Mbinguni  tunaomba ukatupe neema ya kufuata
njia zako,tukasimamie Neno lako,amri na sheria zako
siku zote za maisha yetu...
Ukatuguse kwa mkono wako wenye nguvu,ukatufanye chombo chema
ee Mungu wetu nasi tukatumike kama inavyokupendeza wewe
Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi....



wanauzingira Yerusalemu kama walinda mashamba, kwa sababu watu wake wameniasi mimi Mwenyezi-Mungu. Yuda, mwenendo wako na matendo yako yamekuletea hayo. Hayo ndiyo maafa yaliyokupata, tena ni machungu; yamepenya mpaka ndani moyoni mwako.”

Yeremia 4:17-18

Tazama watoto wako wenye shida/tabu,wote wanaopitia magumu/majaribu mbalimbali
Mungu wetu tunaomba ukawaguse kwa mkono wako wenye nguvu
kila mmoja na mahitaji yake
Mungu wetu tunaomba ukawasamehe pale walipo kwenda kinyume nawe
Yahweh tunaomba ukawape neema ya kuweza kujiombea,kufuata njia zako nazo zikawaweke huru...
Baba wa Mbinguni tunayaweka haya yote mikononi mwako
Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele...
Amina...!!


Asanteni sana wapendwa katika Kristo Yesu kwakuwa nami,Baba wa Mbinguni aendelee kuwatendea sawasawa na mapenzi yake...

Nawapenda.



 Suala juu ya siku ya Sabato

(Mat 12:1-8; Marko 2:23-28)
1Siku moja ya Sabato, Yesu alikuwa anapita katika mashamba ya ngano, na wanafunzi wake wakaanza kuvunja masuke ya ngano, wakaondoa punje zake kwa mikono, wakala. 2Baadhi ya Mafarisayo wakawauliza, “Mbona mnafanya jambo ambalo si halali siku ya Sabato?” 3Yesu akawajibu, “Je, hamjasoma jinsi alivyofanya Daudi pamoja na wenzake wakati walipokuwa na njaa? 4Yeye aliingia katika nyumba ya Mungu, akachukua ile mikate iliyowekwa mbele ya Mungu, akala na kuwapa wenzake. Haikuruhusiwa mtu kula mikate hiyo isipokuwa tu makuhani.” 5Hivyo akawaambia, “Mwana wa Mtu ana uwezo juu ya Sabato.”
Mtu mwenye mkono uliopooza
(Mat 12:9-14; Marko 3:1-6)
6Siku nyingine ya Sabato, Yesu aliingia katika sunagogi, akafundisha. Mle ndani kulikuwa na mtu ambaye mkono wake wa kulia ulikuwa umepooza. 7Waalimu wa sheria na Mafarisayo walitaka kupata kisa cha kumshtaki Yesu na hivyo wakawa wanangojea waone kama angemponya mtu siku ya Sabato. 8Lakini Yesu alijua mawazo yao, akamwambia yule mwenye mkono uliopooza, “Inuka, simama katikati.” Yule mtu akaenda kusimama katikati. 9Kisha Yesu akawaambia, “Nawaulizeni, je, ni halali siku ya Sabato kutenda jambo jema au kutenda jambo baya; kuokoa maisha au kuyaangamiza?” 10Baada ya kuwatazama wote waliokuwa pale, akamwambia yule mtu, “Nyosha mkono wako.” Naye akafanya hivyo, na mkono wake ukawa mzima tena. 11Lakini wao wakakasirika sana, wakajadiliana jinsi ya kumtendea Yesu maovu.
Yesu anateua mitume kumi na wawili
(Mat 10:1-4; Marko 3:13-19)
12Siku moja Yesu alikwenda mlimani kusali, akakesha huko usiku kucha akisali. 13Kesho yake aliwaita wanafunzi wake, na miongoni mwao akawachagua watu kumi na wawili ambao aliwaita mitume: 14Simoni (ambaye Yesu alimpa jina Petro) na Andrea ndugu yake, Yakobo na Yohane, Filipo na Bartholomayo, 15Mathayo na Thoma, Yakobo wa Alfayo na Simoni (aliyeitwa Zelote), 16Yuda wa Yakobo na Yuda Iskarioti ambaye baadaye alikuwa msaliti.
Yesu anafundisha na kuwaponya watu
(Mat 4:23-25)
17Baada ya kushuka mlimani pamoja nao, Yesu alisimama mahali palipokuwa tambarare. Hapo kulikuwa na kundi kubwa la wanafunzi wake na umati wa watu waliotoka pande zote za Yudea na Yerusalemu na pwani ya Tiro na Sidoni. Wote walifika kumsikiliza Yesu na kuponywa magonjwa yao. 18Aliwaponya pia wote waliokuwa wanasumbuliwa na pepo wachafu. 19Watu wote walitaka kumgusa, kwa maana nguvu ilikuwa inatoka ndani yake na kuwaponya wote.
Heri na ole
(Mat 5:1-12)
20Yesu akawageukia wanafunzi wake, akasema:
“Heri nyinyi mlio maskini,
maana ufalme wa Mungu ni wenu.
21Heri nyinyi mnaosikia njaa sasa,
maana baadaye mtashiba.
Heri nyinyi mnaolia sasa,
maana baadaye mtacheka kwa furaha.
22“Heri yenu nyinyi iwapo watu watawachukia, watawatenga, watawatukana na kuwaharibieni jina kwa ajili ya Mwana wa Mtu. 23Wakati hayo yatakapotokea, furahini na kucheza, maana hakika tuzo lenu ni kubwa mbinguni. Kwa maana wazee wao waliwatendea manabii vivyo hivyo.
24Lakini ole wenu nyinyi mlio matajiri,
maana mmekwisha pata faraja yenu.
25Ole wenu nyinyi mnaoshiba sasa,
maana baadaye mtasikia njaa.
Ole wenu nyinyi mnaocheka kwa furaha sasa,
maana baadaye mtaomboleza na kulia.
26Ole wenu nyinyi iwapo watu wote wanawasifu,
maana wazee wao waliwafanyia manabii wa uongo vivyo hivyo.
Kuwapenda maadui
(Mat 5:38-48; 7:12a)
27“Lakini nawaambieni nyinyi mnaonisikiliza, wapendeni maadui zenu, watendeeni mema wale wanaowachukieni. 28Watakieni baraka wale wanaowalaani, na waombeeni wale wanaowatendea vibaya. 29Mtu akikupiga shavu moja mgeuzie pia la pili. Mtu akikunyanganya koti lako mwachie pia shati lako. 30Yeyote anayekuomba mpe, na mtu akikunyanganya mali yako usimtake akurudishie. 31Jinsi mnavyotaka watu wawatendee nyinyi, watendeeni wao vivyo hivyo.
32“Na ikiwa mnawapenda tu wale wanaowapenda nyinyi, je, mtapata tuzo gani? Hakuna! Kwa maana hata wenye dhambi huwapenda wale wanaowapenda wao. 33Tena, kama mkiwatendea mema wale tu wanaowatendeeni mema, mtapata tuzo gani? Hata wenye dhambi hufanya hayo. 34Na kama mnawakopesha wale tu mnaotumaini watawalipeni, je, mtapata tuzo gani? Hata wenye dhambi huwakopesha wenye dhambi wenzao ili warudishiwe kima kilekile. 35Ila nyinyi wapendeni maadui zenu na kuwatendea mema; kopesheni bila kutazamia kurudishiwa, na tuzo lenu litakuwa kubwa, nanyi mtakuwa watoto wa Mungu aliye juu. Kwa maana yeye ni mwema kwa wale wasio na shukrani na walio wabaya. 36Muwe na huruma kama Baba yenu alivyo na huruma.
Juu ya kuwahukumu wengine
(Mat 7:1-5)
37“Msiwahukumu wengine, nanyi hamtahukumiwa; msiwalaumu wengine, nanyi hamtalaumiwa; wasameheni wengine, nanyi mtasamehewa. 38Wapeni wengine wanavyohitaji, nanyi mtapewa. Naam, mtapokea mikononi mwenu kipimo kilichojaa, kikashindiliwa na kusukwasukwa hata kumwagika. Kwa maana kipimo kilekile mnachotumia kwa wengine ndicho atakachotumia Mungu kwenu.”
39Akawaambia mfano huu: “Je, kipofu anaweza kumwongoza kipofu mwenzake? La! Wote wataanguka shimoni. 40Mwanafunzi hampiti mwalimu wake, lakini kila mwanafunzi akisha hitimu huwa kama mwalimu wake. 41Kwa nini wakiona kibanzi jichoni mwa ndugu yako, na papo hapo huioni boriti iliyoko jichoni mwako? 42Au, wawezaje kumwambia ndugu yako, ‘Ndugu, ngoja nikuondoe kibanzi jichoni mwako,’ na huku huioni boriti iliyomo katika jicho lako mwenyewe? Mnafiki wewe! Toa kwanza boriti iliyomko jichoni mwako, na hapo ndipo utaona sawasawa kiasi cha kuweza kuondoa kibanzi kilicho jichoni mwa ndugu yako.
Mtu hujulikana kwa matunda yake
(Mat 7:16-20; 12:33-35)
43“Mti mzuri hauzai matunda mabaya, wala mti mbaya hauzai matunda mazuri. 44Watu huutambua mti kutokana na matunda yake. Ni wazi kwamba watu hawachumi tini katika michongoma, wala hawachumi zabibu katika mbigili. 45Mtu mwema hutoa yaliyo mema kutoka katika hazina bora iliyomo moyoni mwake; na mtu mbaya hutoa yaliyo mabaya kutoka katika hazina mbaya iliyo moyoni mwake, kwa maana mtu huongea kutokana na yale yaliyojaa moyoni mwake.
Wajenzi wa namna mbili
(Mat 7:24-27)
46“Mbona mwaniita ‘Bwana, Bwana,’ na huku hamtimizi yale ninayosema? 47Nitawapeni mfano unaofaa kuonesha alivyo yeyote yule anayekuja kwangu, akasikia maneno yangu na kuyatimiza: 48Huyo anafanana na mtu ajengaye nyumba, ambaye amechimba chini na kuweka msingi wake juu ya mwamba; kukatokea mafuriko ya mto, mkondo wa maji ukaipiga nyumba ile, lakini haukuweza kuitikisa, kwa sababu ilikuwa imejengwa imara. 49Lakini yeyote anayesikia maneno yangu asifanye chochote, huyo anafanana na mtu aliyejenga nyumba juu ya udongo, bila msingi. Mafuriko ya mto yakatokea, mkondo wa maji ukaipiga nyumba ile, ikaanguka na kuharibika kabisa!”

Luka6;1-49

Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)

"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe

Wednesday 21 October 2020

Kikombe Cha Asubuhi; Luka 5...



Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?

Tumshukuru Mungu wetu katika yote...

Asante  Mungu wetu kwa wema na fadhili zako kwetu
Asante kwa ulinzi wako kwetu wakati wote
Asante kwa kutuchagua tena na kutupa
kibali cha kuendelea kuiona leo hii
Asante kwa pumzi/uzima,
afya na kuwatayari kwa majukumu yetu


Utukuzwe ee Mungu wetu,usifiwe Baba wa Mbinguni

Neema yako yatutosha  Mungu wetu..



Kama simba atokavyo mafichoni mwake, mwangamizi wa mataifa ameanza kuja, anakuja kutoka mahali pake, ili kuiharibu nchi yako. Miji yako itakuwa magofu matupu, bila kukaliwa na mtu yeyote. Kwa hiyo, vaa vazi la gunia, omboleza na kulia; maana, hasira kali ya Mwenyezi-Mungu, bado haijaondoka kwetu.

Yeremia 4:7-8

Baba wa Mbinguni tunakuja mbele zako tukijinyenyekeza,
tukijishusha na kujiachilia mikononi mwako

Mungu wetu tunaomba utusamehe dhambi zetu zote
Baba wa Mbinguni nasi tunaomba utupe neema ya kuweza kuwasamehe wale wote waliotukosea,Usitutie majaribuni Mungu wetu tunaomba utuepushe na yule mwovu na kazi zake zote,Jehovah ututakase miili yetu na akili zetu Baba wa Mbinguni tunaomba utufunike kwa  Damu ya Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo wa Nazareti,
Yeye aliteseka kwanza ili sisi tupate kupona....



Mwenyezi-Mungu asema hivi: “Siku hiyo, mfalme na wakuu watakufa moyo; makuhani watapigwa na bumbuazi, na manabii watashangaa.” Kisha nikasema: “Aa, Mwenyezi-Mungu, hakika umewadanganya kabisa watu hawa na mji wa Yerusalemu! Uliwaambia mambo yatawaendea vema, kumbe maisha yao yamo hatarini kabisa!”

Yeremia 4:9-10

Mungu wetu tunaomba ukabariki kazi za mikono yetu 
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe ubunifu na maarifa 

katika utendaji
Jehovah nasi tukatende sawasawa na mapenzi yako
Baba wa Mbinguni tunaomba ukabariki ridhiki zetu
ziingiazo/zitokazo
Mungu wetu nasi tunaomba ukatupe neema ya kuweza
kuwabariki wenye kuhitaji
Yahweh tusipungukiwe katika mahitaji yetu
Mungu wetu ukatupe kama inavyokupendeza wewe



Jehovah tunayaweka maisha yetu mikononi mwako
Baba wa Mbinguni tunaomba ukabariki nyumba/ndoa zetu,
watoto,wazazi wetu,familia/ndugu na wote wanaotuzunguka
Jehovah tunaomba ulinzi wako kwetu na kwa vyote tunavyo vimiliki
Yahweh tunaomba ukatubariki tuingiapo/tutokapo
Mungu wetu tunaomba ukavibariki vyote tunavyoenda kugusa/kutumia
Baba wa Mbinguni ukavitakase kwa Damu ya Bwana wetu Yesu Kristo
Mungu wetu ukatamalaki na kutuatamia
Baba wa Mbinguni tukawe salama rohoni
Mfalme wa amani amani yako ikatawale katika maisha yetu
Mungu wetu ukatupe macho ya kuona na masikio ya kusikia 
sauti yako na kuitii
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe neema ya kufuata njia zako
Yahweh tukasimamie Neno lako amri na sheria zako siku zote 
za maisha yetu

Mungu  wetu ukaonekane katika maisha yetu popote tupitapo na ikajulikane kwamba upo 

Neema zako zikawe nasi Nuru yako ikaangaze katika maisha yetu
Ukatufanye barua njema ee Mungu wetu nasi tukasomeke kama
inavyokupendeza wewe
Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi...



Wakati huo, wataambiwa hivi watu hawa pamoja na mji wa Yerusalemu, “Upepo wa hari kutoka vilele vikavu vya jangwani utawavumia watu wangu. Huo si upepo wa kupepeta au kusafisha, bali ni upepo mkali sana utokao kwangu. Ni mimi Mwenyezi-Mungu nitakayetoa hukumu juu yao.”

Yeremia 4:11-12

Tazama wenye shida/tabu,Mungu wetu tunaomba
 ukawaguse kila mmoja na mahitaji yake
Baba wa Mbinguni tunaomba ukawasamehe pale walipokwenda
kinyume nawe
Mungu wetu ukawape neema ya kujiombea,macho ya rohoni,masikio yakusikia sauti yako,wakafuate njia zako nazo zikawaweke huru
Mungu wetu tunaomba ukasikie kulia kwao
Baba wa Mbinguni tunomba ukawafute machozi yao
Nuru yako ikaangaze katika maisha yao
Mungu wetu tunaomba ukawatendee sawasawa na mapenzi yako
Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele
Amina....!!!



Wapendwa katika Kristo Yesu asanteni sana
kwakuwanami/kunisoma

Mungu Baba aendelee kuwabariki na kuwatendea
kama inavyompendeza yeye
Amani ya Bwana wetu Yesu Kristo na upendo wa Mungu Baba
ukae nanyi daima....

Nawapenda.



 Yesu anawaita wanafunzi wa kwanza

(Mat 4:18-22; Marko 1:16-20)
1Siku moja, Yesu alikuwa amesimama kando ya ziwa Genesareti, na watu wengi walikuwa wamemzunguka wakisongamana, wanasikiliza neno la Mungu. 2Akaona mashua mbili ukingoni mwa ziwa. Wavuvi wenyewe walikuwa wametoka, wanaosha nyavu zao. 3Baada ya Yesu kuingia katika mashua moja iliyokuwa ya Simoni, alimtaka Simoni aisogeze majini, mbali kidogo na ukingo wa ziwa. Akaketi, akafundisha umati wa watu akiwa ndani ya mashua.
4Alipomaliza kufundisha, akamwambia Simoni, “Endesha mashua mpaka kilindini, mkatupe nyavu zenu mpate kuvua samaki.” 5Simoni akamjibu, “Bwana, tumejitahidi kuvua samaki usiku kucha bila kupata kitu, lakini kwa kuwa umesema, nitatupa nyavu.” 6Baada ya kufanya hivyo, wakavua samaki wengi, hata nyavu zao zikaanza kukatika. 7Wakawaita wenzao waliokuwa katika mashua nyingine waje kuwasaidia. Wakaja, wakazijaza mashua zote mbili samaki, hata karibu zingezama.
8Simoni Petro alipoona hayo, akapiga magoti mbele ya Yesu akisema, “Ondoka mbele yangu, ee Bwana, kwa kuwa mimi ni mwenye dhambi!” 9Simoni pamoja na wenzake wote walishangaa kwa kupata samaki wengi vile. 10Hali kadhalika Yakobo na Yohane, wana wa Zebedayo, waliokuwa wavuvi wenzake Simoni. Yesu akamwambia Simoni, “Usiogope; tangu sasa utakuwa ukivua watu.” 11Basi, baada ya kuzileta zile mashua ukingoni mwa ziwa, wakaacha yote, wakamfuata.
Yesu anamponya mwenye ukoma
(Mat 8:1-4; Marko 1:40-45)
12Ikawa, Yesu alipokuwa katika mmojawapo wa miji ya huko, mtu mmoja mwenye ukoma mwili mzima akamwona. Basi, mtu huyo akaanguka kifudifudi akamwomba Yesu: “Bwana, ukitaka, waweza kunitakasa.”
13Yesu akanyosha mkono, akamgusa na kusema, “Nataka! Takasika!” Mara ule ukoma ukamwacha. 14Naye Yesu akamwamuru: “Usimwambie mtu yeyote; bali nenda ukajioneshe kwa kuhani, ukatoe sadaka kwa ajili ya kutakasika kwako kama alivyoamuru Mose kuwathibitishia kwamba umepona.”
15Lakini habari za Yesu zilizidi kuenea kila mahali. Watu makundi mengi wakakusanyika ili kumsikiliza na kuponywa magonjwa yao. 16Lakini yeye alikwenda zake mahali pasipo na watu, akawa anasali huko.
Yesu anamponya mtu aliyepooza
(Mat 9:1-8; Marko 2:1-12)
17Siku moja, Yesu alikuwa akifundisha. Mafarisayo na waalimu wa sheria kutoka katika kila kijiji cha Galilaya, Yudea na Yerusalemu, walikuwa wameketi hapo. Nguvu ya Bwana ilikuwa pamoja naye kwa ajili ya kuponya wagonjwa. 18Mara watu wakaja, wamemchukua mtu mmoja aliyepooza maungo, amelala kitandani; wakajaribu kumwingiza ndani, wamweke mbele ya Yesu. 19Lakini, kwa sababu ya wingi wa watu, hawakuweza kuingia ndani. Basi, wakapanda juu ya paa, wakaondoa vigae, wakamshusha huyo aliyepooza pamoja na kitanda chake, wakamweka mbele ya Yesu. 20Yesu alipoona jinsi walivyokuwa na imani kubwa, akamwambia huyo mtu, “Rafiki, umesamehewa dhambi zako.”
21Waalimu wa sheria na Mafarisayo wakaanza kujiuliza: “Nani huyu anayesema maneno ya kufuru? Hakuna mtu awezaye kusamehe dhambi ila Mungu peke yake!” 22Yesu alitambua mawazo yao, akawauliza, “Mnawaza nini mioyoni mwenu? 23Ni lipi lililo rahisi zaidi: Kusema, ‘Umesamehewa dhambi,’ au kusema, ‘Simama utembee?’ 24Basi, nataka mjue kwamba Mwana wa Mtu anao uwezo wa kuwasamehe watu dhambi duniani.” Hapo akamwambia huyo mtu aliyepooza, “Simama, chukua kitanda chako, uende zako nyumbani.” 25Mara, huyo mtu aliyepooza akasimama mbele yao wote, akachukua kitanda chake akaenda nyumbani kwake huku akimtukuza Mungu. 26Wote wakashangaa na kushikwa na hofu; wakamtukuza Mungu wakisema: “Tumeona maajabu leo.”
Lawi anaitwa kuwa mwanafunzi
(Mat 9:9-13; Marko 2:13-17)
27Baada ya hayo, Yesu akatoka nje, akamwona mtozaushuru mmoja aitwaye Lawi, ameketi ofisini. Yesu akamwambia, “Nifuate!” 28Naye akaacha yote akamfuata. 29Lawi akamwandalia Yesu karamu kubwa nyumbani mwake. Na kundi kubwa la watozaushuru na watu wengine walikuwa wameketi pamoja nao. 30Mafarisayo na waalimu wa sheria wakawanungunikia wanafunzi wake wakisema: “Kwa nini mnakula na kunywa pamoja na watozaushuru na wenye dhambi?” 31Yesu akawajibu, “Wenye afya hawamhitaji daktari; wanaomhitaji ni wale walio wagonjwa. 32Sikuja kuwaita watu wema, bali wenye dhambi, wapate kutubu.”
Suala juu ya kufunga
(Mat 9:14-17; Marko 2:18-22)
33Watu wengine wakamwambia, “Wafuasi wa Yohane Mbatizaji hufunga mara kwa mara na kusali; hata wafuasi wa Mafarisayo hufanya vivyo hivyo. Lakini wafuasi wako hula na kunywa.” 34Yesu akawajibu, “Je, wale walioalikwa harusini hutakiwa wafunge hali bwana arusi yuko pamoja nao? La! 35Lakini wakati utafika ambapo bwana arusi ataondolewa kati yao; wakati huo ndipo watakapofunga.”
36Yesu akawaambia mfano huu: “Watu hawakati kiraka cha nguo mpya na kukitia katika vazi kuukuu; kama wakifanya hivyo, watakuwa wamelikata hilo vazi jipya, na pia hicho kiraka hakitachukuana na hilo vazi kuukuu. 37Wala watu hawatii divai mpya katika viriba vikuukuu; kwani hiyo divai mpya itavipasua hivyo viriba, divai itamwagika, na viriba vitaharibika. 38Divai mpya hutiwa katika viriba vipya. 39Hakuna mtu anayetamani kunywa divai mpya baada ya kunywa divai ya zamani kwani husema ‘Ile ya zamani ni nzuri zaidi.’”


Luka5;1-39

Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)

"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe